Mjue “Wolfhound” wa Ireland
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA IRELAND
“Jitu pole kati ya mbwa wote.”
Hayo yalikuwa baadhi ya maelezo kumhusu wolfhound wa Ireland. Je, umeshawahi kumwona yeyote? Ni kweli kwamba mbwa-mwitu hawapatikani Ireland leo. Lakini walikuwako. Kulikuweko pia nguruwe-dume na kulungu wakubwa. Inasemekana kwamba mbwa-mwitu wa mwisho huko Ireland aliuawa yapata miaka mia mbili iliyopita. Kabla ya hapo, wolfhound walikuwa maarufu kwa kuwinda mbwa-mwitu na vilevile wanyama wengine wakubwa. Kuna simulizi moja la hivi karibuni juu ya wolfhound mmoja aliyepelekwa kwenye Milima ya Rocky, huko Marekani. Simulizi hilo husema kwamba mnamo mwaka wa 1892, “akiwa peke yake aliua mbwa-mwitu arobaini wakati mmoja wa majira ya baridi kali.” Ingawa hivyo, usiwe na wasiwasi. Mbwa wolfhound hawawindi wala kuua watu!
KULINGANA na wanahistoria fulani, huenda wolfhound walikuwako kwa wingi huko Ireland mwaka wa 500 K.W.K. Baadaye Wacelt walitumia wolfhound kwa kazi nyingine mbali na kuwinda. Hekaya na historia pia husema kwamba wafalme na mashujaa wa Ireland walitumia mbwa hao vitani.
Sifa za wolfhound akiwa mbwa wa pekee sana zilienea kotekote ulimwenguni. Mbwa wolfhound walipelekwa pia katika viwanja vya maonyesho huko Roma. Rekodi ya balozi Mroma anayeitwa Quintus Aurelius Symmachus huonyesha kwamba mnamo mwaka wa 393 W.K. alimwandikia ndugu yake barua akimshukuru kwa kupeleka wolfhound saba wa Ireland huko Roma. Yaonekana kwamba mbwa hao waliwasisimua sana Waroma. “Waroma wote waliwastaajabia,” akaandika Symmachus, “ijapokuwa walipendwa sana walihitaji kusafirishwa wakiwa katika vizimba vya chuma.”
Huenda ukubwa wa mbwa hao uliwafanya watu waone kwamba walihitaji kuletwa wakiwa katika vizimba vya chuma. Mbwa wa kiume hufikia kimo cha sentimeta 86 hivi kufikia mabegani, lakini wengine ni wakubwa zaidi. Mbwa wolfhound mkubwa zaidi aliyepata kuwako alikuwa na kimo cha meta moja kufikia mabegani. Kwa kawaida mbwa wa kike huwa na kimo kinachopungua inchi moja au mbili ya kile cha mbwa wa kiume. Urefu huo huwawezesha kupata chakula zaidi kwa urahisi. Mwandishi wa riwaya wa Scotland Bwana Walter Scott alimwonya mmoja wa marafiki wake awe mwangalifu wakati wa chakula cha jioni. La sivyo, wolfhound wake, aliyekuwa na “urefu wa meta mbili hivi kutoka kwa ncha ya pua yake hadi kwa mkia wake,” angekula “chakula kutoka kwa sahani yake bila uhitaji wa kuegemea mezani au kitini.”
Mbwa hao huwa wadogo wanapozaliwa—wakiwa na uzito wa kilogramu 0.7 tu—lakini wanakua kwa haraka sana. Mmiliki mmoja mwenye kuwaonea fahari alisema kwamba vitoto vya mbwa hao “ni viumbe vidogo vyenye kuvutia sana” lakini hubadilika “ghafula kutoka kuwa vitoto vifupi vinene hadi kuwa viumbe virefu, vyenye upole vikiwa hasa na miguu mirefu.”
Hawabweki sana. Kwa asili wao ni mbwa wenye nguvu, walio kimya. Lakini wanapobweka, wanatoa sauti isiyosahaulika. Watu husimulia juu ya mtu fulani aliyesikia mbweko wa wolfhound akasema kwamba ulikuwa “mbweko mzito uliojaa kihoro [aliowahi] kusikia.”
Mbwa wolfhound wa Ireland ameelezwa kuwa “aonekanaye kuwa mkali, mwenye macho makali, nyusi za matimumatimu, na ngozi isiyo laini ya rangi ya kijivu iliyokoza”—mbwa ambaye huenda ukataka kumwepuka ukutanapo naye mara ya kwanza. Lakini imesemwa pia kwamba wao ni “wenye fadhili sana hivi kwamba mtoto aweza kucheza nao.” Ni kama alivyosema mmiliki mmoja mwenye ujuzi, kwamba kwa kweli, ni wenye “urafiki sana.” Si wa rangi ya kijivu tu. Baadhi yao wana ngozi ya rangi nyeupe, ya ngano, nyekundu, au nyeusi.
Mwandishi maarufu wa Ireland Oliver Goldsmith aliwasifu sana. “Mbwa Wolf wa Ireland aliye mashuhuri, “ yeye akasema, “ni mzuri sana na mwenye fahari ajabu . . . , ni mbwa bora zaidi ya wote ulimwenguni.” Bila shaka alivutiwa sana na umbo lao zuri la matimutimu, kutia ndani nyusi, kope, na masharubu zinazowafanya wawe na ile inayoitwa “sura halisi ya Ireland.”
Lakini basi, mbona jamii hiyo ya mbwa ikakaribia kutoweka? Sababu moja ilikuwa umaarufu wao. Wapenzi wa mbwa hao waliwaona kuwa zawadi yenye thamani ambayo ingeweza kutolewa kwa watu mashuhuri kama wafalme. Kwa hiyo “walitafutwa na kupelekwa nchi za ng’ambo kotekote ulimwenguni.” Kama tokeo, walitawanyika katika vikundi vidogo-vidogo kila mahali. Mbali na hivyo, mara baada ya umuhimu wao kwisha wakiwa wawindaji mbwa-mwitu, jamii hiyo ya mbwa ilipuuzwa katika Ireland.
Mnamo 1839, mpenzi mmoja wa wolfhound alieleza hivi juu ya hali hiyo ya kuhuzunisha: “Ni jambo la kusikitisha sana kwamba jamii hii bora ya mbwa inatoweka kwa kasi sana, na bila shaka itatoweka kabisa baada ya miaka michache tusipofanya jitihada fulani ya pekee.” Idadi yao ilikuwa ndogo sana hivi kwamba watu wengi walidai kuwa wolfhound waliyemmiliki alikuwa “wa mwisho katika jamii yake.” Lakini waliokoka.
Waliokolewa na “jitihada ya pekee” ya watu kama vile George A. Graham. Mnamo 1862 alihangaikia hali yao mbaya. Alikusanya wolfhound wengi sana waliobaki ambao aliweza kupata. Kwa kuwazalisha kwa uangalifu, aliandaa msingi uliohitajiwa ili kuweza kuwarudisha katika hali yao ya leo. Pasipo jitihada zake, akasema mwanahistoria mmoja katika mwaka wa 1893, “mbwa waliosalia wa jamii hiyo mashuhuri wangelikuwa wametoweka kabisa leo.”
Mpenzi mmoja aliye mzalishaji mwenye kuheshimika wa wolfhound wa Ireland, Phyllis Gardner, aliandika: “Hakuna kitu hakika ulimwenguni, lakini, bila kutaja misiba yaonekana ni kana kwamba jamii hii mashuhuri imeokolewa kutoka kwa hatari ya kutoweka kabisa, na ingali inazidi kupendwa na wengi.”
[Picha katika ukurasa wa 23]
Vitoto vya “wolfhound,” vyenye umri wa majuma manne
[Picha katika ukurasa wa 23]
“Wolfhound” mpole, katika Newtownards, Ireland Kaskazini