Samaki Hodari Watamu wa Bahari Kuu
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA
KAMA vipanga walivyo na mbio angani, ndivyo samaki hao walivyo na mbio baharini. Wakiwa wepesi na wenye miili laini, wao hupasua maji mithili ya mishale yenye kuwaka moto. Wao huwinda wakati wote bila kutua kamwe. Hata jina lao la kisayansi, Thunnus thynnus, latokana na neno linalomaanisha “mbiombio.” Wao ni sehemu ya jamii mashuhuri inayotia ndani samaki waitwao marlin, spearfish, na chuchunge. Naam, mabingwa hao wa mbio za baharini ni miongoni mwa aina 13 za jodari.
Katika jamii hii hodari kwa mbio, bluefin ndio wanaotia fora. Jodari aina ya southern bluefin hukua kufikia angalau futi sita na kufikia uzito wa kilogramu 200 nao hupatikana kusini mwa ikweta. Hata hivyo majitu ya jamii hiyo ni giant northern bluefin ambao wanapatikana katika Kizio cha Kaskazini. Wao hufikia urefu wa futi tisa au zaidi (ingawa ni nadra sana kupata wenye ukubwa huo kwa sababu wanavuliwa kupita kiasi) na wanaweza kufikia uzito wa kilogramu 700—asilimia 75 ya mwili wake ukiwa misuli mitupu mikakamavu. Lakini ukubwa huo haupunguzi mwendo wa bluefin. Majitu hayo huenda shoti kuliko jodari wengine yakiweza kufikia mwendo wa kilometa 70 hadi 80 kwa saa kwenye mbio fupifupi.
Wameumbwa kwa Mbio Fupi na Mbio Ndefu
Ni nini kinachowawezesha bluefin kwenda kwa kasi hivyo? Gazeti National Geographic laeleza: “Hao bluefin wameumbwa kwa ajili ya mbio kwa sababu robo tatu za mwili wao ni misuli mitupu, miili yao inafaa sana mbio za baharini, wana mioyo yenye nguvu, daima wao hufumbua kinywa kidogo kwa ajili ya hewa, na wana mishipa ya damu inayobadilisha hali ya joto ya mwili bila kutaja mambo mengine.” Hata moyo wenye nguvu wa bluefin ni mkubwa mara kadhaa kuliko moyo wa samaki wengine nao hufanana na moyo wa wanyama kuliko moyo wa samaki. Isitoshe, tofauti na samaki wenye damu baridi, moyo wake hupiga damu yenye joto kidogo kotekote katika mifumo yake ya damu iliyobuniwa kwa njia ya ajabu sana. Ongezeko la joto la damu yake kwa nyuzi kumi za Selsiasi huongeza uwezo wa misuli ya bluefin kwa mara tatu, jambo linalomfanya awe mwindaji hatari wa samaki, ngisi, na vijiumbe vya bahari.
Aonapo chakula kitamu—tuseme, makareli—mara moja mkia wake wenye umbo la mundu humsukuma haraka-haraka ashambulie. Mapezi yake ya kifua na yaliyo karibu na mkia huingia ndani ya matundu ya pekee yaliyo kwenye mwili wake mgumu ili yasipunguze mwendo wake. Hata mbio za kufa na kupona za huyo makareli haziwezi kumwokoa, kwa kuwa bluefin huona kitu kwa macho yake yote mawili, ana masikio makali sana, na ana vitu vyenye kutambua kemikali majini. Anapokaribia kushambulia, mapezi yake huchomoka kwa nukta tu ili apate usawaziko. Kisha, kufumba na kufumbua, afunga mashavu yake na afungua kinywa chake wazi na yule makareli atoweka—amemezwa mzima-mzima.
Kwa sababu ya moyo wake wenye nguvu, damu yake yenye joto kidogo, na mashavu yake makubwa sana, baada ya mbio hizo jodari hupata nguvu haraka kwa mara kumi hivi kuliko samaki mwingine yeyote yule. Lakini hata wanapopumzika—hata wanapolala usingizi—wao huendelea kuogelea kwa sababu wao ni wazito kuliko maji, na hawana mashavu yanayopiga maji yatoke nje ambayo huwawezesha samaki wengine watulie kabisa. Basi, kama papa, jodari hufungua kinywa kidogo wanapokwenda. Wasifu wa jodari waweza kusema tu: “Tangu kuzaliwa hadi kifo ni mbio za masafa marefu, ambazo hukatizwa-katizwa na mbio kali fupifupi.”
Jodari aina ya giant yellowfin ndio maridadi zaidi katika jamii hiyo. Hao yellowfin hukua kufikia futi sita na nusu na wana mraba wa manjano, mapezi madogo ya manjano, na mapezi marefu sana yanayoelekea nyuma. Wanapopitia mawimbi, samaki hao wenye kuvutia hung’aa kama vishale vyenye moto, hasa usiku. Hata watu wa Hawaii wanawaita ahi, yaani “moto.”
Samaki Hao Wamo Mashakani
Nyama yake nyingi yenye rangi nyekundu ambayo ina mafuta-mafuta hufanya jodari apendwe sana kwa mlo. Mapishi ya Kijapani kama vile sashimi na sushi yamefanya bluefin kuwa miongoni mwa vyakula vinavyopendwa zaidi na vilivyo ghali zaidi nchini Japani. Wapenzi wa shushi hulipa pesa nyingi sana kwa mlo mdogo tu wa jodari. Kama ungalisikia wanunuzi wakibishania bluefin mmoja kwenye mnada, ungalidhani wanashindania gari jipya. Ni kawaida kusikia wakitaja dola 11,000 au zaidi. Hata bluefin mmoja mwenye uzito wa kilogramu 324 aliuzwa kwa dola 67,500! “Ni mkubwa kama gari aina ya Porsche, ana mbio kama Porsche, na ana thamani kama Porsche,” akasema mtaalamu mmoja wa mazingira.
Kwa kuwa jodari wanapendwa sana, idadi yao inapungua sana. Hao “wamevuliwa kupita kiasi, wametumiwa vibaya kupita kiasi, [na] kuangamizwa kwa madhumuni ya kupata faida kana kwamba hatutawahitaji tena,” ndivyo kisemavyo kitabu Saltwater Gamefishing. Meli kubwa za kisasa zenye tekinolojia za hali ya juu, kutia ndani uchunguzi unaofanywa na ndege angani, huwashika samaki hao kwa wingi. Kwa mfano, meli inayotumia wavu ionapo kundi kubwa la jodari, hushusha boti ndogo inayovuta wavu kuzunguka samaki hao na kuwazuia wasiponyoke. Kwa upande mwingine, imejulikana kwamba meli za kamba ndefu zinaweza kuvuta kamba inayoweza kufikia kilometa 130. Kwenye kamba kubwa kuna kamba nyinginezo fupifupi zipatazo 2,200, kila kamba ikiwa na ndoana nyingi zenye chambo. Hilo ni tisho kubwa sana kwa jodari! Wale bluefin wakubwa ni wenye thamani sana hivi kwamba boti na ndege “zaweza kuwatafuta bluefin wachache tu hata kwa majuma kadhaa,” lasema shirika la Hazina ya Wanyama Ulimwenguni.
Kuna nchi ambazo zimeweka sheria ya kiwango cha kuvua samaki hao katika maji yake, lakini unawezaje kudhibiti kuvuliwa kwa samaki wa bahari kuu kama jodari? (Jodari mmoja aina ya northern bluefin alishikwa karibu na Japani kisha akatiwa alama na baadaye akashikwa Mexico—umbali wa karibu kilometa 11,000!) Bado haiwezekani kamwe kuwadhibiti. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanajaribu kutia moyo kuvua samaki hao kwa njia ambayo haiwadhuru lakini yalishindwa na watu wenye mabavu zaidi. Hata wakati nchi fulani zimejaribu kudhibiti uvuvi wa jodari, hizo zimezusha tu mgogoro.
Unaweza kujiuliza ni kwa nini wavuvi huharibu samaki, na hata kuhatarisha riziki yao wenyewe ya wakati ujao, kwa kuendelea kupora kabisa samaki wachache waliobaki. Gazeti National Geographic lasema: “Kwa sababu ya upungufu huo wa [samaki] wala wavuvi wa kawaida wala wavuvi wa kibiashara hawawezi kupendelea kuhifadhi samaki kwa hiari kwa sababu hawapati faida. Ni kuwapa tu watu wasio na pupa sana samaki hao. Badala yake, kila mtu huvua samaki zaidi.”
Je, Kuwatia Jodari Alama na Kuwafuga Kutawaokoa?
Jodari aina ya southern bluefin amefanyiwa utafiti sana. Sehemu ya utafiti huo inahusisha kutumia alama za hali ya juu za kielektroni ambazo hutoa habari muhimu kuhusu tabia na hali za makundi ya jodari. Habari hiyo itasaidia kudhibiti mambo ya uvuvi.
Kwa wakati uo huo, ufugaji wa samaki, kutia ndani wa jodari, unaenea sana katika nchi fulani. Na wafugaji wa samaki hao wanapata manufaa kwa sababu hao si mchezo katika kutaga mayai, kwani bluefin wa kike hutaga mayai yapatayo milioni 15 katika msimu mmoja tu! Mpango huo ukifaulu, huenda ufugaji ukaongeza idadi iliyodidimia sana ya samaki hao katika bahari kuu. Kwa kweli twaweza kuhuzunikia sana kutoweka kwa samaki hao hodari wa mbio za bahari na hasa nyota za jamii hiyo, bluefin—samaki maridadi walio watamu pia.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Jodari aina ya “yellowfin”
[Hisani]
Innerspace Visions
[Picha katika ukurasa wa 18]
”Jodari aina ya bluefin”
[Hisani]
Innerspace Visions