Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 8/12 kur. 10-12
  • Mahali Ambapo Pesa Zina Miguu Minne

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mahali Ambapo Pesa Zina Miguu Minne
  • Amkeni!—2012
  • Habari Zinazolingana
  • Twende Kwenye Karamu Nchini Hawaii
    Amkeni!—2002
  • Masomo Yangu ya Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Somo la 2
    Masomo Yangu ya Biblia
  • Tunaazimia Kutimiza Huduma Yetu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
Amkeni!—2012
g 8/12 kur. 10-12

Mahali Ambapo Pesa Zina Miguu Minne

“KATIKA eneo letu, nguruwe ni mali yenye thamani sana katika familia, kwa hiyo kufuga nguruwe ni daraka zito,” anasema Enmarie Kani, msichana mwenye umri wa miaka 17 anayeishi kwenye sehemu za milimani za Papua New Guinea. “Baba yangu aliponiambia nimtunze mtoto wa nguruwe, nilisisimka lakini pia nilikuwa na wasiwasi. Alikuwa mdogo sana hivi kwamba nilidhani atakufa.”

Enmarie alimtunza jinsi gani nguruwe wake mdogo? Na kwa nini nguruwe ni wenye thamani sana sawa na pesa kwa watu wanaoishi katika maeneo ya mashambani ya Papua New Guinea? Enmarie alimwambia hivi mwandishi wa Amkeni!

Tafadhali eleza kuhusu eneo unaloishi.

Ninaishi kwenye nyumba ndogo yenye paa la nyasi katika kijiji kilichoko kwenye Sehemu za Milimani za Magharibi pamoja na wazazi na ndugu na dada zangu wadogo wanne​—⁠wasichana wawili na wavulana wawili. Kijiji hiki kina wakazi 50 hivi, ambao ni watu wangu wa ukoo, na tunaishi kando ya kijito cha maji kilichojipinda-pinda katikati ya vilima vyenye misitu mikubwa.

Watu wengi katika kijiji chetu ni wakulima. Familia yetu ina shamba kubwa ambako tunapanda viazi vitamu, maboga, matango, kahawa, na mimea mingine. Ninapenda kupanda mboga na kufanya kazi za mikono. Pia, ninafanya kazi nyingine kama vile kusafisha nyumba, kufua nguo na, bila shaka, kumtunza nguruwe wetu.

Wewe humtunza vipi nguruwe wenu?

Baba alipomnunua nguruwe wetu mwaka uliopita, alikuwa mdogo sana hivi kwamba ningeweza kumbeba kwa viganja vyangu. Kila siku, nilimlisha ungaunga wa samaki na viazi vitamu vilivyopondwa, maji, chumvi, na maji ya miwa. Wakati wa usiku, sehemu za milimani zinapokuwa na baridi kali, alilala kwenye gunia tupu la mchele lililoning’inia kutoka kwenye dari ya nyumba yetu karibu na mahali tunapowasha moto. Nililala kwenye sakafu karibu naye. Kwa sababu hiyo, nguruwe huyo hakufa na alinawiri vizuri!

Sikumbandika jina lingine. Nilimwita tu Nguruwe, na hilo likawa jina lake. Nilimtunza kama mtoto wangu​—⁠nilimlisha, nikamwosha, na kucheza naye kwa saa kadhaa. Nguruwe wetu alinipenda sana na alinifuata kila mahali nilipoenda.

Alipokuwa mkubwa, nilianza kumzoeza ratiba mpya ambayo tunaifuata hadi leo. Kwa kutumia kamba, ninamwelekeza kwenye shamba letu la mboga​—⁠mwendo wa dakika 15 kutoka nyumbani kwetu. Nikifika huko, ninafunga kamba kwenye mti na kumwacha achimbe shamba hilo siku nzima. Kwa kutumia shingo yake imara na pua lake, anachimbua mizizi na minyoo ya ardhini, na wakati huohuo analima na kuongeza mbolea kwenye mchanga. Jioni mimi humrudisha nyumbani, kisha ninamlisha viazi vitamu vibichi na vilivyopikwa kabla ya kumfungia kwenye kijumba chake apumzike wakati wa usiku.

Kwa nini nguruwe ni muhimu sana kwa watu wa milimani?

Sisi watu wa milimani tuna msemo unaosema, Pesa ni nguruwe na nguruwe ni pesa. Zamani kabla ya sarafu za kawaida kufika katika eneo la milimani, watu walitumia nguruwe kama pesa​—⁠zoea ambalo linaendelea hadi sasa. Kwa mfano, duka moja la kuuza magari katika eneo la milimani liliwapa nguruwe watu waliokuwa wakinunua magari. Makabila fulani husuluhisha mizozo yao kwa kutozana pesa au nguruwe. Na mabwana-arusi wengi huwapa nguruwe wazazi wa msichana au watu wake wa ukoo kama sehemu ya mahari.

Inaonekana kwamba kula nguruwe ni sawa na kula kitega uchumi!

Bila shaka! Kwa kuwa nguruwe wana thamani sana, kwa kawaida tunakula nguruwe kwenye pindi za pekee tu, kama vile wakati wa mazishi au matukio mengine muhimu. Mbali na hayo, baadhi ya makabila ya milimani huchinja nguruwe wengi kwenye sherehe kubwa zilizopangwa ili kabila fulani lijionyeshe kuwa lina utajiri au ili kulipia jambo fulani la fadhili walilofanyiwa.

Familia yenu ina mpango gani na nguruwe wenu?

Nguruwe amezaa watoto kadhaa, na mmoja wao ameuzwa kwa kina 100 (dola 40 hivi za Marekani). Tulitumia pesa hizo kulipa nauli ya basi tulipokuwa tukienda mji wa karibu unaoitwa Banz kwa ajili ya kusanyiko la wilaya la Mashahidi wa Yehova linalofanywa kila mwaka. Huenda baba atawauza watoto wengine wa Nguruwe ili agharimie mahitaji mengine ya kila siku ya familia.

Kwa nini usifuge nguruwe wengi ili upate pesa zaidi?

Mradi wetu si kuwa na pesa nyingi, bali tunataka tuweze kukimu mahitaji ya lazima kama chakula, mavazi, na mahali pa kulala. Familia yetu inakazia zaidi mambo yanayohusiana na ibada. Nayo yanatia ndani kumtumikia Mungu wetu, Yehova; kuhudhuria mikutano ya Kikristo; kuwasaidia wengine kadiri tunavyoweza​—⁠kiroho na kimwili​—⁠na kufanya mambo pamoja tukiwa familia. Tunaishi maisha rahisi, lakini tuna uhusiano wa karibu tukiwa familia na tuna furaha.

Siku hizi ninafanya kazi ya kuajiriwa​—⁠kupalilia mashamba na kufuga nguruwe​—⁠lakini si wakati wote. Kazi kuu maishani mwangu ni kutumika nikiwa Mkristo mweneza-injili, kuwaambia jirani zangu kuhusu kweli za Biblia. Kazi hii, ambayo Yesu aliwaagiza wafuasi wake waifanye, hunifanya niwe na shughuli nyingi karibu juma lote. (Mathayo 28:​19, 20) Ninatamani siku moja nifanye kazi huko Port Moresby kwenye Ofisi ya Tawi ya Mashahidi wa Yehova, ambako machapisho ya Biblia hutafsiriwa katika lugha za kienyeji. Lakini hata kama sitaufikia mradi huo, ninajua kwamba nitapata shangwe kubwa katika utumishi wangu kwa Yehova na kwa kutanguliza mambo ya kiroho maishani. Ninashukuru kwa utegemezo wa kimwili ambao nimepata kutokana na pesa ambazo zina miguu minne.

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 12]

TAKWIMU ZA NGURUWE

● Kisiwa cha New Guinea kina angalau nguruwe milioni mbili wa kufugwa, yaani nguruwe 1 kwa kila wakaaji 3.

● Zaidi ya nusu ya wakazi wa maeneo ya vijijini hufuga nguruwe.

[Ramani katika ukurasa wa 10]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

INDONESIA

PAPUA NEW GUINEA

AUSTRALIA

INDONESIA

PAPUA NEW GUINEA

PORT MORESBY

SEHEMU ZA MILIMANI ZA MAGHARIBI

AUSTRALIA

[Picha katika ukurasa 10, 11]

Tunaelekea shambani

[Picha katika ukurasa wa 11

Wakati wa kuoga

[Picha katika ukurasa wa 11]

Wakati wa kucheza

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki