Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 7/22 kur. 19-20
  • Mbwa Wangu Husikiliza kwa Niaba Yangu!

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mbwa Wangu Husikiliza kwa Niaba Yangu!
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kazi ya Twinkie
  • Mazoezi ya Kupata Ustadi
  • Uandamani Wenye Furaha
  • Je, Watoto Wako Salama Wakiwa na Mbwa Wako?
    Amkeni!—1997
  • Jinsi ya Kumzoeza Mbwa Wako
    Amkeni!—2004
  • Wanyama Ni Zawadi Kutoka kwa Mungu
    Amkeni!—2004
  • Uwezo wa Kunusa wa Mbwa
    Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 7/22 kur. 19-20

Mbwa Wangu Husikiliza kwa Niaba Yangu!

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA

“SIJUI ningefanyaje bila mbwa wangu mdogo!” Dorothy akasema, akimtazama kwa upendo mbwa wake mdogo mwenye rangi nyeupe na hudhurungi na ambaye ni uzao wa aina mbili za mbwa. Mbwa huyo ni jamii ya mbwa wanaoitwa Jack Russell terrier na alikuwa amelala chini ya kiti cha Dorothy akionekana ameridhika. “Nimekuwa na Twinkie kwa miezi michache tu, lakini tayari ameboresha maisha yangu!”

Nilipomchunguza Twinkie kwa makini zaidi niliona kwamba alikuwa amefungiwa hatamu ya rangi ya manjano ambayo ilikuwa imembana vizuri nayo ilikuwa imeandikwa “MBWA ASIKIAYE KWA NIABA YA KIZIWI.” ‘Huyu ni mnyama wa ajabu kama nini!’ Nakumbuka nikiwazia. ‘Anaweza kufanya nini?’

Tulikutana ghafula tulipokuwa miongoni mwa watu 44,000 waliokuwa wamehudhuria Mkusanyiko wa Kimataifa wa “Njia ya Mungu ya Maisha” wa Mashahidi wa Yehova Julai mwaka uliopita jijini London, Uingereza. Kwa kuketi karibu na kipaza-sauti, Dorothy aliweza kusikiliza programu, lakini kwa nini alihitaji mbwa wa kusikia kwa niaba yake? Tulipokuwa tumeketi tukiongea wakati wa pumziko la kula chakula cha mchana, Dorothy alinisimulia hadithi yake.

Kazi ya Twinkie

Dorothy ni kiziwi sana kwa sababu alipokuwa na umri wa miaka mitatu alishikwa na maradhi ya rheumatic fever. Tangu mume wake afe miaka 23 iliyopita, ameishi peke yake, lakini kama alivyoeleza Dorothy, alihitaji mengi zaidi ya uandamani tu alipoendelea kuzeeka. “Viziwi wanaweza kuhisi wamekosa usalama sana wakifikia umri wangu,” akasema. “Nina umri wa miaka 74 na ninaishi katika jengo ambalo lina mtunzaji, lakini huyo mtunzaji anapokuja kuniona, siwezi kusikia kengele ya mlango. Akifikiria kwamba labda mimi ni mgonjwa, nyakati nyingine yeye huingia tu bila mimi kujua; na kunishtua sana. Lakini sasa Twinkie husikia kengele, naye huja kunigusa mguu na kuniongoza kuelekea mlangoni. Vilevile, Twinkie akisikia kelele ya joko langu, yeye hunikimbilia, nami humfuata. Iwapo kuna king’ora cha kutahadharisha juu ya moshi au moto, Twinkie amezoezwa kuvutia uangalifu wangu kisha alale chini akionyesha kwamba kuna hatari kubwa. Kila wakati anaponisaidia, mimi humthawabisha kwa njia ya kipekee, kwa kumpa chakula kitamu.”

Mazoezi ya Kupata Ustadi

Nikawa na udadisi sana. “Ulipataje mbwa wako, na ni nani aliyemzoeza?” nikauliza. Hiyo ikawa ni fursa ya Dorothy kunisimulia kuhusu Mbwa Wasikiao kwa Niaba ya Viziwi, na mpango huo una kusudi la kuwasaidia viziwi nchini Uingereza wapate kujitegemea zaidi na basi kuboresha maisha yao. Tangu mwaka wa 1982 mpango huo umewapa mamia ya viziwi mbwa nchini Uingereza. Mara tu mbwa amezoezwa vizuri, yeye hupelekwa kwa mwenyewe, bila malipo.

Kwa kawaida mbwa wanaorandaranda ndio huchaguliwa, wakiwa wametolewa kwenye vituo vilivyoko nchini kote vya kushughulikia mbwa wanaorandaranda, ijapokuwa baadhi ya mbwa hutolewa na wakuzaji wa mbwa. Huchukua hadi miezi 12 kuzoeza mbwa. Gharama ya kuzoeza mbwa mara nyingi hulipwa na mdhamini ambaye inawezekana iwe ni kampuni au kikundi cha watu ambao hujumlisha michango yao pamoja. Dorothy aliniambia kwamba chama cha kusaidia watu kupunguza unene ndicho kilichofanya hisani ya kumdhamini Twinkie.

Akiwa amechaguliwa, kila mbwa mwenye uwezo wa kusikia kwa niaba ya viziwi, mwenye umri baina ya majuma saba hadi miaka mitatu, huzoezwa kuitikia aina fulani za sauti. Lakini, mwanzoni yeye hupelekwa kwa mtu wa kumfundisha aweze kuishi na watu, na mtu huyo huwa ni mjitoleaji anayeishi na mbwa huyo kati ya miezi miwili hadi miezi minane, kwa kutegemea umri na uzoefu wa mbwa huyo. Mafundisho hayo yanaweza kutia ndani mambo ya kawaida ya kutochafua nyumba, lakini lengo kubwa ni kumfanya mbwa ajue sehemu za umma na usafiri wa umma na kumfanya azoee watu wa umri mbalimbali, kutia ndani watoto na vitoto vichanga. Lengo ni kumfundisha mbwa awe na tabia nzuri katika makao yoyote ambayo huenda akachukuliwa.

Vilevile, nilipata kujua kwamba mashirika mengine hutumia mbwa kuwasaidia watu wenye uhitaji wa pekee. Pamoja na kuzoezwa kutii amri, mbwa hao huzoezwa hasa kuona vitu fulani au kunusa harufu fulani hususa. Mbwa mmoja anayemtunza mwanamke mmoja anayetumia kiti chenye magurudumu amefundishwa kuchukua simu na barua zake na kuramba stempu za barua! Mbwa mwingine huitikia amri 120, kutia ndani hata kuchukua makopo na paketi kutoka kwenye rafu za dukani. Mtu huyo asiyejiweza hutumia tochi kuangazia kitu anachotaka, kisha mbwa huyo humletea vitu hivyo.

Uandamani Wenye Furaha

“Je, kila mtu hutambua thamani ya Twinkie?” nikauliza. “Muuzaji mmoja dukani alikataza Twinkie asiingie,” Dorothy akajibu. “Nafikiri ni kwa sababu alikuwa ameweka vyakula fulani viwe wonyesho hapo, lakini mtazamo wake ulikuwa tofauti sana kwa kuwa hakuelewa ni kwa nini namhitaji Twinkie.”

Sasa nilielewa thamani ya kuwa na mbwa anayesikia nyumbani, lakini bado nilikuwa na swali moja zaidi. Twinkie alikuwa na manufaa gani Dorothy alipokuwa akichangamana kwa furaha na Wakristo wenzake? “Ninaweza kusoma midomo vizuri, na kifaa cha kunisaidia kusikia hunisaidia kuweza kuwa na mazungumzo na mtu,” Dorothy akaeleza. “Watu waonapo jaketi ya manjano ya Twinkie, mara moja wao hutambua kwamba mimi ni kiziwi. Basi wao huzungumza nami moja kwa moja, mara nyingi kwa wazi kadiri wawezavyo. Kwa hiyo si lazima nieleze shida yangu, na jambo hilo hufanya maisha yangu yawe rahisi zaidi.”

Kipindi cha mkusanyiko kilikuwa karibu kuanza, na Twinkie alihitaji matembezi kabla ya kutulia kwenye kipindi cha alasiri. Kabla ya kuondoka, niliinama nikampapasa polepole. Twinkie akafumbua macho yake maangavu akamtazama Dorothy na kutikisa mkia wake. Alikuwa rafiki mdogo mtiifu kwelikweli—nao walipatana kabisa!

[Picha katika ukurasa wa 20]

Twinkie husaidia sana kwenye mikusanyiko

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki