Jinsi ya Kukinza Kunajisiwa
Eric alikuwa mrefu na mwenye sura nzuri, na alitoka kwa familia tajiri. Lori alikuwa mwenye miaka 19 na alikuwa amealikwa kwenye matembezi ya kirafiki na Eric pamoja na mwenzake wa chumbani akiwa na mwenzi wake. Alifika kwenye kikusanyiko kwenye nyumba ya Eric, lakini bila kujua, wale wenzi wawili walikuwa wameamua kwamba hawangekuja. Upesi, wageni wale wengine walianza kuondoka kwenye karamu.
“Nikaanza kufikiri, ‘Jambo fulani si sawa, kuna jambo baya linaloendelea,’ lakini nililipuuza,” yeye akasema.
Mara Erik alipokwisha kuwa na Lori peke yake, alimnajisi. Lori hakuripoti unajisi huo kwa polisi, na baadaye alihama umbali wa kilomita 240 ili kuepuka kumwona Eric tena. Mwaka mmoja baadaye, bado alikuwa na woga wa kwenda matembezi ya kirafiki.
UNAJISI ni tisho linaloongezeka, na ulinzi bora wa mwanamke ni kujua hilo na kujitayarisha. Si kila hali ya unajisi inayoweza kutarajiwa, lakini kujua jinsi wanajisi hufikiri na kupanga ushambulizi wao kwaweza kukusaidia utambue ishara zenye kuonya.a Mithali ya kale husema: “Watu wenye busara wataona taabu ikija na kuiepuka, lakini watu wasiotumia busara wataingia kwenye taabu na kughairi baadaye.”—Mithali 27:12, Today’s English Version.
Njia bora zaidi ya kuepuka hali ya kunajisiwa ni kuepuka wanajisi. Ni lazima utambue juu ya kawaida ya tabia ya mwanamume—hata yule unayemjua vema—inayoweza kumtambulisha kuwa aweza kunajisi. (Ona sanduku, ukurasa 7.) Wanaume wengine watatumia mtindo wa mavazi ya mwanamke au hiari yake ya kuwa peke yake naye kuwa kisababu cha kumnajisi. Ingawa mwanamke halaumiki ikiwa mwanamume ana maoni hayo yaliyopotoka, yeye angekuwa mwenye hekima kutambua mitazamo hiyo.
Usiwe peke yako na mwanamume usiyemjua vema. (Tumia hekima hata kwa yule unayemjua vema.) Mnajisi usiyemjua aweza kuja kwenye nyumba yako akijifanya kuwa mrekebishaji. Chunguza hati zake za kudhibitisha uhalali wake. Mnajisi unayemjua mara nyingi hufanya mnajisiwa awe peke yake kwa kubuni kazi zinazotaka azuru nyumba yake au kwa kudanganya kwamba kutakuwa na kikundi cha watu katika mahali anapopanga kukutana nawe. Usidanganyike.
Ili kuepuka matatizo katika hali za matembezi ya kirafiki, tembeeni katika vikundi au mkiwa na yule anayewasindikiza. Mjue rafiki yako vema, na uweke mipaka imara juu ya kiasi cha ukaribiano wa kimwili, ikiwa kuna wowote ambao utaruhusu. Tahadhari kunywa kileo chochote! Huwezi kuwa macho kuona hatari ikiwa kufikiri kwako kumeathiriwa. (Linganisha Mithali 23:29-35.) Tumaini silika zako. Ikiwa unakosa starehe ukiwa na mtu fulani, usidhani hawezi kutenda vibaya. Ondoka.
Wazazi wa matineja hasa wanahitaji kuzungumza na watoto wao juu ya kukinza kunajisiwa, wakisema wazi kuhusu hali za hatari kwa sababu wanajisi na wanajisiwa wengi ni wachanga.
Tenda Haraka
Si hali zote za unajisi zinazoweza kutarajiwa. Bila kujua, huenda ukajipata ukiwa peke yako ukikabili mwanamume mwenye nguvu zaidi yako anayekusudia kukulazimisha mfanye ngono. Basi iweje?
Tenda haraka, na ukumbuke lengo lako: kutoroka. Mara nyingi mnajisi hujaribu mnajisiwa kabla ya kuamua kushambulia, kwa hiyo ni ja-mbo la maana kuharibu mipango yake upesi iwezekanavyo kabla hajapata uhakika wa kutosha aweze kutenda. Wastadi wa unajisi hutoa njia mbili za kutenda: ukinzani usiotumia nguvu na ule unaotumia nguvu. Unaweza kujaribu ule usiotumia nguvu kwanza, na kisha baada ya kushindwa, ujaribu ukinzani wa kutumia nguvu.
Ukinzani usiotumia nguvu waweza kutia ndani kununua wakati kwa kuzungumza na mnajisi au kujifanya kwamba una ugonjwa wa zinaa hadi kumtapikia mshambulizi wako. (Linganisha 1 Samweli 21:12, 13.) “Mbinu zinategemea tu pale ubuni wa mtu unafika,” akaandika Gerard Whittemore katika kitabu chake Street Wisdom for Women: A Handbook for Urban Survival.
Mbinu zisizo za kutumia nguvu—ambazo zatia ndani kila kitu isipokuwa kupigana kimwili na mnajisi—zahitaji kufikiri kwa utulivu na kwapaswa kukusudiwe kumkengeusha au kumtuliza mshambulizi. Ikiwa ukinzani wako unafanya mshambulizi wako akasirike na kuwa mwenye jeuri zaidi, jaribu jambo jingine. Hata hivyo, usiruhusu ulazimishwe kwenda kwenye sehemu iliyo ya upweke zaidi unapofikiri. Na kumbuka mojawapo njia zenye matokeo zaidi za ukinzani wa kutumia nguvu—kupiga yowe—Linganisha Kumbukumbu la Torati 22:23-27.
Njia nyingine ni kutenda kwa njia hasi kwa kutumia nguvu. Mwambie mshambulizi wako katika maneno dhahiri kwamba hutakubali makusudio yake. Katika hali za unajisi wa matembezi ya kirafiki, huenda ukajaribu mbinu ya kushtua kwa kusema wazi ushambulizi huo ni nini. Kupaza sauti, “Huu ni unajisi! Nitawaita polisi!” kwaweza kumfanya yule ambaye angenajisi afikiri kwa uangalifu kuhusu kusonga mbele.
Pigana
Ikiwa kuzungumza hakufanikiwi, usiogope kukinza kwa kutumia nguvu. Hiyo haimaanishi kwamba utaelekea kuumizwa au kuuawa, wala kujitiisha hakukuhakikishii usalama wako. Kwa hiyo, wastadi wengi wa unajisi hushauri kukinza kwa nguvu.
Kupigana kwaweza kuwa kugumu kwa wanawake kwa sababu tangu utoto wamezoea kuwa wapole, watulivu, na wenye kujitiisha hata wanapotishwa kwa nguvu. Hivyo, unahitaji kuamua kimbele kwamba utakinzana ili kwamba usipoteze wakati muhimu kwa kusitasita wakati wa kushambuliwa.
Unahitaji kukasirika kwa mtu kukutisha au kukusonga. Unahitaji kung’amua kwamba ushambulizi huo umepangiwa kimbele, na mnajisi anakutegemea uweze kujitiisha. Kasirika, si uogope. “Woga wako ndio silaha kubwa zaidi ya mshambulizi,” akasema mtafiti Linda Ledray. Usiwe na wasiwasi kwamba unatenda kupita kiasi au kwamba huenda ukaonekana kuwa mjinga. “Afadhali kuwa mfidhuli kuliko kunajisiwa,” akasema mstadi mmoja. Wanawake ambao wamewakinza wanajisi kwa kufanikiwa mara nyingi walifanya hivyo kwa kutumia nguvu na wakajaribu mbinu zaidi ya moja, kutia ndani kuuma, kupiga mateke, na kupiga mayowe.
Ikiwa unashindwa kumkinza mnajisi, kazia juu ya kuweza kumtambua baadaye. Ikiwezekana, kumkwaruza au kurarua nguo zake kutaacha ushahidi wa damu na vitu vya kuweza kumtambulisha. Lakini kufikia hatua hiyo, huenda usiweze kupigana zaidi tena. Ikiwa ni hivyo, “usijilaumu kwamba ‘ulimwacha’ akakunajisi,” akasema Robin Warshaw katika I Never Called It Rape. “Hauhitaji kupata jeraha au kifo ili ‘kuthibitisha’ ulinajisiwa.”
[Maelezo ya Chini]
a Hakuna hali mbili zinazofanana, na hakuna shauri la kukinza lisilopenyeka. Hata wastadi wa unajisi hutofautiana maoni juu ya ni kiasi gani na aina gani ya ukinzani mnajisiwa apaswa atoe wakati wa kushambuliwa.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Maelezo Juu ya Anayeelekea Kuwa Mnajisi
□ Hukuumiza kihisiamoyo kwa kukutukana, kupuuza maoni yako, au kukasirika au kuhamaki unapotoa dokezo.
□ Hujaribu kudhibiti mambo fulani ya maisha yako, kama vile jinsi unavyovaa na marafiki wako ni nani, ataka kufanya maamuzi yote kwenye matembezi ya kirafiki, kama vile mahali pa kula au sinema gani ya kutazamwa.
□ Huwa na wivu bila sababu.
□ Huwadunisha wanawake kwa ujumla.
□ Hulewa au “kusisimuliwa na pombe” na ajaribu kukufanya ufanye vivyo hivyo.
□ Hukusonga mwe naye peke yenu au mfanye ngono.
□ Haruhusu ulipe gharama za matembezi ya kirafiki na hukasirika ukijaribu kulipa.
□ Ni mwenye jeuri kimwili hata katika njia ndogo, kama vile kukamata na kusukuma.
□ Hukutia wasiwasi kwa kuketi karibu zaidi, kukuzuia njia, kukugusa unapokataa kuguswa, au kuzungumza kana kwamba anakujua sana kuliko vile anavyokujua hasa.
□ Hawezi kushughulikia mfadhaiko bila kukasirika.
□ Hakuoni kama mtu aliye sawa naye.
□ Hufurahia kuwa na silaha na hupenda kuwa mkatili kwa wanyama, watoto, au watu anaoweza kuchokoza.
Kutoka kwa I Never Called It Rape, cha Robin Warshaw.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wanawake waliokinza wanajisi kwa mafanikio mara nyingi walifanya hivyo kwa kutumia nguvu na wakajaribu mbinu zaidi ya moja