Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 11/06 kur. 3-4
  • Swali Gumu Zaidi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Swali Gumu Zaidi
  • Amkeni!—2006
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mvurugo wa Kidini
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Misiba ya Asili?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Misiba ya Asili​—Kwa Nini Imeongezeka Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2011
  • Je, Mungu Anatumia Misiba ya Asili Kuwaadhibu Wanadamu Leo?
    Amkeni!—2012
  • Je, Misiba ya Asili Ni Adhabu Kutoka Kwa Mungu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2006
g 11/06 kur. 3-4

Swali Gumu Zaidi

“KWA NINI?” Nyakati nyingine swali hilo linapoulizwa huonyesha hisia kali za maumivu na uchungu. Mara nyingi watu huuliza swali hilo baada ya misiba au maafa kutokea: Tufani linapiga eneo fulani na kusababisha kifo na uharibifu. Tetemeko la nchi linabomoa jiji kubwa. Shambulizi la kigaidi linabadili siku iliyo na utulivu kuwa yenye kuogopesha na yenye jeuri. Mpendwa wetu anajeruhiwa au kupoteza uhai wake katika aksidenti.

Mara nyingi wale ambao hawana hatia wala ulinzi huwa kati ya watu wanaoathiriwa. Hivi karibuni kumekuwa na misiba mingi kama hiyo hivi kwamba watu wengi wamemlilia Mungu wakimwuliza, “Kwa nini?” Fikiria mifano kadhaa:

◼ “Mungu, kwa nini umetutendea hivi? Tumefanya nini kukukasirisha?” Shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba mwanamke mmoja mzee huko India aliuliza maswali hayo baada ya tsunami kufagilia mbali kijiji chao.

◼ “Mungu alikuwa wapi? Na ikiwa Mungu ana nguvu zote, kwa nini aliruhusu msiba huo utokee?” Maswali hayo yalizushwa na gazeti huko Texas, Marekani, baada ya mtu mwenye bunduki kufyatua risasi ndani ya kanisa akijeruhi na kuua idadi fulani ya waumini wa kanisa hilo.

◼ “Kwa nini Mungu alimwacha afe?” Mwanamke mmoja aliuliza swali hilo baada ya rafiki yake kufa kwa sababu ya kansa na kumwacha mume wake akilea watoto watano.

Si watu hao tu wanaofikiri kwamba Mungu ndiye chanzo cha matatizo yao. Kwa mfano, katika uchunguzi wa karibuni wa Intaneti karibu nusu ya watu wote walioulizwa walihisi kwamba misiba kama tufani husababishwa na Mungu. Kwa nini watu wengi huhisi hivyo?

Mvurugo wa Kidini

Badala ya kutoa majibu yanayoridhisha, viongozi wa kidini huchangia mvurugo uliopo. Na tuchunguze majibu matatu ambayo wao hutoa kwa kawaida.

Kwanza, viongozi wengi wa kidini huhubiri kwamba Mungu huleta misiba ili kuwaadhibu wanadamu wakosaji. Kwa mfano, baada ya jiji la New Orleans, Louisiana, huko Marekani kuharibiwa na Tufani Katrina, viongozi fulani wa dini walidai Mungu ameliadhibu jiji hilo. Walitaja mambo kama vile kuenea kwa ufisadi, kucheza kamari, na ukosefu wa maadili. Wengine hata walitoa maandiko ya Biblia ili kuthibitisha madai yao, wakionyesha pindi ambazo Mungu aliwaharibu waovu kwa gharika au kwa moto. Hata hivyo, hayo si madai ya kweli kuhusu Biblia.—Ona sanduku “Je, Ni Kazi za Mungu?”

Pili, viongozi fulani wa dini husema kwamba Mungu ana sababu zake za kuleta maafa ambayo huwapata wanadamu lakini hatuwezi kuelewa sababu hizo. Watu wengi hawaridhishwi na wazo hilo. Wao hujiuliza, ‘Je, Mungu mwenye upendo anaweza kweli kufanya jambo baya kama hilo kisha akatae kuwafahamisha wale ambao hutamani sana kufarijiwa na ambao huuliza, “Kwa nini?”’ Kwa kweli, Biblia inasema: “Mungu ni upendo.”—1 Yohana 4:8.

Tatu, viongozi wengine wa kidini huhisi kwamba labda Mungu hana nguvu nyingi naye hana upendo. Maelezo hayo vilevile hutokeza maswali mazito. Je, Yule ‘aliyeumba vitu vyote,’ kutia ndani ulimwengu wote, hana uwezo wa kuwazuia watu wasiteseke katika sayari hii moja tu? (Ufunuo 4:11) Yule aliyetupa uwezo wa kupenda, ambaye Neno lake humfafanua kuwa wonyesho halisi wa upendo, anakosaje kuwahurumia wanadamu wanaoteseka?—Mwanzo 1:27; 1 Yohana 4:8.

Bila shaka, hoja hizo tatu ni baadhi ya njia ambazo watu hujaribu kueleza sababu ambayo Mungu huruhusu kuteseka, swali ambalo limewaduwaza watu kwa karne nyingi. Katika makala inayofuata, tutachunguza yale ambayo Biblia inafundisha kuhusu habari hii muhimu ya wakati unaofaa. Kama utakavyoona, maelezo ya Biblia yanayopatana na akili yataondoa mvurugo uliopo. Isitoshe, Biblia huwafariji wote ambao wamepatwa na misiba.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]

Je, Ni Kazi za Mungu?

Je, Biblia inafundisha kwamba Mungu husababisha misiba ya asili tunayoona leo? La hasha! Hukumu za Mungu zinazosimuliwa katika Biblia ni tofauti sana na misiba ya asili. Mungu husoma mioyo ya watu mmojammoja na kuwaharibu wale tu anaowaona kuwa waovu. (Mwanzo 18:23-32) Isitoshe, Mungu hutoa onyo kwanza na hivyo kuwapa waadilifu nafasi ya kuponyoka.

Kwa upande mwingine, misiba ya asili hutokea bila kutoa onyo au baada ya kutoa dalili chache tu. Misiba hiyo huua na kuwalemaza watu bila kubagua. Kwa kiwango fulani, wanadamu wamefanya misiba hiyo kuwa mibaya zaidi kwa kuharibu mazingira na kujenga katika maeneo ambayo matetemeko ya nchi, mafuriko, na hali mbaya ya hewa hutokea mara nyingi.

[Hisani]

SENA VIDANAGAMA/AFP/Getty Images

[Picha katika ukurasa wa 4]

Viongozi wa dini wametoa majibu mengi yenye kuvuruga

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki