Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g03 6/22 kur. 15-17
  • Ndege Maridadi Mwenye Madoa Yanayofanana na Macho

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ndege Maridadi Mwenye Madoa Yanayofanana na Macho
  • Amkeni!—2003
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maonyesho Yao Yenye Kuvutia
  • Maisha ya Familia ya Tausi
  • Tausi Katika Historia
  • Ndege Mwenye Kumeremeta Anayejionyesha
    Amkeni!—2003
  • Jicho la Uduvi Anayeitwa Peacock Mantis
    Amkeni!—2010
  • Manyoya—Ubuni wa Ajabu
    Amkeni!—2007
  • Je, Wanataka Tu Kujirembesha?
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2003
g03 6/22 kur. 15-17

Ndege Maridadi Mwenye Madoa Yanayofanana na Macho

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA

LABDA umekisia kutokana na kichwa hicho kwamba tunaongea kuhusu tausi. Ama kweli, tausi dume anajulikana ulimwenguni kwa sababu ya mkia wake mpana na mrefu.a Lakini je, umewahi kujiuliza manyoya hayo yasiyo na kifani yana kusudi gani na kama kiumbe huyu ana mengi zaidi ya urembo wake?

Tausi ni wa jamii ya kwale, na kuna aina tatu za tausi. Tutazungumza kuhusu tausi wa India, au tausi wa kawaida mwenye rangi ya buluu-kijani na mwenye urefu wa sentimeta 200 hadi 235 kutia ndani mkia wenye urefu wa sentimeta 150. Manyoya ya mkia huo yana rangi ya kijani na dhahabu na yana madoa yanayofanana na macho ya buluu na shaba. Manyoya ya mwili wake hasa ni ya rangi ya buluu-kijani inayong’aa.

Tausi ametangazwa rasmi kuwa ndege wa kitaifa wa India, na bila shaka anaonekana kuwa na sura ya kifalme. Labda ndiyo sababu msemo “mwenye maringo kama tausi” hutumiwa kuhusu mtu mwenye kujivuna. Hata hivyo, ndege huyo si mwenye kujiona kama umbo lake linavyodokeza. Kwa kweli, yeye hufugwa kwa urahisi. Watu fulani humwona tausi kuwa mtakatifu. Kwa sababu hiyo, nyakati nyingine wakulima wa vijijini huko India huvumilia tu ndege hao wanapoharibu mashamba yao ya nafaka.

Maonyesho Yao Yenye Kuvutia

Bila shaka, tausi wanajulikana sana kwa maonyesho yao ya kutanua mkia wao kama feni yenye kuvutia. Kusudi la maonyesho hayo yenye fahari ni nini? Inaonekana kwamba kusudi ni kuwavutia majike.

Tausi jike ni mchaguzi sana, lakini anapenda sana maonyesho hayo. Mkia mpana na mrefu wa tausi uliojaa madoa yenye rangi zinazong’aa humvutia tausi jike. Mara nyingi yeye humchagua tausi dume mwenye maonyesho ya kuvutia zaidi awe mwenzi wake.

Hata hivyo, kutanua mkia ni sehemu moja tu ya maonyesho hayo. Kwanza tausi dume hutanua mkia wake mrefu na kuuinamisha mbele. Kisha huanza kucheza dansi kwa madaha. Mabawa yake yenye rangi ya hudhurungi-nyekundu huning’inia pembeni anapoutikisa mwili wake na kutokeza sauti kwa manyoya yake yenye kusimama. Yeye pia hulia kwa sauti kubwa. Sauti hiyo haipendezi, lakini angalau humjulisha tausi jike kwamba anapendezwa naye.

Mara kwa mara, tausi jike hujaribu kuiga kinyongenyonge dansi ya dume, lakini mara nyingi, hujifanya hapendezwi. Hata hivyo, atavutiwa na dume anayefanya onyesho lenye kutokeza zaidi. Tausi dume anaweza kuwa na majike watano na vifaranga 25 kwa mwaka mmoja.

Maisha ya Familia ya Tausi

Baada ya kipindi cha kutaga mayai, manyoya yake hutoka. Kwa wastani, mkia wa tausi dume una manyoya zaidi ya 200. Wanakijiji wa India walikuwa wakikusanya manyoya hayo na kuyauza katika nchi za Magharibi hadi biashara hiyo ilipopigwa marufuku ili kulinda ndege hao. Nchini humo, bado watu hutengeneza feni na vitu vingine vyenye kuvutia kwa manyoya hayo.

Wakati wa jioni tausi hupanda miti mirefu zaidi ili kupata mahali pafaapo pa kulala. Asubuhi hushuka chini polepole. Umaridadi wa viumbe hao unaweza kukuvutia lakini usitazamie sauti zao zikupendeze. Vilio vyao huharibu kimya wakati wa jioni hadi wanapoanza kutafuta chakula.

Tausi hula kila kitu. Wao hula wadudu, mijusi, na nyakati nyingine hata nyoka wadogo, mbegu, nafaka, dengu na mizizi laini ya mimea.

Ingawa tausi huonekana kuwa mwenye maringo yeye anaweza kuwalinda tausi wengine. Yeye ni mwepesi kugundua hatari. Anapomwona paka anayewinda yeye hukimbia msituni akilia kwa sauti kubwa na kuonya wengine kuhusu hatari hiyo. Madume wengine huanza pia kulia. Wao hukimbia haraka sana wakifuatana. Hata hivyo, tausi majike huwa hawaachi vifaranga wao hata wanapokabili hatari kubwa.

Yaonekana mkia mrefu wenye manyoya mengi haupunguzi mwendo wa tausi, lakini ni kama mkia huo humsumbua anapopuruka. Ingawa hivyo mara tu anapopaa hewani, anaruka kwa mwendo wa kasi sana, akipigapiga mabawa yake haraka-haraka.

Vifaranga wanapofikisha umri wa miezi minane, wanakuwa tayari kuwaacha wazazi wao na kuanza kujitunza wenyewe. Wanapoondoka mama hujitayarisha ili kuwatunza vifaranga wengine tena. Mkia wa madume wachanga huanza kukua wanapokuwa na umri wa miezi minane hivi, lakini mikia yao hukomaa wanapokuwa na umri wa miaka minne. Kisha wanakuwa tayari kuanzisha familia yao wenyewe.

Tausi Katika Historia

Tausi walio hai walijaa kwenye bustani za Ugiriki, Roma, na India nyakati za kale. Sanaa zenye tausi zilipamba makao ya kifalme huko India kwa maelfu ya miaka. Kwa kweli, Kiti cha Enzi cha Tausi kilionwa kuwa mojawapo ya ishara muhimu za utajiri nchini India. Kilikuwa na almasi nyingi, na inaripotiwa kwamba kilikuwa na rubi 108 na zumaridi 116. Kulikuwa na tausi wa dhahabu katika sehemu ya juu na ndio sababu kikapewa jina hilo. Kiti hicho cha enzi kilitengenezwa na kutumiwa tu kwenye sherehe za pekee.

Historia ya Biblia yaonyesha kwamba tausi walikuwa miongoni mwa vitu vyenye thamani vilivyonunuliwa na Mfalme Solomoni. Hebu wazia jinsi ilivyovutia kuwaona tausi wakitembea-tembea katika bustani yake ya kifalme. (1 Wafalme 10:22, 23) Kwa kweli ndege hao hutuonyesha kwamba kuna Mbuni mwenye akili nyingi. Tausi anapocheza dansi akiwa ametanua mkia wake wenye manyoya ya rangi zenye kuvutia, mtu huchochewa kustaajabia stadi za usanii za Yehova, Mungu ‘aliyeumba vitu vyote.’—Ufunuo 4:11.

[Maelezo ya Chini]

a Manyoya hayo humea kutoka mgongoni mwa ndege huyo wala si kutoka mkiani. Tausi hutumia mkia wake kutanua manyoya hayo.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Nyakati nyingine tausi jike hapendezwi na dansi ya tausi dume

[Hisani]

© D. Cavagnaro/Visuals Unlimited

[Picha katika ukurasa wa 17]

Tausi majike huwa mama wazuri sana

[Hisani]

© 2001 Steven Holt/stockpix.com

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Peacock: Lela Jane Tinstman/Index Stock Photography

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

John Warden/Index Stock Photography ▸

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki