Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 11/8 kur. 11-14
  • Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kupambana na Ugavi
  • Je, Mahitaji ya Dawa za Kulevya Yaweza Kupunguzwa?
  • Yale Ambayo Mashahidi wa Yehova Wamefanya
  • Tumaini na Kusudi Halisi
  • Kutoka Kuwa Mlanguzi wa Dawa za Kulevya Hadi Kuwa Mwashi
  • Suluhisho la Tufeni Pote Litakalofaulu
  • Je, Unahitaji Msaada?
  • Jinsi Ambavyo Dawa za Kulevya Haramu Huathiri Maisha Yako
    Amkeni!—1999
  • Maisha Yaliyoharibiwa, Maisha Yaliyopotezwa
    Amkeni!—1999
  • Mbona Watu Hutumia Dawa za Kulevya?
    Amkeni!—2001
  • Kuufanya Ulimwengu Uwe na Uraibu wa Dawa za Kulevya
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 11/8 kur. 11-14

Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?

KUSHINDA vita dhidi ya dawa za kulevya ni mradi wa kusifika, lakini si jambo rahisi. Mambo mawili ndiyo huchochea biashara haramu ya dawa za kulevya—ugavi na mahitaji. Kwa muda upatao nusu karne, serikali na polisi wamejitahidi kupunguza ugavi huo. Dhana yao ilikuwa sahili: Bila dawa za kulevya, hakutakuwa na waraibu.

Kupambana na Ugavi

Ili kutimiza kusudi hilo, vikosi vya polisi wa kupambana na dawa za kulevya, wamenasa mizigo ya dawa za kulevya, na ushirikiano wa kimataifa umefanya walanguzi mashuhuri wa dawa za kulevya watiwe kizuizini. Lakini ukweli mchungu ni kwamba ingawa uangalizi wenye matokeo waweza kuwalazimisha walanguzi wa dawa za kulevya wahamie kwingineko, watafute masoko mengine, au wawe werevu zaidi, hauwazuii. “Hatutawahi kupambana kwa mafanikio na wauzaji wa dawa za kulevya maadamu wao wana pesa za kutosha nasi lazima tujitahidi kupata pesa kutoka kwa bajeti ya taifa,” akakiri mtaalamu mmoja wa mihadarati.

Joe de la Rosa, ofisa wa kuzuia uhalifu wa Polisi wa Gibraltar, alizungumza na Amkeni! kuhusu ugumu wa kudhibiti ulanguzi wa dawa za kulevya kati ya Afrika na Peninsula ya Iberia. “Mnamo mwaka wa 1997 tulinasa kilogramu 400 za bangi ya sanisia,” akasema. “Kwa kweli nyingi yake haikunaswa kutoka kwa walanguzi wa dawa za kulevya; ilipatikana ikielea baharini au imebebwa kwenye fuo za bahari. Jambo hilo lakupa wazo fulani kuhusu kiasi cha dawa za kulevya kinachovuka Mlango Bahari wa Gibraltar kila mwaka. Kiasi tunachonasa ni kidogo sana kwa kuzingatia kiasi kinachoingizwa. Wasafirishaji ambao hufunga safari hizo kutoka Afrika hadi Hispania wana mashua za kasi zinazokimbia zaidi ya mashua za maofisa wa forodha. Na wahisipo kwamba wako hatarini ya kukamatwa, wanatupa tu dawa hizo za kulevya baharini, kwa hiyo tunakosa uthibitisho wa kuwashtaki.”

Polisi hukabili matatizo kama hayo katika sehemu nyingine za ulimwengu. Wasafiri wanaoonekana kuwa wa kawaida, ndege ndogo, meli za kubebea kontena, na hata nyambizi hulangua dawa za kulevya kwenye bahari au kupita kwenye mipaka inayoweza kuvukwa. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa ilipiga hesabu kwamba “angalau asilimia 75 ya dawa za kulevya zinazosafirishwa kati ya mataifa yote zitahitaji kuzuiwa ili kupunguza kwa kiasi kikubwa faida inayotokana na ulanguzi wa dawa za kulevya.” Kwa wakati uliopo, kiwango cha kuzizuia labda hakizidi asilimia 30 kuhusu kokeini—na kuhusu dawa nyingine za kulevya ni kidogo zaidi ya hicho.

Kwa hiyo kwa nini serikali isishambulie chanzo cha tatizo hilo na kuharibu mimea yote ya bangi, mipopi ya kasumba, na mimea ya koka? Hivi majuzi Umoja wa Mataifa ulipendekeza hatua hiyo, lakini si hatua rahisi. Bangi yaweza kukuzwa karibu katika shamba lolote. Sehemu moja kuu ambapo koka hukuzwa huko Andes iko mahali panapoelezwa kuwa pako “nje ya udhibiti wa serikali.” Hali kama hizo ziko katika maeneo ya mbali ya Afghanistan na Burma, ambayo ni maeneo makuu ya kasumba na heroini.

Jambo linalotatanisha hata zaidi ni kwamba walanguzi wa dawa za kulevya wanaweza kubadilika kwa urahisi na kuanza kutumia dawa za kubuniwa ambazo uhitaji wake unazidi kuongezeka. Na maabara za siri zinaweza kutengeneza dawa hizi za sanisia karibu kila mahali ulimwenguni.

Je, uangalizi wenye matokeo zaidi na vifungo vya gereza vikali zaidi vingeweza kupunguza biashara ya dawa za kulevya? Kuna watumiaji wengi sana wa dawa za kulevya, waraibu wengi, na polisi wachache kuwezesha njia hiyo ifanikiwe. Kwa mfano, nchi ya Marekani, ina wafungwa wapatao milioni mbili—wengi wao walifungwa kwa sababu ya makosa yanayohusisha dawa za kulevya. Lakini hofu ya kufungwa gerezani haijazuia watu kutumia dawa za kulevya. Katika nchi nyingi zinazositawi ambapo mauzo ya dawa za kulevya yanaongezeka haraka, polisi wachache sana wasiolipwa mshahara wa kutosha hujikuta hawana nguvu za kuzuia zoea hilo.

Je, Mahitaji ya Dawa za Kulevya Yaweza Kupunguzwa?

Ikiwa jitihada za kupunguza ugavi wa dawa za kulevya zimekosa kufua dafu, vipi juu ya kupunguza mahitaji? “Vita vinavyohusu dawa za kulevya kwa kweli ni pambano la moyoni na akilini, na si suala tu la polisi na mahakama na magereza,” lasema gazeti Time.

Joe de la Rosa, aliyenukuliwa mapema, hali kadhalika aamini kwamba elimu ndiyo njia pekee ya kupambana na dawa haramu za kulevya. “Uraibu wa dawa za kulevya ni tatizo la jamii linalosababishwa na jamii, kwa hiyo tunahitaji kubadili jamii au angalau kubadili njia ya watu ya kufikiri,” asema. “Tunajaribu kuhusisha shule, wazazi, na walimu ili wote wafahamu kwamba kuna hatari, kwamba dawa za kulevya zinapatikana, na kwamba watoto wao wangeweza kuathiriwa.”

Yale Ambayo Mashahidi wa Yehova Wamefanya

Kwa miaka mingi Mashahidi wa Yehova wamejihusisha kwa bidii kuelimisha watu waepuke dawa za kulevya. Wametayarisha habari iliyokusudiwa kusaidia wazazi wawafundishe watoto wao kuhusu hatari za dawa za kulevya.a Zaidi ya hayo, huduma yao imefaulu kusaidia watumiaji na walanguzi wengi wa dawa za kulevya waishi maisha ya kawaida.

Ana, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, alijulishwa kwa Mashahidi wa Yehova kwa sababu dada yake alikuwa amesikia jinsi walivyofanikiwa kusaidia waraibu wa dawa za kulevya. Ana hakupendezwa na Biblia haswa, lakini alienda kwa kusitasita kwenye kusanyiko moja lililofanywa na Mashahidi wa Yehova. Akiwa huko alimwona mwanamume mmoja aliyekuwa mtumiaji sugu wa dawa za kulevya lakini ambaye alikuwa amebadili sura yake na mtindo wake wa maisha. “Nilifikiri kwamba ikiwa angeweza kubadilika, mimi pia ningeweza,” asema Ana. “Badiliko alilofanya lilinisadikisha kwamba nilipaswa kukubali funzo la Biblia.

“Tangu nilipoanza funzo la Biblia mara ya kwanza, niliamua kukaa nyumbani, kwa kuwa nilijua kwamba ikiwa ningeondoka nyumbani, ningekutana na watumiaji wengine wa dawa za kulevya na kuanza kutumia dawa za kulevya tena. Tayari nilijua kwamba dawa za kulevya zilikuwa mbaya na kwamba Mungu hakukubali zoea hilo. Pia nilikuwa nimeona madhara yanayowapata watu wanaotumia dawa za kulevya na madhara niliyokuwa nimesababishia familia yangu. Lakini nilihitaji nguvu za kiroho ili kujiondoa katika utumwa wa dawa za kulevya. Lilikuwa jambo gumu kuondoa sumu hiyo. Kwa muda fulani nililala mchana kutwa huku matokeo ya dawa za kulevya yakipungua. Lakini jitihada nilizofanya zilifaa.”

Tumaini na Kusudi Halisi

Mume wa Ana, Pedro, aliyetajwa pia katika makala iliyotangulia, alijiponyoa kwa njia hiyo hiyo. “Siku moja nilipokuwa nikivuta bangi katika nyumba ya ndugu yangu, niliona kitabu chenye kichwa kilichonivutia,” akumbuka Pedro. “Kilikuwa na kichwa Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele. Nilienda nacho nyumbani, nikakisoma, na kuyachunguza maandiko. Nilikuwa na hakika kwamba nimepata kweli.

“Kusoma Biblia na kuzungumza na wengine kuhusu yale niliyokuwa nikijifunza kulinifanya nihisi vizuri zaidi na kupunguza tamaa ya dawa za kulevya. Nikaamua sitaendelea na mpango wangu wa kuiba kwenye kituo cha petroli kwa kutumia silaha. Rafiki mmoja alikuwa akijifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, na punde si punde nikaiga kielelezo chake. Katika muda wa miezi tisa nilibadili mtindo wangu wa maisha na kubatizwa. Katika pindi hiyo, marafiki wengi wa zamani walinipa dawa za kulevya, lakini nilianza kuzungumza nao juu ya Biblia mara moja. Baadhi yao waliitikia kwa njia ifaayo. Mmoja wao hata alifaulu kuacha uraibu wake.

“Ili kuvunja zoea la uraibu wa dawa za kulevya, unahitaji kuwa na tumaini. Biblia ilinipa tumaini hilo, ilinipa kusudi maishani, na kunionyesha waziwazi maoni ya Mungu juu ya dawa za kulevya na jeuri. Niliona kwamba nilihisi vizuri zaidi nilipokuwa nikijifunza juu ya Mweza Yote—na hakukuwa na madhara yoyote. Baadaye, kushirikiana na watu wanaoishi maisha safi kwenye mikutano ya Mashahidi wa Yehova kulinisaidia nifuatie mwendo huo.”

Kutoka Kuwa Mlanguzi wa Dawa za Kulevya Hadi Kuwa Mwashi

José, mlanguzi wa dawa za kulevya aliyetajwa katika makala iliyotangulia, sasa ni mwashi kwa mara nyingine tena. Haikuwa rahisi kwa upande wake kuacha biashara yenye faida. “Dawa za kulevya hukuletea pesa nyingi sana,” akiri hivyo, “lakini si njia nzuri ya kuchuma pesa. Nawaona vijana wakiwa na bastola na magari yenye kuvutia sana. Familia huvunjika, uhalifu umeenea mitaani pote, na waraibu wengi wa dawa za kulevya huvunja magari, huiba madukani au kunyang’anya watu ili wapate pesa za dawa za kulevya. Wengi huanza na bangi, kisha ecstasy au tembe nyingine, na kisha hujaribu kokeini au hata heroini. Natambua kwamba nilihusika kuingiza wengi katika zoea hilo.

“Kadiri nilivyojifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova, nilizidi kusadiki kwamba ni vibaya kujihusisha na dawa za kulevya. Nilitaka kuwa na dhamiri safi, na mke wangu, ambaye pia alikuwa akijifunza, alitamani dhamiri safi. Bila shaka ni vigumu kuacha kulangua dawa za kulevya. Niliwaeleza wateja wangu na walanguzi wengine kwamba nilikuwa nikijifunza Biblia na nilikuwa nimeacha biashara ya dawa za kulevya. Mwanzoni, hawakuniamini, na hata kufikia sasa wengine bado hawaniamini. Hata hivyo, niliacha karibu miaka miwili iliyopita, na sijajutia hilo kamwe.

“Tangu mwaka uliopita, nimekuwa nikifanya kazi ya uashi ambayo nimesomea. Sasa kwa mwezi mmoja mimi hupata robo ya pesa nilizopata kwa siku moja nikiwa mwuzaji wa dawa za kulevya. Lakini hiyo ni njia bora ya maisha, nami nina furaha zaidi.”

Suluhisho la Tufeni Pote Litakalofaulu

Walanguzi wachache wa dawa za kulevya wenye moyo mkuu wameacha biashara ya dawa za kulevya. Na njia mbalimbali za kufanya watumiaji wa dawa za kulevya waishi maisha ya kawaida zimewasaidia washinde uraibu wao. Lakini, kama kikirivyo kitabu World Drug Report, “kwa watumiaji wa dawa za kulevya wa muda mrefu, kujiepusha nazo kwa muda mrefu si jambo la kawaida.” Kwa kusikitisha, kwa kila mraibu anayesaidiwa kuishi maisha ya kawaida, watu wapya kadhaa hunaswa kwenye zoea hilo. Ugavi na mahitaji yanazidi kuongezeka.

Ikiwa vita dhidi ya dawa za kulevya itashinda, lazima kuwe na suluhisho la tufeni pote kwa sababu tatizo hilo tayari ni la tufeni pote. Kwa habari hii, Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulika na Dawa za Kulevya yasema: “Ingawa matumizi mabaya ya dawa za kulevya, ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu unaohusiana na tatizo la dawa za kulevya katika nchi nyingi yalionwa kuwa vitisho vikuu kwa usalama, umma haukufahamu uhakika wa kwamba dawa haramu za kulevya zilikuwa tatizo la tufeni pote ambalo halingeweza kutatuliwa tena na jitihada za kitaifa peke yake.”

Lakini je, serikali za ulimwengu zitaungana ili kuondoa pigo hilo la tufeni pote? Kufikia sasa matokeo yaliyopatikana hayatii moyo. Hata hivyo, Biblia inaelekeza kwenye serikali ya kimbingu itakayovuka mipaka yote ya kitaifa kuwa suluhisho la mwisho. Biblia inatuhakikishia kwamba Ufalme wa Mungu, unaotawalwa na Yesu Kristo, utadumu “milele na milele.” (Ufunuo 11:15) Kwa sababu hiyo, chini ya Ufalme wa Mungu, elimu ya kimungu itahakikisha kwamba hakutakuwa na mahitaji ya dawa za kulevya. (Isaya 54:13) Na matatizo ya kijamii na ya kihisia-moyo ambayo huwafanya watu washindwe na tamaa ya kutumia dawa za kulevya, yatatoweka milele.—Zaburi 55:22; 72:12; Mika 4:4.

Je, Unahitaji Msaada?

Hata sasa, tumaini katika Ufalme wa Mungu mikononi mwa Kristo linawachochea watu wakatae dawa za kulevya. Ikiwa ungependa habari zaidi, tafadhali wasiliana na Mashahidi wa Yehova katika eneo lako.

[Maelezo ya Chini]

a Ona sura ya 34 ya kitabu Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, yenye kichwa “Kwa Nini Ukatae Madawa ya Kulevya?,” kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 11]

Kukamatwa kwa watumiaji wa dawa za kulevya

[Hisani]

K. Sklute/SuperStock

[Picha katika ukurasa wa 12]

Pedro na mke wake, Ana, wakijifunza Biblia pamoja na watoto wao

[Picha katika ukurasa wa 13]

Pedro akiweka vifaa vya ulinzi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki