Wakati Kansa Iwekwapo Kuwa Siri
SIKU moja katika Mei 1987, niliokota toleo la Juni 8 la Amkeni! nikaanza kusoma ile safu “Kutoka kwa Wasomaji Wetu.” Mara hiyo, nikaona kihabari fulani kutoka Japani kilichosomeka hivi:
“Sisi twataka kuwashukuru kwa zile makala juu ya kansa mlizochapisha. (Oktoba 8 na Oktoba 22, 1986, kwa Kiingereza) Mwaka uliopita binti yetu, ambaye hakuwa amepata kamwe ugonjwa wa siku moja katika muda wa miaka 16, kwa ghafula alitambuliwa kuwa mwenye dalili za kifua kikuu na kulazwa hospitali kwa miezi sita. Halafu, kwa sababu hakukuwa na viini vya kifua kikuu, akaondolewa hospitali.”
‘Ni ajabu!’ mimi nikawaza. ‘Hapo pana msichana ambaye amepatwa na yale yale yaliyonipata.’ Nikaendelea kusoma:
“Lakini mwezi uliofuata tulipata kujua kwamba alikuwa na kansa ya kikoromeo na kwamba kansa hiyo ilikuwa imehama kwenda kwenye mapafu yake. Mara hiyo alipasuliwa kuondoa kikoromeo chake na tezi za umajimaji wenye kukizunguka, na kuondolewa sehemu ya mapafu yake. Sasa yeye anapata matibabu ya kobalti.”
Mimi nilikuwa nimepata upasuaji uo huo. Nikawa mwenye shuku. ‘Je! hii ingeweza kuwa ikisema juu yangu?’ nikashangaa. ‘Lakini mimi sina kansa, au ninayo?’ Moyo wangu ulikuwa ukidunda huku macho yangu yakipiga mbio kusoma sehemu iliyobaki ya kihabari hicho:
“Upasuaji wake ulifanikiwa, naye anaishi maisha ya kawaida. Lakini sisi wazazi, tulihangaika daima na kuwa na wasiwasi tufanye nini kumsaidia binti yetu. Kupitia makala zenu tulihisi uhakikishio na kupata tena amani ya akili. Makala hizo ziliandaa mwelekezo mzuri juu ya jinsi tuwezavyo kumtia moyo binti yetu katika wakati ujao.—H. K., Japani.”
Ala, hizi ni herufi za kwanza za majina ya Baba! Basi je, mimi ndiye msichana huyo? Nikamwendea mbio mama yangu. “Umeng’amua kwamba ilisema juu yako, sivyo?” akasema na kutabasamu. Alikuwa akijaribu sana kusoma uso wangu. Hivyo ndivyo nilivyopata habari kwa mara ya kwanza kwamba nina kansa.
Kwa Nini Sikupashwa Habari Mapema
Katika Japani si desturi kuambia mgonjwa wakati kansa ionekanapo. Madaktari wangu walielekeza wazazi wangu washirikiane na mwongozo huo. Kwa kweli, Mama alikuwa amekuwa na mwelekeo wa kunipasha habari, lakini Baba hakuafiki. Alifanya wasiwasi juu ya uwezekano wa mimi kukata tamaa naye akasita-sita. Hivyo basi walitatanika kati ya kunipasha au kutonipasha habari za ugonjwa huo.
Halafu mfululizo wa makala juu ya habari ya kansa ukatokea katika matoleo ya Oktoba 8 na 22, 1986 ya Amkeni! (kwa Kiingereza) Baada ya kuyasoma, wazazi wangu waliamua kwamba kwenye wakati ufaao, yawapasa kuniambia juu ya kansa yangu. Ingawa hivyo, kwanza baba yangu aliandika barua ya uthamini kwa makala hizo kwenye Watch Tower Society katika Japani. Barua yake ilipochapishwa katika Amkeni!, wazazi wangu walihisi kwamba mkono wa Yehova, yule Mungu wa Biblia, ulikuwa nyuma ya tukio hilo. Ilikuwa njia yenye fadhili ya kuniacha mimi nijue juu ya kansa yangu, kwa kuwa mshangao wa kuona barua ya baba yangu wakati huo ulilemea hisia-moyo nyingine zote.
Hisia zangu hazikuwa zile za hofu, kwa maana mimi naamini kwa moyo mweupe lile fundisho la Biblia juu ya hali ya wafu. Lasema kwamba “hawajui neno lo lote.” (Mhubiri 9:5) Pia mimi naitumaini ahadi ya Biblia kwamba “wote waliomo makaburini [maziara ya ukumbusho, NW]” watarudi katika ufufuo.—Yohana 5:28, 29.
Kwa upande mwingine, lililonishusha moyo lilikuwa wazo hili: ‘Nikifa, wazazi wangu watakuwa wapweke kama nini watakapokuwa wakingojea ufufuo wangu.’ Waona, mimi ndiye mtoto wao wa pekee. ‘Yehova bila shaka atategemeza wazazi wangu kuipita miaka yao ya upweke,’ mimi nikasababu na kupuuza wazo hili lenye kushusha moyo.
Kuwekwa Hospitali
Katika Aprili 1985, miaka miwili tu kabla ya kuinua ile Amkeni! yenye barua ya baba yangu, niliandikishwa katika shule ya sekondari. Nilikuwa na miaka 15 tu. Baada ya kuchunguzwa hali ya kimwili, katika Mei nilipokea taarifa ikinishauri hivi: “Mpanuko Usiofaa wa Mirija ya Pumzi—Wahitaji uchunguzi kamili.”
Hata ingawa nilihisi sikuwa na kasoro, neno hilo gumu lilinitia mawazo mazito. Nilikuwa sijapata kamwe ugonjwa mkubwa, na kila mtu alinifikiria kuwa msichana mwenye afya. Hata hivyo, nilienda hospitali moja ya kwetu kuchunguzwa kikamili. Huko nikatajwa kuwa mwenye kifua kikuu na mara hiyo nikalazwa hospitali.
Maisha katika ile sehemu ya wagonjwa wa kifua kikuu hayakupendeza katu. Kwa miezi sita hakuna mtu wa nje ya hospitali hiyo aliyeruhusiwa kunizuru isipokuwa wazazi wangu. Barua kutoka kwa marafiki Wakristo na mirekodio ya kanda za mikutano ya Kikristo iliniimarisha na kunisaidia nipigane na majonzi yangu. Kuongezea hilo, kusoma vichapo vya Watch Tower Society pia kulinizuia nisijifikirie binafsi tu. Lakini zaidi ya yote, uhusiano wa kibinafsi pamoja na Mungu ulinisaidia kudumisha mtazamio chanya.
Azimio Langu Kumtumikia Mungu
Wajua, wazazi wangu walianza kujifunza Biblia nilipokuwa na umri wa miezi minne, nao walinilea kukubali mafundisho ya Biblia kuwa ukweli. Nilipoongezeka umri, asante kwa mazoezi ya wazazi wangu, nilikuja kuthamini sana uhusiano wangu pamoja na Yehova na nikasitawisha imani katika yeye kwa nia yangu mwenyewe. Nilijiweka wakfu kwa Yehova na kuonyesha wakfu wangu kwa ubatizo katika maji siku ya Desemba 4, 1982, nilipokuwa na miaka 13.
Basi, baada ya karibu miezi sita katika hospitali, niliruhusiwa kuondoka katika Oktoba 1985. Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, niling’amua jinsi hewa ya nje ilivyo ya kupendeza wakati mtu awezapo kutembea-tembea kwa uhuru. Ili kuonyesha uthamini wangu, niliamua kutumikia nikiwa mhudumu wa wakati wote wa muda, au painia msaidizi. Hivyo basi katika Novemba na Desemba pia, nilitumia saa 60 katika utumishi wa kujitolea wa Kikristo. Hata hivyo, katika Desemba nikajua kwamba ilikuwa lazima nilazwe hospitali tena ili kupasuliwa kikoromeo. Kule kufikiria tu kuwekwa hospitali kulifanya nilie.
Suala la Damu
Neno la Mungu huagiza Wakristo ‘waendelee kushika mwiko wa damu,’ nami nikiwa mtumishi aliyejiweka wakfu wa Yehova, nilitaka kufanya kila jambo kumpendeza. (Matendo 15:29, NW) Kwa kuwa upasuaji wangu ulipasa kufanywa, niliongea na daktari wangu nikaeleza kwa nini singeweza kukubali kutiwa damu mishipani. Alistahi msimamo wangu na kuniambia nisifanye wasiwasi juu ya hilo.
Hata hivyo, siku iliyotangulia upasuaji, niliingizwa upesi katika chumba cha hospitali ambamo madaktari zaidi ya kumi na wawili walikuwa wakingoja. Wapasuaji hao, ambao sikuwa nimeonana nao kamwe, walipaswa kuwapo kwenye upasuaji wangu. Moyo wangu ulipiga haraka zaidi kwa kukabiliwa na wanakazi wengi hivyo.
“Tungependa kuzungumza nawe upasuaji wa kesho,” akaanza yule daktari msimamizi. “Tutafungua mapafu yako na pia kikoromeo. Sasa, kuhusu ulilosema juu ya kutiwa damu mishipani, je! una uhakika kwamba wataka sisi tufanye sawasawa na ulivyosema hata dharura zisizotazamiwa zikitokea?”
“Ndiyo, nina uhakika kabisa,” nikajibu huku madaktari wakisikiliza kwa makini sana. “Tafadhali fanyeni kama nilivyoomba.”
Halafu baadhi yao wakaanza kuuliza maswali, kama vile: “Kwa nini hutakubali kutiwa damu mishipani?” “Hivyo ndivyo wewe hasa unavyohisi?” Wote walisikiliza kwa staha huku mimi nikijibu maswali yao. Mkazo wangu wa kwanza ukatoweka, nami nikaeleza jinsi nilivyokuja kukubali maoni ya Mungu juu ya damu. Pia nilielewesha wazi kwamba uthamini wangu mwenyewe wa sheria ya Mungu, wala si msongo wowote kutoka kwa wazazi wangu, ndio ulionisukuma kuomba upasuaji usio wa damu. Madaktari walistahi maoni yangu kwa fadhili na kunitia moyo nisifanye wasiwasi, kwa maana wangejitayarisha vizuri sana kwa ajili ya upasuaji.
Upasuaji na Utibabu wa Kobalti
Upasuaji ulihusisha kufungua shingo yangu na kuondoa koromeo, tezi za umajimaji mweupe wa mwili, na kisehemu cha mapafu. Madaktari waligundua kwamba kile ambacho hapo kwanza walikuwa wamekitaja kuwa kifua kikuu kwa kweli kilikuwa na vikuzi vyenye kansa vilivyokuwa vimehama kutoka kwenye kikoromeo. Hata hivyo, sikuambiwa kamwe kwamba upasuaji huo ulithibitisha kwamba nilikuwa na kansa.
Kwa kuwa madaktari walikuwa wamegusa nyuzi zangu za sauti wakati wa upasuaji, waliwaonya wazazi wangu kwamba huenda nikalazimika kufanyiwa upasuaji mwingine ndipo niweze kusema. Hivyo basi madaktari na pia wazazi wangu waliona shangwe mno niliporudiwa na fahamu na kuuliza hivi: “Hamkutumia damu, au vipi?”
Asante kwa jitihada za moyo mweupe wa madaktari hao, upasuaji ulifanikiwa, nami nilidumisha dhamiri safi ya Kikristo. Hata hivyo, madaktari waliwaambia wazazi wangu: ‘Labda yeye aweza kuishi kwa muda wa miaka minne tu. Huenda hata akafa mwakani. Hatimaye atakuwa na tatizo la kupumua, naye atakufa kwa maumivu makali. Tangu sasa na kuendelea atapoteza uzani hata kama atakula namna gani. Tafadhali mwe tayari kukabili matokeo hayo.’ Bila shaka, mimi sikujua lolote juu ya utabiri huo wa kuhuzunisha. Lakini wazazi wangu walishtuka, na huzuni yao ikawa kubwa sana.
Baada ya upasuaji katika Januari 1986, nililazwa hospitali kupata matibabu ya kobalti katika Februari na tena katika Novemba ya mwaka uo huo. Daktari aliyeingia katika chumba cha matibabu alilindwa kwa aproni maalumu na vivao vya mikononi. Alitoa vibonge viwili kutoka chombo mviringo cha metali akanipa nimeze. Nikafyonza vitu vya mnururisho, ambavyo vingefanya kazi kwa ndani. Hivyo, mimi nilitoka-toka mnururisho na hivyo basi ilikuwa lazima nilazwe kwenye chumba cha faragha kwa vipindi vya juma moja moja. Nilitenganishwa na mionano ya watu wote wa kutoka nje, isipokuwa wauguzi waliokuja kunilisha.
Lazima niseme kwamba, nilishangaa kuona matayarisho yale yote mengi na kustaajabishwa na uzito wa matibabu hayo. Hata hivyo, kama ilivyo desturi katika Japani, uhakika wa kwamba nilikuwa na kansa uliwekwa ukiwa siri yenye kulindwa sana isinifikie.
Kwa kuwa chumba hicho kilikuwa kimefichika nusu chini ya ardhi na kizuizi kilijengwa kuzuia mponyoko wa mnururisho, sikuweza kuona mengi kupitia madirisha. Ilichangamsha moyo kama nini marafiki Wakristo walipozuru na kunipungia mkono! Nilihisi upendo wao, ambao ulinitegemeza wakati wa kulazwa kwangu mahali pa upweke.
Kutimiza Mradi Wangu Maishani
Nilipokuwa katika matibabu ya kobalti, mwuguzi mmoja aliniuliza ni nini kilichoniendeleza nikiwa mchangamfu hivyo. Nikamwambia kwamba kujifunza Biblia kulikuwa kumenipa amani ya akili. (Zaburi 41:3) Maongezi hayo yaliamsha kupendezwa kwake, naye akaanza kujifunza Biblia.
Kuongea na wengine juu ya Mungu wangu kumenifurahisha sikuzote. Hivyo basi muda wote tangu miaka yangu ya uchanga, umekuwa mradi wangu kuwa mhudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova. Ili kufikia mradi huo, ilikuwa lazima nisawazishe masomo yangu ya shule na huduma pamoja na pigano langu dhidi ya kansa. Nilifurahi kama nini kuwekwa rasmi kwenye huduma ya wakati wote nikiwa painia wa kawaida mara tu nilipomaliza shule katika Machi 1988!
Bila shaka, ugonjwa wangu haujaponywa kabisa. Ingawa sasa sihisi nikiwa mnyonge sana, huwa ni lazima nilazwe hospitali mara kwa mara ili kuchunguzwa. Lakini hata katika hospitali, mimi huweza kuongea na madaktari, wauguzi, na wagonjwa wenzangu juu ya tumaini ambalo Mungu hutoa la uhai wa milele katika ulimwengu mpya.—Ufunuo 21:3, 4.
Wakati mmoja mfanya kazi wa hospitali aliwaambia wazazi wangu: “Huku mapafu yake yakiwa yameathiriwa sana, apaswa kuwa akihema-hema apate hewa, akiwa na maumivu makali apumuapo na kukaa-kaa bila la kufanya. Lakini Rie anaenda huku na huku. Nashindwa kuelewa hilo. Je! ni dini yenu imfanyayo kuwa mtendaji na mchangamfu hivyo?”
Kwa kweli, mimi nina siri ambayo hunitegemeza hivi kwamba sivunjiki moyo. Ni uhusiano wangu na Yehova Mungu. Yeye hunitia nguvu ili nisijiachilie kushindwa na ugonjwa wangu. (Wafilipi 4:13) Ndiyo sababu, ingawa nasumbuliwa na kansa, mimi hudumisha amani ya akili wala sipotezi tumaini. Bila shaka, ningependa kuishi moja kwa moja hadi ndani ya ulimwengu mpya wenye kufanyizwa na Yehova ambamo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Lakini hata kutukie nini, hata kifo kinichukue, mimi nina uhakika kwamba Yehova hatanisahau ikiwa nitaendelea kumpendeza.—Kama ilivyosimuliwa na Rie Kinoshita.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Nimetumikia nikiwa mhudumu wa wakati wote tangu Machi 1988