Utawala wa Kibinadamu Wapimwa Katika Mizani
Sehemu ya 5: Mamlaka Isiyo na Mipaka Ni Baraka au Laana?
Autokrasi: serikali ya mtu mmoja kuwa na mamlaka isiyo na mipaka; Umamlaka (“authoritarianism”): utumiaji wa uwezo wa utawala bila idhini ya wanaotawalwa, si ya kupita kiasi kama utawala wa mamlaka kamili (totalitarianism”); Udikteta: serikali iliyo na mtawala ambaye hana wajibu kwa sheria wala tengenezo rasmi lolote; Utawala wa mamlaka kamili (“totalitarianism”): udhibiti wenye kutoka mahali pakuu pa kati ukiendeshwa na baraza la kiautokrasi, ukifanya raia watoe utii kamili kwa mamlaka ya Nchi.
SERIKALI za kimamlaka, ambazo kwa muda mrefu zimetawala kikamili na kunyima watu mmoja mmoja uhuru, hutukumbusha maneno kama “-a udhalimu,” “-a ukorofi,” na “-a uonevu.” Zikiwa zinatukuza utaifa sana, ni tawala zinazoongoza kila tawi la serikali, zinazochunga kwa uangalifu raia zao, na kupiga marufuku shughuli zisizoendeleza masilahi ya taifa hata ikiwa shughuli hizo hazidhuru taifa. Ni sikitisho kwamba historia ya kibinadamu haikosi kamwe kuripotiwa kuwa yenye serikali za kimamlaka.
Uwezo wa Kadiri Tu
The World Book Encyclopedia inasema: “Serikali ya Kirusi chini ya czars ilikaribia kuwa autokrasi kamili.” Lakini si utawala wote wa kimamlaka ulio na uwezo kamili; mamlaka yazo hasa ni ya kadiri. Na serikali zote za kimamlaka si autokrasi, yaani serikali zinazoongozwa na mtawala mmoja, dikteta au czar. Serikali nyingine huenda zikatawalwa na kikundi cha watu, labda na baraza la kijeshi, au wachache wenye uwezo wote au utajiri mwingi.
Hata demokrasi zaweza kuwa za kimamlaka. Ni kweli kwamba zina vyama vya kisiasa, zinakuwa na uchaguzi wa kura, zinadumisha mahakama za kisheria, zinajivunia kuwa na bunge au baraza la kutengeneza sheria. Hata hivyo, kadiri ambayo serikali inatawala mashirika mbalimbali hayo, ikiyalazimisha kufanya itakavyo, kwa kadiri hiyo basi serikali hiyo huwa ya kimamlaka, hata iwe imefanyizwaje. Si kwamba ilifanyizwa iwe hivyo kwa kujua. Wakati wa vita au vipindi vya msukosuko, hali ingebidi kuipa serikali mamlaka ya kudhibiti mambo ya dharura. Labda dharura hiyo ilikwisha; lakini mamlaka ya dharura haikwisha.
Tawala za kifalme ni za kimamlaka kwa kadiri zinazotofautiana. Lakini tawala za kifalme zilizo kamili kwa kadiri kubwa zimebadilishwa na tawala za kifalme zenye mipaka. Mabaraza ya kutunga sheria na yawezekana katiba zilizoandikwa zinaweka mipaka ya mamlaka ambayo tawala hizo za kifalme zinaweza kutumia, zikipunguza uwezekano wa tawala hizo kuwa za kimamlaka. Kwa hiyo, watu mmoja mmoja hufurahia sana tawala za kifalme zilizo na uwezo wenye mipaka kuliko zile tawala za kifalme za zamani zilizokuwa na mamlaka kamili.
Hata wakati tawala za kifalme zilipokuwa nyingi, uwezo wazo ulikuwa na mpaka. Profesa wa historia Orest Ranum aeleza kwamba “wengi wa wafalme walikosa ile tabia ya moyoni na uwezo halisi wa kuwalemea kabisa raia zao katika utawala au kukandamizia mbali wachache wenye ubaguzi wa rangi na wenye kufuata utamaduni kama vile Hitler au Mussolini au Stalin walivyoweza kufanya.” Kwa wazi, maadili bora na sifa nzuri za mfalme—au ukosefu wazo—ndizo zilizoamua ingekuwaje. Kwa vyovyote, asema Ranum: “Hakuna serikali ya kifalme yenye utawala kamili inayoweza kufikia serikali yenye mamlaka kamili ya ki-siku-hizi kwa kadiri ya kutawala mambo ya kitamaduni na kiuchumi.”
Kuwa na Lengo la Utawala Kamili
Wakati wa miaka ya 1920 na 1930, aina mpya ya serikali ya kimamlaka ilijitokeza ulimwenguni katika nchi za Italia, Urusi na Ujerumani, ikitokeza ulazima wa kuitafutia jina la kuifafanua vya kutosha. Katika mabara hayo vyombo vya habari vilikuwa vimekuja chini ya udhibiti wa Serikali. Polisi walikuwa wamekuwa watumishi wa chama cha kisiasa kinachotawala na hawakuwa tena watumishi wa umma. Propaganda, uzuizi wa kiserikali wa habari zisizofaa, sheria kali za kiserikali, uchunguzi wa polisi wa siri, na hata nguvu zilikuwa zikitumiwa ili kukandamiza upinzani. Wananchi walikuwa wakilazimishwa kufuata mawazo ya kisiasa na ya kijamii ya serikali. Waliokataa waliadhibiwa wakiitwa wasaliti. Neno “umamlaka-kamili” (“totalitarianism”) likaonekana linafaa—nchi inayofuatia mradi wayo yenyewe, ikidhibiti kikamili raia wayo wote.
Gazeti la Ujerumani Informationen zur politischen Bildung (Habari ya Elimu ya Kisiasa) laelezea zaidi hivi: “Taifa linalokuwa na lengo la udhibiti kamili, likitofautiana na utawala wa kimamlaka, haliridhiki na kuchukua vyeo rasmi vya mamlaka. Halipendelei kuwapa watu walo hata uhuru wenye mipaka wenye kuhusu bali linadai utii na kuungwa mkono kwa bidii kwa fundisho lalo nyakati zote. Madai hayo yasiyo na mipaka hutaka nchi yenye utawala kamili iongoze maeneo ambayo kwa kawaida hayaingiliwi na serikali, kama vile familia, dini na wakati wa starehe. Ili kutimiza matakwa hayo, ni lazima nchi yenye utawala kamili ieneze mfumo wa kitengenezo unaoweza kusimamia kila mtu nyakati zote.”
Bila shaka, kwa maoni ya Nchi hiyo na masilahi yayo, serikali ya utawala kamili inafanikiwa sana. Lakini haiwezekani kuidumisha, asema mwandishi wa magazeti Charles Krauthammer. Kuna mambo mengi mno yanayohitaji kudhibitiwa. “Kwa vipindi vifupi sana mwaweza kufunga watu gerezani, hata kuwapiga risasi,” yeye asema, “lakini baadaye unakosa risasi, magereza, nguvu, hata watu wa kuadhibiwa. . . . Ni mageuzo ya kudumu pekee yanayoweza kuufaa utawala kamili, na mageuzo ya kudumu hayawezekani. Hata utawala wa kikorofi wahitaji usingizi.”
Je! Ulisababishwa na ‘Jamii ya Umma’?
Nadharia nyingi zimetajwa kueleza kwa nini umamlaka, hasa katika kadiri yao na mafanikio yao ya juu kabisa, utawala wa mamlaka kamili, umekuwa mwingi hivyo katika karne ya 20. Kulingana na The World Book Encyclopedia, “theluthi mbili za kwanza za miaka ya 1900 zilikuwa kipindi cha badiliko kubwa—labda badiliko lililo la haraka sana na lenye kuenea sana katika historia yote.” Bila shaka, jambo hilo limetokeza sana elekeo la kuwako utawala wa mamlaka kamili.
Ongezeko kubwa la idadi ya watu, watu kuhamia mijini, na maendeleo ya kitekinolojia ni matukio ya ki-siku-hizi ambayo yamesaidia kuunda ile iitwayo jamii ya tungamano. Neno hilo laonyesha jamii ya kiviwanda yenye mashirika makubwa yenye uongozi kutoka mahali pamoja, ya kiofisi, yasiyo ya kibinafsi. Ni jamii ya watu ambamo mahusiano ya kibinadamu huelekea kuwa ya kijuu-juu na kufifia. Ni jamii ambamo, kati ya watu wengi mno, watu mmoja mmoja wanatafuta daima asili za ukoo wao na hisia ya kujiona kuwa sehemu ya jumuiya.
Ni jambo la kubishaniwa juu ya kadiri ambavyo jamii ya tungamano ilisaidia kukuza utawala wa mamlaka kamili. Kulingana na yule mwanasayansi wa kisiasa mzaliwa wa Ujerumani aliye mfu sasa, Hannah Arendt, jamii hiyo ilikuwa na uvutano mwingi. Kitabu chake The Origins of Totalitarianism chaeleza kwamba utawala wa mamlaka kamili umejengwa, si juu ya tabaka mbalimbali, bali juu ya matungamo ya watu ambao “kwa sababu ya wingi wao tu, kutojali kwao, au kwa sababu zote mbili, hawawezi kufanyizwa kuwa tengenezo lolote lenye msingi wa masilahi moja, kuwa vyama vya kisiasa au serikali za manispaa au matengenezo ya kikazi au vyama vya wafanya kazi.”
Arendt pia ataja sababu nyingine zilizosaidia ukuzi wa utawala wa mamlaka kamili: ubeberu, upinzani kwa jamii zenye asili ya Kishemu, na kuvunjika-vunjika kwa ule muundo wa tangu zamani wa taifa ambalo ndilo serikali pia.
Ubeberu?
Kabla tu ya karne hii, ukoloni uliongeza mwendo. Mwanauchumi wa Uingereza John Atkinson Hobson ataja tarehe za 1884 hadi 1914 kuwa kipindi cha ule ambao sasa huitwa ubeberu mpya. Huo ulikuwa ni utumizi wa mamlaka kamili wa serikali za kifalme na za kidemokrasi kwa ajili ya kupanua milki zazo. Kuwa na mamlaka nyingi kuliko nchi nyinginezo kulipatikana ama kwa kuzitwaa moja kwa moja ama kwa kutawala mambo yazo ya kisiasa na ya kiuchumi kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Hobson afasiri ubeberu kuwa hasa jambo la kiuchumi. Kwa hakika, mara nyingi namna hiyo mpya ya ukoloni haikuhusika sana na mamlaka ya kisiasa kama ilivyohusika na mpanuko wa kiuchumi na kufanyizwa kwa masoko mapya kwa ajili ya bidhaa za taifa.
Jambo hilo lilionekana wazi hasa katika ile iliyokuja kuitwa Harakati ya Kumiliki Afrika. Tayari katika miaka ya mapema ya 1880, Uingereza, Ufaransa, na Ureno zilikuwa na koloni nyingi. Lakini Ubelgiji na Ujerumani zilipoonyesha kutupa jicho kwa wivu, kukuru-kakara ilianza. Upesi Afrika yote ikawa chini ya utawala wa Ulaya, isipokuwa Ethiopia na Liberia. Waafrika weusi walilazimishwa kutazama wakiwa kando huku Walowezi weupe “Wakristo” wakichukua bara lao.
Marekani pia ikaja kuwa mamlaka ya kibeberu. Katika mwisho-mwisho wa karne ya 19, ilichukua Alaska, Hawaii, Visiwa vya Filipino, Guam, na Samoa na pamoja na visiwa vingine vya Pasifiki, na pia Puerto Riko na visiwa vingine vya Karibea. Yenye umaana wa kupendeza ni maelezo ya Henry F. Graff, profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Columbia, ambaye aandika: “Matendo ya wamisionari Wakristo yalikuwa na uvutano kama ule ule wa walimu wa kisheria katika kufanyiza ubeberu wa kisasa.” Lakini kama wamisionari hawa wa Jumuiya ya Wakristo wangalikuwa ni Wakristo wa kweli, basi wangalibaki bila kuwamo katika harakati ya kumiliki Afrika na pia milki nyingine za kikoloni, kwa kulingana na maneno ya Yesu: “Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.”—Yohana 17:16; Yakobo 4:4.
Enzi ya ubeberu yasemekana kuwa iliisha 1914. Lakini sivyo roho yake ya kutawala kimamlaka. Roho hiyo ilionyeshwa wazi na Cecil Rhodes, waziri mkuu wakati wa miaka ya 1890 wa eneo ambalo sasa ni sehemu ya Afrika Kusini, aliposema: “Mpanuko ni mambo yote.” Akiwa mwenye bidii kupanua milki ya Uingereza, wakati mmoja alijigamba hivi: “Ningeweza kujitwalia sayari ikiwa ningekuwa na uwezo.” Roho hiyo ya ubinafsi bado inachochea mataifa kutawala, kwa kadiri inavyowezekana, miongozo ya kisiasa na kiuchumi ya mabara mengine kwa faida yao. Kwa mfano, Japani baada ya kushindwa kutawala kijeshi, nyakati nyingine hushtakiwa kuwa inajaribu sasa “kutawala” kiuchumi.
Je! Kupindua Utawala wa Kimamlaka Ndilo Suluhisho?
Uwezo usio na mipaka wenye kutumiwa na wanadamu wasiofuata kanuni na wenye pupa ni laana, wala si baraka. Maneno ya Mfalme Sulemani wa kale yanafaa sana: “Tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.”—Mhubiri 4:1.
Chini ya utawala wa kimamlaka ‘machozi ya waliodhulumiwa’ kwa kweli yamekuwa mengi. Hata hivyo, Mikhail Gorbachev alionya hivi katika kitabu chake Perestroika cha 1987: “Inawezekana kukandamiza, kulazimisha, kuhonga, kuvunja au kulipua, lakini kwa muda fulani tu.” Kulingana na hilo, hata ujapokuwa uwezo “upo upande wa wanaowadhulumu,” wananchi wameamka mara kadhaa kutupilia mbali kongwa la serikali ya kimamlaka. Mapinduzi ya umwagikaji damu wa Nicolae Ceauseşcu pamoja na majeshi yake ya usalama, “Securitate,” ni mfano wa jambo hilo.
Kupindua utawala wa kimamlaka kwa kweli kwaweza kuleta utulizo. Lakini pia ni kweli kama vile methali moja ya Kiburma husema, kwamba “mnapokuwa na mtawala mpya ndipo mnapotambua uzuri wa mtawala wa awali.” Ni nani awezaye kuhakikisha kwamba utawala uliokuwa mbaya hautabadilishwa na utawala mbaya hata zaidi?
Kutaja mfano mmoja tu, utawala wa kimamlaka katika bara moja la Amerika ya Kilatini ulipinduliwa. Watu walijawa na tumaini kwamba mambo yangebadilika kuwa bora, lakini je, yalibadilika? Likitoa maelezo juu ya hali ya miaka ya baadaye, gazeti moja la habari lilisema kwamba maisha yalikuwa yamekuwa “magumu zaidi tu.” Likiongea juu ya infleshoni yenye kuongezeka kasi, gazeti hilo lilitaja fedha ya kitaifa kuwa “karibu haina thamani,” likaomboleza juu ya vifaa vya afya ambavyo havitoshei, na likataja kwamba ugonjwa wa ukosefu wa vyakula vya kufaa mwili ulikuwa ukiongezeka. Baada ya muda, utawala huo pia uliondolewa mamlakani.
Je! si wazi kabisa kwamba utawala wa kibinadamu kwa kila namna yao umepatikana kuwa umepungua? Na bado watu wanaendelea kutafuta serikali iliyo bora kabisa. Mifano miwili ya kutokeza juu ya tamausho ambamo jambo hilo laweza kuongoza, likitumbukiza mataifa mazima katika kukata sana tumaini bila “mfariji,” itazungumzwa katika toleo letu linalokuja.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mfano wa autokrasi iliyokaribia kuwa kamili ulikuwa Urusi chini ya watawala wa czars
[Hisani]
Alexander II iliyofanywa na Krüger, karibu 1855