Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 11/8 kur. 8-10
  • Maisha Yaliyoharibiwa, Maisha Yaliyopotezwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maisha Yaliyoharibiwa, Maisha Yaliyopotezwa
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Kukwepa Uhalisi wa Mambo”
  • “Kujihusisha Sana na Dawa za Kulevya”
  • Kutoka Kuwa Mwashi Hadi Kuwa Mlanguzi wa Dawa za Kulevya
  • Pesa Zako na Uhai Wako!
  • Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?
    Amkeni!—1999
  • Jinsi Ambavyo Dawa za Kulevya Haramu Huathiri Maisha Yako
    Amkeni!—1999
  • Ni Nani Wanaotumia Dawa za Kulevya?
    Amkeni!—2001
  • Mbona Watu Hutumia Dawa za Kulevya?
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 11/8 kur. 8-10

Maisha Yaliyoharibiwa, Maisha Yaliyopotezwa

“DAWA za kulevya ni kama nyundo kubwa,” asema Dakt. Eric Nestler. Kwa kweli, kiasi kidogo cha kemikali hizo zilizo kama nyundo kubwa chaweza kufisha. “Kwa kielelezo, kokeini iliyosafishwa, imejulikana kuwa iliua watu mara ya kwanza walipoitumia,” chaeleza kitabu Drugs in America.

Dawa mpya za sanisia zaweza kutokeza hatari kubwa hivyo. “Vijana wanaoweza kudanganywa kwa urahisi ambao hununua dawa za kulevya kwenye karamu za ‘rave’ hawawezi kuwa na habari yoyote kuhusu jambo ambalo mchanganyiko wa kemikali utafanyia ubongo wao,” chaonya kichapo World Drug Report cha Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kwa vijana wengi uraibu wa dawa za kulevya hutukia hatua kwa hatua, kama ionyeshwavyo na mifano ifuatayo.

“Kukwepa Uhalisi wa Mambo”

Pedro,a mmojawapo wa watoto tisa, alizaliwa katika ujirani wenye jeuri katika jiji la Córdoba, Hispania. Hali yake ya utotoni ilikuwa yenye kufadhaisha kwa sababu ya uraibu wa alkoholi wa baba yake. Pedro alipokuwa na umri wa miaka 14, binamu yake alimzoeza kuvuta bangi. Baada ya mwezi mmoja akawa mraibu.

“Kutumia dawa za kulevya kulikuwa njia ya kupitisha wakati,” aeleza Pedro, “kukwepa uhalisi wa mambo, na njia moja ya kuwa mshiriki wa kikundi. Nilipokuwa na umri wa miaka 15, mbali na bangi nilianza kutumia LSD na amfetamini. Dawa ya kulevya niliyoipenda zaidi ilikuwa LSD, na ili kupata pesa za kuinunua, nikawa mwuzaji wa muda wa dawa za kulevya. Nililangua hasa bangi. Wakati mmoja, baada ya kutumia LSD kupita kiasi, sikuweza kulala usiku kucha, na nilihisi kana kwamba nilikuwa nimerukwa na akili. Jambo hilo liliniogofya. Nilihisi kwamba nikiendelea kutumia dawa za kulevya, ningeishia ama jela ama ningekufa. Lakini tamaa ya dawa za kulevya ilinifanya nipuuze hofu hiyo. Nikawa mraibu mkubwa sana wa LSD na kuhitaji dawa hiyo ya kulevya zaidi ili niwe katika hali ya kupumbaa. Licha ya matokeo yenye kuogopesha, sikuweza kuacha. Sikujua jinsi ya kuepuka hali hiyo.

“LSD haikuwa bei rahisi, kwa hiyo nilijifunza kuiba kwenye maduka ya kuuza vito, kuwanyang’anya watalii mikoba, na kuibia wapita njia saa na vibeti. Nilipofikia umri wa miaka 17, nilikuwa nimejiimarisha nikiwa muuzaji wa dawa za kulevya katika mji wa kwetu, na nyakati nyingine nilishiriki unyang’anyi wa kutumia silaha. Kwa sababu ya sifa ya kuwa mhalifu mwenye tabia mwitu katika ujirani wangu, nilipewa jina la utani el torcido, linalomaanisha ‘aliyepotoka.’

“Unapochanganya dawa za kulevya na vileo, utu wako hubadilika, mara nyingi unakuwa na tabia mwitu. Na tamaa ya kupata dawa za kulevya zaidi ni kubwa sana hivi kwamba inashinda kabisa dhamiri yako. Maisha yanakuwa na mabadiliko ya ghafula, na unaishi kwa kuduwazwa na dawa za kulevya.”

“Kujihusisha Sana na Dawa za Kulevya”

Ana mke wa Pedro, alikulia Hispania katika mazingira mazuri ya familia. Alipokuwa na umri wa miaka 14, Ana alikutana na wavulana wachache kutoka shule iliyokuwa karibu ambao walivuta bangi. Mwanzoni alichukizwa na tabia yao ya kiajabu-ajabu. Lakini Rosa mmojawapo wa marafiki wasichana wa Ana, alivutiwa na mmoja wa wavulana hao. Alimsadikisha Rosa kwamba kuvuta bangi hakungemdhuru na kwamba angefurahia kufanya hivyo. Kwa hiyo, Rosa alijaribu dawa hiyo ya kulevya na kumpa Ana.

“Ilinifanya nihisi vizuri, na baada ya majuma machache, nilikuwa nikivuta bangi kila siku,” asema Ana. “Baada ya mwezi mmoja hivi, bangi haikuniduwaza tena, kwa hiyo nikaanza kutumia amfetamini pamoja na kuvuta bangi.

“Punde si punde mimi na rafiki zangu tulikuwa tumejihusisha kabisa na dawa za kulevya. Tungezungumza kuhusu ni nani ambaye angetumia dawa za kulevya nyingi zaidi bila kupatwa na madhara yoyote na aliyelewa zaidi. Hatua kwa hatua, nilijitenga na watu kwa ujumla, na kwenda shuleni kwa nadra sana. Sikutosheka na bangi na amfetamini tena, kwa hiyo nilianza kujidunga sindano za dawa iliyotengenezwa kwa afyuni niliyoipata katika maduka mbalimbali ya kuuzia dawa. Wakati wa kiangazi tungeenda kwenye maonyesho ya roki, mahali ambapo ilikuwa rahisi daima kupata dawa za kulevya kama vile LSD.

“Siku moja mama alinishika nikivuta bangi. Wazazi wangu walifanya jitihada zote walizoweza ili kunilinda. Waliniambia kuhusu hatari za dawa za kulevya, na wakanihakikishia upendo na hangaiko lao. Lakini niliona jitihada zao kuwa zinaingilia maisha yangu isivyofaa. Nilipokuwa na umri wa miaka 16 niliamua kutoroka nyumbani. Nilijiunga na kikundi fulani cha vijana waliosafiri Hispania kote wakiuza mikufu ya kujitengenezea na kutumia dawa za kulevya. Miezi miwili baada ya hapo, nilikamatwa na polisi huko Málaga.

“Polisi waliponipeleka kwa wazazi wangu, walinipokea kwa moyo mkunjufu, na nikaaibika kwa yale niliyokuwa nimefanya. Baba yangu alikuwa akilia—jambo ambalo sikuwa nimewahi kuliona. Nilijuta kuumiza hisia zao, lakini majuto hayo hayakuwa makubwa vya kutosha kunifanya niache kutumia dawa za kulevya. Niliendelea kutumia dawa za kulevya kila siku. Nilipokuwa sijalewa, nyakati nyingine nilifikiri juu ya hatari hizo—lakini si kwa muda mrefu.”

Kutoka Kuwa Mwashi Hadi Kuwa Mlanguzi wa Dawa za Kulevya

José, mwanamume mwenye familia na mwenye urafiki, alilangua dawa za kulevya kutoka Morocco hadi Hispania kwa muda wa miaka mitano. Alipata kujihusishaje? “Nilipokuwa nikifanya kazi ya uashi, mfanyakazi mwenzi alianza kulangua dawa za kulevya,” aeleza José. “Kwa kuwa nilihitaji pesa, nilijiambia ‘Kwa nini nisifanye kazi hiyo?’

“Ilikuwa rahisi kununua bangi huko Morocco—nyingi kadiri ambavyo ningeweza. Nilikuwa na mashua ya kasi ambayo ingeweza kukwepa polisi kwa urahisi. Baada ya kusafirisha dawa za kulevya hadi Hispania, niliziuza kwa kiasi kikubwa, takriban kilogramu 600 kwa wakati mmoja. Nilikuwa na wateja watatu au wanne tu, na walichukua dawa zote za kulevya nilizoweza kuwaletea. Ijapokuwa polisi walifanya upelelezi, dawa hizo za kulevya hazikugunduliwa. Sisi walanguzi wa dawa za kulevya tulikuwa na vifaa bora zaidi kuliko polisi.

“Nilipata pesa nyingi sana kwa urahisi. Safari moja kutoka Hispania hadi Afrika Kaskazini ingeweza kuleta pesa zipatazo dola za Marekani 25,000 hadi 30,000. Punde si punde, nilikuwa na wanaume 30 wa kunifanyia kazi. Sikuwahi kukamatwa kwa sababu nilimlipa mtoa habari mmoja ili kunishauri nilipokuwa ninasakwa.

“Nyakati fulani nilifikiri kuhusu mambo ambayo dawa hizi za kulevya zingeweza kuwafanyia wengine, lakini nilijifariji kwamba bangi ni dawa ya kulevya ambayo si kali na isiyoua mtu yeyote. Kwa kuwa nilikuwa nikipata pesa nyingi, sikufikiri sana juu ya hilo. Mimi mwenyewe sikuwa nikitumia dawa za kulevya kamwe.”

Pesa Zako na Uhai Wako!

Kama ionyeshwavyo na mifano hiyo, dawa za kulevya zinadhibiti maisha ya watu. Mara tu unapokuwa mraibu, kujiponyoa huwa jambo gumu na lenye kufadhaisha. Kama kisemavyo kitabu Drugs in America, “katika sehemu za Magharibi mwa Marekani, magaidi walielekezea watu bunduki zao kwenye nyuso na kudai, ‘Pesa zako au uhai wako.’ Dawa za kulevya haramu ni mbaya zaidi kuliko waasi wa kale. Hudai vyote viwili.”

Je, kuna kitu chochote kinachoweza kukomesha tatizo lisilozuilika la dawa za kulevya? Makala ifuatayo itachunguza baadhi ya utatuzi.

[Maelezo ya Chini]

a Baadhi ya majina katika mfululizo huu wa makala yamebadilishwa.

[Blabu katika ukurasa wa 8]

“Katika sehemu za Magharibi mwa Marekani, magaidi walielekezea watu bunduki zao kwenye nyuso na kudai, ‘Pesa zako au uhai wako.’ Dawa za kulevya haramu ni mbaya zaidi kuliko waasi wa kale. HUDAI VYOTE VIWILI”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

JE, MTOTO WAKO ATAKATAA DAWA ZA KULEVYA?

NI MATINEJA GANI WANAOWEZA KUWA HATARINI ZAIDI?

a. Wale wanaotaka kuonyesha kwamba wanajitegemea na wako tayari kukabili hatari zozote.

b. Wale wasiopendezwa sana na miradi ya masomo au ya kiroho.

c. Wale wasiopatana na jamii.

d. Wale wasiofahamu waziwazi lililo sawa na lililo baya.

e. Wale wanaoona kwamba wazazi wao hawawategemezi na ambao hutiwa moyo na rafiki zao watumie dawa za kulevya. Wachunguzi wameona kwamba “ubora wa uhusiano wa kijana mbalehe pamoja na wazazi wake waonekana kuwa ulinzi bora zaidi dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.”—Italiki zimeongezwa.

UNAWEZA KUWALINDAJE WATOTO WAKO?

a. Kwa kuwa na uhusiano wa karibu na mawasiliano mazuri pamoja nao.

b. Kwa kuwaelewesha waziwazi lililo sawa na lililo baya.

c. Kwa kuwasaidia wawe na miradi hususa.

d. Kwa kuwafanya wahisi kwamba wao ni sehemu ya familia yenye upendo na jumuiya yenye uchangamfu.

e. Kwa kuwafundisha juu ya hatari za matumizi mabaya ya dawa za kulevya. Watoto wanahitaji kujua waziwazi kwa nini wanapaswa kukataa dawa za kulevya.

[Hisani]

Chanzo: United Nations World Drug Report

[Picha katika ukurasa wa 9]

Dawa za kulevya zilizonaswa huko Gibraltar

[Hisani]

Courtesy of Gibraltar Police

[Picha katika ukurasa wa 10]

Nilikuwa na mashua ya kasi kama hii, ambayo ingeweza kukwepa polisi kwa urahisi

[Hisani]

Courtesy of Gibraltar Police

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]

Godo-Foto

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki