Kirusi Kiuacho Chakumba Zaire
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AFRIKA
KIKWIT, Zaire, ulioko kandokando ya msitu wa mvua wa kitropiki ni mji uliopangwa kiholela. Gaspard Menga Kitambala, mwenye umri wa miaka 42, aliyekuwa akiishi nje ya mji huo, alikuwa ndiye Shahidi wa Yehova wa pekee katika familia yake. Menga alikuwa muuzaji wa makaa. Alichoma makaa yake ndani sana kwenye msitu, kuyafunga matita, na kuyabeba kichwani hadi Kikwit.
Katika Januari 6, 1995, akawa mgonjwa. Alianguka mara mbili njiani akirudi nyumbani toka msituni. Alipofika nyumbani, alisema kwamba alikuwa na maumivu ya kichwa na homa.
Siku chache zilizofuata, aliendelea kudhoofika. Januari 12, familia yake ilimpeleka Hospitali Kuu ya Kikwit. Mashahidi katika kutaniko la Menga waliisaidia familia kumtunza katika hospitali. Kwa kuhuzunisha, hali yake ikawa mbaya zaidi. Alianza kutapika damu. Damu ilivuja bila kuzuilika toka mapua na masikio. Akafa Januari 15.
Upesi wengine katika familia ya Menga waliokuwa wameugusa mwili wake wakawa wagonjwa. Kufikia mapema Machi, watu 12 wa ukoo wa karibu wa Menga walikuwa wamekufa, kutia ndani mke wake na wawili wa watoto wao sita.
Aprili katikati, wafanyakazi wa hospitali wakaanza kuwa wagonjwa na kufa kwa njia ileile waliyokufa Menga na familia yake. Upesi hayo maradhi yakaanza kuenea katika miji mingine katika hilo eneo. Ni wazi kwamba, msaada kutoka nje ulihitajiwa.
Mchunguzi mkuu wa virusi katika Zaire, Profesa Muyembe, alienda Kikwit Mei 1. Baadaye aliliambia Amkeni!: “Tulifikia mkataa wa kuwa Kikwit ulikuwa na maambukizo mawili yenye kuenea: moja likiwa kuhara kunakosababishwa na bakteria, na lile jingine lilikuwa homa kali ya kuvuja damu isababishwayo na kirusi. Bila shaka, tulihitaji kuhakikisha ugunduzi huu. Hivyo tukakusanya damu kutoka kwa wagonjwa na kuipeleka ichunguzwe kwenye Vitovu vya Kudhibiti Maradhi katika Atlanta, Marekani.”
Vitovu vya Kudhibiti Maradhi vilithibitisha kile Muyembe na madaktari wengine katika Zaire walikuwa wakishuku. Hayo maradhi yalikuwa Ebola.
Maradhi Yenye Kufisha
Kirusi cha Ebola ni hatari sana. Chaweza kuua upesi sana. Hakuna chanjo dhidi yacho, na hakuna tiba ijulikanayo kwa walio na maradhi hayo.
Ebola ulitambuliwa kwa mara ya kwanza katika 1976. Ulipewa jina la mto wa Zaire, maradhi hayo yalishambulia kusini mwa Sudan na muda mfupi baadaye kaskazini mwa Zaire. Ulitokea tena kwa kiwango kidogo katika 1979 huko Sudan. Baada ya hilo, isipokuwa katika visa vya hapa na pale vya watu kufa kutokana na dalili za maradhi ya Ebola, maradhi hayo yalipotea kwa miaka mingi.
Kirusi cha Ebola ni hatari sana hivi kwamba wanasayansi wanaokichunguza katika Atlanta hufanya hivyo katika maabara yanayotunzwa sana yaliyojengwa yakiwa na mfumo wa upitishaji hewa usioruhusu kijiumbe-maradhi chochote kipitishwacho hewani kiponyoke. Kabla ya kuingia kwenye maabara, wanasayansi huvalia “mavazi ya angani.” Wao huoga kwa kutumia dawa za kuua vijidudu waondokapo. Vikundi vya madaktari vilivyokuja Kikwit vilikuja na vitu vya kujilinda—mifuko ya mikono na kofia za kutumiwa mara moja na kutupwa, miwani kubwa-kubwa, na ovaroli za pekee zisizoruhusu hicho kirusi kupenya.
Tofauti na wanasayansi hao, wakazi wengi wa Kikwit walikosa ujuzi na vifaa vya kujilinda. Wengine wakijua, walihatarisha au kupoteza uhai wao kwa kuwatunza wapendwa wagonjwa. Wagonjwa na wafu walibebwa mgongoni au kwenye mabega ya marafiki na familia bila ulinzi wowote. Matokeo yalikuwa vifo vya wengi; hicho kirusi kiliangamiza familia nzima-nzima.
Kuzuia Mweneo
Jumuiya ya kimataifa iliitikia kilio cha Kikwit cha kutaka msaada wa kifedha na vifaa vya kitiba. Vikundi vya wachunguzi vilikuja kwa ndege kutoka Ulaya, Afrika Kusini, na Marekani. Kusudi lao la kuja lilikuwa na sehemu mbili: kwanza, kusaidia kuzuia mweneo; na pili, kugundua mahali kilipoishi kirusi kati ya vipindi viwili vya mashambulio.
Ili kusaidia kuzuia mweneo, wafanyakazi wa afya walienda mtaa kwa mtaa wakitafuta yeyote aliye na dalili za huo ugonjwa. Wagonjwa walipelekwa hospitalini, ambapo wangeweza kutengwa na wengine na kutunzwa kwa usalama. Waliokufa walifungwa kwa plastiki na kuzikwa upesi.
Kampeni kubwa sana ilianzishwa ili kuwatolea wafanyakazi wa afya na watu wote kwa ujumla habari sahihi juu ya hayo maradhi. Sehemu ya ujumbe huo ulionya sana dhidi ya mazoea ya kidesturi ya kuzika, ambayo yalitia ndani familia kushika na kuosha maiti kidesturi.
Kutafuta Chanzo
Wanasayansi walitaka kujua kirusi hicho kilitoka wapi. Lijulikanalo ni: Virusi si viumbe-huru, viwezavyo kula, kunywa, na kuongezeka vyenyewe tu. Ili kusalimika na kuzaana, ni lazima vishambulie na kutumia kwa faida yao muundo tata wa seli-hai.
Kirusi kimwambukizapo mnyama, kwa kawaida uhusiano huwa wa kuishi pamoja kwa upatani—mnyama hakiui kirusi, nacho kirusi hakimwui mnyama. Lakini mwanadamu agusanapo na mnyama aliyeambukizwa na kwa njia fulani kirusi chaingia mwilini mwa mwanadamu, hicho kirusi chaweza kuua.
Kwa kuwa kirusi cha Ebola huua watu, na tumbili, upesi sana, wanasayansi huamini kwamba kirusi hicho lazima huishi katika kiumbe kingine tofauti. Maofisa wa afya wakigundua ni aina gani ya kiumbe ambacho hubeba hicho kirusi, basi wataweza kuchukua hatua zenye mafanikio za kudhibiti na kuepuka mashambulio ya siku zijazo. Swali ambalo halijajibiwa juu ya Ebola ni, Kirusi hicho hukaa wapi kati ya vipindi vya mashambulio kwa mwanadamu?
Ili kujibu hilo swali, watafiti lazima wakifuate kirusi hicho hadi chanzo chake. Jitihada za kutafuta kiumbe chenye kirusi hicho wakati uliopita hazikufanikiwa. Lakini ambukizo hilo katika Kikwit liliandaa fursa mpya.
Wanasayansi walisadiki kuwa jeruhi wa kwanza wa ambukizo la Kikwit alikuwa Gaspard Menga. Lakini aliambukizwaje? Ikiwa ilikuwa kupitia mnyama fulani, ilikuwa aina gani ya mnyama? Kiakili, jibu laweza kupatikana katika msitu ambamo Menga alikuwa akifanya kazi. Vikundi vya kukusanya viliweka mitego 350 sehemu mbalimbali ambapo Menga alikuwa akichomea makaa. Vilinasa wanyama wagugunao, panya, todi, mijusi, nyoka, mbu, usubi, kupe, kunguni, chawa, funza, na viroboto—jumla ya wanyama wadogo 2,200 na wadudu 15,000. Wanasayansi waliovalia mavazi ya kujilinda, waliwaua hao wanyama kwa kutumia gesi ya nusu-kaputi. Kisha wakapeleka violezo vya tishu hadi Marekani, ambapo vingeweza kuchunguzwa hatua kwa hatua ikiwa vina kirusi hicho.
Kwa kuwa mahali kirusi kiwezapo kujificha ni pengi mno, hakuna uhakika wa kwamba chanzo kitapatikana. Dakt. C. J. Peters, kiongozi wa tawi la pekee la visababisha magonjwa la CDC, alisema: “Nadhani kuwa sasa uwezekano wa kupata makao ya kirusi cha Ebola ni asilimia 50 tu.”
Mweneo Wapotea
Katika Agosti 25, hilo ambukizo lilitangazwa rasmi kuwa limekwisha, kwa sababu ya kutokuwepo kwa visa vipya kwa muda wa siku 42, muda ulio mrefu mara mbili ya ule muda wa utamio wa kirusi hicho. Kwa nini maradhi hayo hayakuenea sana? Sababu moja ni jitihada za kimataifa za kitiba zilizofanywa ili kuzuia huo mweneo. Sababu nyingine iliyopunguza huo mweneo ni hatari ya hayo maradhi yenyewe. Kwa kuwa yalitokea na kuua upesi na kuwa ulienezwa kupitia kugusana tu, hayakuenea na kuwapata watu wengi.
Rekodi rasmi zaonyesha kwamba watu 315 walipata maradhi hayo na kwamba 244 kati yao walikufa—kiwango cha asilimia 77 cha vifo. Ebola kwa sasa ni tulivu. Katika ulimwengu mpya wa Yehova, kirusi Ebola kitanyamazishwa milele. (Ona Isaya 33:24.) Kwa sasa, watu wanajiuliza, ‘Je, Ebola itatokea ili kuua tena?’ Huenda. Lakini hakuna ajuaye mahali na wakati.
[Sanduku katika ukurasa wa25]
Mweneo wa Ebola kwa Kulinganishwa na Maradhi Mengine
Ebola ni muuaji, hata hivyo tisho kubwa kwa Waafrika husababishwa na maradhi yasiyo hatari zaidi. Wakati wa mweneo huo, maradhi mengineyo yaliua majeruhi wayo bila ya ulimwengu kujua. Iliripotiwa kuwa mamia machache ya kilometa mashariki mwa Kikwit, watu 250 waliambukizwa majuzi na polio. Kaskazini-magharibi, aina ifishayo ya kipindupindu ilishambulia Mali. Kusini, katika Angola watu 30,000 waliambukizwa ugonjwa wa malale. Katika eneo kubwa la Afrika Magharibi, maelfu yalikufa kwa sababu ya ambukizo la utando-ubongo. Gazeti The New York Times likasema: “Kwa Waafrika, swali lisumbualo ambalo huzuka ni kwa nini makabiliano ya [Afrika] ya kila siku na magonjwa yenye kufisha na yawezayo kuzuiwa hayachochei hata kidogo dhamiri ya ulimwengu.”
[Picha katika ukurasa wa 24]
Wanasayansi wanatafuta chanzo cha kirusi kiuacho