Kuishi na Maradhi ya Cystic Fibrosis
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA JIMMY GARATZIOTIS
Katika Julai 25, 1998, nilipelekwa hospitalini haraka nikiwa na maumivu makali kwenye kifua. Moyo wangu ulikuwa sawa, lakini mapafu yangu yalikuwa yameambukizwa vibaya sana hivi kwamba nilipumua kwa shida kwelikweli. Nilikuwa na umri wa miaka 25 tu, na uhai wangu ulikuwa hatarini.
SIKU mbili baada ya kuzaliwa, madaktari waliwaambia wazazi wangu kwamba nilikuwa na homa kali ya nyongo ya manjano. Walisema kwamba ikiwa singetiwa damu mishipani, ama ningekufa ama kupatwa na madhara ya ubongo. Niliokoka bila kutiwa damu mishipani—na bila madhara ya ubongo.
Nilipatwa na matatizo ya afya yenye kutatanisha na nimonia pindi kwa pindi miaka miwili ya kwanza ya maisha yangu. Hatimaye daktari alinipima na kupata kwamba nina maradhi ya cystic fibrosis (CF). Wakati huo, watu wenye maradhi hayo waliishi kwa wastani wa umri wa miaka saba. Lakini kwa sababu ya maendeleo ya kitiba, watoto wengi zaidi na zaidi wenye CF wanaishi na kufikia kuwa watu wazima.
CF Ni Nini?
CF ni kasoro ya kurithiwa. Husababisha matatizo makali sana ya kupumua, na mara nyingi watu wenye CF wanakuwa na matatizo makubwa sana katika kumeng’enya chakula chao.
Takriban mtu 1 kati ya watu 25 ana chembe ya urithi yenye kasoro ya CF. Katika visa vingi watu wenye chembe hiyo ya urithi huwa hata hawana habari, kwa kuwa hawaonyeshi dalili zozote za maradhi hayo. Ikiwa baba na mama wana chembe hiyo ya urithi, kuna uwezekano wa asilimia 25 kwamba mtoto mmoja atakuwa na CF.
Kisa changu ni kati ya visa vilivyo nadra ambapo CF iligunduliwa kwa sababu ya vivimbe vilivyokuwa ndani ya mianzi ya pua. Kama tokeo la hilo, madaktari walichochewa kupima kiasi cha chumvi katika jasho langu, ambalo ndilo jaribio la kawaida zaidi la CF. Mara nyingi chumvi iliyo katika ngozi hugunduliwa na wazazi au babu na nyanya ambao hugundua ladha ya chumvi kwenye midomo yao baada ya kumbusu mtoto.
Kukua kwa vivimbe ndani ya mianzi ya pua yangu kulidhoofisha uwezo wangu wa kupumua, kwa hiyo nimehitaji kufanyiwa upasuaji karibu kila mwaka kwenye mianzi ya pua yangu ili kuondoa vivimbe hivyo. Upasuaji huo husumbua sana, na husababisha maumivu makali sana kabla ya kupona. Pia ni hatari kwa sababu ya kuvuja damu. Lakini nimefanyiwa upasuaji mara nyingi, na upasuaji wote umefanywa bila kutumia damu. Ninashukuru kama nini kutoishi na matatizo au wasiwasi unaoweza kuletwa na kutiwa damu mishipani!
Kukabiliana na Maradhi Hayo
Ijapokuwa maradhi yangu hunizuia kufanya mambo fulani, ninajaribu kuwa mtendaji kadiri niwezavyo. Siku ya pekee maishani mwangu ilikuwa Agosti 1, 1987, nilipobatizwa kuonyesha wakfu wangu kwa Yehova Mungu.
Ninapoamka asubuhi, ninapumua mchanganyiko wa ventolin na kufuatiwa na mchanganyiko wa chumvi. Huo husaidia kulegeza umajimaji ulio katika mapafu yangu na kufungua vilango vyangu vya hewa ili niweze kupumua kwa urahisi zaidi. Tiba hiyo huchukua muda upatao dakika 15. Baadaye ninapata tibamaungo kwa dakika 40 hadi saa moja ili kulegeza na kuondoa umajimaji katika mapafu yangu. Kisha ninapata tiba nyingine ya kupumua, wakati huu ni tiba ya kiuavijasumu ili kupigana na ambukizo. Mimi hurudia hatua hizo alasiri na tena jioni.
Tiba hiyo ya vipindi vitatu huchukua muda wa saa nne hivi kila siku. Kwa kawaida mimi hula baadaye kwa kuwa matibabu yangu hufanya kazi vizuri zaidi tumbo linapokuwa tupu. Licha ya utaratibu huo wa tiba unaochukua wakati kila siku, nimelifanya liwe zoea kuhudhuria mikutano ya kutaniko la Kigiriki la Mashahidi wa Yehova huko London, Ontario, Kanada. Jioni za mikutano mimi huahirisha tiba yangu hadi saa nne za usiku. Baraka ambazo nimepata kwa kuhudhuria mikutano zazidi kwa mbali mambo ambayo nimehitaji kudhabihu. Kushiriki katika huduma kwa ukawaida kumekuwa jambo la maana kwangu.
Kushiriki Imani Yangu
Kulazwa hospitalini mara kwa mara kumenipa fursa za pekee za kushiriki imani yangu ya Kikristo. Wakati mmoja nilikuwa na fursa ya kuongea na kasisi wa kanisa la Othodoksi ya Ugiriki, aliyekuwa amelazwa katika chumba kingine. Alisema kwamba nilikuwa kijana mwenye kuheshimika na kwamba alifikiri nilikuwa kielelezo kizuri kwa vijana katika jumuiya ya Wagiriki. Hakujua kuwa nilifahamu kwamba alikuwa akiongoza upinzani dhidi ya huduma ya Mashahidi wa Yehova miongoni mwa watu waliozungumza Kigiriki.
Wageni walipokuja kumwona kasisi huyo, angewatuma waje kuniona. Wageni wake walitambua nyuso za washiriki wa familia na marafiki waliokuja kuniona kuwa watu waliowatembelea katika huduma. Baadhi ya wageni wa kasisi huyo walikaa kwa muda, lakini wengine walirudi wakiwa wameshangaa na kumwuliza kasisi huyo kwa nini aliwatuma wakawaone Mashahidi wa Yehova. Hata baada ya kutambua kwamba nilikuwa Shahidi, mazungumzo yetu ya Biblia yaliendelea. Tulizungumzia vichwa kama vile jina Yehova, Utatu, na msimamo wa kutokuwamo katika mambo ya kisiasa wa Mashahidi wa Yehova katika Ugiriki. Tulipokuwa tukizungumza, ningeweza kuona kwamba upinzani wake ulikuwa ukipungua.
Kasisi huyo alikiri kwamba alijua kweli kuhusu baadhi ya vichwa vya Biblia ambavyo tulizungumzia lakini akakiri kuwa hakufundisha kweli kuhusu mambo hayo kwa kuhofu kupoteza kazi yake. Baadaye mimi na Esther, dada yangu mchanga, tulizuru nyumbani mwake, na akakubali fasihi ya Biblia. Upinzani dhidi ya kazi yetu ya kuhubiri katika eneo hilo ulipungua. Kwa hakika, wengi waliosikia itikio lililofaa kuelekea kweli la kasisi huyo walianza kusikiliza. Ingawa hivyo, mara baada ya hapo, kasisi huyo alipewa mgawo mpya mahali penginepo.
Jambo jingine la maana lilitokea likiwa tokeo la kushiriki imani yangu katika mojawapo ya pindi nilizolazwa hospitalini. Nilizungumza na kijana anayeitwa Jeff, aliyekuwa amekuja kutembelea babu yake. Mazungumzo zaidi yaliongoza kwenye funzo la Biblia pamoja naye. Halafu, Jeff akataka kuhudhuria mikutano ya kutaniko. Ingawa kwa kawaida nilikuwa nikihudhuria kutaniko moja huko London, kwa muda fulani nilisafiri hadi Stratford iliyo karibu ili kumpeleka mikutanoni huko. Lengo lilikuwa asaidiwe na mtu fulani aliyeishi karibu na nyumbani kwake.
Kwa kusikitisha, Jeff alishindwa kustahimili msongo kutoka kwa familia yao na hakuendelea kiroho. Hata hivyo, nilipokuwa nikihudhuria mikutano huko Stratford, nilifahamiana na Deanne Stewart. Tulikuwa tumekutana tuliposhiriki ujenzi wa Jumba la Ufalme. Tukawa na uhusiano na kuoana Juni 1, 1996.
Hali Yangu Yabadilika
Kwa kusikitisha, majuma matatu baada ya kufunga ndoa, nikawa mgonjwa sana. Hali hiyo ilifanya nilazwe hospitalini mara kwa mara na kuongoza kwenye hali ya dharura iliyotajwa mwanzoni. Tangu wakati huo nimekuwa nikitumia kifaa cha kunipa oksijeni saa 24 kwa siku. Nakabiliana na homa, kutokwa jasho usiku, ugonjwa wa ngozi ya nje ya mapafu, kupoteza usingizi kwa sababu ya kukohoa usiku, na maumivu katika viungo vyangu, miguu, na kifua. Nyakati nyingine pia ninakohoa damu, jambo ambalo linatisha kwa sababu kukohoa kusipokoma, kungeweza kutokeza kifo cha ghafula.
Sasa, nikiwa na mke wangu mpendwa kando yangu akiwa mwandamani na msaidizi, ninashiriki kutoa ushahidi kwa madaktari, madaktari wa tibaviungo, wagonjwa, na wafanyakazi wengine wa afya kwenye hospitali na vilevile nyumbani wanapozuru. Ijapokuwa matatizo yangu ya kitiba ni magumu, tunaona pindi hizo zote kuwa fursa za kulisifu jina la Yehova.
Kinachonifanya Nistahimili Sasa
Kwa sababu ya hali yangu iliyobadilika, mimi na Deanne tuna simu ya pekee ambayo hutuwezesha kusikiliza na kushiriki katika mikutano ya kutaniko. Uandalizi huo wenye upendo hututia moyo sana na kutufanya tuhisi kwamba tungali sehemu yenye kutenda ya kutaniko, hata ingawa mara nyingi hatuwezi kuwapo kimwili tena.
Kwa kuongezea, sasa huduma yetu yatia ndani kuwapigia watu simu na kushiriki tumaini letu linalotegemea Biblia. Tumeanzisha mafunzo ya Biblia tunayoyaongoza kwa njia ya simu. Tunapata shangwe kubwa kwa kuzungumza na watu tusiowajua kuhusu Yehova na maandalizi yake ya ajabu kwa wanadamu waaminifu katika ulimwengu mpya wenye uadilifu.
Utegemezo wa baba na mama yangu umekuwa kitia-moyo chenye kuimarisha na kufariji. Nina deni kubwa sana hasa kwa Yehova kwa kunipa Deanne, ambaye amenikubali nikiwa na maradhi yangu na sasa anatimiza fungu kubwa kunisaidia nivumilie.
Ninapofikia hatua za mwisho za maradhi yangu, ninazidi kusonga mbele kwa kutafakari tumaini langu la wakati ujao. Kusoma Biblia kila siku pamoja na Deanne hutufariji sote. Najua kwamba wakati ujao ulio karibu, nitakuwa na afya nzuri bila uhitaji wa kutibiwa kila siku ili nipumue tu. Katika Paradiso iliyoahidiwa, nitakapokuwa na mapafu yenye afya, ninajiona nikikimbia kwenye uwanja ulio wazi. Nataka hivyo tu—kukimbia kwenye uwanja ulio wazi kwa muda fulani ili nifanyie mapafu yangu majaribio.
Kupiga taswira akilini juu ya baraka za ulimwengu mpya ulioahidiwa na Mungu hunisaidia kukabiliana na hali hiyo kila siku. Mithali 24:10 husema: “Ukizimia siku ya taabu, nguvu zako ni chache.” Badala ya kuona kwamba nguvu zangu ni chache, ninaona kwamba Yehova hunipa nguvu ipitayo ya kawaida. (2 Wakorintho 4:7) Jambo hilo hunisaidia kutoa ushahidi kuhusu jina lake na makusudi yake na vilevile kukabiliana na chochote anachoruhusu—iwe ni kuokoka mwisho wa mfumo huu wa mambo kwenye Har–Magedoni au kufa sasa na kufufuliwa baadaye katika ulimwengu wake mpya.—1 Yohana 2:17; Ufunuo 16:14-16; 21:3, 4.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Nikiwa na mke wangu, Deanne, ambaye hunitegemeza sana