Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 8/8 kur. 15-17
  • Ndege Ambaye Hubusu Maua

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ndege Ambaye Hubusu Maua
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sarakasi Zenye Kustaajabisha
  • Mlaji-Mlafi
  • Taratibu za Kutafuta Uchumba
  • Makao Yenye Kupendeza
  • Ni Wasioogopa
  • Ulimi wa Ndege Mvumaji
    Amkeni!—2010
  • Ulimi wa Ndege Mvumaji
    Je, Ni Kazi ya Ubuni?
  • Uumbaji Unatufundisha Nini Kuhusu Ujasiri?
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo—2020
  • Kuwatazama Ndege—Je, Kwavutia Kila Mtu?
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 8/8 kur. 15-17

Ndege Ambaye Hubusu Maua

WABRAZILI humwita beija-flor—ndege ambaye hubusu maua. Jina hilo lafaa daraka alilo nalo ndege mvumaji miongoni mwa maua yanayochanua. Watazamaji wengine, wanapoona manyoya mengi ya ndege huyo, huwaita viumbe hawa wadogo “vito vilivyo hai” au “vipande vyenye kupendeza vya upinde wa mvua” na kupatia aina nyingine za ndege huyo majina mengi sana, kama vile yakuti-topazi, zumaridi yenye tumbo linalometameta, au nyotamkia yenye mkia wa shaba.

Rangi hiyo yenye kuvutia huonekana hasa kwenye manyoya ya kipekee kuzunguka koo na taji la ndege wavumaji wa kiume. Manyoya yao yana tabaka za chembe zilizojazwa hewa, na chembe hizo hupinda mawimbi ya nuru kuwa rangi za upinde wa mvua kama vile mamilioni ya mapovu madogo ya sabuni yawezavyo kufanya.

Ufafanuzi wenye kupendeza wa ndege mvumaji wa rangi ya kikahawia nyekundu, anayepatikana hasa magharibi mwa Amerika Kaskazini, unapatikana katika kitabu Creature Comforts, cha Joan Ward-Harris: “Manyoya yake yaliyo kama kito, yako kwenye koo—sehemu inayozunguka koo . . . Yanaenea hadi kwenye mashavu yake na chini ya kidevu chake hadi kwenye koo na kifuani, kama kitambaa cha mtoto afungwacho shingoni alapo. Sura yenye mwako ya sehemu inayozunguka koo inastaajabisha—ndege huyo huonekana kuwa mkubwa mara mbili zaidi ya ukubwa wake wa kawaida na huonekana kana kwamba anawaka kihalisi.” Ndege huyo mwekundu anapopuruka kwa kasi, shingo yake yaweza kumweka rangi ya urujuani, zumaridi, au hata rangi zote za spektra. Akigeuka kutoka kwenye nuru, sehemu inayozunguka koo yake hugeuka rangi kwa ghafula na kuwa mahameli nyeusi kabisa.

Sarakasi Zenye Kustaajabisha

Ndege wavumaji wanajulikana kwa sarakasi bora kabisa. Kwa kitambo kidogo, mmoja atazunguka-zunguka kwenye ua, akinywa mbochi yake, huku mabawa yake yakivuma na kutia ukungu. Kisha, kwa ghafula, kiumbe huyo mdogo mwenye uwezo hujivurumisha mbele, nyuma, upande, au hata kujipindua, huku akipigapiga mabawa yake mara 50 hadi 70—wengine wanasema 80—kwa sekunde moja! Inaripotiwa kwamba anaweza kufikia mwendo wa kilometa 50 hadi 100 kwa saa na kisha kusimama kwa ghafula. Ni nini humwezesha ndege mvumaji kufanya matendo haya ya ajabu?

Ufunguo unapatikana kwenye sehemu za mwili zilizoumbwa kwa njia ya ajabu. Misuli iliyositawi vizuri, iliyokazwa kwenye mfupa wa kidari, hufanyiza asilimia 25 hadi 30 ya uzito wa mwili wake. Mabawa yake, ambayo ni thabiti kutoka kwenye bega hadi kwenye ncha ya bawa, humpa nguvu za kuyapiga juu na chini, badala ya kuyapiga tu kuelekea upande wa chini kama ilivyo na ndege wengine. Hivyo, kwa kupiga juu na chini anaweza kujiinua na kujisogeza mbele, huku kiungo cha bega kikimruhusu ajipindue kwa digrii 180. Si ajabu kwamba sarakasi za ndege huyo zaweza kukuvutia!

Je, wavumaji wangeweza kupita mtihani wa uvumilivu? Kwa hakika. Kwa mfano, kila mwaka ndege fulani wavumaji wa rangi nyekundu huhama zaidi ya kilometa 3,000 kutoka kwenye makao yao ya baridi kali katika Mexico hadi kaskazini ya mbali ya Alaska. Hatari za njia nyembamba za milima mirefu, bahari, na halihewa mbaya haziwashtui.

Mlaji-Mlafi

Mapenzi ambayo ndege wavumaji hufanya na maua wanayoyazuru hutimiza kusudi la maana—mchavusho-tambuko. Hata hivyo, wao huvutiwa kihalisi na mbochi. Ili kupata nguvu nyingi alizo nazo, mvumaji anahitaji kula mbochi yenye kabohidrati nyingi karibu nusu ya uzito wake (wengine husema mara mbili) ya uzito wake kila siku. Unaweza kuwazia uwiano unaotakikana wa chakula kwa binadamu?

Tofauti na ndege wengine, ndege wavumaji hutembea kwa nadra sana. Wao hula wanapopuruka. Wakiwa na midomo yenye urefu na umbo linalotofautiana kulingana na aina zake, wao huchagua maua yaliyochanua yatakayofaa midomo yao. Nao hupata mbochi kutoka kwa maua ya rangi zote, kutia ndani yale yasiyokuwa na harufu. Wao pia hula nzi wa matunda na wadudu kwenye mimea. Ndege huyo hupataje mbochi kutoka kwenye maua anayoyabusu?

Chombo cha mvumaji ni ulimi wake. Joan Ward-Harris aandika: “Ulimi wa mvumaji ni mrefu, mwembamba, umegawanyika na una manyoya machache kwenye ncha yake; umegawanywa na mikunjo miwili, inayotokeza kanda ndogo sana ambamo mbochi hupitishwa kwa mvuto mpaka inapomezwa.”

Ukiwavutia ndege wavumaji kwenye kifaa cha kuandalia chakula karibu na dirisha lako, hutachoka kamwe na vitumbuizo utakavyoonyeshwa na ndege hawa wenye nguvu. Hata hivyo, fanya hivyo tu ikiwa uko tayari kuwashughulikia kwa msimu mzima, kwa kuwa watategemea chakula chako wanapolea familia yao katika kiota kilicho karibu.

Taratibu za Kutafuta Uchumba

Aina fulani za ndege wavumaji katika Amerika ya Kati na ya Kusini huvutia wapenzi wao wa kike kwa kuimba kwao. Ndege mvumaji anayeitwa wine-throated wa Guatemala, ndiye anayejua kuimba zaidi kwa kubadili sauti. Na wimbo wa ndege mvumaji mwenye masikio meupe husikika kama “sauti yenye kupendeza ya kengele ndogo iliyotengenezwa kwa fedha.” Hata hivyo, wengi hawajulikani kama waimbaji stadi. Wao hurudia-rudia tu noti chache zenye mvumo mkubwa tena na tena au nyakati fulani huimba midomo ikiwa imefumbwa na sehemu inayolinda koo ikiwa imejitokeza.

Wavumaji wengine hufanya maonyesho ya sarakasi yenye kuvutia katika taratibu zao za kutafuta uchumba. Ndivyo ilivyo na mvumaji mwekundu, ambaye hushuka kwa kasi kutoka juu kufikia tu mahali ndege wa kike anapotazama na kisha—kabla hajafikia yule wa kike—huruka juu kwa ghafula na kufanyiza herufi J. Hufanyiza herufi J kwenda na kurudi mpaka anaporudi kwenye sehemu ya juu kabisa au kupuruka na mwenzi wake mpya. Wakati wa maonyesho haya aweza kupiga mabawa yake mara mia mbili kwa sekunde moja!

Makao Yenye Kupendeza

Mtazamaji mmoja adai kwamba kiota cha ndege mvumaji “ni mojawapo ya vitu vyenye kupendeza zaidi ulimwenguni.” Joan Ward-Harris alimwonyesha ripota wa Amkeni! kiota alichokuwa amepata. Kilikuwa na upana wa sentimeta 4.5 na kina kipatacho sentimeta 1, kilijengwa kwa njia ya kwamba watoto wa nyuki-bambi wanapokua, makao yao yenye kustarehesha yangepanuka ili kuwatosha. Ni jambo linalopendeza kushikilia kiota kwenye kiganja chako—kikombe kidogo sana kilichotengenezwa kwa mimea myororo. Pia viota vimetengenezwa kwa manyoya laini yaliyofumwa pamoja na tando za buibui. Ndani yake mna mayai mawili au matatu meupe kabisa, “kama lulu zinazolingana kabisa.”

Mama anapolisha makinda yake, huingiza mdomo wake ndani kabisa ya koo zao ndogo, akicheua lishe inayotakikana. Kwa kawaida baada ya majuma matatu tu, makinda huondoka kwa kuongozwa na silika, wakijilisha na kukua mpaka wakati silika zao zinapowaongoza kusafiri mbali kuelekea sehemu zenye halihewa isiyo baridi sana.

Ni Wasioogopa

Tabia ya kushangaza ya ndege mvumaji ni hali yake ya kutoogopa. Unaweza kujionea jambo hilo hasira zinapopanda kuhusu eneo la malisho. Huko Amerika Kusini ndege wawili aina ya coronet wa rangi ya mahameli-zambarau walionekana wakimtimua kwa ujasiri tai aliyekuwa amevamia mahali palipo na viota vyao, wakionyesha utayari wa kupambana na Jitu inapokuwa lazima. Lakini nyakati nyingine ndege wavumaji huuawa na maadui wengineo, kama vile nyoka, vyura, tando za buibui, maua yenye miiba, na wakusanyaji wa kibinadamu.

Hata hivyo, wanadamu wengi hufanya urafiki na ndege wavumaji na kuwangojea kwa hamu warudipo kila msimu ili kuendeleza mtindo wao wa maisha wenye kusudi. Kuchunguza vito hivi vya uumbaji vyenye kung’aa kwa ukaribu zaidi kwa hakika kutazidisha upendezi wako kuwaelekea—wakiamua kubusu maua yaliyoko shambani mwako.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

MAMBO HAKIKA JUU YA NDEGE WAVUMAJI

• Kukiwa na aina 320 za ndege wavumaji, hao ndio jamii ya pili kwa ukubwa katika Kizio cha Magharibi

• Ndio warembo zaidi katika jamii ya ndege: Ndege anayeitwa bee hummingbird wa Kuba ana urefu wa sentimeta sita kutoka kwenye ncha ya mkia wake hadi kwenye ncha ya mdomo wake

• Ndege mvumaji mkubwa zaidi ana urefu wa sentimeta 22 na anapatikana magharibi mwa Amerika Kusini kuanzia Ekuado hadi Chile

• Makao yao hasa yatia ndani maeneo ya ikweta kuvuka Amerika Kusini kuanzia usawa wa bahari hadi zaidi ya meta 4,500 na vilevile visiwa fulani vya Karibea na Pasifiki

• Wakati wa miezi ya kiangazi wanapatikana kaskazini ya mbali ya Alaska na kusini ya mbali ya Tierra del Fuego

• Wakati mmoja, mamilioni walichinjwa ili kuandaa vitu vya urembo kwa wafanyabiashara wa Ulaya wanaoshona kofia za wanawake, yaelekea aina fulani ziliangamizwa

[Picha]

Giant (ukubwa wake halisi)

Ndege mvumaji aina ya “bee” (ukubwa wake halisi)

[Hisani]

© C. H. Greenewalt/VIREO

© 1990 Robert A. Tyrrell

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ndege mvumaji mwekundu

[Hisani]

THE HUMMINGBIRD SOCIETY / Newark Delaware USA

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ndege mvumaji aina ya “Bee” (picha imekuzwa)

[Hisani]

© 1990 Robert A. Tyrrell

[Picha katika ukurasa wa 15]

“Antillean mango”

[Hisani]

© 1990 Robert A. Tyrrell

[Picha katika ukurasa wa 16]

“Rufous-breasted hermit”

[Hisani]

© 1990 Robert A. Tyrrell

[Picha katika ukurasa wa 16; 17]

“Anna’s” (picha imekuzwa)

[Hisani]

Patricia Meacham/Cornell Laboratory of Ornithology

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ndege mvumaji aina ya “Ruby-throated” wa kike na makinda yake

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki