Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g05 11/22 kur. 2-3
  • Itakuwaje Chakula Kikiisha?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Itakuwaje Chakula Kikiisha?
  • Amkeni!—2005
  • Habari Zinazolingana
  • Ugumu wa Kulisha Majiji
    Amkeni!—2005
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Upungufu wa Chakula Uliopo Duniani Leo?
    Habari Zaidi
  • Chakula cha Wote—Je, ni Ndoto Tu?
    Amkeni!—1997
  • 1. Tumia Busara Unaponunua Chakula
    Amkeni!—2012
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2005
g05 11/22 kur. 2-3

Itakuwaje Chakula Kikiisha?

KATIKA sehemu fulani, watu wanaoishi majijini hufikiri kwamba sikuzote watapata chakula cha kutosha kwa bei nafuu wanapoenda madukani au sokoni. Kunapokuwa na chakula, huenda wanunuzi wasifikirie kwa uzito kuhusu jinsi chakula kinavyosafirishwa na kugawanywa. Hata hivyo, wakati wa shida, watu huanza kufikiria mambo yanayohusika katika kusafirisha chakula hadi madukani. Ikiwa kwa sababu fulani kunakuwa na tatizo la usafirishaji wa chakula, matokeo yanaweza kuwa mabaya.

Fikiria jambo lililotukia katika nchi moja yenye matatizo ya kiuchumi huko Afrika Kaskazini. Baada ya serikali kukatiza msaada wa kifedha kwa wakulima, bei ya mkate iliongezeka maradufu mara moja. Ili kupinga jambo hilo, umati wenye hasira ulizusha ghasia barabarani, ukivunja madirisha ya maduka na kushambulia benki na posta. Ghasia zilienea kotekote nchini na hali ya hatari ikatangazwa. Katika jitihada za kuzima ghasia hizo, polisi walifyatulia umati risasi na inasemekana kwamba watu 120 waliuawa na wengine wengi wakajeruhiwa.

Jambo lililotukia nchini Uingereza mnamo Septemba 2000 linaonyesha kwamba tatizo la kugawanywa kwa chakula linaweza kutokea hata katika nchi zilizositawi. Waandamanaji waliokuwa wakipinga ongezeko la bei ya mafuta walifunga barabara zinazotoka katika viwanda vya kusafisha mafuta na kuzuia malori ya kusafirishia mafuta. Baada ya siku chache, vituo vya petroli havikuwa na mafuta, nayo magari na malori yakakosa petroli na hivyo kukatiza njia za kusafirishia chakula. Maduka nchini kote ambayo kwa kawaida hutegemea kuletewa chakula kulingana na uhitaji, hayakuwa na chochote.

Kuna matatizo mbalimbali yanayohusiana na kugawanywa kwa chakula katika nchi zinazositawi. Kwa sababu ya matatizo mbalimbali, kutia ndani, ukame, matatizo ya kiuchumi, misukosuko ya kijamii , na vita, “kukosa utaratibu na matatizo ya usafirishaji wa chakula hutokea mara nyingi,” kinasema kichapo Feeding the Cities cha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). “Matatizo hayo yanapotokea, hata ingawa huenda yakaathiri sehemu fulani tu au yakawa ya muda mfupi, maskini ndio huumia.”

Wataalamu wanaamini kwamba idadi inayoongezeka haraka ya wakaaji wa majijini itatokeza “matatizo makubwa sana” kwa watu wanaosafirisha na kugawanya chakula. Inakadiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2007, zaidi ya nusu ya watu ulimwenguni watakuwa wakiishi mijini. Kulingana na shirika la FAO, “itakuwa vigumu sana na mwishowe haitawezekana kusafirisha na kugawanya chakula kinachofaa na cha bei nafuu kwa [wakaaji wa majijini].”

Kusafirisha na kugawanya chakula ili watu wakipate madukani ni jambo muhimu sana. Kwa hiyo, njia za kusafirisha chakula ni zenye kutegemeka kadiri gani? Kwa nini wataalamu wana wasiwasi kwamba njia za kusafirisha na kugawanya chakula zitakosa kutosheleza mahitaji ya watu? Je, kutakuwa na wakati ambapo hakuna mtu atakayekuwa na wasiwasi wa kupata chakula?

[Picha katika ukurasa wa 2]

Kushoto: Soko linaloelea, Thailand

[Hisani]

© Jeremy Horner/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 3]

Uporaji wakati wa ukosefu wa chakula

[Hisani]

BETAH/SIPA

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki