Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 4/8 kur. 13-17
  • Sehemu 2: Wafalme, Kama Nyota, Huinuka na Kuanguka

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sehemu 2: Wafalme, Kama Nyota, Huinuka na Kuanguka
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Umoja Kupitia Wingi wa Mtu Mmoja
  • Wafalme Katika Mavazi ya Kidini
  • Enzi ya “Monarchy” Wenye Mamlaka Kamili
  • “Miungu” Yashushwa Kuwa Mihuri
  • Umeonekana Kuwa na Upungufu
  • Nyota ya Aina Tofauti
  • Sehemu ya 5: Mamlaka Isiyo na Mipaka Ni Baraka au Laana?
    Amkeni!—1991
  • Sehemu ya 10: Hatimaye Serikali Kamilifu!
    Amkeni!—1991
  • Ni Nini Kimepata Mamlaka?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Ufalme wa Mungu
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 4/8 kur. 13-17

Utawala wa Kibinadamu Wapimwa Katika Mizani

Sehemu 2: Wafalme, Kama Nyota, Huinuka na Kuanguka

Monarchy: serikali inayoongozwa na mkuu wa serikali aliyerithi, kama vile mfalme au maliki; Ufalme: namna ya serikali ya kimonarki yenye kuongozwa na mfalme au malkia; Milki: eneo kubwa ambalo kwa kawaida hutia ndani kikundi cha mataifa, serikali, au vikundi vya watu chini ya uongozi wa mamlaka moja iliyo kuu, sanasana huongozwa na maliki.

“IKAWA siku za Amrafeli mfalme wa Shinari.” Hapo, kama ianzavyo sura ya 14 ya Mwanzo, Biblia hutumia neno “mfalme” kwa mara ya kwanza. Kama Amrafeli lilikuwa jina la Mfalme Hammurabi ajulikanaye sana, kama wanavyodai wengine, sisi hatujui. Tunachojua ni kwamba, hata yeye awe alikuwa nani, wazo la ufalme wa kibinadamu halikutokana na Amrafeli. Mamia kadhaa ya miaka iliyopita, Nimrodi, ijapokuwa hakuitwa mfalme, kwa wazi alikuwa mmoja. Kwa kweli, yeye ndiye aliyekuwa mfalme wa kwanza wa kibinadamu katika historia.—Mwanzo 10:8-12.

Ni kweli, hatuna vitu vya kale vilivyochimbuliwa vinavyorejezea Mfalme Nimrodi au Mfalme Amrafeli. “Enmebaragesi, mfalme wa Kishi, ndiye mtawala wa kale zaidi wa Kimesopotamia ambaye kumhusu kuna maandishi asilia yaliyochongwa,” chasema The New Encyclopædia Britannica. Kutoka Kishi, serikali ya jiji ya kale katika Mesopotamia, lilitokea neno la Kisumeri la mtawala, linalomaanisha “mwanamume mkuu.” Ijapokuwa tarehe inayopewa utawala wa Enmebaragesi hutofautiana na kronolojia ya Biblia, bado yatoa ukadiriaji wa wakati wa kipindi kinachokubalika na Biblia na, lililo la maana zaidi, huonyesha chanzo cha utawala wa kibinadamu kuwa mahali pale pale duniani kama inavyoonyeshwa na Biblia.

Umoja Kupitia Wingi wa Mtu Mmoja

Utawala wa kiukoo wa Kichina, Shang, au Yin, hufikiriwa kwa ujumla kuwa ulianza wakati fulani kati ya karne ya 18 na ya 16 K.W.K., ijapokuwa tarehe hiyo si hakika. Kwa vyovyote, monarchy ndio namna ya kale zaidi ya serikali ya kibinadamu. Pia umeenea sana.

Neno “monarchy” latoka kwa maneno ya Kigiriki moʹnos, linalomaanisha “pekee,” na ar·kheʹ, linalomaanisha “utawala.” Kwa hiyo, umonarki hukabidhi mamlaka kamili kwa mtu mmoja anayetumika kwa haki yake mwenyewe akiwa kiongozi wa kudumu wa serikali. Katika monarchy kamili, amri ya mfalme ilikuwa ni sheria. Ndiyo kusema, yeye hufanyiza wingi akiwa mmoja.

Sikuzote monarchy umeonwa kuwa wenye kusaidia kuunganisha mataifa. John H. Mundy, ambaye hufundisha historia ya Ulaya ya enzi za katikati, hueleza kwamba katika nyakati za enzi za katikati, nadharia ya kisiasa “ilitoa hoja kwamba kwa sababu hautambui tofauti za vyama fulani, muundo wa monarchy uliyafaa maeneo makubwa yenye masilahi ya kijimbo yenye kutofautiana na yenye kupingana.” Mara nyingi maeneo hayo makubwa yenye ‘masilahi ya kijimbo yenye kupingana’ yalikuwa ni tokeo la ushindi wa kijeshi, kwa kuwa wakati wote wafalme walikuwa ni viongozi wa kijeshi. Kwa kweli, mwanahistoria W. L. Warren asema kwamba ushindi katika vita “kwa kawaida ulionwa kuwa takwa la kwanza kwa ufalme wenye kufanikiwa.”

Kwa hiyo, namna ya serikali ya monarchy ilichangia kusimamishwa kwa mamlaka za ulimwengu kama Milki ya Ugiriki chini ya Aleksanda Mkuu, Milki ya Roma chini ya Makaisari, na, hivi karibuni zaidi, Milki ya Uingereza. Hii ya mwisho, ikiwa katika mafanikio yayo makubwa zaidi mapema katika karne ya 20, iliunganisha karibu robo ya idadi ya watu wa ulimwengu na robo ya eneo lao la ardhi chini ya mtawala mmoja.

Wafalme Katika Mavazi ya Kidini

Wafalme wengi wa kale walijidaia uungu. Ni kama alivyoonelea mwanahistoria George Sabine: “Kuanzia na Aleksanda, wafalme wa Ugiriki walihesabiwa pia miongoni mwa miungu ya majiji ya Ugiriki. Mfalme aliyefanywa kuwa mungu alitambulika kotekote katika Mashariki na mwishowe hilo likawa lazima lifuatwe na wamaliki Waroma.” Yeye asema kwamba imani hiyo katika uungu wa wafalme iliendelea katika Ulaya “katika umbo moja au jingine, hadi kufikia nyakati za ki-siku-hizi.”

Katika Amerika ya Kati na ya Kusini, mataifa ya Aztec na Inca yalionwa kuwa monarchy mtakatifu. Katika Asia haikuwa mpaka 1946 kwamba Maliki Hirohito wa Japan, aliye mfu sasa, akaacha dai lake la kuwa mzao wa kibinadamu wa 124 wa mungu-jua wa kike Amaterasu Omikami.

Ingawa si wafalme wote waliodai uungu, wengi wao angalau walishikilia kwamba walikuwa na tegemezo la kimungu. Uchaguzi wa mtu mmoja peke yake awakilishe Mungu duniani ulileta haiba ya kikuhani. John H. Mundy aeleza kwamba “wazo la kale kwamba wafalme wenyewe walikuwa wa kikuhani lilienea hadi Magharibi, likifanya mwana-mfalme awe kiongozi mwenye kusimamia kanisa lake na mkurugenzi wa mitume walo.” Lilikuwa wazo la kidini “lililotolewa kutoka uenzi wa Konstanino wa kanisa na serikali [wakati wa karne ya nne W.K.], na kwa kanisa kukubali wakati huo wazo la Neoplato.” Baraka ya kidini aliyopewa wakati wa kutawazwa ilitia fahari kwenye utawala wa mfalme kwa kuupa uhalali ambao kama sivyo haungekuwapo.

Katika 1173, Henry 2 wa Uingereza alianza kutumia cheo “Mfalme kwa neema ya Mungu.” Hilo liliongoza kwenye wazo lililojulikana baadaye kuwa haki ya kimungu ya wafalme, likimaanisha kwamba uwezo wa mfalme ulikuwa wa urithi. Ilidhaniwa Mungu alidhihirisha uchaguzi wake kwa uhakika wa kuzaliwa. Katika 1661, Louis 14 wa Ufaransa alitokeza tafsiri yenye kupita kiasi ya fundisho hilo kwa kujitwalia uongozi kamili wa kiserikali. Yeye aliona upinzani kuwa dhambi dhidi ya Mungu aliyemwakilisha. “L’état c’est moi! [Mimi ndiye Serikali],” akajigamba.

Wazo kama hilo lilitokea katika Scotland karibu na wakati uo huo. Alipokuwa angali anatawala Scotland akiwa James 6 lakini kabla ya kuwa Mfalme James 1 wa Uingereza katika 1603, mfalme huyo aliandika hivi: “Wafalme huitwa Miungu . . . kwa sababu wao huketi juu ya kiti cha enzi cha MUNGU duniani, na watamtolea [Y]eye hesabu ya usimamizi wao.” Hatujui ni kwa kadiri gani imani hiyo ilimwongoza James aidhinishe kutafsiriwa kwa Biblia katika Kiingereza. Sisi twalijua tokeo, King James Version, ambayo ingali yatumiwa sana na Waprotestanti.

Enzi ya “Monarchy” Wenye Mamlaka Kamili

Tangu Enzi za Katikati za mapema na kuendelea, monarchy ulikuwa ndio namna ya serikali iliyokuwapo. Wafalme walisitawisha njia ya gharama ndogo na ya kuwafaa kutawala kwa kukabidhi mamlaka makabaila walio maarufu. Wao nao, walisimamisha mfumo wa kisiasa na kijeshi unaojulikana kuwa feudalism. Kwa sababu ya kutoa utumishi wa kijeshi na mwingineo, makabaila hao waliwapa vibaraka vyao ardhi. Lakini kwa kadiri ambavyo makabaila hao wa feudal walivyokuwa wenye matokeo na nguvu zaidi, ndivyo ilivyoelekea sana ufalme ungevunjika-vunjika kuwa maeneo tofauti-tofauti chini ya mamlaka ya feudal.

Isitoshe, mfumo huo wa feudal uliwanyang’anya raia fahari na uhuru wao. Walipigiwa ubwana na makabaila wa kijeshi, wakikaliwa hasa na daraka la kuwapa malipo yao. Akiwa amenyimwa elimu na fursa za kitamaduni, “kabwela alikuwa na haki chache ambazo zingeweza kutekelezwa na sheria dhidi ya bwana mwenye kutawala eneo lake,” chasema Collier’s Encyclopedia. “Yeye hangeweza kuoa, kuwapokeza warithi wake umilikiji wa shamba lake, wala kuondoka kwenye eneo hilo bila ya kibali cha bwana huyo.”

Hiyo haikuwa njia pekee ya kutawala katika monarchy wenye mamlaka kamili. Wafalme fulani walikabidhi vyeo vya usimamizi kwa watu mmoja mmoja ambao baadaye wangeweza kuondolewa kwenye cheo, ikionwa ni lazima. Wafalme wengine walikabidhi serikali ya mtaa kwa matengenezo yaliyopendwa na wengi ambayo yalitawala kwa njia ya mila na msongo wa kijamii. Lakini kwa hivi au vile njia hizo zote zilikuwa haziridhishi. Ijapokuwa hayo, waandikaji wa karne ya 17, kama vile Sir Robert Filmer wa Uingereza na Jacques-Bénigne Bossuet wa Ufaransa, wangali walitetea mamlaka kamili kuwa ndiyo namna pekee iliyofaa ya serikali. Hata hivyo siku zayo zilikuwa zimehesabiwa.

“Miungu” Yashushwa Kuwa Mihuri

Ijapokuwa imani ya kijumla kwamba wafalme wangemjibu Mungu peke yake, msongo ulikuwa umeongezeka kwa muda mrefu ili kuwafanya wajibu sheria, desturi, na mamlaka za kibinadamu. Kufikia karne ya 18, “wafalme walitumia usemi tofauti na ule wa wenye enzi wa karne ya kumi na saba,” chasema The Columbia History of the World, hata hivyo, kikiongeza kwamba “chini na nyuma ya usemi huo wao wangali walikuwa wenye enzi kuu.” Kisha chaeleza kwamba “wakati Frederick Mkuu alipojiita mwenyewe ‘mtumishi wa kwanza wa serikali’ na kukanusha haki ya kimungu ya wafalme, yeye hakuwa akifikiria kuacha mamlaka.”

Hata hivyo, baada ya Maasi ya 1688 katika Uingereza na Maasi ya Ufaransa ya 1789, wakati wa mamlaka kamili ukawa umekwisha kwa sehemu kubwa. Kidato kwa kidato, monarchy wenye mamlaka kamili ukaachia njia monarchy uliowekewa mipaka wenye sheria zilizotungwa au katiba, au vyote viwili. Tofauti na karne ya 12 wakati ambapo “ufalme ulikuwa kile ambacho mfalme angeweza kuufanya, na kile ambacho raia zake walikuwa tayari kukubali,” tukinukuu mwanahistoria W.L. Warren, leo mamlaka ya kisiasa ya wafalme na malkia walio wengi imewekewa mipaka mingi.

Bila shaka, wafalme wachache wangali wana mamlaka nyingi. Lakini walio wengi walikwisha poteza zamani utukufu wao wa “uungu” na wanaridhika kutumika kama muhuri, kitovu cha mamlaka ambacho kukizunguka watu wanaweza kutiwa moyo waungane katika roho ya uaminifu. Monarchy uliowekewa mipaka umejaribu kudumisha zile sehemu zenye kuunganisha za utawala wa mtu mmoja huku ukifutilia mbali sehemu zao mbaya kwa kukabidhi mamlaka halisi sheria zilizotungwa.

Wazo la monarchy uliowekewa mipaka lingali lapendwa na wengi. Hivi majuzi katika 1983, Krishna Prasad Bhattarai, kiongozi wa Nepali Congress Party katika Nepal, alitetea monarchy ‘kuwa kizuizi cha mchafuko,’ akisema kwamba ‘Mfalme ni wa lazima ili kudumisha nchi ikiwa na umoja.’ Na ingawa katika 1987 Wafaransa walikuwa wakifanya matayarisho ya mwisho ya kusherehekea mwadhimisho wa 200 wa Maasi ya Ufaransa, asilimia 17 ya wale walioombwa maoni walipendelea kurejeshwa kwa monarchy. Mshiriki wa kikundi kimoja cha wataka monarchy alisema: “Mfalme ndiyo njia pekee ya kuunganisha taifa ambalo limegawanywa kwa muda mrefu sana na mzozo wa kisiasa.”

Mwaka uo huo, gazeti Time lilionelea hivi: “Ufalme hutokeza uaminifu labda kwa sababu wafalme ndio mifano mikuu ya mwisho ya enzi yetu ya kilimwengu, maumbo pekee yaliyo makubwa zaidi ya binadamu ambao wangali waweza kuaminika haraka huku wakiishi katika fumbo. Ikiwa Mungu amekufa, basi Malkia na aishi maisha marefu!” Lakini likiyatazama mambo kwa uhalisi zaidi, liliongeza kwamba “mamlaka ya enzi kuu ya Malkia [wa Uingereza] yategemea hasa umeremeti wake wa kuwa bila uwezo.”

Umeonekana Kuwa na Upungufu

Monarchy wenye mamlaka kamili hauridhishi. Kwa asili huo si imara. Muda si muda, kila mtawala hufa na lazima mahali pake pachukuliwe na mwandamizi, ambaye mara nyingi huchaguliwa kwa sababu ya ukoo wala si kwa sababu ya adili za juu au uwezo. Ni nani anayeweza kutoa uhakikisho kwamba mwana atakuwa mwema kama baba yake? Au ikiwa baba ni mbaya, kwamba mwana wake atakuwa afadhali?

Pia, kama Cristiano Grottanelli anavyotaja, “uchaguzi wa mwandamizi wa kifalme” mara nyingi “umewekewa masharti yenye matakwa machache, hivi kwamba mashindano hutoke miongoni mwa wale washiriki wa ukoo wa kifalme wanaougombea. Hivyo kipindi kinachofuata kifo cha mfalme kwa kawaida huwa kipindi cha mchafuko wa kijamii (na kilimwengu), kihalisi na kimfano pia.”

Ukiwa ni utawala wa mtu mmoja, ufaaji wa monarchy wenye mamlaka kamili hutegemea kufaa kwa yule aliye mtawala wao. Vipawa vyake na sifa zake bora zaweza kuonekana katika serikali yake lakini ndivyo ilivyo na udhaifu wake pia, mipaka, na ukosefu wa maarifa. Hata wenye damu ya kifalme ni wasiokamilika. Wafalme wabaya husimamisha serikali mbaya, wafalme wema yawezekana wakasimamisha serikali bora, lakini ni mfalme mkamilifu peke yake awezaye kusimamisha aina ya serikali ambayo binadamu hutamani na wanayostahili kuwa nayo.

Monarchy wenye bunge au wenye mipaka hupungukiwa pia. Katika karne hii, kule United Kingdom, wafalme na malkia wa Uingereza walio kama muhuri husimamia mvunjiko wa milki iliyo kubwa zaidi na yenye nguvu zaidi ambayo ulimwengu umepata kuona.

Nyota ya Aina Tofauti

Wafalme, kama nyota, huinuka na kuanguka—isipokuwa mmoja. Kujihusu mwenyewe, Yesu Kristo asema kwamba yeye ni “Shina na Mzao wa Daudi; ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.” (Ufunuo 22:16) Akiwa mzao wa moja kwa moja wa Mfalme Daudi kwa kulingana na mnofu, Yesu astahili kuwa Mfalme wa serikali ya kimungu ya Mungu. Akiwa “ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi,” Yesu pia ndiye “nyota ya mchana” ambayo Petro alisema ingeinuka na kufanya siku ipambazuke.—2 Petro 1:19, NW; Hesabu 24:17; Zaburi 89:34-37.

Kwa sababu ya mambo hayo ya hakika, je! ni jambo la hekima jinsi gani kutumainia nyota zenye kuanguka za monarchy wa kibinadamu zitoe uongozi? Badala yake, je! hekima haitaki kwamba tuweke matumaini yetu kwa Mfalme aliyekusudiwa na Mungu, Yesu Kristo, “Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana; ambaye yeye peke yake [kushinda wafalme wote wa kibinadamu] hapatikani na mauti.” (1 Timotheo 6:15, 16) Tayari akiwa amekwisha inuka akiwa Mfalme asiyeonekana katika mbingu, karibuni ataleta asubuhi ya ulimwengu mpya. Yeye ni nyota—mfalme—ambaye, kwa kuwa amekwisha inuka sasa, hataanguka kamwe!

[Picha katika ukurasa wa 14]

Afapo hata mfalme wa kibinadamu aliye bora zaidi huacha kazi yake katika mikono ya mtu asiyejulikana atakuwaje

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki