Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 9/8 kur. 20-23
  • Biashara ya Tufeni Pote—Jinsi Inavyokuathiri

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Biashara ya Tufeni Pote—Jinsi Inavyokuathiri
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uchumi wa Tufeni Pote Ni Nini?
  • Je, Kuna Faida na Hasara?
  • Athari Zenye Kuenea Zinazoweza Kukufanya Uwe Tajiri au Maskini
  • Unazidisha Utajiri, Unazidisha Umaskini
  • Kuchochewa na Pupa—Je, Ni Mwelekeo Unaofaa?
  • “Shindano Kubwa Mno la Kujipatia Nguvu na Maadili”
  • Kuunganisha Ulimwengu-Mazuri na Mabaya Yanayotarajiwa
    Amkeni!—2002
  • Je, Kuunganisha Ulimwengu Kutatatua Matatizo Yetu Kweli?
    Amkeni!—2002
  • Ukurasa wa Pili
    Amkeni!—2002
  • Njia ya Kuunganisha Ulimwengu Ambayo Itakufaidi
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 9/8 kur. 20-23

Biashara ya Tufeni Pote—Jinsi Inavyokuathiri

PETER alipopoteza kazi yake katika shirika la kimataifa lililokuwa limemwajiri kwa miaka 20, taarifa ya kumwachisha kazi ililaumu hasa “sera ya uchumi wa tufeni pote.” Pesa ya Thailand, inayoitwa baht, ilipopoteza karibu nusu ya thamani yake, waziri wa fedha wa nchi hiyo alionekana kwenye televisheni akilaumu vikali “uchumi wa tufeni pote.” Bei ya mchele ilipoongezeka kwa asilimia 60 katika nchi fulani huko Kusini-Mashariki ya Asia, magazeti ya habari yalitangaza hivi: “Ni Uchumi wa Tufeni Pote!”

Uchumi wa tufeni pote ni nini hasa? Ni jinsi gani na kwa nini unaathiri nchi yenu na vilevile pesa zako? Ni nini kinachosababisha mwelekeo huo?

Uchumi wa Tufeni Pote Ni Nini?

Uchumi wa tufeni pote ni hali ya uchumi ambayo ni badiliko dhahiri kutoka uchumi wa kimataifa hadi uchumi wa tufeni pote. Katika “soko la dunia nzima,” la leo bidhaa hutokezwa kwa kiwango cha kimataifa, na pesa huzunguka mahali popote na kuvuka mipaka haraka. Ni biashara ambayo karibu haina mipaka. Katika mfumo huu, mashirika ya kimataifa yana uwezo mkubwa sana huku watega-uchumi wasiojulikana wakichangia ufanisi wa mali au kusababisha mshuko mbaya sana wa kiuchumi katika sehemu yoyote ya ulimwengu.

Uchumi wa tufeni pote ndio kisababishi na vilevile matokeo ya mabadiliko makubwa ya mawasiliano. Unachochewa na maendeleo makubwa katika mawasiliano, kuongezeka sana kwa uwezo wa kompyuta, na kubuniwa kwa njia za mawasiliano, kama vile Internet. Tekinolojia hii inasaidia kuondoa magumu ya umbali. Kukiwa na tokeo gani?

Je, Kuna Faida na Hasara?

Kulingana na watetezi wake, uchumi wa tufeni pote unaweza kuwa ni biashara kubwa na kitega-uchumi ambacho hujenga uchumi na kuchochea biashara hata katika nchi maskini zaidi ulimwenguni. Kwa mfano, katika miaka ya 1990 peke yake, watega-uchumi wa kigeni wametoa dola za Marekani trilioni moja kwa mifumo ya kiuchumi inayositawi. Kuongezeka kwa vitega-uchumi vya kimataifa kumewezesha kujengwa kwa barabara, viwanja vya ndege, na viwanda katika mataifa maskini zaidi. Kwa kweli uchumi wa tufeni pote umekuwa kani ambayo imeboresha kiwango cha maisha kwa wengine katika nchi fulani ulimwenguni kote. Peter Sutherland, mwenyekiti wa taasisi ya Overseas Development Council, asema kwamba “hadi hivi majuzi, ilichukua vizazi viwili ili kuboresha maradufu kiwango cha maisha, lakini katika China, kiwango cha maisha sasa huboreka maradufu kila baada ya miaka 10.” Uchumi wa tufeni pote unaonwa kuwa unatokeza fursa zisizo na kifani kwa mabilioni ya watu. Kupanuka sana kwa biashara ya ulimwenguni pote kumetokeza kilele cha utengenezaji na ustadi na kutokeza kazi mpya.

Hata hivyo, wachambuzi wake wanabisha kwamba uchumi wa tufeni pote unaweza pia kuporomosha mifumo ya kiuchumi kwa ghafula. Kwa kutumia tu kompyuta pesa za taifa zinaweza kupoteza thamani upesi sana, na kupunguza kabisa thamani ya fedha ambazo wafanyakazi waliweka akiba katika muda wote wa maisha yao. Maneno yenye kuogofya ya mtaalamu mashuhuri katika Soko la Fedha la Marekani yanaweza kufanya watega-uchumi wenye hofu wauze hisa zao katika Asia, na kusababisha pengo kubwa sana la kifedha ambalo hatimaye linaweza kufanya mamilioni ya watu wawe maskini. Baraza la wakurugenzi linaweza kuamua kufunga kiwanda katika Mexico na badala yake kufungua kingine Thailand—kukitokeza kazi katika Asia huku mamia ya familia katika Amerika ya Latini wakipatwa na ufukara.

Wengi wanadai kwamba uchumi wa tufeni pote umefanya maisha yawe magumu zaidi kwa watu wengi na kwamba unatisha kufanya sehemu nyingine za ulimwengu zisiendelee. “Si sadfa kwamba kutofaulu kwa mifumo mingi ya kiuchumi katika sehemu zilizo kusini ya Sahara katika Afrika hudhihirisha kutoweza kuchangamana kwa uchumi wa ulimwengu na hivyo, kushindwa kufanya biashara kwa mafanikio na kuvutia watega-uchumi,” akasema Sutherland.

Athari Zenye Kuenea Zinazoweza Kukufanya Uwe Tajiri au Maskini

Jambo hilo linakuhusuje? Mifumo ya kiuchumi ya mahali penu, ya kitaifa na ya kimkoa imefungamanishwa na inategemeana. Hivyo, matatizo ya mfumo mmoja wa kiuchumi huenda yakaenea na kuathiri mifumo mingineyo—kutia ndani ya nchi yenu. Mathalani, tatizo la kifedha la tufeni pote ambalo liliharibu kabisa Asia katika 1997 na Urusi na Amerika ya Latini katika 1998 na 1999 sasa linatisha kutokeza madhara makubwa kwa ufanisi wa Marekani, nchi za Ulaya, na mataifa mengine yalioimarika kiuchumi. Mifumo ya kiuchumi iliyoonekana kuwa inafanya vizuri wakati mmoja imepatwa na matatizo katika pindi iliyofuata—yaelekea si kwa sababu ya tukio lolote jipya bali kwa sababu ya mvurugo wa kifedha katika nchi za ng’ambo. Wataalamu wa mambo ya kiuchumi wanaita hali hii “athari ya kiuchumi.” Lionel Barber wa Financial Times asema hivi: “Mivurugo ya kifedha inatokea katika pindi ile ile na katika visa vingi huimarishana. Athari ya kiuchumi haionwi tena kuwa hatari; ni jambo hakika maishani.”

Kwa hiyo, ulimwenguni pote uchumi wa tufeni pote umeunganisha maisha yakawa mfumo mmoja wa kiuchumi. Hata uwe unaishi wapi, athari za kiuchumi kama hizo zinakuathiri katika njia moja au zaidi. Fikiria mifano ifuatayo. Brazili ilipoacha kudhibiti pesa zake katika Januari 1999, wafuga-kuku wa Argentina walishtuka kugundua kwamba Wabrazili walikuwa wakiuza kuku kwenye maduka makubwa kwa bei rahisi zaidi kuliko zao huko Buenos Aires. Isitoshe, kuzorota kwa uchumi katika mataifa mengi tayari kulikuwa kumepunguza bei ya mbao, maharagwe ya soya, maji ya matunda, nyama ya ng’ombe, na jibini za Argentina. Bei za chini na kupungua kwa wanunuzi zilisababisha viwanda vya huko vya kutengenezea bidhaa za maziwa vifungwe, na kufanya mamia ya watu wapoteze kazi.

Wakati huohuo, wafuga nguruwe huko Illinois, Marekani, waliona kwamba ingawa walipata ufanisi mkubwa wa kuuzia nchi za Asia nyama ya nguruwe wakati uliopita, sasa walilazimika kupunguza bei zao, kwa kuwa wanunuzi walipungua na mashindano ya biashara yalikuwa makali. “Hatujawahi kupata hasara kubwa namna hiyo katika biashara ya nyama ya nguruwe, hata wakati wa Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi,” akaomboleza mkulima mmoja. Katika nchi hiyo hiyo, wafanyakazi wa viwanda vya chuma walifutwa kazi, kwa kuwa makampuni yao yalikuwa yakikabiliana na mauzo mengi ya chuma kutoka China, Japani, Urusi, Indonesia, na nchi nyinginezo—ambazo zote zilikuwa na fedha yenye thamani ndogo na kufanya bidhaa zao ziwe za bei ya chini sana. Kwa sababu ya kukosa wanunuzi katika Asia, nafaka ambayo ilikosa kuuzwa ilirundamana huko Marekani, jambo lililowafadhaisha sana wakulima wa nchi hiyo.

Athari za uchumi wa tufeni pote huzidishwa na hali ya benki na hazina za malipo ya uzeeni katika nchi zenye utajiri kukopesha au kutega uchumi katika “masoko yanayoinuka”—jambo linalopata mifumo fulani ya kiuchumi katika nchi zinazositawi. Hivyo, wakati mifumo hiyo ya kiuchumi ilipoporomoka wakati wa tatizo la kifedha la 1997 hadi 1999, jambo hilo liliathiri raia wa kawaida moja kwa moja ambao walipaswa kulipwa malipo ya uzeeni au waliokuwa wameweka pesa kwenye benki zilizopata hasara. Karibu kila mtu amehisi hofu ya kupata hasara, ama kwa njia ya moja kwa moja ama isiyo ya moja kwa moja.

Unazidisha Utajiri, Unazidisha Umaskini

Tunapochunguza kwa uangalifu uchumi wa tufeni pote tunaona kwamba umetokeza vikundi vya watu walio matajiri sana katika nchi maskini na kutokeza umaskini mwingi sana katika nchi tajiri. Jinsi gani hivyo? Katika kitabu chake When Corporations Rule the World, David Korten atoa jibu kwa sehemu akisema hivi: “Ukuzi wa haraka wa kiuchumi katika nchi maskini huwezesha kuwe na viwanja vya ndege vya kisasa, televisheni, barabara kuu, na maduka makubwa yenye visafisha hewa pamoja na bidhaa za elektroni zilizo tata na mavazi ya watengenezaji mashuhuri kwa ajili ya watu wachache wanaoweza kugharamia. Hauboreshi kiwango cha maisha cha walio wengi. Ukuzi wa aina hii hutaka bidhaa ziuzwe nje ili kujipatia fedha za kigeni za kununua vitu wanavyotamani matajiri. Hivyo, mashamba ya maskini hutwaliwa ili kukuza mazao ya kuuzwa nje. Wakulima wa mashamba hayo hatimaye hujipata wakijikimu kwenye maeneo ya vibanda ya mjini huku wakilipwa pesa kidogo zisizoweza kugharimia mahitaji ya msingi na viwanda vinavyotokeza bidhaa za kuuzwa nje. Familia huvunjika, jamii huvurugika kufikia kiwango cha kuvunjika, na jeuri huenea. Kisha watu wachache ambao wamenufaika na ukuzi wa kiuchumi huhitaji fedha za kigeni zaidi ili kununua silaha za kujilinda dhidi ya wale ambao hawajafanikiwa.”

Ulimwenguni pote, uchumi wa tufeni pote umesababisha mkazo mkubwa sana kwa wafanyakazi huku serikali zikipunguza mishahara na hali za kazini katika jitihada za kuvutia watega-uchumi wa kigeni wakiwaahidi gharama za chini. Ingawa nchi fulani zilizositawi hivi karibuni zimenufaishwa na kuongezeka kwa bidhaa zinazouzwa nje likiwa ni tokeo la biashara huria ya tufeni pote, mataifa maskini zaidi hayajanufaika.

Ukosefu wa usawa tufeni pote ni tatizo kubwa kadiri gani? Fikiria takwimu moja tu iliyonukuliwa na Korten: “Sasa [katika 1998] kuna mabilionea 477 ulimwenguni, walioongezeka kutoka 274 pekee katika 1991. Jumla ya rasilimali zao yakaribia kutoshana na jumla ya mapato ya mwaka mmoja ya nusu ya maskini wote —watu bilioni 2.8.” Kisababishi ni nini? “Hili ni tokeo la moja kwa moja la uchumi wa tufeni pote usiosimamiwa ifaavyo.”

Kuchochewa na Pupa—Je, Ni Mwelekeo Unaofaa?

Kosa la msingi la uchumi wa tufeni pote ni gani? Akieleza kuhusu tatizo la kiuchumi la mwaka wa 1997 hadi 1998 mhariri Jim Hoagland alisema kwamba wanahistoria wa wakati ujao “watapata mfululizo wa fursa ambazo hazikutumiwa, kasoro katika ushirikiano wa kimataifa na pupa ya kibinadamu.” Watu fulani hujiuliza: ‘Je, kunaweza kuwa na amani na ufanisi wa tufeni pote kukiwa na mfumo wa kiuchumi unaochochea ushindani kati ya matajiri wachache na maskini walio wengi katika pambano la kufa na kupona? Je, ni jambo linalofaa kiadili kwa washindi wachache kufurahia utajiri kupindukia huku idadi kubwa zaidi ya walioshindwa wakiwa na uhitaji wenye kudhalilisha?’

Kwa kweli, pupa kubwa na ukosefu wa maadili umetokeza ulimwengu ambao umekosa kabisa usawa wa kiuchumi. Maneno yaliyotamkwa na mwanasheria mmoja miaka 2,000 iliyopita yangali kweli: “Kupenda fedha ni mzizi wa mambo mabaya ya namna zote.” (1 Timotheo 6:10) Je, serikali za kibinadamu ziko tayari kupambana kwa mafanikio na dosari hizo za kiasili za mwanadamu asiyekamilika? Fernando Cardoso, rais wa Brazili alionyesha hangaiko lake kwa kusema hivi: “Kazi ya kufikiria hali njema ya kiuchumi ya kibinadamu katika enzi ya Uchumi wa Tufeni Pote imekuwa tatizo kubwa, kwa kuwa sote twahitaji kukabili . . . pengo la kiadili ambalo limesababishwa na kujihusisha sana na ulimwengu wa biashara.”

“Shindano Kubwa Mno la Kujipatia Nguvu na Maadili”

Katika mhadhara aliotoa kwa Kongamano la 22 la Ulimwengu la Jumuiya ya Ukuzi wa Kimataifa Korten alishuku baadhi ya manufaa za uchumi wa tufeni pote. Alisema kwamba kuna “shindano kubwa mno la kujipatia nguvu na maadili kati ya watu karibu kila mahali na taasisi za uchumi wa tufeni pote. Tokeo la shindano hilo huenda likaamua kama karne ya 21 itaashiria kutumbukia kwa jamii ya kibinadamu kwenye utawala mbaya wenye pupa, jeuri, uhitaji, na uharibifu wa mazingira, mambo ambayo yangeweza kusababisha tutoweke kabisa. Au kuibuka kwa jamii zenye ufanisi na ustaarabu ambapo watu wote wanaweza kuishi kwa amani mtu na mwenzake na kwa upatano na sayari.”

[SAnduku/Picha katika ukurasa wa 22]

“ULIMWENGU UNAZIDI KUSHIRIKIANA”

Usemi huo ulitumiwa kwenye uhariri katika gazeti la Asiaweek la Februari 26, 1999, ambalo lilitaarifu hivi: “Ulimwengu unazidi kushirikiana, kwa sababu ya biashara huria, fedha zinazopatikana kwa urahisi zaidi, habari na tekinolojia. . . . Mbinu ya kufanikiwa ni kuhusisha wengine: kadiri maeneo na mataifa mengi yanavyounganishwa kwenye mfumo wa ulimwengu wote, ndivyo soko la watengenezaji bidhaa ulimwenguni pote liwavyo kubwa zaidi.”

Pia lilisema: “Kukosa kufanikiwa kwa mifumo ya kiuchumi kulikoathiri Asia Mashariki, Urusi na Brazili [katika miaka ya karibuni] kumeonyesha kwamba katika ulimwengu huu unaoshirikiana kiuchumi na kitekinolojia, ni jambo lisilo la busara kujenga eneo moja huku mengine yakiporomoka.”

Makala hiyo hiyo ilionya dhidi ya kushusha Asia kwenye “hali ya chini kiuchumi na kisiasa,” ikiwakumbusha wasomaji kwamba “mifumo ya kiuchumi ya pili na ya tatu kwa ukubwa ulimwenguni ingali ni Japani na China.” Iliendelea kusema: “Idadi tu ya watu katika Asia kwa hakika ni kubwa sana.” Mabilioni ya Waasia hawawezi kupuuzwa. Kwa kweli, tunaishi katika uchumi wa tufeni pote, na vizuizi vya kibiashara vimepunguzwa.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Uchumi wa tufeni pote umelaumiwa kwa kupanua pengo kati ya matajiri na maskini

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki