Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 9/8 kur. 24-27
  • Kiumbe Mwepaji—Mchukiwa Tena Mpendwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kiumbe Mwepaji—Mchukiwa Tena Mpendwa
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mchukiwa Tena Mpendwa
  • Kuwinda Wakiwa Vikundi-Vikundi
  • Uwasiliano wa Mbwa-Mwitu
  • Kiumbe Mzuri
  • Kuacha Asili Ijirekebishie Mambo
  • Wakati Ujao wa Mbwa-Mwitu
  • Kuishi Katika Amani
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Kwa Nini Kuna Maonyo Mengi Bandia?
    Amkeni!—1993
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1995
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 9/8 kur. 24-27

Kiumbe Mwepaji—Mchukiwa Tena Mpendwa

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA KANADA

CANIS LUPUS. Yule pale juu ya ukingo mrefu wa miamba-miamba, aonekana kiwiliwili tu gizani kwa kumulikwa na nuru ya mwezi, ameinua kichwa, mkia wa manyoya mengi u kati ya miguu yake, masikio yamerudishwa nyuma, kinywa ki wazi—mlio wake mrefu unapenya anga la usiku.[1] Naam, kule kuufikiria tu mlio wake mrefu huleta mitetemo ya hofu na msisimko!

NI WATU wachache wamepata pendeleo la kuona kiumbe huyu mzuri lakini mwepaji—ambaye sanasana huitwa mbwa-mwitu wa kijivu au mbwa-mwitu wa mitini—akiwa mwituni.[2] Hata hivyo, mnyama huyu wa kuvutia hukumbusha mtu taswira nyingi mbalimbali.

Mchukiwa Tena Mpendwa

Vyovyote vile adhaniwavyo, neno “mbwa-mwitu” huchochea sana hisiamoyo za watu. Yeye amekuwa akieleweka vibaya, akionewa, na kuhofiwa. Watu fulani humdharau mbwa-mwitu kwa sababu ni mnyafuaji. Mbwa-mwitu wameudhiudhi wenye-shamba na wenye-mifugo kwa kunyemelea kondoo, ng’ombe, na mifugo wengine. Hekaya na ngano zimechangia sifa yake mbaya. Nani hajasikia zile semi za “mbwa-mwitu katika vazi la kondoo” na “kumzuia mbwa-mwitu mlangoni”? Hadithi humsimulia kuwa “Jibwa-Mwitu Baya.” Hadithi moja ya jinsi hiyo hueleza juu ya mbwa-mwitu akitisha kula msichana mdogo.[3] Hii imewapa watu wazo la kwamba mbwa-mwitu hushambulia watu.

Hata hivyo, wanasayansi na wanabiolojia huwaona mbwa-mwitu vingine.[4] Wao huwachukua kuwa viumbe wenye haya mno wajaribuo kuepuka wanadamu iwezekanavyo.[5] Hakika, kulingana na makala ya majuzi iliyotokea katika gazeti GEO, kwa kweli mbwa-mwitu huhofu mwanadamu.[7] Mbwa-mwitu wajapokuwa na sura kali, haionekani kuna msingi wa kuamini kwamba mbwa-mwitu wenye afya wa Amerika Kaskazini ni hatari kwa mwanadamu.[6]

Mwanabiolojia Paul Paquet, ambaye amefanya utafiti mwingi wa mbwa-mwitu, akiri kwamba awapenda viumbe-mwitu hawa tangu utoto wake. Ameandika baadhi ya maono yake. Adai ameona mbwa-mwitu mara nyingi wakionyesha furaha, upweke, na ucheshi. Wakati mmoja aliona mbwa-mwitu mzee aliyelemaa asiweze tena kuwinda akiletewa chakula na wanakundi wengine. Hata ingawa mbwa-mwitu huyo alikuwa amechakaa umri, bado kundi hilo lilithamini uhai wake likawa likitunza uhai wake.[8] Hata hivyo, tabia hii ya kuwinda kwa kikundi imeelekea kuwatokomeza kabisa.

Kuwinda Wakiwa Vikundi-Vikundi

Kuwinda wakiwa vikundi-vikundi ndiyo jinsi ya mbwa-mwitu ya kutosheleza njaa yao na kulisha watoto wao.[9] Ingawa hivyo, lazima itambuliwe kwamba ni tatizo lenye kuwaudhi wenye-shamba kwa kondoo na ng’ombe kuuawa na mbwa-mwitu. Akiwa mnyafuaji mwenye mwono mzuri sana, hisi ya kunusa kwa urahisi, usikizi mzuri, na umo hodari isivyoaminika—na pia mwenye umbo lifaalo kukimbia na kurukaruka—mbwa-mwitu afaa sana kwa kuwinda. Pia ni mtegea-nasibu. Ungekuwa upumbavu kufikiri kiumbe mjanja huyu angeacha aponyokwe na windo lolote lipatikanalo rahisi awezalo kushika au kudakia—hasa kondoo wakubwa wanono na ng’ombe.[11] Ingeweza kusemwa kwamba mbwa-mwitu “hunufaisha” windo lao mwituni kwa kuua mawindo rahisi zaidi, wasio na afya na walio wanyonge kwa kupunguza idadi isiyotakikana, hivyo wakiwaachia chakula kingi zaidi wale wenye afya.[12]

Uwasiliano wa Mbwa-Mwitu

Namna gani ule mlio mrefu wa kuogofya usikikao mbali na kumwogopesha msikilizaji? Kwa mbwa-mwitu hii ni starehe ya kirafiki tu—namna ya uwasiliano. Mbwa-mwitu ambaye ametengeka mawindoni huenda akapanda kigongo cha ardhi na kuwatolea mlio mrefu wanakundi wengineo.[13] Au huenda mlio mrefu ukatumiwa kueleza eneo alipo. Nyakati fulani mbwa-mwitu huelekea kutoa mlio mrefu kuonyesha furaha tu.[14] Kundi likutanapo ili kutoa mlio mrefu, ungekaribia kufikiri wanafurahia hafla ya nyimbo. Ingesikika vizuri zaidi kama wangeimba kwa upatani, lakini wao huonekana kila mmoja akipendelea mgambo wake.[15] Bila shaka wana njia nyingine ya kuwasiliana pia. Kuna zile ambazo zimesemwa kuwa ni kulialia kwikwi, kukoroma, kubweka, kulia kwichikwichi, na kulia ng’wing’wi kwa vijibwa-mwitu kipangoni.[16] Pia uwasiliano wa msimamo hutumiwa kuhakikisha cheo cha kijamii na ufungamano miongoni mwa lile kundi.[17]

Kiumbe Mzuri

Mtazame kwa ukaribu kiumbe huyu mzuri ajabu. Angalia manyoya yaliyomfunika ya kijivu hasa (mengine huwa ya rangi nyeusi-nzito), yaliyochanganyika na manyoya meupe, meusi na kahawia.[18] Angalia sana macho yake maangavu ya manjano yaliyokodolewa kwa kupenya. [19]Chunguza alama zake za usoni. Zote hizi humfanya mbwa-mwitu mnyama wa kuvutia sana. Hata hivyo, mahangaiko yanatamkwa juu ya wakati wake ujao. Je, kuna sababu ya kuhangaika?

Ni kwamba, ile kawaida iliyokuwako sehemu kubwa ya Ulaya, Asia, na Amerika Kaskazini—kuona mbwa-mwitu—sasa ni nadra katika Kanada, Alaska, na mikoa isiyo na watu wengi ya Marekani, Ulaya, na Urusi. Watu wanasema lazima watafutie mbwa-mwitu fulani nafasi katika mbuga teule. Kwa kuwa wanadamu wamejifunza kuishi na wanyafuaji kama tai, dubu, na simba-milima, kuna wale wanaouliza, “Mbona tusiishi na mbwa-mwitu pia?”

Kuacha Asili Ijirekebishie Mambo

Jawabu ni kulinda, si kuondolea mbali wala kudhibiti. Sasa mbuga zaonwa kuwa maeneo salama kwa wanyama, si pori zilizohifadhiwa kustarehesha watu tu. Kulingana na gazeti Canadian Geographic, wasimamizi wa mbuga wangependa kuona mfumo-mazingira wenye kujirekebisha wenyewe kiasili. Baada ya yule mnyafuaji mkuu, mbwa-mwitu, kutokuwa kwenye Mbuga ya Kitaifa ya Banff, Kanada kwa miaka 40, alijirudisha mwenyewe miaka ya 1980 kwenye milima Rocky ya kusini—idadi ikiwa 65 tu, lakini tukio lenye dalili nzuri kwa maoni ya wengi.[20] Ufaransa yaripoti kurudi kwa mbwa-mwitu baada ya kutokuwako kwa miaka 50.a Katika Italia pia mbwa-mwitu anarudi na aweza kusikika akitoa mlio mrefu kule Tivoli, karibu na Roma.[21]

Kuna ufikirio wa kurudisha katika Mbuga ya Kitaifa ya Yellowstone, Marekani, jamii ya mbwa-mwitu iliyo katika hatari ya kutokomezwa. Mbwa-mwitu walikuwa sehemu ya mfumo wa kiasili wa mkoa huo zaidi ya miaka 40 iliyopita, kabla hawajamalizwa. Sasa watu wengi, hasa wageni wa mbuga, wataka warudi. Hata hivyo, biashara ya mifugo inahangaika sana juu ya kurudishwa kwa mbwa-mwitu katika eneo lao. “Mbwa-mwitu warudishwapo Yellowstone, itakuwa lazima kuwasimamia mbwa-mwitu nje ya mbuga hiyo,” asema mwanabiolojia wa mbwa-mwitu L. David Mech.[22]

Wakati ujao utakuwaje kwa kiumbe huyu aishiye katika ulimwengu usioeleweka sana na wanadamu?

Wakati Ujao wa Mbwa-Mwitu

Idadi ya watu wanaounga mkono kurudishwa kwa mnyama ambaye imekuwa shida kuvumiliwa na wanadamu muda mrefu sana yaonyesha badiliko la mtazamo. Kitabu The Wolf—The Ecology and Behavior of an Endangered Species chataarifu: “Bado kuna wakati wa kuokoa jamii hii katika shida ilimo. Kama itaokolewa au la yategemea ujuzi wa mwanadamu juu ya mazingira na tabia ya mbwa-mwitu, kuendelea kwake kuzitafiti njia za mbwa-mwitu, na kujifunza kwake kumfikiria mbwa-mwitu si kuwa mshindani bali kiumbe mwenzake ambaye ni lazima waishiriki dunia pamoja.”[23]

Kuishi Katika Amani

Maisha ya pamoja kati ya watu na mbwa-mwitu huenda yakawa yaliboreka miaka michache iliyopita, lakini palipo na mpambano, amani ya kweli haiwezi kufikiwa. Lazima hii iachiwe wakati ujao wa hivi karibuni ambapo, chini ya serikali ya Ufalme wa Muumba, uhasama na hofu yote zitaondolewa kuwe na mtazamo wa kutumainiana na kushiriki mambo pamoja na kiumbe huyu mwenye nguvu lakini aliye mwepesi wa hisia na mwenye haya.

Kwa kupendeza, Biblia huonyesha tabia za mbwa-mwitu katika vikao mbalimbali vya kiunabii, ikituwezesha tumwone kwa maoni tofauti-tofauti. Kwenye Matendo 20:29, 30, watu waasi-imani huelezwa kitamathali kuwa “mbwa-mwitu wakali” ambao wangeshambulia kutaniko la Kikristo lililo kama kondoo na kuondoa zizini washirika fulani mmoja-mmoja.

Unabii mbalimbali katika kitabu cha Biblia cha Isaya, ingawa haujapata utimizo wa mwisho, hueleza juu ya wanyama tuwajuao leo kuwa adui kwa adui wakikaa pamoja kwa amani. Angalia kwamba hakuna ule uhusiano wa mwindwa-na-mnyafuaji kwenye Isaya 65:25: “‘Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng’ombe . . . Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema BWANA.”

Ingawa jitihada za mwanadamu zaonyesha kwamba anajaribu kumvumilia mbwa-mwitu, andiko lililonukuliwa sasa hivi latuhakikishia kwamba Mungu amemwekea mahali katika mfumo wake mpya wa mambo. Sayari Dunia wakati huo itakuwa makao yenye kushirikiwa na namna zote za uhai, kutia na Canis lupus.

[Maelezo ya Chini]

a Ona “Kuutazama Ulimwengu” katika Amkeni! la Januari 22, 1994.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Thomas Kitchin/Victoria Hurst

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Thomas Kitchin

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki