Kuutazama Ulimwengu
Kipima-moyo
Vyombo vya kutambua wevi vilivyoko sasa kwenye maduka na vituo vingi vya ununuzi huenda vikawa hatari kwa afya ya watu wanaovaa kipima-moyo ili kudhibiti mpigo wao wa moyo. Jarida la kitiba la Kifaransa Le Concours Médical laripoti kwamba madaktari katika Ufaransa walijulishwa taabu hiyo na mgonjwa anayefanya kazi kwenye duka kuu ambaye alilalamika kwamba mpigo wa moyo wake uliongezeka upesi kila wakati alipokaribia kaunta za kukagulia za duka hilo. Katika kujaribu vipima-moyo mbalimbali zaidi ya 30, kikundi hicho cha madaktari kilipata kwamba uga za sumakuumeme zilizofanyizwa na mifumo ya kutambua wevi zilisababisha vipima-moyo vingi kufanya kazi vibaya, wakati mwingine vibaya zaidi. Madaktari waonya kwamba wale wenye vipima-moyo wapaswa kujulishwa hatari hiyo.
Desturi Iliyo Hatari
Hivi karibuni kliniki katika San Antonio, Texas, ilipata hesabu isiyo ya kawaida ya maombi ya wasichana matineja wapimwe ili kujua kama wana UKIMWI. Uchunguzi ulionyesha kwamba wasichana hao walikuwa wakifanya ngono pamoja na “washiriki wa genge lenye HIV” bila kujihadhari hiyo ikiwa sehemu ya desturi ya kuweza kukubaliwa nao. Kulingana na Daily News la New York, maofisa hao walisema kwamba wasichana hao wa miaka 14 na 15 “walikuwa wakifanya hivyo ili kuwa sehemu ya genge” na “kuthibitisha kwamba wao ‘wana nguvu vya kutosha’ kutoweza kupata virusi vya UKIMWI.” Wengi wa wasichana hao hujiunga na magenge wakitafuta upendo na faraja ambayo hawapati nyumbani. Lakini maisha ya magenge huwaletea jeuri, ngono za ovyoovyo, na magonjwa yanayopitishwa kingono. Likinukuu maelezo ya ofisa mmoja, Daily News lilisema kwamba “wengi wa wasichana hao hutoka kwenye familia zilizovunjika. Wengi wametendwa vibaya na washiriki wa familia.”
Je! UKIMWI Unapita Udhibiti?
Je! kusambaa kwa UKIMWI ulimwenguni pote kumeshindwa kudhibitiwa? Huenda ikawa, yasema ripoti yenye kurasa 1,000 iliyotayarishwa na Mwungano wa Tufe Lote wa Sera ya Ukimwi katika Chuo Kikuu cha Harvard katika United States. Kulingana na The Guardian Weekly, ripoti hiyo yaonyesha kwamba hakuna taifa ambalo limeweza kukomesha usambaaji wa UKIMWI na kwamba wale wanaosema kwamba ugonjwa huo umefikia kilele katika Ulaya huenda wanakosea. Ripoti hiyo yasema: “Mweneo wa HIV/Ukimwi unaingia sehemu mpya, yenye kuhatarisha. Kadiri tisho la tufeni pote liongezekavyo, kuna dalili nyingi za kuongezeka kwa kinaa, kujikana kunakoendelea, na ubaguzi unaotokea tena.”
Udhia wa Wafanyakazi Wanawake
Uchunguzi wa hivi karibuni kwenye Hospitali ya Toronto, katika Toronto, Kanada, ulionyesha kwamba asilimia 70 ya wafanyakazi wayo wanawake walilalamika kwa kuudhiwa kingono kazini. Kulingana na The Toronto Star, asilimia 2 ya wanawake waripoti kuwa wameumizwa kingono, na asilimia 1 waripoti kuwa wametolewa vitisho ili wafanye ngono. Wanawake wengi wasema kwamba “wamezungumziwa kwa njia ya kukosa heshima au njia isiyofaa ya vivi-hivi” na asilimia kubwa “walilalamika juu ya mizaha ya kingono.” Gazeti Star laripoti kwamba karibu asilimia 60 ya wafanyakazi wanawake “walihisi kutokuwa salama katika sehemu nyingine za” hospitali.
Masomo ya Biblia Katika Chuo Kikuu cha Kijapani
Uchunguzi wa hivi karibuni wa wanafunzi katika idara ya fasihi ya Chuo Kikuu cha Waseda chenye fahari cha Japani ulionyesha kwamba “wanafunzi wengi walikuwa na hamu ya kujifunza zaidi juu ya vitabu vyenye ufasaha na hasa Biblia, ambayo ilionekana kuwa ya muhimu ili kuelewa tamaduni za kigeni,” laripoti The Daily Yomiuri. Chuo Kikuu hicho, ambacho kilikuwa tayari kimepata sifa kwa upande wa fasihi, kiliongeza masomo ya Biblia katika mafunzo yacho kuanzia masomo ya masika ya 1993. Tangu Idara ya Elimu ipatie vyuo vikuu uhuru zaidi wa kurekebisha programu za mafundisho yao miaka miwili iliyopita, hiki kilikuwa kisa cha kwanza katika Japani ambapo wanafunzi waliruhusiwa kushiriki katika kutayarisha mwongozo wa masomo ya shule.
Mkazo wa Kukimbia Polepole
Kukimbia poleple hulaza viungo vya mwili mara kumi zaidi ya kuendesha baiskeli, kulingana na uchunguzi kutoka Kliniki ya Chuo Kikuu cha Kurekebi-Mifupa katika Berlin, Ujerumani. Wakitumia chombo cha nyonga bandia hasa kwa kusudi hili, wanasayansi katika chuo kikuu hicho walifaulu kwa mara ya kwanza katika kupima mkazo uliotiwa kwenye viungo mbalimbali wakati wa utendaji mbalimbali. “Ijapokuwa ilikuwa ikifikiriwa kwa ujumla kwamba wenye kukimbia polepole hukaza sana kano na viungo vyao kuliko watu wanaoendesha baiskeli,” laripoti Süddeutsche Zeitung, “hata watafiti wenyewe walishangazwa na tofauti hiyo kubwa.”
Umalaya wa Watoto Wasitawi Katika Esia
“Ukiwa na umri wa miaka kumi wewe ni mtu mzima mchanga, ukiwa na miaka ishirini wewe ni mwanamke mzee, ukiwa na miaka thelathini wewe umekufa.” Huo, kulingana na gazeti National Geographic Traveler, ni msemo ujulikanao sana juu ya watoto malaya wa Bangkok, Thailand. Kuna watoto malaya karibu milioni moja katika Esia, wengi wao wako chini ya umri wa miaka kumi. Utalii, lataarifu gazeti hilo, unategemeza biashara hiyo isiyo halali. Mashirika mengi ya wanaovutiwa kingono na watoto katika Australia, Japani, United States, na Ulaya Magharibi hutegemeza ‘utalii wa ngono’ kwenye nchi za Esia. The Times la London liliripoti hivi majuzi kwamba kila mwaka wasichana wapatao 5,000 “huandikishwa” kutoka milima ya Nepal kuwa malaya katika nyumba za makahaba za Bombay, India. Wanaokadiriwa kuwa 200,000 wako huko sasa, karibu nusu yao wakiwa wameambukizwa HIV, vile virusi vinavyosababisha UKIMWI. Biashara iliyopangwa vizuri hata hupeleka wasichana Ulaya Magharibi na United States.
Ibada ya Haraka
“Kwa nini ibada ya kanisa ianze saa tano asubuhi na kuchukua muda wa saa moja hivi au zaidi? Swali hilo, lililozushwa hivi majuzi na mhudumu wa kanisa la Baptisti katika Florida, U.S.A., kulingana na ripoti ya Associated Press katika Times-West Virginian, limeongoza kwenye suluhisho la kutabirika. Kasisi huyo atoa “Ibada ya Haraka Iliyo Kamili ya Dakika 22” ambayo anadai kuwa, hiyo, itampa wakati wa “kutoa mahubiri, kuongoza wimbo, kusoma Maandiko, kusema sala na kuacha kutaniko lake litoke kanisani.” Mahubiri yenyewe yatakuwa ya dakika nane, yakimruhusu mhudumu huyo “kufanyia kanisa yale ambayo [mkahawa wa chakula cha haraka] wa McDonald ulifanyia chakula,” kulingana na shirika la habari la Associated Press. Hata hivyo, ripoti hiyo yaongezea kwamba, “wakati mwingi utatengwa kwa ajili ya kupitisha kisahani cha kukusanya pesa.”
Kukomesha Homa ya Kidinga Popo
Uchunguzi katika Thailand waonyesha tumaini fulani la kudhibiti homa ya kidinga popo, ugonjwa ambao unadhoofisha karibu watu 100,000 katika nchi hiyo kila mwaka. Homa ya kuambukizwa na mbu ni vigumu kufisha, lakini katika Kusini mwa Esia unajulikana kuwa ugonjwa wa kuua kwa watoto. Ile Aëdes aegypti hueneza homa ya kidinga popo. Hata hivyo, programu zinazotegemea dawa za kuua wadudu ili kukomesha ugonjwa huo zimethibitika kuwa bila matokeo, ghali, na zisizopendwa, kulingana na Medical Post la Kanada. Hivi karibuni, wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Mahidol cha Bangkok wamepata kwamba mahali pa kawaida na pa maana pa mbu kuzalia palikuwa katika mitungi mikubwa ya kuhifadhia maji ambayo watu wanaweka nyumbani kwao. Kwa hiyo walitengeneza vifuniko vya mitungi hiyo ambavyo vyatoshea vizuri kabisa kama kofia za kuvaa mtu anapooga na hali vinaruhusu kutoa maji na kuijaza tena. Vinapotumiwa vizuri, vifuniko hivyo vilikuwa na matokeo kwa asilimia 100 kwa kuua viluwiluwi hivyo vyenye kueneza ugonjwa, wanasayansi waligundua. Vijiji vyenye kutumia vifuniko hivyo viliona kiwango cha homa ya kidinga popo kikishuka kutoka kati ya asilimia 11 na 22 hadi asilimia 0.4
Kupunguza Mkazo wa Macho
Ikiwa unasumbuka na mkazo wa macho kwa kutazama kiwambo cha televisheni au kompyuta yako, unaweza kupata kitulizo kwa kuiweka tu chini na kuielekeza juu. Pendekezo hili, kutoka New England Journal of Medicine, lategemea lile wazo la kwamba watu hupepesa macho yao mara chache na kuyafungua wazi zaidi wanapotazama kwa ulalo kuliko wanapotazama kuelekea chini. Kupepesa mara chache kwamaanisha kutia macho umaji-maji mara chache, na kuyafungua wazi zaidi huongeza kukauka kwa tabaka yenye kulinda ya umajimaji ya macho.
Makanisa Yauzwa
Kanisa la Roma Katoliki katika Italia halijui hasa lina majengo mangapi ya kidini, lakini jambo moja ni hakika: Haliwezi kuyasitawisha yote. Hesabu ya majengo ya kanisa yaliyoachwa yanayooza polepole inaongezeka kila siku. Hivyo basi, Pietro Antonio Garlato, msimamizi wa Baraza la Urithi wa Kitamaduni wa Kanisa la Italia, alisema kwamba kanisa linafikiria kama liuze majengo kadhaa ambayo hayatumiwi tena kwa makusudi ya kidini. Ni makanisa mangapi yatakayouzwa? “Kisio la kijuujuu la kwanza,” akaelezea askofu katika Il Messaggero, “laonyesha hesabu ya asilimia 10” la makanisa zaidi ya 95,000 katika Italia.
Kelele Kupita Kiasi
Uchunguzi wa karibuni wa tatizo la kelele katika Berlin, Ujerumani, limepata kwamba watu wengi huishi na viwango hatari vya kelele za juu sana. Gazeti Süddeutsche Zeitung laandika kwamba asilimia 40 ya nyumba za jijini zimo kando ya barabara kuu, “ambapo karibu sikuzote kuna kelele nyingi sana.” Kwa kweli, wakati wa mchana kiwango cha kelele katika asilimia 95 ya vyumba vinavyokabili barabara ni chenye kupita juu zaidi kile kipimo cha sauti cha 65 kinachokubalika. Katika moja kati ya tano ya vyumba hivyo, kiwango cha kelele ni kipimo cha sauti cha 75. Viwango vya kelele za saa za usiku pia vilikuwa juu sana katika karibu barabara zote zilizochunguzwa. Kelele za juu zinajulikana kwa kuvuruga mawasiliano, ukazaji fikira, na uwezo wa kutumia weledi.