Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kudhibiti Woga Nilipokuwa nikisoma makala kuhusu woga (Julai 22, 1998), nilihisi kana kwamba nilikumbatiwa na mkono wenye faraja. Hatimaye, mtu fulani alielewa matatizo ambayo mke wangu amevumilia muda wote wa maisha yake. Woga wa watu umemtaabisha sana. Sikuweza kuelewa kamwe jinsi alivyokuwa akiteseka. Hofu yake kuu ya kusema mbele ya watu, kutumia simu, kuchangamana na wengine, na pia hisi za kutaka kuzimia na pia hofu ya ghafula—dalili zote hizi zilifafanuliwa katika makala zenu. Ilikuwa kana kwamba hali yake ilikuwa imefunuliwa wazi. Watu wengi wameielewa vibaya hofu kuu ya mke wangu nao wameiona kuwa ufidhuli au tabia ya kutopenda watu. Ni tumaini langu kwamba watu wa namna hiyo watasoma makala hizi bora sana.
M. C., Scotland
Mapema mwaka huu, uchunguzi ulionyesha kwamba mwanangu aliye na umri wa miaka kumi ana woga wa kuwa katika sehemu za peupe. Limekuwa pambano gumu. Kuna mambo mawili yaliyonipendeza katika makala hizo. Jambo la kwanza lilikuwa “Watu ‘Wenye Hisia Kama Zetu.’” Sehemu hii ilimsaidia sana mwanangu kuelewa kwamba si yeye peke yake aliye na tatizo hilo. Jambo la pili ni jinsi makala hizi zilivyoandikwa kwa njia yenye ufikirio. Makala hizi hazimhukumu wala kumdunisha mtu, bali ziliandikwa kwa njia ya upendo, fadhili, hekima na kisha kwa upendo mwingi.
K. J., Australia
Nilifikiri makala hizi zilikuwa nzuri kwa sababu zilikazia uangalifu mambo ambayo mtu anaweza kufanya. Mlieleza hatua muhimu zinazofanya kudhibiti woga kuwezekane. Jambo hili lilinifanya nihisi kwamba naweza kupata msaada ninaohitaji ili kufanya maendeleo.
J. I., Japani
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwangu kuhisi kwamba kwa kweli hali yangu ilifahamika. Siwezi kueleza jinsi inavyofariji kujua kwamba Yehova anaelewa mateso ambayo hofu ya watu inaweza kusababisha. Makala hizi ziliwasaidia pia marafiki wangu kuelewa kwa wazi zaidi matatizo niliyo nayo.
G. O., Ujerumani
Nilishangazwa na hisia moyo mnayoonyesha kwa wale walio na woga wa watu kama mimi. Makala hizi ndicho kitu tulichohitaji. Ilitia moyo kama nini kujua kwamba wengine pia wana tatizo kama langu! Niko tayari kukabiliana na woga huu na kuushinda.
S. D., Italia
Kwa Nini Siwezi Kukaza Fikira? Nilitokwa na machozi ya shangwe niliposoma makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Siwezi Kukaza Fikira?” (Julai 22, 1998) Nina umri wa miaka 18 nami natumikia katika huduma ya wakati wote. Nilihangaika kwa sababu singeweza kukaza fikira, jambo ambalo ni la muhimu katika kuwasaidia watu kwenye huduma ya shambani. Nilikuwa nimeanza kuwa na mshuko wa moyo kwa sababu singeweza kukumbuka na kuchanganua mambo. Ni kweli kwamba, Yehova huandaa chakula kwa wakati unaofaa, kama isemavyo Biblia.
A. R. C. R., Marekani
Madokezo kwa Wasafiri Dokezo moja ambalo haliko katika “Madokezo kwa Wasafiri,” katika ile makala “Kidingapopo— Homa Isababishwayo na Kuumwa” (Julai 22, 1998), ni kutumia chandarua ya kuzuia mbu usiku, na hasa ile yenye dawa ya kuua wadudu.
I. H., Uingereza
Tunathamini maelezo ya msomaji. Dokezo hili ni muhimu sana, katika kuzuia malaria. (Ona “Amkeni!” la Julai 22, 1997, ukurasa wa 31.) Hata hivyo, kulingana na Vitivo vya Kudhibiti Maradhi vya Marekani, mbu anayesababisha homa ya kidingapopo “hupendelea kuwauma watu wakati wa mchana.” Mbu huyo huuma mara nyingi “kwa saa chache asubuhi baada ya mapambazuko na baadaye alasiri kwa saa chache kabla ya giza kuingia.” Na kwa sababu hiyo, kutumia chandarua usiku huenda kusiwe na matokeo sana katika kuzuia ugonjwa huu.—Mhariri.