Afya na Usalama wa Ulaya
Na Mleta-Habari wa Amkeni! Katika Uingereza
ZAIDI ya wanaume na wanawake 16,000 wanafanya kazi kwenye makao makuu ya Watch Tower Bible and Tract Society na ofisi zake za tawi 109. Baadhi ya watu hao wenye kujitolea hufanya kazi kwenye uchapaji, karakana, na udumishaji wa mashine. Lakini hata migao yao iwe ipi, wao huwa na mazoea yafaayo ya kazi, ambayo hulinda uhai wao na afya yao.
Kiwango cha juu kilichowekwa na ofisi ya tawi ya Uingereza na kiwanda chake huko Mill Hill ya London kilitambuliwa waziwazi mwaka wa 1998, baada ya Juma la Ulaya la Usalama na Afya la Mwaka wa 1997. Bakuli la fuwele lililoandikwa maneno “Juma la Ulaya la Usalama na Afya—Mshindi wa Tuzo 1997” lilikabidhiwa Sosaiti. Ni nini kilichoongoza kupewa kwao tuzo hiyo yenye sifa?
Mwaka wa 1994 Watch Tower Society ilipeleka mchanganuo wenye kina wa jinsi ya kupunguza madhara ya mgongo kazini kwa Idara ya Afya na Usalama (HSE). Mwishoni mwa kampeni hiyo, Sosaiti ilipokea cheti cha idara hiyo ya Afya na Usalama kwa utegemezo wake. Mwaka wa 1996 Sosaiti iliombwa ikusanye na kuandika ripoti fupi juu ya shughuli zake za afya na usalama. Baada ya hapo, “Watchtower Bible & Tract Society ilikabidhiwa cheti kwa sababu ya mchango wao uliothaminiwa” kwa afya na usalama.
Mwaka uliofuata, 1997, idara hiyo ya Afya na Usalama iliomba Watch Tower ishiriki katika kampeni yake ya Ulaya ya afya na usalama. Kwa wakati unaofaa Sosaiti ilipeleka makala yenye kina, na picha za kuonyesha kwamba kwa kuunganisha chombo kimoja-kimoja cha umeme kwenye mfumo mkuu wa kuondoa vumbi inawezekana kupunguza vumbi kutoka kwenye karakana ya mbao kwa asilimia 90 na vipande-vipande vya mbao kwa asilimia 100, kwa gharama ya pauni zisizozidi 250.
Tokeo ni kwamba, Sosaiti ilikuwa mojawapo ya washindi 30 wa tuzo walioalikwa kukutana na wawakilishi wa Tume ya Ulaya na serikali ya Uingereza na vilevile mwenyekiti wa Tume ya Afya na Usalama. Alipokuwa anakabidhi bakuli lililoandikwa, alisema hivi: “Pongezi, kwa Watch Tower!”
[Picha katika ukurasa wa 31]
Watch Tower yapewa tuzo kwa viwango vyake vya juu vya afya na usalama