Je, ni Kazi ya Ubuni?
Ngozi ya Papa
● Unapotazama ngozi ya papa unaweza kufikiri ni nyororo. Lakini ukiigusa, utatambua kuwa ngozi hiyo ni kama msasa unapopitisha mkono wako kutoka upande wa mkia kuelekea kichwa.a
Fikiria hili: Magamba madogo yanayofanya ngozi ya papa iwe hivyo humsaidia katika njia mbili. Kwanza, yanagawa maji na hivyo yanamruhusu papa aogelee bila kuzuiwa sana na maji. Pili, magamba hayo huchezacheza anapoogelea, na hivyo kuzuia vimelea kuishi katikati ya magamba hayo.
Vitu mbalimbali vinaweza kutengenezwa kutokana na muundo wa ngozi ya papa. Kwa mfano, wanasayansi tayari wametengeneza mavazi ya kuogelea ambayo kwa sababu ya kuwa na muundo wa ngozi ya papa, yanaweza kuongeza mwendo wa mwogeleaji kwa angalau asilimia tatu hivi. Wanaamini kuwa mbinu kama hiyo inaweza kutumiwa kuunda magari na mashua zinazoweza kwenda kwa kasi zaidi.
Pia, wataalamu wanatumai kuiga usafi wa ngozi ya papa katika kutengeneza rangi ya kupaka sehemu ya nje ya mashua itakayozuia vimelea na ambayo haitadhuru sana mazingira kama ile inayotumika sasa. Pia wanaweza kutumia ujuzi huo kutengeneza dawa na vifaa vya kitiba ambavyo vitapunguza uwezekano wa kupatwa na maambukizo katika hospitali.
Una maoni gani? Ngozi ya papa inayomwezesha kusonga kwa kasi bila kutumia nishati nyingi, na pia yenye uwezo wa kuzuia maambukizo ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?
[Maelezo ya Chini]
a Huwezi kuhisi ni kama msasa ukiigusa kuanzia kichwa kuelekea mkia.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Magamba ya papa yaliyoongezwa ukubwa
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]
Scales: © Eye of Science/Photo Researchers, Inc.; shark: © Image Source/age fotostock