Mto Danube—Laiti Ungeweza Kuzungumza!
Na Mleta-habari Wa Amkeni! Katika Ujerumani
Kwa zaidi ya karne moja na nusu, Wajerumani mashuhuri zaidi waliowahi kuwapo wamekodoa macho kwa uthabiti—lakini hawajaona—chini ya Mto Danube. Jambo hilo linawezekanaje? Mnamo mwaka wa 1842, Mfalme wa Bavaria Ludwig wa Kwanza alikamilisha Valhalla,a hekalu la marumaru lililojengwa kwa Ufundi wa Ugiriki ambalo lilikusudiwa kuwaheshimu Wajerumani mashuhuri waliokufa.
JENGO maarufu la Ujerumani lililo kando ya Mto Danube kwenye vilima vilivyo karibu na Regensburg, Ujerumani, lina sanamu nyingi zenye vichwa na mabega ya watu zinazowakilisha wanaume na wanawake mashuhuri. Jengo hilo limeiga muundo wa hekalu la Parthenon kwenye Acropolis kule Athene.
Kikao hicho kinafaa. Wakuu hao, washairi, wasanii, wanasiasa, wanasayansi, na wanamuziki—kutia ndani watu mashuhuri kama vile Beethoven, Einstein, Goethe, Gutenberg, Kepler, na Luther—walifahamu vizuri Mto Danube. Wengi wao waliishi kwenye kingo zake, wakavuka maji yake, au kutangaza sifa zake. Lingekuwa simulizi lililoje ambalo Mto Danube ungesimulia—laiti ungeweza kuzungumza!
Si Maji Yanayotiririka Tu
“Kwa maoni ya wanajiografia, mito ndiyo hubeba masimbi na biashara,” aandika mwanahistoria Norman Davies. Hata hivyo, asema kwamba “kwa wanahistoria, mito hubeba utamaduni, mawazo, na nyakati nyingine mahitilafiano. Mito inafanana na uhai wenyewe.” Mto Danube hutiririka kwenye mipaka ya nchi kumi—Ujerumani, Austria, Slovakia, Hungaria, Kroatia, Yugoslavia, Bulgaria, Rumania, Moldova, na Ukrainia—kwa hiyo una unamna-namna mwingi wa utamaduni, mawazo, na mahitilafiano. Basi haishangazi kwamba jumuiya nyingi zilizo kandokando ya Mto Danube zimechangia sehemu kubwa ya historia ya Ulaya, au hata ya ulimwengu.
Kwa mfano, lifikirie jiji kuu la Austria, Vienna. Kwa muda mrefu jiji hilo limekuwa na vitovu vyenye sifa vya utamaduni wa ulimwengu, likiwa na majumba ya opera, majumba ya sinema, majumba ya ukumbusho, majumba ya kihistoria, na maktaba. Limekuwa mashuhuri kwa karne nyingi kwa ajili ya mikahawa yake na vilabu. Okestra ya Vienna Philharmonic Orchestra inaonwa kuwa mojawapo ya okestra bora zaidi ulimwenguni. Chuo Kikuu cha Vienna, kilichoanzishwa mnamo mwaka wa 1365, ndicho cha kale zaidi katika nchi zinazozungumza Kijerumani.
Kuhusu mawazo, kichapo The New Encyclopædia Britannica chaliita jiji la Vienna la mwanzo wa karne kuwa “mahali panapofaa kwa ajili ya mawazo—mema na yenye kudhuru—ambayo yangeuelekeza ulimwengu wa sasa.” Miongoni mwa watu walioathiriwa kwa kiasi fulani katika miaka waliyoishi huko ni Theodor Herzl, mwanzilishi wa Dini ya Uyahudi; Sigmund Freud, mwanzilishi wa tiba nafsia; na Adolf Hitler, ambaye hatuhitaji kusema mengi zaidi juu yake.
Kutenganisha “Ustaarabu na Ukatili”
“Katika nyakati za kale, Mto Danube uliwakilisha mojawapo ya mipaka mikubwa zaidi ya Peninsula ya Ulaya,” asema Norman Davies. Aeleza hivi: “Ukiwa kwenye mpaka wa Milki ya Roma katika karne ya kwanza W.K., kwa Kilatini Danuvius . . . ulitenganisha ustaarabu na ukatili.”
Miji kadhaa ya Danube, ilishiriki fungu kubwa katika historia ya Milki ya Roma na baadaye, ile iliyoitwa Milki Takatifu ya Roma. Kwa mfano, Bratislava, kitovu cha kitamaduni katika Slovakia na ambacho leo ni jiji kuu lake, kilitumika kikiwa jiji kuu la Hungaria kuanzia 1526 hadi 1784. Na kwa muda fulani kasri yenye fahari, yenye urefu wa meta 100 juu ya Mto Danube, ilikuwa makao ya familia ya kifalme ya Austria. Vienna lilipotishwa na majeshi ya Ufaransa na ya Bavaria mnamo mwaka wa 1741, Maria Theresa ambaye baadaye alikuja kuwa malkia alikimbilia huko ili kupata usalama.
Maria Theresa alikuwa wa Familia ya Habsburg. Enzi hiyo ya nasaba ya wafalme—mojawapo ya enzi zilizo kuu zaidi za Ulaya—inawakilishwa ifaavyo miongoni mwa sanamu zenye vichwa na mabega ya watu katika Valhalla.b Familia hiyo mashuhuri, iliyojulikana kuanzia karne ya 10, ilipata mamlaka katika karne ya 13 na ilimiliki sehemu kubwa ya Ulaya ya Kati—mara nyingi kwa sababu ya ndoa zilizofungwa kwa hila. Francis Ferdinand, mrithi wa kiti cha ufalme cha Habsburg, aliuawa huko Sarajevo mnamo mwaka wa 1914, na hivyo kuchochea kuanza kwa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.
Maji Yaliyojaa Damu
Milki zimekuwako na kupita, zikitokeza mabadiliko ya kisiasa ya daima kwa Mto Danube. Ulikuwa mpaka wa Milki ya Byzantine ya karne ya 11 na 12. Baadaye, sehemu kubwa ya mto huo, ilitiririka katika Milki ya Uturuki, huku miji ya Danube kama vile Belgrade na Budapest ikikaliwa na Waturuki. Hata Vienna lilizingirwa bila mafanikio mnamo mwaka wa 1529 na tena mnamo mwaka wa 1683.
Basi haishangazi kwamba mwandishi Mjerumani Werner Heider asema: “Hakuna mto wowote katika Ulaya unaofanana na Danube katika umaana wake wa kihistoria.” Mwandishi mwingine asema kwamba wakati wa kale mto huo ulitumika kuwa “njia kuu ya uvamizi dhidi ya Ulaya kutoka mashariki kwa ajili ya Wahun, Watarta, Wamongol, na Waturuki.”
Pia Mto Danube umeharibiwa katika vita vya wakati wa karibuni zaidi. Mwandishi William L. Shirer aandika: “[Mnamo 1941] kwenye usiku wa Februari 28 vikosi vya Jeshi la Ujerumani vilivuka Mto Danube kutoka Rumania na kujipanga mahali pafaapo katika Bulgaria.” Mnamo 1945, miaka minne baadaye, “Warusi, baada ya kuteka Vienna katika Aprili 13, walikuwa wakielekea Danube, na kikosi cha Tatu cha Jeshi la Marekani kilikuwa kikivuka mto huo kutoka upande wa chini ili kukutana nao.”
Simulizi la Mto Danube la utamaduni na mawazo mara nyingi sana limekuwa simulizi la mapambano, na mara nyingi maji yake yalijazwa damu iliyomwagwa katika vita vya mwanadamu. Lakini umejazwa kwa njia nyingine vilevile.
Si wa Rangi ya Buluu Tena
Wakati Johann Strauss, Jr., alipotunga msowero “The Blue Danube” mnamo 1867, yaelekea maji hayo kwa kupatana na mambo hakika yaliakisi rangi ya buluu ya anga lililomulikwa na jua. Lakini vipi leo?
Kutoka kwenye chanzo chake katika Black Forest ya Ujerumani, Mto Danube unajipinda kuelekea kusini-mashariki kwa umbali upatao kilometa 2,850 hadi kwenye Bahari Nyeusi. Ndio wa pili kwa urefu katika Ulaya baada ya Mto Volga. Mfumo wake wa kuchukua maji ni wenye urefu wa kilometa za mraba 817,000. Hata hivyo, ujenzi wa Bwawa la Gabcikovo, sehemu ya mradi wa umeme wa nguvu za maji ulioko kwenye Mto Danube kati ya Vienna na Budapest, umeathiri mazingira. Kulingana na kichapo kimoja, bwawa hilo “limesababisha upungufu mbaya sana wa maji ya kunywa yenye madini kandokando ya Mto Danube, limekausha maelfu ya hekta za msitu na kinamasi na kupunguza uvuaji wa samaki katika sehemu nyingine zilizo upande wa chini wa Mto Danube kwa asilimia 80.”
Kama ungeweza kuzungumza, labda Mto Danube wa leo ungesitasita kueleza jinsi ambavyo umeathiriwa na kutokuwa na ujuzi kwa binadamu na pupa. Pamoja na mito mingine mikubwa mitatu inayoishia kwenye Bahari Nyeusi, Mto Danube umechangia kufanya Bahari Nyeusi kuwa “mojawapo ya bahari zilizochafuliwa zaidi ulimwenguni,” kulingana na gazeti la Urusi Rossiiskaya Gazeta. Jarida hilohilo lasema juu ya Bahari Nyeusi kuwa “inapatwa na kifo chenye maumivu makali,” likisema kwamba katika miaka 30 iliyopita, “umekuwa mfereji wa maji machafu wa nusu ya Ulaya—mahali pa kutupia takataka nyingi sana zenye misombo ya fosforasi, zebaki, DDT, mafuta, na takataka nyingine zenye sumu.”
Ni hadithi yenye kuhuzunisha kama nini kuhusu mambo yaliyoipata delta ya Danube! Kuzunguka Izmail, Ukrainia, karibu na mahali ambapo mto huo huingia kwenye Bahari Nyeusi, madhara ya ikolojia ni yenye kuogofya. Mwari ambao wakati mmoja walipatikana katika eneo hilo sasa hupatikana kwa nadra sana. Gazeti la Ujerumani Geo lasema kwamba kuhifadhiwa daima kwa “unamna-namna mwingi wa mimea na wanyama . . . ni kipimio cha udhibiti wa mazingira wa kimataifa.”
Simulizi la Kufurahisha Zaidi Litasimuliwa Hivi Karibuni
Mnamo mwaka wa 1902 mkazi mpya aliwasili katika Tailfingen, mji ulioko takriban kilometa 60 kaskazini-mashariki ya chemichemi ya Mto Danube, katika mojawapo ya mito inayoingia katika mto huo. Mkazi huyo alikuwa Margarethe Demut. Neno “Demut” katika Kijerumani lamaanisha “Unyenyekevu.” Kwa sababu alihubiri juu ya “enzi ya ufanisi,” punde si punde wakazi wa sehemu hiyo walikuwa wakimwita Golden Gretle. Muda mfupi baada ya hapo, mji wa Tailfingen ulikuwa na mojawapo ya makutaniko ya kwanza ya Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani.
Mnamo 1997 Mashahidi wa Yehova 21,687 waliokuwa wakitumikia katika makutaniko 258 katika jumuiya za Danube, zilizo katika nchi kumi, walikuwa wameunganika kuhubiri ujumbe huu wa Ufalme wa Mungu uliosimamishwa.
Kwa kuwa Mungu amekusudia kwamba dunia itadumu milele na itakaliwa, Mto Danube utatiririka kwa muda usio dhahiri. (Zaburi 104:5; Isaya 45:18) Ikiwa ndivyo, litakuwa jambo lenye kuridhisha kama nini kwamba baada ya simulizi la karne nyingi za tamaduni zenye kasoro, mawazo ya kibinadamu yenye kasoro, na mapambano yenye umwagikaji wa damu, hatimaye mto huo utakuwa na simulizi lenye kupendeza zaidi litakalosimuliwa. Watu wenye furaha na wenye afya watakuwa wakiishi kwenye kingo zake, bila kugawanywa tena na mipaka ya kisiasa au na lugha. Wote watakuwa wakiinua sauti zao kumsifu Muumba Mtukufu. Na hakutakuwa tena na uhitaji wa Valhalla ya kuheshimu wanadamu waliokufa, kwa kuwa wote wanaostahili watakuwa wamerudishwa kwenye uhai.—Yohana 5:28, 29.
Wazo la Mto Danube wenye shangwe laweza kutukumbusha juu ya Zaburi 98:8, 9, inayosema: “Mito na ipige makofi . . . kwa maana [Yehova] anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, na mataifa kwa adili.” Ebu wazia simulizi lenye kusisimua ambalo Mto Danube wa rangi ya buluu utakaokuwa maridadi tena, utaweza kusimulia!
[Maelezo ya Chini]
a Katika mithiolojia ya Ujerumani, Valhalla lilikuwa jumba walimokaa miungu; katika mithiolojia ya Skandinavia, lilikuwa jumba la mashujaa waliouawa.
b Maria Theresa, Rudolf wa Kwanza, Maximilian wa Kwanza, na Charles wa Tano wanaheshimiwa vivyo hivyo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16, 17]
KANDOKANDO YA MTO DANUBE
ULM, UJERUMANI
Mnamo mwaka wa 1879, Albert Einstein, ambaye ugunduzi wake wa sayansi ulisaidia kubadili historia ya hivi karibuni ya ulimwengu, alizaliwa huko Ulm. Inasemekana kwamba “katika nyakati zake alitambuliwa kuwa mmojawapo wa watu wenye ubunifu zaidi katika historia ya kibinadamu”
[Picha]
WELTENBURG, UJERUMANI
REGENSBURG, UJERUMANI
Mwastronomia Kepler alikufa katika sehemu hiyo mnamo mwaka wa 1630, muda mrefu baada ya Mto Danube kuvukwa katika karne ya 12 na Steinerne Brücke (Daraja la Mawe), ambalo wakati huo lilionwa kuwa ujenzi wa kustaajabisha
MAUTHAUSEN, AUSTRIA
Jumuiya hii ndogo kwenye Mto Danube ilikuwa mahali ambapo palikuwa na kambi za mateso za Nazi. Baadhi ya makumi ya maelfu ya watu waliofungwa jela hapo walikuwa Mashahidi wa Yehova, kutia ndani Martin Poetzinger, ambaye baadaye alikuja kuwa mshiriki wa Baraza lao Linaloongoza
[Picha]
VIENNA, AUSTRIA
[Picha]
BRATISLAVA, SLOVAKIA
[Hisani]
Geopress/H. Armstrong Roberts
BELGRADE, YUGOSLAVIA
Kichapo The World Book Encyclopedia chasema kwamba jiji la Belgrade lilikumbwa na “mapambano ya kisiasa na ya kijeshi” yaliyodumu “kwa mamia ya miaka.” Majeshi “yalishambulia na kuharibu Belgrade zaidi ya mara 30”
NIKOPOL, BULGARIA
Mji huu ulikuwa ngome muhimu baada ya kuanzishwa kwa milki ya Byzantine na Heraclius mnamo mwaka wa 629 W.K. Mnamo mwaka wa 1396 sultani wa Ottoman Bayezid wa Kwanza alimshinda Mfalme Sigismund wa Hungaria huko, hivyo akianzisha karne tano za utawala wa Kituruki
GIURGIU, RUMANIA
Mnamo mwaka wa 1869, reli ya kwanza ya Rumania iliunganisha Giurgiu na jiji jirani linalojulikana la Bucharest, lililoko kilometa zipatazo 65 kuelekea upande wa kaskazini. Mnamo mwaka wa 1954 daraja la reli na barabara lililovuka Danube liliunganisha Rumania na Bulgaria na liliitwa kwa kufaa Friendship Bridge
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UJERUMANI
Black Forest
Tailfingen
Ulm
Weltenburg
Regensburg
Valhalla
AUSTRIA
Mauthausen
Vienna
SLOVAKIA
Bratislava
Bwawa la Gabcikovo
HUNGARIA
Budapest
KROATIA
YUGOSLAVIA
Belgrade
BULGARIA
Nikopol
RUMANIA
Giurgiu
Bucharest
MOLDOVA
UKRAINIA
Izmail
Delta ya Danube
BAHARI NYEUSI
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
BUDAPEST, HUNGARIA
Budapest, jiji ambalo wakati mmoja liliitwa Malkia wa Danube, linafanyizwa hasa na Buda, ulioko upande wa magharibi wa Mto Danube, na Pest ulioko upande wa mashariki. Kufikia mwaka wa 1900, karibu sehemu moja kwa nne ya wakazi wa hapo walikuwa Wayahudi—jumuiya ambayo karibu itoweshwe kabisa wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili