Mwenye Mwendo wa Kasi, Asiyepuruka, na Anayevutia Sana—Mbuni
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kenya
MIONGONI mwa twiga, pundamilia, nyumbu, na swala ambao hutembea-tembea kwenye mbuga kubwa sana ya Afrika, mna viumbe fulani wa ajabu sana waliopata kuumbwa na Muumba. Watu wanaowaona hutiwa kicho na ukubwa wao, kimo chao kikubwa, miguu yao yenye nguvu, na manyoya yao maridadi kama sufu. Wakiwa na urefu wa meta 2.5 na uzito wa kilogramu 155, ndio ndege wakubwa zaidi.
Kama Ngamia Anayetembea kwa Madaha
Zamani za kale mbuni alipewa jina struthocamelus, ambalo ni mchanganyiko wa Kilatini na Kigiriki, linalorejezea ule uonwao kuwa ufanano wake na ngamia. Kama ngamia, mbuni anaweza kuvumilia joto jingi nao husitawi katika maeneo ya jangwa. Pia ana kope nyingi ambazo ni ndefu, zinazolinda macho yake makubwa na vumbi la mbuga. Miguu yake ni mirefu na myembamba, na nyayo zake ni zenye nguvu na zenye mnofu, zikiwa na vidole viwili tu. Watazamaji hushangazwa na mwendo wake, uvumilivu wake na sifa nyingine zinazofanana na za ngamia, wanapomwona mbuni akitembea kwa madaha kwenye nyanda zilizo wazi.
Mbuni hulisha miongoni mwa wanyama wengine wenye kwato, akila karibu kila kitu ambacho hutambaa. Mbuni hula kitu chochote na hali tu wadudu, nyoka, panya, mizizi, na mimea mingi bali pia humeza vipande vya mbao, makombe, mawe, vijiti, na karibu kitu chochote kidogo, cha rangi nyangavu.
Kwa sababu ya ukubwa na uzito wake, hawezi kupuruka. Hata hivyo, miguu yake yenye misuli ina nguvu vya kutosha kumfanya awe mmojawapo wa viumbe wenye mwendo wa kasi zaidi duniani. Anapokimbia katika maeneo ya jangwa, anaweza kufikia mwendo wa kilometa 65 kwa saa! Mbuni “humdharau farasi na mwenye kumpanda,” yasema Biblia. (Ayubu 39:18) Kwa kupatana na maoni hayo, mwendo wa kasi wa ndege huyo na uwezo wake wa kukimbia masafa marefu sana humwezesha awashinde kwa urahisi wanyama wengi wanaowinda wenye miguu minne ambao hukimbia kwa kasi zaidi.
Tabia Yake ya Kujamiiana
Wakati wa majira ya kujamiiana, mbuni wa kiume hucheza dansi za uchumba zenye madaha. Akipiga magoti mbele ya mbuni wa kike, yeye hunyoosha manyoya yake makubwa ya bawa ya rangi nyeupe na nyeusi na kuanza kuyatikisa kwa utaratibu. Kama mapepeo mawili makubwa, hujongea kutoka upande mmoja hadi mwingine. Shingo yake isiyo na manyoya na miguu huanza kugeuka rangi na kuwa waridi nyangavu, ambayo hutofautiana kwa njia yenye kuvutia na manyoya ya mwili ya rangi nyeusi tititi. Anapobembeza shingo yake ndefu kutoka upande mmoja hadi mwingine, yeye hupiga ardhi kwa nguvu kwa miguu yake.
Yaelekea maonyesho hayo yenye madoido na yenye madaha hukusudiwa kumvutia mbuni wa kike mwenye rangi ya hudhurungi isiyokolea. Hata hivyo, mara nyingi vya kutosha, wakati mbuni wa kiume anapoendelea na dansi ya uchumba ya majira ya kujamiiana, mbuni wa kike hutembea-tembea akidonoa ardhi, bila kutoa uangalifu na kutojali rabsha zinazoendelea kando yake.
Mbuni wa kike anapochaguliwa, yule wa kiume huchagua mahali pa kujenga kiota. Atachimba shimo lisilo na kina mavumbini mahali fulani katika mbuga iliyo wazi na kuelekeza mbuni kadhaa wa kike mahali hapo. Baada ya majuma mawili au matatu, kiota kitakuwa na dazani mbili au zaidi za mayai, yaliyotagwa na mbuni hao wa kike.
Katika muda wote wa majuma sita ambapo mayai yataatamia, mbuni wa kiume atalalia mayai usiku, na mbuni mmoja wa kike atafanya hivyo mchana. Kufikia hatua hii mayai huweza kudhuriwa nayo hutafutwa na simba, fisi, mbweha, na hata tai-mzoga wa Misri, ambao hupasua mayai hayo kwa kuyaangushia mawe.
Mayai Makubwa, Vifaranga Wakubwa Mno
Mayai ya rangi nyeupe na ya kijivujivu ya mbuni ndiyo makubwa zaidi ulimwenguni na kila yai laweza kuwa na uzito wa kilogramu 1.5. Kaka lake ni gumu nalo hung’aa na sehemu ya juu inafanana na kauri iliyong’arishwa. Kila yai linatoshana na mayai 25 ya kuku, nayo mayai ya mbuni yanathaminiwa sana kwa sababu ya lishe yao na ladha tamu. Nyakati nyingine makaka matupu hutumiwa na Wasan, ambao huyajaza maji.
Yai kubwa linapofikia hatua ya kuanguliwa, hutokeza kifaranga mkubwa mno! Vifaranga walioanguliwa hawawezi kujilinda, lakini wao hukua haraka na ni wakimbiaji. Katika muda wa mwezi mmoja, miguu yao yenye nguvu huwawezesha kukimbia kwa mwendo unaokaribia kilometa 55 kwa saa!
Vifaranga hutegemea ulinzi kutoka kwa wazazi. Ni ngano kusema kwamba mbuni huzamisha kichwa chake ndani ya mchanga anapokabili hatari. Kinyume na hilo, wazazi wa ndege wanaweza kuwa wakali sana wanapolinda makinda yao, wakiwafukuzia mbali wanyama wanaowinda kwa kuwapiga mateke yenye nguvu. Mbinu nyingine wanayotumia kujilinda ni kumkengeusha mnyama anayewinda kwa kujifanya kuwa wamejeruhiwa, hivyo wakiondoa uangalifu kwa makinda yao na kujielekezea kwao wenyewe. Hata hivyo, mnyama anayewinda akiwakaribia sana, kwa kawaida wazazi hugeuka na kukimbia ili kuokoa uhai wao, huku wakiacha wachanga wao wajitegemee wenyewe. Taarifa ya Biblia huthibitika kuwa ya kweli, kwa kuwa kwenye pindi hizo mbuni “huyafanyia ukali makinda yake, kana kwamba si yake.”—Ayubu 39:16.
Manyoya Mengi Sana
Mwanadamu amevutiwa na mbuni kwa maelfu ya miaka. Picha zilizochongwa kwenye mawe huonyesha wafalme Wamisri wakiwinda mbuni kwa kutumia nyuta na mikuki. Ustaarabu fulani uliwaona mbuni kuwa watakatifu. Wachina walithamini sana mayai ya mbuni yaliyo mazuri na waliyatoa kama zawadi zenye thamani kwa watawala. Kwa maelfu ya miaka, manyoya mengi laini ya mbuni yameremba mavazi ya kichwani ya majenerali wa kijeshi, wafalme, na wakuu wa Afrika.
Katika karne ya 14, manyoya ya mbuni yalithaminiwa sana na Wanaulaya wanaopenda mitindo. Lakini, haikuwa rahisi kuwinda mbuni kwa kutumia mikuki na mishale, kwa kuwa mnyama huyo huona vizuri sana na hutoroka hatari kwa wepesi. Wakati huo, mbuni hawakukabili hatari ya kuangamizwa.
Kisha, katika karne ya 19, manyoya ya mbuni yakaingia kwenye mtindo tena. Wakati huo, wawindaji waliua mamilioni ya mbuni kwa kutumia silaha za kisasa. Kuanzishwa kwa mashamba ya mbuni labda kuliokoa ndege hawa wakubwa wasiopuruka wasitoweshwe. Sasa wakiwa wanazalishwa utekwani, mbuni wamefugwa ili manyoya yao yatumiwe kwa ajili ya mitindo na kwa dasta za manyoya. Ngozi yao hutumiwa kutengeneza glavu laini za ngozi na mikoba, na nyama yao huuzwa katika mikahawa fulani.
Leo mbuni wenye fahari bado hutembea-tembea katika nyanda za Afrika. Hata ingawa makao yao ya zamani yamepunguzwa sana na katika maeneo mengine mbuni wameangamizwa, wanaendelea kuishi katika maeneo yaliyojitenga yenye vichaka wanayoyapendelea. Akiwa hapo anaweza kuonekana akikimbia kwelikweli kwenye nyanda akiwa na manyoya mengi yaliyo laini, akicheza dansi taratibu za uchumba, au akilinda kiota chake chenye mayai makubwa. Kwa kweli, ndege huyu mwenye mwendo wa kasi asiyepuruka ni kiumbe mwenye mabawa mwenye kuvutia sana ambaye hupendeza na kustaajabisha watu wanaomtazama.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mbuni wa kiume
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Mbuni ni baadhi ya viumbe wenye mwendo wa kasi zaidi duniani
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Nyayo zao zaweza kuwa silaha zenye nguvu
[Picha katika ukurasa wa 18]
Mbuni wa kike