Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g16 Na. 6 kur. 4-6
  • Jilinde Dhidi ya Magonjwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jilinde Dhidi ya Magonjwa
  • Amkeni!—2016
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • 1 MAJI
  • 2 CHAKULA
  • 3 WADUDU
  • 4 WANYAMA
  • 5 WATU
  • Njia za Kuboresha Afya Yako
    Amkeni!—2015
  • Njia ya 4—Linda Afya Yako
    Amkeni!—2011
  • Kirusi Kiuacho Chakumba Zaire
    Amkeni!—1996
  • Kwa Nini Yamerudi?
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2016
g16 Na. 6 kur. 4-6

HABARI KUU | JINSI YA KUJILINDA NA MAGONJWA

Jilinde Dhidi ya Magonjwa

MAJIJI mengi ya zamani yalizungukwa na kuta kubwa. Ikiwa adui angebomoa sehemu fulani ya ukuta, usalama wa jiji lote ungekuwa hatarini. Mwili wako ni sawa na jiji lenye ukuta. Afya yako inategemea jinsi unavyoimarisha ulinzi. Chunguza mambo matano yanayoweza kusababisha magonjwa na jinsi unavyoweza kujilinda.

Mwanamke na binti yake wakiwa sokoni

1 MAJI

HATARI: Vimelea wengi wanaweza “kuingia” moja kwa moja katika mwili wako kupitia maji machafu.

JINSI YA KUJILINDA: Njia bora zaidi ya kujikinga ni kulinda chanzo cha maji ili kisichafuliwe. Ukijua kwamba maji unayotumia yana vimelea au si salama, unapaswa kuyatibu.a Hifadhi maji ya kunywa kwenye chombo kilichofunikwa, na uchote kwa kutumia chombo safi. Usitumbukize mikono yako kwenye chombo chenye maji safi. Inapowezekana, ishi mahali au katika nyumba zenye mfumo mzuri wa kuondoa taka ili kuepusha kuchafua vyanzo vya maji.

2 CHAKULA

HATARI: Vimelea hatari vinaweza kuwepo au kuingia kwenye chakula chako.

JINSI YA KUJILINDA: Chakula au matunda yenye bakteria, huenda yakaonekana kuwa salama na mazuri. Kwa hiyo uwe na kawaida ya kuosha vizuri matunda na mboga kabla ya kuzitumia. Hakikisha kwamba mikono yako, vyombo vya chakula, na mazingira ya jikoni, ni safi kabla ya kuanza kutayarisha na kuandaa chakula. Baadhi ya vyakula vinahitaji kupikwa kwa joto la kiwango fulani ili kuua vimelea hatari. Uwe mwangalifu, usile chakula kilichoachwa wazi au chenye harufu au ladha mbaya, kwa kuwa hiyo ni dalili ya kwamba chakula hicho kimejaa vimelea. Hifadhi haraka kwenye friji chakula ambacho hutakitumia wakati huo. Epuka kutayarisha chakula kwa ajili ya wengine unapokuwa mgonjwa.b

3 WADUDU

HATARI: Baadhi ya wadudu wanaweza kukuambukiza vimelea hatari vilivyo katika miili yao.

JINSI YA KUJILINDA: Dhibiti maambukizi yanayosababishwa na wadudu kwa kukaa ndani ya nyumba au kwa kuvaa nguo zinazofunika mwili kama vile sweta na suruali. Lala ndani ya chandarua chenye dawa, na upake dawa za kujikinga na wadudu. Ondoa vyombo vyenye maji yaliyotuama, mahali ambako mbu wanaweza kuzaliana.c

4 WANYAMA

HATARI: Vimelea vinavyoishi katika miili ya wanyama ni hatari kwa afya yako. Kinyesi cha wanyama ni hatari kama ilivyo tu na kung’atwa au kuchubuliwa nao.

JINSI YA KUJILINDA: Ili kupunguza ukaribu na wanyama, baadhi ya watu wameamua kuwafugia nje ya nyumba zao. Nawa mikono baada ya kumshika mnyama wa kufugwa, na epuka kabisa kugusana na wanyama wa porini. Ikiwa mnyama amekuchubua au kukung’ata, osha jeraha hilo kisha nenda kupata ushauri wa daktari.d

5 WATU

HATARI: Baadhi ya vimelea vinaweza kuingia mwilini mwako kupitia umajimaji unaotoka baada ya mtu kukohoa au kupiga chafya. Pia, vimelea vinaweza kuenea kupitia kugusana kimwili kwa kukumbatiana na kusalimiana kwa mikono. Vimelea kutoka kwa watu wengine vinaweza pia kupatikana kwenye vitasa vya milango, vishikio vya ngazi, simu, rimoti, skrini za kompyuta na kibodi.

JINSI YA KUJILINDA: Usitumie vifaa kama vile, wembe, mswaki, au taulo na watu wengine. Epuka kugusa umajimaji kutoka kwa wanyama au watu wengine, kutia ndani damu na vitu vinavyotokana na damu. Ni muhimu sana kunawa mikono yako vizuri na kwa ukawaida. Hiyo ni moja ya njia bora za kuepuka kueneza magonjwa.

Inapowezekana ni vizuri ubaki nyumbani unapokuwa mgonjwa. Taasisi ya U.S. Centers for Disease Control and Prevention inapendekeza kwamba unapokohoa au kupiga chafya ni vizuri utumie leso au kitambaa, badala ya kufanya hivyo kwenye mikono.

Methali ya kale inasema hivi: “Mtu mwerevu ni yule ambaye ameona msiba na kujificha.” (Methali 22:3) Tutapata matokeo mazuri tukitumia ushauri huo katika dunia hii iliyojaa magonjwa hatari! Hivyo, jitahidi kupata habari za karibuni kwa kuwasiliana na wataalamu wa afya, na ujilinde kwa kudumisha usafi. Imarisha ulinzi wako, na hivyo, upunguze hatari za kuambukizwa magonjwa!

a Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza mbinu mbalimbali za kufanya maji yawe safi na salama nyumbani. Mbinu hizo zinatia ndani kuyatibu maji kwa dawa, kuyaanika juani, kuyachuja, na kuyachemsha.

b Kwa habari zaidi kuhusu usalama wa chakula, soma Amkeni! la Juni 2012 ukurasa wa 3-9.

c Ili kujua njia mbalimbali za kujilinda na ugonjwa wa malaria, soma Amkeni! la Julai 2015 ukurasa wa 14-15.

d Kwa kawaida majeraha yaliyosababishwa na mnyama mwenye sumu yanahitaji kutibiwa haraka na wataalamu wa tiba.

Jinsi ya Kujikinga Wakati wa Magonjwa ya Mlipuko

Mwanamke akinawa mikono yake

Mwaka wa 2014, virusi vya ugonjwa wa Ebola vilienea kwa kasi katika nchi za Afrika Magharibi, na habari hizo zikaenea duniani kote. Ofisi za tawi za Mashahidi wa Yehova katika nchi hizo zilianzisha kampeni ambayo ilisaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza kuenea kwa maambukizi. Wawakilishi wa Mashahidi walieleza jinsi walivyoshughulikia hali hiyo.

  • Hotuba

    Mliwasaidiaje watu kuelewa hatari waliyokabili?

    Tulifanya mpango wa kuwaelimisha watu ili kuwajulisha jinsi virusi vya ugonjwa huo huenea, na kuwaonya kuhusu mambo wanayopaswa kuepuka. Hilo liliwaondolea wasiwasi na woga.

  • Kunawa mikono

    Mashahidi wa Yehova walichukua hatua gani hususa?

    Tulimpima kila mtu aliyekuja katika eneo letu la ibada kwa kutumia kipima joto kinachofanya kazi bila kugusa mwili. Kila mtu aliepuka kugusana na wengine isivyo lazima, kwa kuepuka kusalimiana kwa mikono na kukumbatiana. Pia, tuliwahimiza watu kunawa mikono mara nyingi kila siku. Kulikuwa na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kunawa mikono kwa maji yaliyotiwa dawa.

  • Simu

    Iliwezekanaje kuendelea kufanya ibada na kazi yenu ya kufundisha Biblia kwa ukawaida?

    Kulikuwa na vizuizi vya serikali katika maeneo fulani, kwa hiyo mikutano ya watu wote ilisimamishwa kwa muda. Katika maeneo hayo, familia zilikutana kwenye nyumba za watu ili kufanya ibada. Baadhi ya wahubiri walitumia simu kujifunza na watu Biblia. Njia hiyo iliwaepusha kukutana na watu moja kwa moja.

  • Kalenda

    Mlifanya nini ikiwa mtu fulani alionyesha dalili za ugonjwa?

    Tuliwajulisha wenye mamlaka. Mtu yeyote ambaye alikuwa amemgusa mtu mwenye ugonjwa wa Ebola, amehudhuria mazishi, au kuonyesha dalili fulani alipaswa kujitenga na wengine kwa siku 21, muda ambao ulitosha kuonyesha wazi ikiwa ana virusi vya ugonjwa wa Ebola.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki