Kidingapopo Homa Isababishwayo na Kuumwa
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Filipino
BILA kuonekana, mbu atua juu ya mkono wa msichana mdogo. Mdudu huyo atoboa ngozi kwa wepesi na kufyonza damu. Baada ya muda mfupi, mama amtupia jicho bintiye na kumwona mbu huyo. Kwa mchapo wa haraka, amepuruka. Je, huo ndio mwisho wake? Labda sivyo. Mdudu huyo aweza kuwa ameenda, lakini kujidukiza ndani ya damu ya mtoto huyo kumeacha viumbehai visivyotakiwa ambavyo vyaweza kusababisha maradhi.
Katika majuma mawili mtoto aanza kuhisi baridi, kuumwa kichwa, maumivu nyuma ya macho, maumivu makali kwenye viungo na homa kali. Ugonjwa uzidipo, awa na vipele vyekundu na kuishiwa nguvu kabisa. Ameambukizwa kidingapopo, homa isababishwayo na kuumwa na mbu.
Hata hivyo, ikiwa mtoto hasa alikuwa ameambukizwa kidingapopo hapo awali, aweza kupatwa na aina mbaya sana ya maradhi haya, yaitwayo homa ya kidingapopo ya kuvuja damu (DHF). Ukiwa nayo, mishipa ya damu huvuja, ikisababisha kutokwa damu kwenye ngozi. Mtu aweza kuvuja damu ndani ya mwili. Matibabu yanayofaa yakikosekana, mgonjwa aweza kupatwa na mshtuko na matatizo ya mzunguko wa damu, ikisababisha kifo cha haraka.
Kidingapopo ni nini hasa? Je, chaweza kukuathiri? Unaweza kujikingaje pamoja na familia yako? Na tukichunguze kwa makini.
Kidingapopo Ni Nini?
Kidingapopo kinachoitwa pia breakbone fever, ni mojawapo tu ya maradhi mengi yawezayo kusababishwa na kuumwa na mbu. Kisababishi halisi cha maradhi haya ni virusi. Mbu aliyeambukizwa (yaani, mbu ambaye hapo awali amemwuma mtu aliyeambukizwa) hubeba kirusi hiki katika matezi yake ya mate. Amwumapo mtu ili apate damu, yeye huingiza kirusi hicho kwa mwanadamu.
Kuna aina nne za virusi vya kidingapopo. Kuambukizwa na aina moja hakutokezi kinga kwa aina zile nyingine tatu. Baada ya kuambukizwa mara ya kwanza, ikiwa mtu aumwa na mbu abebaye aina ile nyingine, tokeo laweza kuwa kidingapopo cha kuvuja damu.
“Sehemu Mbili kwa Tano za Watu Ulimwenguni” Wamo Hatarini
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kidingapopo chatisha uhai wa watu bilioni 2.5, “sehemu mbili kwa tano za watu ulimwenguni.” Gazeti Asiaweek liliripoti hivi: “Zaidi ya nchi 100 za kitropiki na zilizo karibu na tropiki zimeripoti kuzuka kwa kidingapopo, na makumi ya mamilioni ya visa vipya huripotiwa kila mwaka, asilimia 95 ya walioambukizwa wakiwa watoto.”
Haijulikani waziwazi ni lini kidingapopo kilipogunduliwa duniani. Ripoti moja katika Cairo juu ya “homa ya goti” katika mwaka wa 1779 yaweza kuwa ilirejezea kidingapopo. Tangu wakati huo kidingapopo kimeripotiwa ulimwenguni pote. Hasa tangu Vita ya Ulimwengu ya Pili, kidingapopo kimeathiri sana afya ya binadamu, kuanzia na Asia ya Kusini-Mashariki. Aina mbalimbali za kirusi hicho zikaanza kuenea, na hili likatokeza namna hatari sana ya kidingapopo cha kuvuja damu. Kichapo kimoja cha WHO chasema hivi: “Kuzuka kwa mweneo wa kwanza kabisa wa homa hii ya kuvuja damu katika Asia kulitambuliwa katika Manila mwaka wa 1954.” Nchi nyingine zikafuatia, hasa Thailand, Vietnam, Malasia, na maeneo jirani. Mweneo huo wa mapema wa kidingapopo katika Asia ya Kusini-Mashariki ulisababisha vifo vya kati ya asilimia 10 hadi 50 ya watu walioambukizwa, lakini watu walipojifunza mengi zaidi juu ya maradhi haya, idadi ya vifo ilipungua.
Tangu miaka ya 1960, uzembe katika miradi ya kudhibiti mbu abebaye kirusi hiki umechangia ongezeko kubwa mno la kidingapopo. Kidingapopo kilipokua kinaenea, ndivyo kidingapopo cha kuvuja damu kilivyoenea pia. Ni nchi 9 tu zilizokuwa na mlipuko wa maradhi haya kabla ya 1970, lakini kufikia mwaka wa 1995 idadi hii ilifikia nchi 41. Shirika la WHO lakadiria kwamba kila mwaka, visa 500,000 vya kidingapopo cha kuvuja damu husababisha watu walazwe hospitalini.
Ingawa maradhi haya hayajulikani sana katika maeneo yasiyo ya kitropiki, katika visa fulani wasafiri katika maeneo yaliyo na maradhi haya wameambukizwa na kupeleka maradhi haya kwao. Kwa kielelezo, kuelekea mwisho wa mwaka wa 1996, The New York Times liliripoti visa vya kidingapopo katika Marekani—Massachusetts, New York, Oregon, na Texas.
Hatari Hususa za Kidingapopo cha Kuvuja Damu
Kama ilivyotajwa mapema, kidingapopo cha kuvuja damu ni hatari kwa uhai. Hatari moja ya kidingapopo cha kuvuja damu ni kwamba watu hudhani kwamba hiyo si hatari sana. Wengi hufikiri hiyo ni mafua. Lakini, kukosa kuchukua hatua kwaweza kuruhusu maradhi hayo yafikie hatua mbaya zaidi ambapo hesabu ya vigandishadamu hupungua kwa haraka, kuvuja huanza (katika sehemu za ndani au kwenye fizi, pua, au ngozi), na msongo wa damu hudidimia. Mgonjwa aweza kupoteza fahamu. Wakati familia itambuapo kwamba hali imekuwa mbaya, tayari mgonjwa huwa amepatwa na mshtuko. Wanamkimbiza hospitali. Afikapo huko, madaktari wapata kwamba tayari moyo wake unaacha kupiga. Kwa sababu yuko mahututi umajimaji huingizwa kupitia mishipa.
Kuilinda Familia Yako
Ni nini kiwezacho kufanywa ili kupunguza athari za maradhi haya? Ikiwa familia yaishi mahali palipo na kidingapopo na mmoja katika familia apatwa na homa kali izidiyo siku moja, kwa hekima familia yapaswa kumwona daktari. Ni muhimu hasa ikiwa mgonjwa ana dalili nyinginezo za kidingapopo, kama vile vipele au maumivu ya misuli na viungo au nyuma ya macho.
Daktari aweza kupima damu. Kidingapopo kisicho cha kuvuja damu chaweza kuhitaji tiba sahili tu. Lakini ikiwa kupimwa kwaonyesha kwamba ni kidingapopo cha kuvuja damu, yaelekea daktari atapendekeza tiba ya mgonjwa kuongezewa umajimaji kwa uangalifu. Hiyo yaweza kutia ndani umajimaji wa kunywa kama ule utumiwao na mtu anayehara, au, katika hali hatari zaidi, kuongezwa maji ya Ringer au maji ya chumvi, au mengineyo kupitia mishipa. Katika kutibu visa vya mshtuko, daktari aweza kutoa maagizo ya dawa fulani za kusaidia kuongeza mpigo wa damu na kurudisha vigandishadamu.
Mtu akivuja damu sana huenda madaktari wakapendekeza kutiwa damu mishipani. Huenda wengine wakapendekeza upesi njia hii bila kufikiria njia za badala. Hata hivyo, pamoja na kuvunja sheria ya Mungu, kwa kawaida njia hii huwa si ya lazima. (Matendo 15:29) Uzoefu umeonyesha kwamba kudhibiti kwa uangalifu umajimaji wa mwilini wakati maradhi yaanzapo ndilo jambo la maana zaidi katika matibabu. Ushirikiano kati ya mgonjwa na daktari katika jambo hili waweza kuondoa mabishano juu ya suala la kutiwa damu mishipani. Mambo haya yote hukazia umaana wa kuchukua hatua ya haraka wakati mtu anaposhuku kidingapopo cha kuvuja damu.—Ona sanduku “Kina Dalili Zipi?”
Hatua za Kujikinga
Mojawapo wa wabebaji wakuu wa kirusi cha kidingapopo ni mbu aitwaye Aedes aegypti. Aina hii ya mbu ni ya kawaida katika maeneo ya kitropiki na yaliyo karibu na tropiki ulimwenguni pote. (Ona ramani inayoandamana na makala hii.) Mbu hawa waitwao Aedes aegypti husitawi katika maeneo yaliyo na watu wengi. Njia moja ya kudhibiti maradhi hayo ni kudhibiti mbu.
Si rahisi kudhibiti mbu ulimwenguni pote. Hata hivyo, kuna mambo uwezayo kufanya ili kupunguza hatari hiyo nyumbani kwako. Mbu wa kike hutaga mayai ndani ya maji. Buu laweza kukua katika chombo chochote kiwezacho kuhifadhi maji kwa juma moja hivi, kama vile tairi zilizotupwa, mikebe, chupa, au vifuu vya nazi. Kuondoa vitu hivyo kutaondoa maeneo ya kuzalia ya mbu. Kwa kuongezea, inapendekezwa kwamba ugeuze ndoo na mashua zitazame upande wa chini. Kuondoa maji yaliyotulia kwenye mifereji kwaweza kusaidia pia. Kwa kupendeza, mwanzoni mwa mwaka wa masomo wa 1997/98, wizara ya afya katika Filipino ilipinga matumizi ya vyungu vya kuotesha maua katika madarasa ya shule kwa sababu hii.
Ikiwa mtu fulani nyumbani aambukizwa kidingapopo, chukua hatua za kuzuia asiumwe na mbu ambaye baadaye aweza kuambukiza wengine. Makao yaliyo na kiwambo kizuri na yaliyo na hewa safi yaweza kuwa kinga.
Namna gani chanjo? Kufikia sasa hakuna dawa ya chanjo ifaayo inayopatikana. Utafiti unafanywa ili kutokeza moja, lakini ugumu hutokezwa na jambo la kwamba kinga kamili ingehitaji kukingwa kutokana na aina zote nne za kidingapopo. Chanjo kwa aina moja tu kwa kweli ingeweza kuongeza hatari ya kushikwa na kidingapopo cha kuvuja damu. Watafiti wanatumaini kwamba dawa ya chanjo yaweza kupatikana kwa muda wa miaka mitano hadi kumi.
Watafiti wengine wamekuwa wakijaribu mfikio mwingine. Kwa kubadilisha jeni wanatumaini kuzuia virusi vya kidingapopo visijirudufishe katika mate ya mbu. Mpango huu ukifaulu, mbu ambao jeni zao zimebadilishwa wangepitishia wazao wao kinga kwa kidingapopo. Ingawa maendeleo fulani yamefanywa, bado haijulikani itafaulu kiasi gani.
Kwa wakati huu, kuondoa kabisa kidingapopo kunaonekana hakuwezekani. Lakini kuchukua tahadhari nzuri kwaweza kukusaidia pamoja na wapendwa wako kuepuka hali zitishazo uhai kutokana na kidingapopo—homa isababishwayo na kuumwa.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Kina Dalili Zipi?
Dalili za kidingapopo na homa ya kidingapopo ya kuvuja damu (DHF)
• Homa kali ya ghafula
• Kuumwa sana na kichwaa
• Maumivu nyuma ya macho
• Maumivu ya misuli na viungo
• Kuvimba kwa tezi za limfu
• Vipele
• Uchovu
Dalili za hususa zaidi kwa kidingapopo cha kuvuja damu
• Kupoteza fahamu kwa ghafula
• Kuvuja damu kwa ngozi
• Kutokwa damu sehemu fulani hususa
• Ngozi baridi iliyo chepechepe
• Kutotulia
• Mshtuko pamoja na mpwito dhaifu (dalili za mshtuko wa kidingapopo)
Usichelewe kumwona daktari uonapo dalili hizo. Watoto hasa huwa katika hatari kubwa zaidi
[Maelezo ya Chini]
a Wataalamu wa kitiba husema kwamba aspirini yapasa kuepukwa kwa sababu inaweza kuzidisha kutokwa damu.
[Sanduku katika ukurasa wa 23]
Madokezo kwa Wasafiri
Mara kwa mara, wasafiri ambao huzuru maeneo ya kitropiki huambukizwa kidingapopo, lakini homa ya kidingapopo ya kuvuja damu huwa nadra sana kwa sababu kwa aina hii iliyo hatari sana kwa kawaida mtu huambukizwa baada ya ambukizo la pili la kidingapopo. Yafuatayo ni madokezo ya usalama kwa ajili ya wasafiri:
• Valia shati la mikono mirefu na suruali ndefu
• Tumia kizuia-mbu
• Epuka maeneo yaliyo na watu wengi
• Kaa katika nyumba ambayo waweza kufunga madirisha na kuzuia mbu
• Ukipatwa na homa urudipo nyumbani, mweleze daktari mahali uliposafiri
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 23]
Maeneo yaliyoenea kidingapopo hivi karibuni
Maeneo yaliyo hatarini kwa mlipuko wa kidingapopo
Maeneo ya “Aedes aegypti,” mbu abebaye kidingapopo
[Hisani]
Chanzo: Centers for Disease Control and Prevention, 1997
© Dr. Leonard E. Munstermann/Fran Heyl Associates, NYC
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mahali ambapo mbu waweza kuzaana ni (1) tairi zilizotupwa, (2) mfereji wa mvua, (3) vyungu vya kuoteshea maua, (4) ndoo au vyombo vingine, (5) mikebe iliyotupwa, (6) mapipa
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]
© Dr. Leonard E. Munstermann/Fran Heyl Associates, NYC