Je, Tisho la Nyuklia Limekwisha?
KWA miaka zaidi ya 40, ulimwengu ulikuwa umetishwa na Har-magedoni yenye kuletwa na nyuklia. Kisha, mnamo 1989, Ukuta wa Berlin uliporomoka—mwanzo wa kuanguka kwa Ukomunisti wa Sovieti. Punde baada ya hapo, mataifa yenye uwezo mkubwa yalikuwa yamekubaliana kuacha kuelekezeana makombora. Huku “Har-magedoni” yenye kuletwa na nyuklia ikiwa imekomeshwa, au angalau kuahirishwa, ulimwengu ulishusha pumzi baada ya muda mrefu.
Hata hivyo, wataalamu wengi wanahisi kwamba ni mapema sana kusherehekea. Mnamo 1998 saa inayojulikana sana inayoashiria siku ya mwisho ya The Bulletin of the Atomic Scientists ilisogezwa mbele kwa dakika tano ikafikia dakika tisa kabla ya katikati ya usiku—jambo lililoonyesha wazi kwamba bado tisho la nyuklia lilikuwepo.a Ni kweli kwamba hali ya ulimwengu imebadilika. Mataifa mawili yenye uwezo mkubwa wa nyuklia hayazozani tena kuhusu silaha za nyuklia. Sasa mataifa kadhaa yana uwezo wa nyuklia! Kwa kuongezea, wataalamu wanahofu kwamba baada ya muda mfupi vikundi fulani vya magaidi vitapata vifaa vya nururishi na kutengeneza bomu la atomu lisilokuwa la hali ya juu.
Zaidi ya hayo, licha ya kupunguzwa kwa kiwango kikubwa, mataifa ya Marekani na Urusi yangali na zana zenye kutisha za makombora ya nyuklia. Kulingana na kikundi cha utafiti kilichoitwa Halmashauri ya Sera ya Nyuklia, kwa sasa kuna silaha za nyuklia zipatazo 5,000 ambazo ziko tayari kufyatuliwa. “Kwa hiyo,” ripoti yao yataarifu, “ikiwa amri ya kuyafyatua ingetolewa chini ya hali za sasa, makombora 4,000 [ya masafa marefu] (2,000 kwa kila upande) yangeelekea kwenye shabaha zao kwa muda wa dakika chache na mengineyo 1,000 [makombora yanayorushwa na nyambizi] yangeelekea mahali yalipolengwa muda mfupi baada ya hapo.”
Kuwepo kwa zana hizi hutokeza uwezekano wa kuzuka kwa vita kwa aksidenti au iliyopangwa kimbele. “Aksidenti mbaya ingeweza kutumbukiza ulimwengu kwenye machafuko ya msiba mkubwa wa nyuklia-joto, kinyume cha mapenzi ya viongozi wa kisiasa,” aonya mtaalamu mmoja mashuhuri wa Urusi Vladimir Belous. Kwa hiyo, ingawa Vita Baridi huenda ikawa imekwisha, kwa kweli tisho la maangamizi ya nyuklia lingalipo. Lakini tisho hilo ni kubwa kadiri gani? Je, silaha za nyuklia zitapata kuondolewa kabisa duniani? Masuala hayo yatashughulikiwa katika makala zifuatazo.
[Maelezo ya Chini]
a Saa inayoashiria siku ya mwisho kwenye jalada la The Bulletin of the Atomic Scientists ni ishara ya jinsi ulimwengu unavyodhaniwa kuwa umekaribia “katikati ya usiku” ya vita vya nyuklia. Katika miongo mingi ambayo imepita, akrabu ya dakika ya saa hiyo imesogezwa ili kuonyesha mabadiliko katika hali ya kisiasa ya ulimwengu.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Milipuko kwenye ukurasa wa 2 na wa 3: U.S. National Archives photo