Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 7/22 kur. 4-7
  • Macho Yote Yakuangaliapo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Macho Yote Yakuangaliapo
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Hofu za Woga wa Watu
  • Hao Hujaribuje Kukabiliana na Hali?
  • Kudhibiti Hali ya Kuogopa Watu
    Amkeni!—1998
  • Kuteswa na Woga
    Amkeni!—1998
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • Mitandao ya Kijamii Inaniathirije?
    Vijana Huuliza
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 7/22 kur. 4-7

Macho Yote Yakuangaliapo

“Mateso” ndivyo Jerry alifafanuavyo. Yeye asema: “Kila wakati nilipoingia darasani ningeanza kutoka jasho jingi, nilihisi kana kwamba nimejazwa pamba mdomoni, na niliona kama siwezi kuongea—hata kama uhai wangu ungekuwa hatarini. Kisha ningeanza kusikia joto kali likipanda mikono yangu na miguu yangu hadi usoni na ningebadilika kuwa mwekundu—kana kwamba nilikuwa nabadilika rangi mwili wote.”

JERRY ana woga wa watu, hali ya kuhofu sana kuchunguzwa na wengine na kuaibishwa hadharani. “Mtu mwenye woga wa watu huamini kwamba kila mtu anamtazama,” chasema kijitabu kimoja kilichochapishwa na Shirika la Marekani la Magonjwa ya Wasiwasi. “Wasiwasi huo waweza kutokeza hali kama za hofu ya ghafula kutia ndani moyo kupiga kwa nguvu, hali ya kuzirai, kukosa hewa, na kutokwa na jasho jingi.”

Huenda wengine wakaelekea kupuuza hofu za wale wenye woga wa watu, wakisema kwamba watu hao wajilazimishe tu kupuuza haya zao “wakachangamane na watu.” Ni kweli kwamba sehemu ya kukabiliana na woga wa watu yatia ndani kukabili hofu zako mwenyewe. Lakini, kuna tofauti kubwa kati ya haya na woga wa watu. “Tofauti na haya ya kawaida,” asema Jerilyn Ross, “woga wa watu ni mbaya sana hivi kwamba unahitilafiana na utendaji wa kawaida, kazini, shuleni, na katika karibu mahusiano yote na watu wengine.”

Uchunguzi umedokeza kwamba maisha za mamilioni ya watu zimeathiriwa na woga wa watu.a Ebu ona baadhi ya hofu ambazo zimehusishwa na hali hii yenye kudhuru.

Hofu za Woga wa Watu

Kusema mbele ya watu. Doug akumbuka jinsi alivyoshikwa na hofu alipokuwa akitoa hotuba fupi kwa kikundi kidogo cha wakazi wa huko kwao. “Kwa ghafula nilianza kutokwa na jasho jembamba,” yeye asema. “Moyo ulikuwa ukipiga kama ngoma. Nilikuwa natetemeka. Koo yangu ikawa kana kwamba inajifunga, nikashindwa kutoa maneno.” Ni kweli kwamba karibu kila mtu hushikwa na wasiwasi anaposimama mbele ya wasikilizaji. Lakini mtu mwenye woga wa watu hushikwa na ogofyo kuu lisilopungua, na halipungui hata kwa mazoezi. Kwa hakika, Doug akaja kuona hata fursa ndogo tu ya kuzungumza kuwa kama tisho kwa uhai wake.

Kula mbele ya wengine. Kwa kuwa wenye kuogopa watu huamini kwamba wanachunguzwa, hata mlo rahisi tu waweza kuwa mateso makubwa ajabu. Wao wana wasiwasi kwamba mikono yao itatetemeka, kwamba wataangusha chakula au kwamba watakosa mdomo, au hata kwamba watakuwa wagonjwa. Hofu hizo zaweza kutimia. Kitabu Dying of Embarrassment chasema: “Kadiri unavyokuwa na wasiwasi kwamba unaweza kufanya jambo fulani lenye kuaibisha, ndivyo unavyozidi kuhangaika. Kadiri unavyohangaika, ndivyo unavyoelekea kuanza kutetemeka au kufanya mambo ya ghafula yasiyofaa. Tatizo hilo laweza kuzidi mpaka iwe vigumu kupeleka chakula au kinywaji mdomoni bila kukiangusha au kukimwaga.”

Kuandika mbele za wengine. Wakiogopa kwamba mikono yao itatetemeka au kwamba wataonekana wakiandika vitu visivyoweza kusomeka, wengi wenye kuogopa watu hushikwa na hofu wanapolazimika kutia sahihi kwenye hundi au kuandika jambo lolote wakitazamwa na wengine. Kwa mfano, Sam aliaibika sana alipoambiwa na mwajiri wake awe akitia sahihi kitabu cha rekodi ya kazi mbele ya askari-mlinzi kila asubuhi kabla ya kazi kuanza. “Nilishindwa,” asema Sam. “Mkono wangu ulikuwa ukitetemeka sana hivi kwamba ilikuwa ikinibidi niudhibiti kwa mkono mwingine ili niweze kuandika kwenye mstari na bado hungeweza kusoma maandishi yangu.”

Kutumia simu. Dakt. John R. Marshall asema kwamba wengi wa wagonjwa anaowatibu waliungama kwamba wao waliepuka kutumia simu kwa kadiri iwezekanavyo. “Waliogopa kwamba wao wangeshindwa kujibu ifaavyo,” yeye asema. “Wengine waliogopa kwamba kwa sababu wangepotewa na maneno, ukimya wenye aibu ungefuata na wanapochanganyikiwa na maneno, wasiwasi ungefanya sauti zao zibadilike, zitetemeke, au hata kuwa juu sana. Wao waliogopa kwamba wanaweza kugugumiza, au kwa njia nyinginezo za aibu waonyeshe kwamba wana woga.”

Kuchangamana na watu. Watu fulani huogopa karibu hali yoyote inayohusisha kuchangamana na wengine. Mara nyingi, wao hasa huogopa kuangaliana na wengine macho kwa macho. “Wale wenye woga sana wa watu mara nyingi hawana uhakika watazame wapi na hawajui wafanye nini wanapotazamwa na wengine,” yasema The Harvard Mental Health Letter. “Wao huepuka kutazama wengine kwenye macho kwa sababu wao huhisi kwamba hawajui wakati wa kuwatazama watu na wakati wa kutazama mahali pengine. Wao hudhani kwamba wengine watawafikiria vibaya.”

Kuna hofu nyinginezo zinazohusika na woga wa watu. Kwa mfano, wengi huogopa sana kutumia vyoo vya umma. Wengine huogopa kununua vitu wakitazamwa na muuzaji. “Mimi hujifikiria sana hivi kwamba mara nyingi hata sioni kitu ninachotazama,” asema mwanamke mmoja. “Sikuzote mimi hutazamia kwamba yule mtu kwenye kaunta atasisitiza kwamba niamue kile ninachotaka kununua na nisiwapotezee wakati wao.”

Hao Hujaribuje Kukabiliana na Hali?

Wale ambao hawana ugonjwa huo hawaelewi uchungu wa wale wenye woga wa watu. Mtu mmoja mwenye woga wa watu afafanua hali yake kuwa “aina mbaya zaidi ya aibu uwezayo kuwazia!” Mtu mwingine akiri hivi: “Sikuzote mimi hufikiria kujiua.”

Kwa kuhuzunisha, wengi wenye woga wa watu huanza kunywa vileo katika jitihada za kujaribu kuondoa wasiwasi wao.b Ingawa vileo vinaweza kutuliza mtu kwa muda tu, hatimaye kunywa vileo kupindukia huongeza tu matatizo ya mtu huyo. Dakt. John R. Marshall asema: “Wagonjwa kadhaa ninaowatibu ambao hawajazoea kunywa penye watu wamejikuta wakibugia vileo na kulewa chopi—wakijaribu kujituliza kabla ya kikusanyiko cha kirafiki au wakati huo, kumbe ndipo wanapojiaibisha vibaya zaidi mbele ya wale ambao hao waliogopa sana.”

Labda mbinu ya kukabiliana na hali hiyo ambayo ni ya kawaida sana miongoni mwa wenye woga wa watu ni kuwaepuka watu wengine. Ndiyo, wengi huepuka tu hali zinazowatia hofu. “Niliepuka hali nyingi sana kadiri iwezekanavyo, hata kuzungumza kwenye simu,” asema mtu mmoja mwenye woga wa watu aitwaye Lorraine. Lakini, baada ya muda watu wengi wenye matatizo hayo hugundua kwamba kuepuka hali wanazoogopa huwafanya kuwa wafungwa tu badala ya kuwalinda. “Baada ya muda,” asema Lorraine, “upweke na uchovu ungenishinda.”

Kuepuka watu kwaweza “kuwa mtego wa kujinasia,” aonya Jerilyn Ross. “Na kila tendo la kuepuka watu,” aongezea, “hufanya iwe rahisi kuangukia mtego huo tena—mpaka huko kuepuka watu kunapotukia kwenyewe tu.” Wengine wenye woga wa watu hukataa daima mialiko ya mlo au hukataa kazi zinazohusisha kuchangamana na watu. Matokeo ni kwamba hawawezi kujifunza kukabili hofu zao na kuzidhibiti. Kama Dakt. Richard Heimberg anavyosema, “maisha zao zimejaa mambo mengi ya kuwaziwa tu ambayo hata hayakutukia ya jinsi walivyokataliwa na mawazo ya makosa ambayo wangefanya katika kazi ambazo hata hawakujaribu kufanya kwa sababu waliziepuka.”

Lakini, kuna habari njema kuhusu woga wa watu: Unaweza kutibiwa. Bila shaka haiwezekani—hata haitakikani—kuondoa kila aina ya wasiwasi. Lakini, wale ambao wana woga wa watu wanaweza kujifunza kudhibiti hofu zao, na Biblia ina mashauri mazuri yawezayo kusaidia.

[Maelezo ya Chini]

a Yafaa ijulikane kwamba karibu kila mtu ana hofu fulani za watu. Kwa mfano, watu wengi huwa na wasiwasi wanapofikiria kuzungumza mbele ya wasikilizaji. Lakini, woga wa watu hasa unahusu wale ambao hofu zao ni nyingi sana hivi kwamba hawawezi kutenda kama ilivyo kawaida yao.

b Uchunguzi waonyesha kwamba wengi ambao wana woga wa watu ni waraibu wa vileo na kwamba wengi wa waraibu wa vileo ni wenye woga wa watu. Ni gani huanza? Inadaiwa kwamba thuluthi moja ya waraibu wa vileo wana historia ya kuwa na hofu za ghafula au aina fulani ya woga wa watu kabla ya wao kuanza kunywa.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Kwa mtu mwenye woga wa watu, kuchangamana na watu kwaweza kuwa mateso makubwa ajabu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki