Jinsi ya Kukabiliana na Unajisi
Miaka thelathini na tatu iliyopita Mary alinajisiwa akitishwa kwa kisu. Leo, moyo wa Mary humdunda-dunda na viganja vyake kutokwa jasho anapojaribu kusimulia hayo. “Ni mojawapo jambo lenye kuaibisha sana ambalo mwanamke aweza kupatwa nalo,” yeye akasema huku akilengwa na machozi. “Ni jambo baya sana, lenye kuhofisha.”
KUNAJISIWA kwaweza kuwa mojawapo matukio yenye kuumiza sana kihisiamoyo katika maisha ya mtu, na matokeo yayo yaweza kudumu kwa muda wa maisha yote. Katika uchunguzi mmoja, karibu theluthi moja ya wanajisiwa wote waliookoka waliohojiwa walikuwa wamefikiria kujiua, na wengi wao walisema kwamba ono hilo liliwabadili kabisa.
Athari zaweza kuwa zenye kutisha hasa ikiwa mwanamke alijua mshambulizi wake. Mnajisiwa aliyeshambuliwa na mtu anayemjua huelekea kutopata utegemezo wa wengine kwa sababu ama hasemi kile kilichompata ama asema na hakuna anayeamini kwamba huo ulikuwa unajisi. Kwa kuwa aliumizwa na mtu aliyemtumaini, inaelekea sana kwamba atajilaumu na kushuku uwezo wake wa kukadiri wengine.
Kubali Msaada
Mwanzoni, wanajisiwa wengi wanaookoka huwa na mshtuko na kukana kwamba walinajisiwa. Mwanamke mmoja alinajisiwa muda mfupi kabla ya mtihani muhimu wa koleji. Aliweka ule unajisi kando akilini mwake hadi alipomaliza mtihani. Mwokokaji mwingine wa unajisi alisema: “Sikutaka kukumbuka lolote juu yalo kwa sababu mtu niliyemtumaini aligeuka akanishambulia. Sikujua kwamba ungeweza kunajisiwa na mtu unayemjua. Huenda ikasikika kuwa upuzi, lakini wazo hilo liliniacha nikiwa sina tumaini. Nilihisi nikiwa mpweke sana.”
Wanawake wengine huendelea kukana yale yaliyotukia kwa kutowaambia wengine juu ya kunajisiwa kwao. Wao huficha shambulizi hilo kwa miaka mingi, jambo ambalo huwachelewesha kupona na husababisha matatizo mengine ya kihisiamoyo ambayo mwokokaji huenda asing’amue kwamba yanatokana na unajisi huo.
Mara nyingi kupona hakuanzi hadi unapozungumza na wengine. Rafiki unayemtumaini aweza kukusaidia kuona kwamba kile kilichokupata kilikuwa kunajisiwa kwa kweli na hakukuwa kosa lako. Mithali ya kale husema: “Rafiki hupenda sikuzote; na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.” (Mithali 17:17) Pia, wachungaji wa kiroho wanaweza kuthibitika kuwa “mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba.” (Isaya 32:2; 1 Wathesalonike 5:14) Kuhusu wanajisiwa wengine, kuwasiliana na kituo cha unajisi au mshauri mstadi kwaweza kuhitajiwa ili kuwasaidia kuelewa hisi zao.
Mara nyingi waokokaji huogopa kuzungumzia kunajisiwa kwao kwa sababu ya hisi za hatia, hasa ikiwa waliamshwa kingono wakati wa shambulio hilo. Huenda wakahisi kuwa wachafu na wasiofaa kitu na kujilaumu kwa kunajisiwa—hata ingawa hakuna mwingine anayestahili kulaumiwa ila mnajisi.
“Kuwa na rafiki mzuri wa kuzungumza naye kulileta mabadiliko,” akasema Mary, aliyezungumza na Mkristo mwenzake. “Ningeweza kuzungumza naye na nisihisi nimechafuka na nimeaibika kwa kunajisiwa.”
Mtegemeze
Kwa upande mwingine, hakungefaa na si kuonyesha upendo kwa marafiki wa mnajisiwa kueleza mambo vingine au kujiamulia wenyewe ikiwa “kwa kweli alinajisiwa.” Usidokeze kamwe kwamba alifurahia au kwamba kulikuwa kukosa adili. Jambo la maana sana ambalo rafiki aweza kufanya anapoulizwa asaidie ni kumwamini. Mpe uhakika. Sikiliza wakati anapotaka kuzungumza, lakini usimsonge akuambie mambo yote.
Ikiwa unajisi huo ulitukia karibuni, marafiki waweza kusaidia mnajisiwa apate matibabu na kuandaa mahali salama pa kuishi. Mtie moyo aripoti unajisi huo, lakini mwache afanye maamuzi. Ametoka tu kupata ono ambalo kwalo amenyang’anywa udhibiti wote. Acha apate kiasi cha udhibiti huo tena kwa kumwacha achague jambo la kufanya.
Familia za wanajisiwa lazima zikinze msukumo wa kuitikia hali hiyo kihisiamoyo. Huenda wakataka kupata mtu wa kulaumu kwa unajisi huo au watake kumlipiza kisasi mnajisi, mambo ambayo hayamsaidii mnajisiwa. (Warumi 12:19) Kumlaumu yeyote isipokuwa mnajisi kwa yale yaliyotukia ni bure, na kutaka kulipiza kisasi ni hatari. Kutafanya mwokokaji awe na wasiwasi juu ya usalama wa wapendwa wake badala ya kukazia juu ya kupona kwake.
Familia zapaswa pia kutambua kwamba waokokaji wengi huona ngono kwa njia tofauti baada ya kunajisiwa. Akilini mwao, ngono imekuwa silaha, na huenda wakaona vigumu kufanya ngono kwa wakati fulani, hata na mtu wanayempenda na kumtumaini. Hivyo, mume hapaswi kumhimiza mke wake arejee kwenye utendaji wa ngono hadi anapokuwa tayari. (1 Petro 3:7) Familia zaweza kusaidia kwa kujenga sifa ya mwanamke kijana na kumwonyesha kwamba bado anapendwa na kuheshimiwa yajapokuwa yale yaliyompata. Utegemezo mwendelevu utahitajiwa wakati mwokokaji anapopitia zile hatua ambazo wakati mwingine huwa ndefu kuelekea kupona kihisiamoyo.
Kukabiliana na Woga na Mshuko wa Moyo
Wanawake ambao wamenajisiwa husema kwamba itikio lao lenye kuwalemea zaidi ni woga. Wanajisiwa wengi hawakutarajia kuokoka ushambulizi huo. Baadaye huenda wakaogopa kunajisiwa tena au huenda hata wakaogopa kumwona mnajisi bila kukusudia.
Woga uliohisiwa wakati wa kunajisiwa waweza kuletwa na sauti, harufu, na mahali palepale. Ikiwa mwanamke alinajisiwa katika kijia chembamba, huenda akaogopa kuenda katika kijia. Ikiwa alinajisiwa akiwa nyumbani, huenda asihisi akiwa salama humo tena na huenda akalazimika kuhama. Hata kunusa marashi yanayofanana na yale ambayo mnajisi alikuwa nayo kwaweza kuleta kumbukumbu zisizopendeza.
Ingawa ni visa vichache vya unajisi vinavyotokeza kutungwa mimba, wanajisiwa wengi huhofu juu ya uwezekano walo. Kwa haki, wengi pia huona wasiwasi kuhusu ikiwa wameambukizwa ugonjwa wa zinaa. Karibu nusu hupata hisi za kushuka moyo, kukosa tumaini, na kutojistahi, ambako kwaweza kuendelea kwa majuma kadha hadi miezi kadha. Huenda pia wakang’ang’ana na mahangaiko, hofu, na wasiwasi.
Ingawa huenda wanawake wasiweze kuzuia kunajisiwa, baadaye wanaweza kudhibiti fikira, hisi, na maitikio yao kwa ushambulizi huo. Wanaweza kujifunza kubadili fikira hasi kwa maoni chanya juu yao.
“Badala ya kujiambia jinsi ulivyo mdhaifu, bure, au hoi, jifunze kujiambia jinsi unafanikiwa na jinsi umefanya maendeleo tangu punde baada ya kushambuliwa,” akasema Linda Ledray katika Recovering From Rape. “Kila siku ambayo unahisi hulemewi sana na fikira na hisi hasi, jiambie, ‘Ninajifunza kudhibiti mambo.’”
Woga waweza pia kushindwa kwa kujifunza kutambulisha kile hasa kinachouleta. Mnajisiwa anapotambua kianzishaji, aweza kujiuliza, Woga huo ni halisi kadiri gani? Kwa mfano, akimwona mtu anayefanana na yule mnajisi, anaweza kujikumbusha kwamba yeye si ndiye mnajisi na kwamba hatamuumiza.
Njia nyingine inayopendekezwa ya kumaliza woga ni kuondoa hisi ya woga kwa utaratibu. Mwanamke afanya orodha ya utendaji au hali ambazo aogopa, akizipanga kuanzia zile zisizomwogopesha sana hadi zile zenye kumwogopesha sana. Kisha ajiwaza mwenyewe akiwa katika hali isiyomwogopesha sana hadi inapoonekana kuwa haimwogopeshi tena. Kisha asonga katika orodha hiyo hadi anapostarehe anapofikiria hali zote.
Kwa msaada wa rafiki, anaweza kusonga mbele kufanya utendaji huo katika maisha halisi, kama vile kuenda nje ya nyumba usiku au kuwa peke yake. Hatimaye anaweza kudhibiti woga wake ili kwamba usiathiri maisha yake ya kila siku. Hata hivyo, kuogopa kufanya utendaji fulani—kama vile kupitia kijia chembamba chenye giza usiku—ni jambo la kawaida, na kusingekuwa na kusudi kujaribu kushinda wasiwasi katika hali hizo.
Kuelekeza Hasira Upande Mwingine
Waokokaji wa unajisi pia hupata hisi za hasira, ambazo kwanza zaweza kuelekezewa wanaume wote lakini, kadiri wakati upitavyo, mara nyingi huelekezewa mnajisi. Mara nyingi watu waliokasirika huelekeza hasira yao kotekote. Wengine huitikia kwa kufichilia hisi zao. Hata hivyo, hasira yaweza kuelekezwa ifaavyo na njia ambayo mtu anashughulika na hasira yake yaweza kumsaidia apone. Maandiko husema: “Mwe na hasira, ila msitende dhambi.”—Waefeso 4:26.
Kwanza, waokokaji hawahitaji kuogopa kuonyesha hasira. Wanaweza kuzungumza juu yayo kwa wengine. Kuhusika katika shughuli za kisheria au kuweka rekodi kwaweza kuwa njia ya kutolea hasira. Wanaweza pia kuondoa hasira kwa kufanya utendaji wa kimwili, kama vile tenisi, mpira wa raketi, mpira wa mikono, kutembea, kukimbia, kuendesha baiskeli, au kuogelea, ambao una manufaa za ziada za kusaidia kushinda mshuko wa moyo.
Unaweza kuanza tena kudhibiti maisha yako.
Ni Nini Kitakomesha Unajisi?
Kukomesha unajisi kunatia mengi zaidi ya wanawake kuepuka wanajisi na kupigana nao. “Ni wanaume wanaonajisi na wanaume wakiwa pamoja ndio wenye uwezo wa kukomesha unajisi,” akasema mwandikaji Timothy Beneke katika kitabu chake Men on Rape.
Unajisi hautakoma hadi wanaume watakapoacha kuwatenda wanawake kama vitu tu na kujifunza kwamba mahusiano yenye mafanikio hayategemei usimamizi wenye jeuri. Kwa mtu mmoja mmoja, wanaume wakomavu wanaweza kuongea na kuwavuta wanaume wengine. Wanaume na wanawake pia wanaweza kukataa kukubali mizaha ya kingono, kutazama sinema zinazoonyesha uchokozi wa kingono, au kuunga mkono watangazaji wanaotumia ngono ili kuuza bidhaa. Biblia hushauri: “Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wala kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu, wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru.”—Waefeso 5:3, 4.
Wazazi wanaweza kufunza kustahi wanawake kwa mfano wao. Wanaweza kufunza wana wao kuwaona wanawake kama vile Yehova Mungu anavyowaona. Mungu hana upendeleo. (Matendo 10:34) Wazazi wanaweza kuwafunza wana wao kuwa marafiki wa wanawake na kujihisi wamestarehe kati yao, kama Yesu alivyofanya. Wanaweza kuwafunza wana wao kwamba ngono ni tendo la upole la upendo kuelekea mwenzi wa ndoa tu. Wazazi wanaweza kuonyesha waziwazi kwamba jeuri haitavumiliwa, wala kuwatawala wengine hakutathaminiwa. (Zaburi 11:5) Wanaweza kuwatia moyo watoto wao kuzungumza mambo ya ngono kwa wazi nao na kukinza msongo wa kufanya ngono.
Tatizo Litakalokwisha Hivi Karibuni
Hata hivyo, unajisi hautakoma bila mabadiliko makubwa katika jumuiya ya ulimwengu. “Unajisi si tatizo la mtu mmoja tu [bali] ni tatizo la familia, tatizo la jumuiya, na pia tatizo la kitaifa,” akasema mtafiti Linda Ledray.
Biblia huahidi jumuiya ya ulimwenguni pote isiyo na jeuri, ambapo mwanadamu ‘hatamtawala tena mwingine kwa hasara yake.’ (Mhubiri 8:9; Isaya 60:18) Wakati utakuja hivi karibuni ambapo Yehova Mungu hatavumilia zaidi utumizi mbaya wa uwezo, kutia unajisi.—Zaburi 37:9, 20.
Katika jumuiya hiyo ya ulimwengu mpya, watu wote wataelimishwa kuwa wenye amani na watapendana bila kujali jinsia, kabila, au taifa. (Isaya 54:13) Wakati huo, watu wapole wataishi bila woga wa marafiki au watu wasiowajua na “watajifurahisha kwa wingi wa amani.”—Zaburi 37:11
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Ukinajisiwa
□ Tafuta msaada wa kitiba.
□ Ukitaka, omba kwamba mshauri wa wanajisiwa aandamane nawe katika shughuli za kitiba na kisheria ikiwa anapatikana.
□ Waite polisi haraka iwezekanavyo. Washauri hupendekeza kuripoti kwa ajili ya usalama wako na usalama wa wanawake wengine. Kuripoti ni tofauti na kushtaki, lakini ukichagua kushtaki baadaye, kesi yako itadhoofishwa kwa ripoti iliyocheleweshwa.
□ Hifadhi ushahidi. Usioge, usibadilishe mavazi, usioshe au kuchana nywele, wala usiharibu alama za vidole au alama za miguu.
□ Wafanyakazi wa tiba watakusanya ushahidi na watajaribu kuona ikiwa kuna magonjwa ya zinaa au utungaji mimba. Ikiwa wanakupa dawa za kuzuia kutungwa mimba, zinazomezwa baada ya ngono, Wakristo wapaswa watambue kwamba dawa hizo zaweza kufanya mwili utungue mbegu iliyotungwa.
□ Fanya yote uwezayo ili uhisi salama—badilisha kufuli, ishi na rafiki, imarisha mlango wako—iwe unaonekana kuwa unatenda kupita kiasi au la.
□ Zaidi ya yote, yategemee Maandiko upate faraja, ukisali kwa Yehova, hata kuita jina lake kwa sauti, wakati na baada ya ushambulizi. Wategemee wazee na washiriki wa karibu kundini ili wakutegemeze. Hudhuria mikutano iwapo yawezekana, na utafute ushirika wa Wakristo wenzi katika huduma.