Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 11/22 kur. 18-20
  • Tulijifunza Kumtegemea Mungu Kupitia Majanga

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tulijifunza Kumtegemea Mungu Kupitia Majanga
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uzalishaji
  • Matatizo Yazuka Baadaye
  • Kujifunza Kuitibari Zaidi Katika Yehova
  • JoAnn Arudi Nyumbani
  • Maisha Yetu Leo
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2000
  • Je, Umetenga Wakati wa Kujifunza Biblia?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Kutumika Wakati wa Ongezeko Kubwa Ajabu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
  • “Nimeshika Imani”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 11/22 kur. 18-20

Tulijifunza Kumtegemea Mungu Kupitia Majanga

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA ROSIE MAJOR

Nilikuwa na mimba ya miezi mitano ya mtoto wangu wa kwanza wakati mama-mkwe wangu alipotambua kwamba miguu yangu ilionekana kuwa imevimba isivyo kawaida. Katika siku hiyo Machi 1992, mimi na mume wangu Joey hatungeweza kujua kwamba jambo ambalo tulielekea kukabili lingetahini tegemeo letu katika Yehova.

JUMA moja baadaye daktari wangu wa uzazi aligundua kwamba msongo wangu wa damu ulikuwa umepanda sana. Alipopendekeza kwamba nilazwe hospitalini ili nichunguzwe, nilihangaika bila shaka. Uchunguzi ulionyesha kwamba nilikuwa na ugonjwa wa preeclampsia, tatizo la ujauzito linaloweza kufisha.a

Daktari aliyekuwa katika hospitali hiyo alipendekeza kwa dhati kwamba utungu uchochewe mara moja ili kunilinda mimi na mtoto. Mimi na mume wangu tulifadhaika. “Lakini mtoto hata hajafikisha umri wa majuma 24!” nilitweta. “Mtoto wetu angeweza kuokokaje akiwa nje ya tumbo la uzazi?” “Nitajasiria kuahirisha hatua hiyo kwa muda mfupi,” daktari huyo akajibu kwa fadhili. “Hata hivyo, ikiwa hali yako itazorota, nitalazimika kumzalisha.” Siku 13 zilipita, lakini hali yangu ilizorota upesi sana. Daktari alimwita mume wangu, na tulifanya uamuzi mgumu wa kuendelea na uzalishaji.

Uzalishaji

Usiku uliotangulia uzalishaji, Dakt. McNeil, daktari wa watoto, alikutana nasi ili kutueleza jambo ambalo tungekabili kwa kuwa na mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati—uwezekano wa madhara ya ubongo, mapafu ambayo hayajakomaa kiasi cha kufanya kazi ifaavyo, na uwezekano wa matatizo mengine. Nilisali kwa ajili ya “amani ya Mungu izidiyo fikira yote kwa ubora” na kwa nguvu za kukubali na kukabiliana na chochote ambacho kingetokea. (Wafilipi 4:7) Asubuhi iliyofuata mtoto wetu alizaliwa kwa njia ya kupasuliwa tumbo. Alikuwa na uzito wa gramu 700 tu. Tulimwita JoAnn Shelley.

Siku tano baadaye nilirudi nyumbani mikono mitupu. Binti yangu mdogo alibaki katika wadi maalum ya watoto wadogo, akipigania uhai wake. Baada ya majuma mawili JoAnn alishikwa na nimonia. Tulishukuru hali yake ilipokuwa nafuu, lakini siku chache baadaye alipatwa na ambukizo la utumbo na akahitaji kuhamishwa hadi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Baada ya siku nyingine sita, JoAnn alipata nafuu kwa njia fulani na hata akaanza kuongeza uzito. Tulishangilia! Lakini shangwe yetu ilikuwa ya muda mfupi. Dakt. McNeil alituarifu kwamba JoAnn alikuwa na ugonjwa wa damu. Alidokeza kupata homoni ya sanisia iitwayo erythropoietin (EPO) ili kuchochea ukuzi wa chembe nyekundu za damu za JoAnn. Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova hapa katika Bahamas iliwasiliana na wawakilishi wa Huduma za Habari za Kihospitali katika Brooklyn, New York. Upesi walimwandalia Dakt. McNeil habari za karibuni zaidi juu ya kupatikana na matumizi ya EPO, na akaanza kuitumia kwa matibabu.

Matatizo Yazuka Baadaye

Majuma kadhaa yenye wasiwasi yalipita. Kufikia sasa JoAnn alikuwa akipambana na ambukizo katika matumbo yake, ugonjwa wa ghafula uliokuwa ukisababisha kutoweza kupumua (vipindi kadhaa bila kupumua), kupungua kwa hemoglobini, na nimonia ya mrija wa hewa mwilini. Tulihofu kwamba mojawapo ya matatizo hayo lingeweza kuwa tatizo la mwisho ambalo lingesababisha kifo chake. Lakini JoAnn alifanya maendeleo pole kwa pole. Alipokuwa na umri wa miezi mitatu, alikuwa angali hospitalini na alikuwa na uzito wa kilogramu 1.4 tu. Lakini kwa mara ya kwanza maishani mwake alikuwa akipumua kwa kujitegemea bila kuongezewa oksijeni. Hemoglobini yake ilikuwa ikiongezeka kufikia kiwango cha kawaida. Daktari alisema kwamba ikiwa uzito wake ungeongezeka kwa gramu nyingine 500, tungempeleka nyumbani.

Majuma matatu baadaye JoAnn alikabili hali mbaya sana ya kutoweza kupumua. Alipopimwa kisababishi hakikupatikana. Hali za kutoweza kupumua zilitukia mara kwa mara na mara nyingi zilihusiana na kula. Hatimaye, ilijulikana kwamba JoAnn alikuwa na tatizo la tumbo na umio wa chakula lililokuwa likitukia mara kwa mara. Umio wa chakula haukuwa ukijifunga baada ya kula, kwa hiyo chakula kilichokuwa kwenye tumbo lake kilirudi hadi kwenye koo. Jambo hilo lilipotokea, alisakamwa na akaacha kupumua.

Mapema mwezi wa Oktoba, JoAnn alipata ambukizo la kirusi katika wadi ya watoto. Watoto wengi waliozaliwa kabla ya wakati walikuwa wakifa kutokana na kirusi hicho katika wadi hiyo. Akiwa amedhoofika hivyo, JoAnn alipatwa na tatizo la muda mrefu la kushindwa kupumua ambalo hakuwa amewahi kulipata. Jitihada zote za kumsaidia ziliambulia patupu. Daktari wa watoto alikuwa amefikia hatua ya kutangaza kuwa amekufa, wakati ambapo kwa hali zisizoweza kuelezeka alianza kupumua—kisha akapatwa na tatizo la ghafula la kupumua. Kwa mara nyingine tena aliwekwa kwenye chombo cha kupitisha hewa, na tulikuwa na hakika kwamba huo ulikuwa mwisho wa JoAnn. Lakini aliokoka, nasi tukamshukuru Yehova.

Kujifunza Kuitibari Zaidi Katika Yehova

Matatizo tuliyokabili kabla JoAnn hajazaliwa yangeweza kulinganishwa na kuanguka kutoka kwenye mashua karibu na gati, mahali ambapo tungeweza kuogelea tu hadi ufuoni. Sasa ilionekana kana kwamba tulikuwa tumeanguka katikati ya bahari, mahali ambapo hungeweza kuona nchi kavu. Tunapokumbuka yaliyotupata, tunang’amua kwamba kabla hajazaliwa nyakati nyingine tulijitegemea sana. Lakini kupitia mambo yaliyotupata sisi na JoAnn, tumejifunza kuitibari katika Yehova katika hali zisizoweza kusuluhishwa na binadamu. Tulijifunza kufanya kama alivyoshauri Yesu—kushughulika na siku moja kwa wakati wake. (Mathayo 6:34) Tulijifunza kumtegemea Yehova, ijapokuwa nyakati fulani hatukujua jambo mahususi la kusali juu yake. Sasa twamshukuru Yehova kwa ajili ya hekima ya Biblia na “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida,” inayotuwezesha kukabiliana na magumu hayo makali.—2 Wakorintho 4:7.

Wakati wa matatizo, mara nyingi niliona ugumu wa kudumisha usawaziko wa kihisia-moyo. Nilikuwa nikifikiri tu juu ya JoAnn. Mume wangu Joey, alikuwa mwenye thamani sana katika kuniandalia usawaziko wa kiroho. Ninamshukuru sana kwa ajili ya hilo.

JoAnn Arudi Nyumbani

Afya ya JoAnn iliboreka hatua kwa hatua. Siku moja alivuta kihalisi mrija wa chombo cha kupitisha hewa kutoka kinywani mwake. Sasa Dakt. McNeil aliona kwamba JoAnn angeweza kurudi nyumbani. Tulijawa na furaha! Katika matayarisho ya kumpokea nyumbani, tulijifunza namna ya kumlisha kwa mpira. Pia tuliweka chombo cha kumpa oksijeni, tukakodi chombo cha kuchunguza mpigo wa moyo na kupumua, na kwenda kwenye mtaala wa kumhuisha wakati wa hali ya dharura. Hatimaye, katika Oktoba 30, 1992, JoAnn alitoka hospitalini. Alikuwa ametumia muda wa siku 212 katika wadi maalum ya watoto wadogo, ndivyo na sisi pia.

Mwanzoni kabisa, washiriki wa familia na washiriki wa kutaniko la kwetu la Mashahidi wa Yehova walithibitika kuwa baraka kweli kweli kutoka kwa Yehova. Walikuja na kusafisha nyumba na ua, wakapika vyakula, wakatusaidia kwenda hospitalini, na kumtunza JoAnn ili niweze kulala. Hivyo tukaja kujua sifa zenye kupendeza za nyutu zao ambazo hatukuwa tumezijua. Kwa mfano, wengine walishiriki nasi mawazo ya kiroho yaliyowasaidia washinde magumu yao wenyewe.

Maisha Yetu Leo

Tumejitahidi sana kumwandalia JoAnn msaada wa kitiba unaopatikana kwa ajili ya matatizo yake mengi. Alipokuwa na umri wa miezi 19, tulipata habari kwamba JoAnn ana ugonjwa wa kupooza ubongo—kwa sababu ya madhara ya ubongo. Kisha, katika Septemba 1994, alifanyiwa upasuaji mkubwa kwa ajili ya ugonjwa wa tumbo na wa kutoweza kupumua uliokuwa ukimpata mara kwa mara. Mnamo 1997, JoAnn alianza kupatwa na magonjwa ya ghafula-ghafula yenye kutishia uhai. Jambo linalopendeza ni kwamba baada ya kufanya marekebisho katika ulaji wake, magonjwa hayo ya ghafula-ghafula yalikoma. Matatizo ya afya ya JoAnn yamechelewesha ukuzi wake wa kimwili. Lakini sasa anahudhuria shule ya pekee na anaendelea vizuri. Hawezi kutembea, na hawezi kuzungumza sana, lakini huandamana nasi kwenye mikutano yote ya Kikristo na kwenye huduma ya nyumba hadi nyumba. Anaonekana kuwa mwenye furaha.

Yehova ametuandalia faraja nyingi katika nyakati hizi zenye magumu. Tumeazimia kuendelea kumtegemea na ‘kumfurahia BWANA’ licha ya magumu yasiyotarajiwa. (Habakuki 3:17, 18; Mhubiri 9:11) Tunatazamia kwa hamu dunia Paradiso iliyoahidiwa na Mungu, ambapo mpendwa wetu JoAnn atafurahia afya kamilifu.—Isaya 33:24.

[Maelezo ya Chini]

a Ugonjwa wa preeclampsia huzuia mishipa ya damu ya mwanamke mwenye mimba isipanuke, jambo linalosababisha shida ya mtiririko wa damu kwenye viungo vyake na vilevile kwenye kondo la nyuma na kijusu kinachokua. Ijapokuwa kisababishi cha maradhi hayo hakijulikani, kuna uthibitisho fulani unaodokeza kwamba maradhi hayo hurithiwa.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Binti yetu JoAnn

[Picha katika ukurasa wa 20]

Licha ya kupungukiwa kwake, JoAnn ni mtoto mwenye furaha

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki