Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 3/8 kur. 3-5
  • Mambo Halisi ya Unajisi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mambo Halisi ya Unajisi
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mbona Kukawa Ongezeko Hilo?
  • “Unajisi wa Pili”
  • Ngano na Uhalisi wa Unajisi
  • Jinsi ya Kukabiliana na Unajisi
    Amkeni!—1993
  • Kuepuka Msiba Wa Kulalwa Kinguvu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1982
  • Jinsi ya Kukinza Kunajisiwa
    Amkeni!—1993
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 3/8 kur. 3-5

Mambo Halisi ya Unajisi

KATIKA muda unaokuchukua kusoma hadi mwisho wa ukurasa huu, mwanamke mmoja atakuwa amenajisiwa mahali fulani katika United States. Atakuwa peke yake na atatishwa kwa tendo la jeuri lenye kuaibisha na mtu fulani ambaye labda amjua. Huenda akapigwa. Huenda akakinza. Bila shaka atahofia kuuawa.

Unajisi ni uhalifu wa jeuri unaokua haraka sana katika United States, ambayo tayari ina kimojapo kiwango cha juu zaidi cha unajisi ulimwenguni. Kulingana na ripoti za polisi, visa 16 vya kujaribu kunajisi hutokea, na wanawake 10 hunajisiwa kila saa moja. Ongezea hilo kwenye uhakika wa kwamba unajisi usioripotiwa waweza kuwa mara kumi zaidi!

United States si ndiyo nchi pekee yenye tarakimu hizo zenye kuhofisha. Katika Ufaransa idadi ya wanajisiwa walioripoti kuwa walinajisiwa ilipanda kwa asilimia 62 kati ya 1985 na 1990. Kufikia 1990, visa vya unajisi viliongezeka mara mbili katika Kanada kufikia 27,000 katika miaka sita tu. Ujerumani iliripoti kisa kimoja cha unajisi wa wanawake kwa kila dakika saba.

Unajisi huumiza wanaume wasio na hatia pia.a Wanaume “huteseka kwa kuishi katika jumuiya ambapo nusu ya idadi ya watu wana sababu nzuri za kuwa wenye chuki, shuku, na woga,” akasema mwanasaikolojia Elizabeth Powell. Huenda wao pia wakaathiriwa kwa kuwajibika kuishi wakiwahofia wake, mama, dada, binti, na marafiki zao, au wakalazimika kukabiliana na hisi za hatia na uchungu wakati mtu wanayependa anaponajisiwa.

Mbona Kukawa Ongezeko Hilo?

Unajisi husitawi katika jumuiya zinazokubali jeuri na utumizi mbaya wa ngono kwa wanawake. Katika nchi kadhaa, tangu uchanga wao, wanaume na wanawake hupewa ujumbe wenye kuharibu usio wa kweli kuhusu ngono, kupitia vyombo vya habari, familia, na marika wao. Wao hujifunza mawazo yenye sumu kwamba ngono na jeuri zinafungamana na kwamba wanawake wako ili kuandalia wanaume uradhi wa kingono, bila kujali mapenzi ya wanawake.

Angalia mtazamo wa Jay, karani wa faili mwenye miaka 23. “Jumuiya husema kwamba ni lazima uwe na ngono maridhawa na wanawake wengi tofauti-tofauti ili uwe mwanamume kabambe,” yeye akasema. “Ni nini hutukia ikiwa hufanyi hivyo? Basi je, wewe ni mwanamume kabambe?” Kwa sababu ya msongo huo, ikiwa mwanamke angemkasirisha au kumfadhaisha, labda angemnajisi.

Mitazamo hiyo ya jeuri na uchokozi dhidi ya wanawake ni ya kawaida katika jumuiya zenye unajisi mwingi, aamini mtafiti Linda Ledray. “Sanasana mnajisi anaigiza tu hati inayokubalika ya jumuiya,” yeye akasema. Sinema na televisheni zimefanyiza pia hati hiyo ya jumuiya yenye kuharibu. Unajisi ni kichwa kikuu cha kawaida katika pornografia, lakini pornografia si ndiyo kisababishi pekee. Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba filamu za jeuri zisizo na mambo ya ngono hufanya kuwe na mitazamo yenye uchokozi zaidi kuelekea wanawake kuliko filamu zenye upotovu wa ngono lakini bila jeuri. Televisheni inahusishwa pia wakati “inapoonyesha ngono yenye kudhibiti mwingine vibaya inayoweza kupatikana popote,” Powell akasema. Ni ujumbe upi unaotoka kwa vyombo vya habari? “Unapokasirika, umiza mtu.”

Ujumbe huo hutumiwa katika mahusiano ya kila siku, kwa matokeo yenye msiba. Katika ulimwengu unaozidi kuwa wenye kuendekeza, mara nyingi wanaume huhisi kwamba wanawake wanawawia ngono, hasa ikiwa mwanamume amnunulia vitu mwanamke au mwanzoni alionekana kuwa alikubali madokezo yake ya kingono.

“Kwa habari ya ngono, kusema ‘la’ mara nyingi huwa hakumaanishi kitu wakati maneno hayo yanaposemwa na mwanamke,” asema mwandishi habari Robin Warshaw. Na mara nyingi, tokeo ni kunajisiwa.

“Unajisi wa Pili”

Kathi alikuwa mwenye umri wa miaka 15 aliponajisiwa na washiriki watatu wa timu ya magongo ya shule yao ya upili. Familia yake ilipopeleka mashtaka mahakamani, yeye aliepukwa na kuudhiwa na marafiki, majirani, na watu asiowajua. “Unaweza kutarajia wavulana watende kivulana,” familia hiyo ikaambiwa. Shuleni Kathi alitukanwa, na ujumbe wenye kutisha uliachwa kwenye kabati yake. Wale waliomnajisi walipewa adhabu ya kufanyiwa uchunguzi na kufanya kazi ya jumuiya na wakafanikiwa kuwa wanamichezo mashuhuri wa shule hiyo. Kathi aliadhibiwa kwa kuudhiwa-udhiwa miezi mingi. Hatimaye alijiua.

Kisa cha Kathi ni mfano wenye msiba wa vile mara nyingi wanajisiwa hutendwa vibaya kwanza kimwili na mnajisi, kisha kihisiamoyo na wengine. Wanawake wengi hupata kwamba mitazamo na mawazo yasiyofaa kuhusu unajisi hufanya wanajisiwa walaumiwe kwa ajili ya uhalifu huo. Marafiki, familia, polisi, madaktari, mahakimu, na wasaidizi wa mahakimu—wale wanaopaswa kusaidia mnajisiwa—waweza kuwa na mawazo hayo yasiyofaa na kumuumiza mnajisiwa karibu kwa kiasi kilekile alichoumizwa na mnajisi. Tatizo la lawama ni kubwa sana hivi kwamba wengine wameliita “unajisi wa pili.”

Ngano za unajisi hufanyiza hisi bandia ya usalama. Kwa maneno mengine, ikiwa unaweza kupata kosa fulani katika tabia ya mnajisiwa—alivaa nguo zenye kumbana au akaenda nje usiku akiwa peke yake au kwa kweli alitaka kufanya ngono—wewe au wapendwa wako mtakuwa salama ikiwa mwenendo huo unaepukwa; kwa hiyo hutanajisiwa kamwe. Lile wazo jingine, kwamba unajisi ni tendo la jeuri lisilo na sababu ambalo laweza kumpata yeyote, hata awe amevaa kivipi, ni lenye kuhofisha sana kuweza kukubalika.

Mwanamke mmoja aliyenajisiwa na mtu aliyemfikiri kuwa “mwema, mwenye kustahika,” asisitiza: “Jambo lililo mbaya zaidi ni kuamini kwamba hilo halitakupata.”

Ngano na Uhalisi wa Unajisi

Yafuatayo ni baadhi ya mawazo yasiyofaa yanayodumu kuhusu unajisi yanayotumiwa ili kumlaumu mnajisiwa na kuchochea mitazamo inayotia moyo wanajisi:

Ngano: Unajisi hutukia wakati tu mwanamke anaposhambuliwa na mtu asiyemjua.

Uhakika: Wanawake wengi wanaonajisiwa hushambuliwa na mtu wanayemjua waliokuwa wamemtumaini. Uchunguzi mmoja ulipata kwamba asilimia 84 ya wanajisiwa waliwajua washambulizi wao na kwamba asilimia 57 ya unajisi ulitukia kwenye miafikiano ya matembe-zi. Mmoja kati ya wanawake 7 walioolewa atanajisiwa na mume wake mwenyewe.b Unajisi ni wenye jeuri na wenye kushtua kihisiamoyo iwe mshambulizi ni mtu usiyemjua, mwenzi, au mtu uliyepanga naye matembezi.

Ngano: Ni unajisi ikiwa tu mwanamke aonyesha baadaye ushahidi wa kukinza, kama vile majeraha.

Uhakika: Iwe walikinza kimwili au la, ni wanawake wachache wanaoonyesha ushahidi unaoonekana, kama vile majeraha au mikato.

Ngano: Mnajisiwa analaumika pia isipokuwa tu ikiwa anakinza kwa bidii.

Uhakika: Kwa fasili, unajisi hutukia wakati nguvu au tisho la kutumia nguvu linapotumiwa ili kumchafua mtu kingono, kwa njia yoyote ile, dhidi ya mapenzi ya mtu huyo. Kule kutumia nguvu kwa mnajisi dhidi ya mnajisiwa asiyeshirikiana ndiko kunakomfanya awe mnajisi. Hivyo, mnajisiwa hana hatia ya uasherati. Kama vile mharimiwa, huenda akawajibika kukubali jambo asilotaka kwa sababu ya uwezo anaotambua kuwa juu yake kutoka kwa mtu mwingine. Mwanamke anapolazimishwa ajitiishe chini ya mnajisi kwa sababu ya kutishwa au kuvurugika, haimaanishi kwamba anaafiki tendo hilo. Kibali kinategemea uchaguzi bila kutishwa na ni wenye kusikizwa, si wa kupuuzwa.

Ngano: Unajisi ni tendo la ashiki.

Uhakika: Unajisi ni tendo la jeuri. Wanaume hunajisi, si hasa kwa ajili ya ngono, bali ili kuhisi uwezo juu ya mtu mwingine.c

Ngano: Mwanamke aweza kumchezea au kumvuta mwanamume kufikia kiasi ambacho yeye hawezi kudhibiti hamu yake ya ngono.

Uhakika: Wanaume wanaonajisi hawana hamu kubwa ya ngono kuliko wanaume wengine. Badala yake, theluthi moja ya wanajisi wote hushindwa kumaliza tendo la kujamii. Katika visa vingi unajisi ni tendo lililopangwa, si hamu zisizozuilika. Wanajisi wasiofahamiana na wanajisiwa na wale wanaofahamiana nao, wote huwapangia kwa hila wanajisiwa wao—mtu wasiyemjua kwa kumnyemelea mnajisiwa hadi anapokuwa peke yake, mtu wanayemjua kwa kupangia hali ambapo yuko peke yake.

Ngano: Wanawake hudanganya kuhusu unajisi ili kumlipiza kisasi mwanamume au kwa sababu wanahisi kuwa wenye hatia kwa kufanya ngono.

Uhakika: Ripoti bandia za unajisi hutukia kwa kiasi kilekile kama cha uhalifu mwingineo wenye jeuri: asilimia 2. Kwa upande ule mwingine, watafiti wanakubali kwamba unajisi hauripotiwi sana.

Ngano: Mwanamke anaweza “kuomba” anajisiwe kwa kuvaa nguo zenye kuamsha nyege, kunywa kileo, kuacha mwanamume alipe gharama za matembezi, au kwenda kwa nyumba yake.

Uhalisi: Kutumia uamuzi mbaya, kukosa utambuzi au kupuuza mambo, hakumaanishi kwamba mwanamke anastahili kunajisiwa. Wanajisi hulaumika kikamili kwa ajili ya unajisi huo.

[Maelezo ya Chini]

a Karibu mnajisiwa 1 kati ya 10 ni mwanamume.

b Unajisi katika ndoa hutukia wakati mume anapomshinda nguvu mke wake na kufanya ngono kwa nguvu. Huenda waume wengine wakaamini kwamba “mamlaka” ambayo mtume Paulo anasema mwanamume anayo juu ya mwili wa mke wake ni kamili. Hata hivyo, Paulo pia alisema kwamba ‘waume wapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe.’ Mtume Petro asema kwamba waume wapaswa ‘kuwapa wake zao heshima, kama chombo kisicho na nguvu.’ Hiyo inapinga jeuri au ngono ya kulazimishwa.—1 Wakorintho 7:3-5; Waefeso 5:25, 28, 29; 1 Petro 3:7; Wakolosai 3:5, 6; 1 Wathesalonike 4:3-7.

c “Lengo la uhalifu huo si ‘ngono’ bali badala yake tendo la ngono ndiyo silaha ambayo mnajisi hutumia ili kufanya uhalifu wa jeuri.”—Wanda Keyes-Robinson, chifu wa tarafa, Idara ya Hatia ya Kingono, Jiji la Baltimore, Maryland.

[Blabu katika ukurasa wa 3]

Katika United States, mwanamke 1 kati ya kila 4 huenda amekwishanajisiwa au kumekuwa jaribio la kumnajisi

[Blabu katika ukurasa wa 3]

Unajisi husitawi katika jumuiya zinazokubali jeuri na utumizi mbaya wa ngono

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki