Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Makala Yaokoa Uhai Tulipomtembelea mwanamume mmoja anayeitwa Lenny, alituambia kwamba makala yenye kichwa “Kidingapopo—Homa Isababishwayo na Kuumwa” (Julai 22, 1998) iliokoa uhai wa mpwa wake wa kike. Aliugua homa kwa siku kadhaa, na alikuwa ametokwa na vipele; lakini wazazi wa msichana huyo walifikiri ni ukambi tu. Lenny alipokumbuka makala hiyo, alitafuta gazeti hilo na kusoma tena sehemu iliyokuwa ikieleza dalili za kidingapopo. Kisha akawasihi wazazi wa mpwa wake wa kike wampeleke msichana wao hospitalini. Madaktari walithibitisha kwamba alikuwa na homa ya kidingapopo ya kuvuja damu. Lenny alisifu gazeti la Amkeni! kwa kumsaidia kumwokoa mpwa wake wa kike, na baadaye akakubali funzo la Biblia la nyumbani.
J.M.L., Ufilipino
Maradhi ya Marfan Katika makala “Kukabiliana na Maradhi ya Marfan—Viungo Vinapoteguka” (Februari 22, 2001), Michelle alisema yeye humeza vidonge vya afyuni kila siku. Mkristo anawezaje kutumia dawa inayosababisha uraibu?
S. D., Marekani
Ingekuwa vibaya iwapo Mkristo angetumia dawa ili kusisimuka au kulewa tu. Hata hivyo, daktari akimpendekezea mgonjwa dawa ya kulevya ili kumaliza maumivu, haiwezi kusemwa kuwa anaimeza ili kupata raha. Kwa wazi, hata katika hali kama hizo, Mkristo apaswa kufikiria uwezekano wa kuwa mraibu na madhara mengine yanayoweza kusababishwa na dawa hiyo.—Mhariri.
Simulizi la Michelle limenitia moyo. Japo anapatwa na maumivu daima, ninavutiwa sana na jinsi ambavyo haruhusu hali yake imzuie kumtumikia Yehova kwa moyo wote.
J. G., Guam
Cheche za Mnururisho Makala yenu yenye kichwa “Cheche za Mnururisho—Suala Linalohangaisha,” ilinivunja moyo. (Februari 22, 2001) Hampaswi kutumia mbinu za kuwatisha watu ili kuendeleza maoni yenu ya Biblia. Mwapaswa kuzungumzia mambo hatari kwa njia inayofaa. Kwa mfano, umeme ukitumiwa kwa uangalifu, unaweza kuwa salama kwa kiasi fulani. Hata hivyo, watu wengi wanauawa kwa umeme kila mwaka. Je, hilo lamaanisha kwamba twapaswa kuishi tukiogopa umeme? Jambo la hakika ni kwamba nchi zote zitahitaji nguvu zaidi za umeme wakati ujao, na yaonekana sasa kutumia mitambo ya nyuklia ndiyo njia bora na salama zaidi ya kusambaza nguvu za umeme. Hatupaswi kuogopa nishati ya nyuklia.
R. S., Kanada
Hayo ni masuala tata, na twathamini maelezo ya waziwazi ya msomaji huyo. Hata hivyo, hatuoni kwamba tulitumia “mbinu za kuwatisha watu” katika makala yetu. Hatukujaribu kuwaogofya wasomaji wetu. Wala hatukushutumu nishati ya nyuklia. Badala yake, tulikazia mahangaiko ya kweli ya watu wengi kuhusiana na nguvu za nyuklia, na tukataja kwamba Ufalme wa Mungu ndio utakaotatua kabisa tatizo la uhaba wa nishati.—Mhariri.
Bima Nikiwa wakala wa bima, nilithamini sana mfululizo wa makala wenye kichwa “Bima—Je, Kweli Waihitaji?” (Februari 22, 2001) Wateja wengi hutatanika sana kuhusu bima. Ni vigumu kuelewa ni kwa nini ulipie kitu ambacho hutakitumia kamwe. Hivyo, nilifurahia mfano wenu juu ya kubeba gurudumu la ziada. Asanteni kwa habari hiyo iliyoandikwa vyema.
C. P., Marekani
Kutoka Kisiri Asanteni kwa makala yenu “Vijana Huuliza . . . Kuna Kosa Gani Kutoka Kisiri?” (Februari 22, 2001) Mimi huhuzunika sana ninapoona jinsi vijana fulani Wakristo huwa wapumbavu. Msichana mmoja mchanga alitoka kisiri ili kwenda kwenye karamu na akabakwa. Hakuna aliyemsaidia. Tafadhali endeleeni kuwaonya vijana wetu!
J. N., Marekani