Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Vitu vya Kuchezea vya Afrika Ilikuwa makala yenye kupendeza sana kama nini ya “Vitu vya Kuchezea vya Afrika Bila Malipo”! (Machi 22, 1993) Nikiwa mwalimu wa sanaa, najua jinsi lilivyo jambo la maana kuchochea hali ya ubuni ya watoto katika kizazi hiki cha televisheni na michezo ya kompyuta. Wazazi watumiapo wakati ili kutengeneza vitu pamoja na watoto wao, pia wanaweka kumbukumbu zenye kudumu!
D. B., Ujerumani
Nina umri wa miaka saba. Niliipenda makala hiyo, na nilifiri kwamba lilikuwa jambo zuri kwamba [watoto Waafrika] hujitengenezea vitu vyao vya kuchezea! Inaonekana kuwa inafurahisha, na ningependa kujaribu kufanya hivyo.
M. S., United States
Kunajisiwa Mfululizo wenu wa makala za “Kunajisiwa—Hofu Kuu ya Wanawake” ulikuwa murua. (Machi 8, 1993) Nina umri wa miaka 14, na nimesikia juu ya wasichana wachanga zaidi yangu ambao wamenajisiwa. Lakini ni mpaka niliposoma makala hiyo ndipo machozi yaliponidondoka, na nilitambua kwamba jambo hili ni zito kuliko nilivyofikiri. Asanteni sana.
S. B., United States
Wakati wa mwaka wangu wa kwanza katika shule ya sekondari, nilinajisiwa na mtu aliyekuwa “rafiki wa familia.” Kwa miaka michache iliyopita nilikuwa nikifikiri kuwa nilifanya uasherati. Sasa naweza kuona kwamba Yehova ajua halikuwa kosa langu! Nasikitika tu kwa kukosa kupata msaada upesi.
A. S., United States
Programu nyingi hushughulikia kupona kutokana na kunajisiwa, lakini hazisemi jinsi ya kuepuka. Kwa hakika ni muhimu kukinga kuliko kutibu! Kwa upande huo makala hiyo ilinisaidia kwa kiasi kikubwa, na kwa kweli itasaidia wanawake kila mahali ambao ndio wanaoendelea kupatwa na jambo hilo sana.
J. A. M., Brazil
Nilishambuliwa na mtu aliyetaka kuninajisi nje ya nyumba yangu. Nilipigana jinsi sijapata kupigana kamwe na kupiga mayowe nikiita jina la Yehova kwa sauti ya juu na mara nyingi hivi kwamba mbwa walianza kubweka. Mshambulizi wangu hatimaye alichoka na mayowe yangu na akakimbia. Napendekeza kwamba kila mtu afuate madokezo yenu. Ikitegemea hali zinazohusika, matendo yetu yaweza kutokeza tofauti kubwa.
S. P., United States
Karibu miaka 20 iliyopita, nilinajisiwa na mtu ninayemjua. Sikuripoti kamwe kwa sababu niliona haya. Hata sikuongea juu ya jambo hilo hadi miaka mitatu iliyopita nilipotibiwa. Ni wakati huo tu ndipo nilipomwambia mume wangu. Sasa alielewa hisia zangu za kuepuka ngono. Nilipomaliza kusoma makala zenu, nililia kwa shangwe—si kwa uchungu—kwa mara ya kwanza katika miaka 20, na nikamshukuru Yehova.
T. P., United States
Uvumbuzi wa Anga Nimemaliza kusoma makala murua za uvumbuzi wa anga katika matoleo ya Amkeni! ya Septemba 8 1992 Kiingereza. Ijapokuwa sijui mengi kuhusu jambo hili, maelezo yaliyo wazi ambayo mmetoa yamenipendeza sana. Naamini kwamba makala hizo zitatusaidia kuthamini zaidi makusudi ya Yehova kwa ajili ya ainabinadamu tiifu.
W. D. F., Kosta Rika
Tunawaandikia kuwashukuru kwa jitihada ya kukusanya zile makala juu ya uvumbuzi wa anga. Baada ya kusoma makala ya mwisho, tulimshukuru Yehova kwa shangwe, Mungu mjua yote ambaye alipanga ulimwengu wote mzima kwa njia ya ajabu jinsi hiyo. Tunatazamia kwa hamu mfumo mpya, wakati atakapopatia wanadamu watiifu wenye bongo kamilifu fursa ya kuelewa vizuri zaidi ulimwengu wote mzima.
I. N. O na J. N. O., Nigeria