Kuutazama Ulimwengu
Hangaiko Zaidi Juu ya Damu
Watafiti wa kitiba wa Australia wanahofia kwamba virusi iwezayo kuua huenda ilichanganyikana na akiba ya damu ya taifa hilo. Ile virusi iitwayo human T-lymphotropic virus (HTLV-1) ni “binamu” ya virusi ya UKIMWI na yaweza kusababisha aina ya ugonjwa wa leukemia isiyo ya kawaida na maradhi ya mfumo wa neva. Virusi hiyo yapatikana sana katika Japan, Papua New Guinea, Visiwa vya Solomon, na Australia (miongoni mwa Waaborijini). Kulingana na ripoti, wanaume wawili Waaustralia tayari wamekufa kutokana na leukemia ihusikayo na virusi hiyo, na mtu wa tatu ametambuliwa kuwa augua uharibifu wa neva. Virusi hiyo ya HTLV-1 huenezwa kwa njia sawa na UKIMWI, yaani kupitia kufanya ngono, kujidunga dawa za kulevya, kunyonyesha matiti, utiaji-damu mishipani, na wakati wa kuzaa. Mkurugenzi wa Huduma ya Utiaji-Damu Mishipani ya Shirika la Msalaba Mwekundu la New South Wales asema kwamba visababishi “viko kwa wazi” kuweza kupitishwa kwa virusi kupitia utiaji-damu mishipani, kulingana na The Courier Mail, ambalo ni gazeti la Brisbane. Virusi hiyo imepatikana katika angalau watoaji damu sita katika Australia.
Vidonda vya Tumbo na Kuvuta Sigareti
“Kulingana na habari kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni, karibu asilimia 10 ya idadi ya watu ulimwenguni wamepata kuwa na vidonda vya tumbo, wanavyo, ama watakuwa navyo,” asema mstadi wa maradhi ya tumbo Dakt. Thomas Szego wa Hospitali ya Albert Einstein katika São Paulo, laripoti Jornal da Tarde. Ingawa kuwasha kwa tumbo kwaweza kutokeza vidonda vya tumbo, “kuwasha kudogo kwa tumbo ni sehemu ya kuzeeka kwa tumbo,” habari hiyo yaendelea kusema. Hata hivyo, mambo kama mkazo wa akili wenye kuendelea, kufunga kula, na kutumia kileo au dawa za tiba vibaya yaweza kuwasha tumbo. Hata hivyo, Dakt. Szego aonya hivi: “Kama ningeulizwa nitaje kitu kimoja chenye kudhuru tumbo zaidi, ningechagua sigareti. Inadhuru sana utando wa umajimaji wa tumbo.” Yeye aongezea hivi: “Pamoja na mate, mvutaji humeza masalio ya sigareti, huongeza utolewaji wa asidi na kupunguza kinga za tumbo.”
Mbwa-Mwitu Warudi
Mbwa-mwitu wa kijivu amerudi Ufaransa baada ya kutoweka kwa miaka 50, lasema gazeti la Kifaransa Terre Sauvage. Ingawa pindi fulani mbwa-mwitu hao walikuwa wengi huko na kotekote Ulaya, wao karibu waangamizwe kutoka Ulaya ya Magharibi kupitia kuwindwa, kupewa sumu, na kukosa makao. Wakilindwa katika Italia tangu 1977, hesabu ndogo ya mbwa-mwitu iliokoka katika milima ya Apennine ya Italia. Kwa kufanyizwa kwa Mbuga ya Kitaifa ya Mercantour mnamo 1989 katika kusini-mashariki mwa Ufaransa na kuwapo kwa wingi wa makundi ya paa waitwao chamoisi, kondoo-mwitu, na kulungu, yaonekana kwamba mbwa-mwitu wanaanza kutwaa tena Ufaransa wakivuka mpaka kutoka Italia wakitafuta chakula chao cha asili na eneo kubwa zaidi. Ingawa mbwa-mwitu wamelindwa kisheria katika Ufaransa tangu 1989, mwanabiolojia Luigi Boitani asema hivi: ‘Hatari kubwa zaidi kwa mbwa-mwitu ni hofu kuu ya wanadamu kuwaelekea.’
Nguvu Isiyo Ghali
Nguvu ya trekta imeleta mabadiliko makubwa katika ukulima. Na bila shaka imenufaisha viwanda vya gari na mafuta. Hata hivyo, wengi bado wapendelea kutumia wanyama wenye kukokota mizigo. Gazeti Farmer’s Weekly laripoti juu ya moja ya mashamba makubwa zaidi ya machungwa ulimwenguni, karibu na mji wa Potgietersrust wa Afrika Kusini, linalofuga nyumbu walo lenyewe kwa ajili ya usafirishaji. Wanyama wa kubeba mizigo hawahitaji ujuzi wa kipekee wa kudumishwa, wala hawahitaji spea wala mafuta yanayoingizwa nchini. “Wao waweza kupewa masalio ya mazao ama kulishwa katika shamba lililo tupu,” laeleza Farmer’s Weekly. Gazeti hilo lamalizia kwamba nguvu ya wanyama yapaswa “itumiwe kwa kiwango kikubwa zaidi katika miradi ya uhandisi, ujenzi na kutengeneza au kurekebisha barabara katika sehemu za mashambani za Afrika kuliko inavyotumiwa sasa.”
Ferrari Bandia
Noti, hundi, tepu, na mifuko ya kimtindo na mavazi ya jeans ni mambo ya kawaida kwa watengenezaji stadi wa vitu bandia. Lakini hivi karibuni polisi wa Italia wamegundua biashara ya kuiga gari fulani, ile Ferrari ya zamani. Wakitumia spea, picha, na plani za zamani, mekanika ambao wakati mmoja walifanya kazi kwa watengenezaji wa gari hilo maarufu walikuwa wakifanya kazi kwa ustadi mkubwa katika kutokeza magari “kamili” ya aina ya magari yaliyotokezwa katika miaka ya 1950 na 1960 na kuyauza kwa wakusanyaji yakiwa magari yale halisi. Kwa kufikiria bei za magari ya zamani katika soko la kimataifa, “huo ulikuwa ulaghai wa dola milioni nyingi,” laripoti La Repubblica.
Mamilioni ya Watoto Chokora
“Kuna watoto zaidi ya milioni 100 wanaoishi katika barabara za miji, na angalau nusu yao hutumia dawa za kulevya,” laripoti Shirika la Afya Ulimwenguni. Uchunguzi wa majiji makubwa, kama vile Rio de Janeiro, Manila, Lusaka, Montreal, na Toronto, ulionyesha tofauti kidogo kati ya uchunguzi huo kuhusu matumizi ya dawa za kulevya na watoto chokora. Kulingana na mratibu wa utafiti huo, mstadi wa uchumi Hans Emblad, “yaonekana kwamba kupatikana kwa dawa za kulevya ni jambo linaloamua idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya.” Lakini aendelea kusema, “wenye mamlaka, kama ilivyo na mashirika ya kijamii yahusikayo na watoto chokora, huelekea kupuuza kabisa tatizo la dawa za kulevya.” Ingawa wengine “hujaribu kufukuza watoto hao,” kulingana na Emblad, “tatizo ni kwamba hawana mahali pa kwenda.” Ile ripoti katika O Estado de S. Paulo yaongeza kwamba watoto chokora “wataka kuendelea kuishi.”
Neti Ndefu Zaidi ya Zote
Wasichana wa arusi wapatao mia moja walihitajiwa kubeba neti ya arusi iliyo ndefu zaidi ulimwenguni; nguo nyeupe yenye urefu wa meta 305 “ilifuata” wenzi hao wachanga wanaotoka Naples, Italia, walipopita wakafunge ndoa mbele ya watazamaji wenye mshangao. Mbuni wa mitindo aliyebuni neti hiyo ndefu ya arusi amekuwa akitaka kupata rekodi hiyo kwa muda fulani, na hadi kufikia sasa hakuwa amepata bibi-arusi ambaye angekubali kuivaa. Kisha akakutana na bibi-arusi kutoka Naples, na “ndoto ikatimia,” akasema mbuni huyo mwenye kuridhika. Na rekodi ya hapo awali ilikuwa gani? Neti iliyovaliwa na bibi-arusi Mfaransa iliyokuwa na urefu wa meta 278.
Kuzuia UKIMWI
“Kuna mapengo ya wazi kati ya Wizara ya Elimu, walimu, na wazazi juu ya namna ya kushughulikia elimu ya UKIMWI,” laripoti gazeti la Japani Mainichi Shimbun. Bishano latokea juu ya kikaratasi cha habari juu ya elimu ya UKIMWI kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya sekondari, kilichokuwa na kichwa AIDS—For Accurate Understanding. Kikaratasi hicho kilisema hivi: “Ambukizo [la UKIMWI] laweza kuzuiwa kama kondomu zatumiwa vizuri.” Wizara hiyo ilipokea barua na simu nyingi kuhusu kikaratasi hicho, asilimia 90 za barua hizo zikiwa zenye kuchambua. Wachambuzi fulani walisisitiza kwamba “kudhibiti utendaji wa ngono kwapaswa kufundishwa badala ya matumizi ya kondomu.” Gazeti moja lililotayarishwa na shirika moja la biashara la kubandikwa katika ubao wa matangazo wa shule lilionyesha juu ya kuepuka UKIMWI na likakubaliwa kwa kusifiwa. Lilikazia ubikira.
Ushuhuda wa Kasuku
Kasuku alikuja kuwa shahidi muhimu katika mahakama moja katika jimbo la kusini mwa India la Kerala. Gazeti Indian Express liliripoti kesi hiyo ya mahakamani yenye kuhusu majirani waliokuwa na mzozano juu ya ni nani aliyekuwa mwenye kasuku. Ili kutatua mzozo huo, hakimu aliamuru kasuku huyo aletwe mahakamani na atoe ushahidi. Ushahidi muhimu sana ulitolewa wakati kasuku huyo mwenye kushirikiana vizuri alipotaja kwa kasi bila kushurutishwa majina ya watoto wa familia iliyokuwa hapo awali imeripoti kupotea kwa kasuku. Kwa sababu ya kasuku mwaminifu, hakimu wa wilaya aliamua kesi kwa kupendelea familia hiyo.
Michezo ya Bunduki ya Leza
“Kusudi la mchezo huo ni kufyatua mwingine na wewe mwenyewe usifyatuliwe mara nyingi,” laripoti The Globe and Mail la Toronto, Kanada. Mchezo wa zamani wa kimbia-nikuguse umekuwa wa tekinolojia ya juu sasa. Baada ya dakika kumi ya kufyatua wengine kwa miale ya nuru katika uwanja wa michezo wa kisasa, wenye uchafu, na wenye kujazwa ukungu ukiwa na “muziki wenye sauti ya juu,” mshiriki mmoja aliueleza kuwa “waondoa mkazo wa akili.” Mamia ya vituo vya vitumbuizo kama hivyo vyatokea ghafula katika Amerika Kaskazini, Uingereza, Ulaya, Australia, na Israel. Kuna fadhaiko inayoendelea kukua kwamba vitumbuizo kama hivyo huendeleza jeuri. Profesa Robert Stebbins wa soshiolojia wa Chuo Kikuu cha Calgary alisema hivi katika gazeti The Globe: “Hakuna ishara iliyo wazi kati ya michezo ya kivita yenye kuleta matatizo mengi na ile ambayo huonwa kuwa yafaa, kama vile mchezo wa chesi ukiwa na ngome zao na majeshi yao. Kusudi ni lenye jeuri.” Mchezaji mmoja tineja alisema hivi: “Yaonekana kuwa ajabu kuendeleza mchezo unaohusika na vita kwa ajili ya kujifurahisha. . . . Unapofikiria ule ujumbe jambo hilo hutokeza, hauonekani kuwa sawa.”
Wapiganaji-Vita Wanaoendelea Kuvuta Sigareti
Kwa sababu ya vita, chakula na bidhaa nyinginezo muhimu zimekuwa nadra sana kupatikana katika Bosnia na Herzegovina. Lakini katika jiji la Sarajevo, hata baada ya miezi kadhaa ya kuzingiwa, kiwanda kimoja kiliendelea kutengeneza sigareti. Kulingana na gazeti New York Times, katika nchi hiyo yenye kukumbwa na vita, watu wengi hunung’unika zaidi juu ya ukosefu wa sigareti kuliko kunung’unika juu ya ukosefu wa chakula, maji, ama risasi. Watu wamekuwa tayari kulipa kati ya dola 5 na dola 50 kwa ajili ya paketi moja tu ya sigareti. Gazeti Times lilisema kwamba mtu yeyote aliyependekeza au “kujaribu kupiga marufuku uvutaji wa sigareti katika mikahawa, ofisi, ama mahali pengine popote kwa hakika angejikuta akielekezewa bunduki.”