‘Kila Mahali Magonjwa ya Kuambukiza’
MAGONJWA ya kuambukiza ya kadiri isiyo na kifani yalikuwa sehemu iliyotabiriwa ya “ishara ya kuwapo [kwa Yesu Kristo] na ya umalizio wa mfumo wa mambo. (Mathayo 24:3, NW) Mwandishi wa Gospeli ya Luka aongeza jambo hili dogo ambalo halitajwi katika masimulizi ya Mathayo na Marko. (Mathayo, sura 24 na 25; Marko, sura 13) Maradhi ya kuambukiza na magonjwa yenye kuleta uharibifu mwingi yangetukia “kila mahali” katika siku za mwisho. (Luka 1:3, UV; 21:11, Habari Njema kwa Watu Wote) Je! magonjwa kama hayo yangetoka wapi?
“Wanasayansi wanajua vairasi (viini vidogo vinavyoambukiza) kadhaa zinazojificha katika tropiki ambazo—ikiwa nguvu za asili zingezichochea kidogo tu—zingesababisha vifo vingi kuliko vile ambavyo vyaelekea kutokana na ambukizo la UKIMWI,” lataarifu jarida Science News. “Hata kama orodha ya vairasi zilizomo ulimwenguni haibadiliki, watafiti wasema, tropiki tayari zina vairasi za kutosha kuambukiza na kuua sehemu kubwa za wakaaji wa Dunia.”
Jambo linalofanya muhula wetu uwe wenye kupatwa na magonjwa hayo kwa urahisi zaidi ni ongezeko la haraka la idadi ya watu duniani na mahitaji makubwa zaidi ya ulimwengu uliojaa watu. “Historia inaonyesha kwamba maambukizo ya ghafula ya kivairasi yenye kuhatarisha uhai yametokea mara nyingi wakati watu wamehamia mabara yasiyopata kutembelewa na watu au wakati hali za maisha katika miji mikubwa zilipoharibika katika njia zenye kutokeza mahali papya ambapo vairasi ziliweza kujificha,” yasema Science News. Wanadamu wanapoingia mahali penye vairasi ambapo hapakufikika mbeleni, mara nyingi maambukizo mapya ya kivairasi hutokea. Jambo hilo hilo hutukia wadudu waenezapo makao yao wakati tabia za hali-anga za dunia zinapobadilika. “Kuongezea hayo,” lasema gazeti hilo, “tekinolojia za ki-siku-hizi za kitiba kama vile kutia damu mishipani na kuatika viungo vya mwili zimeandalia vairasi njia mpya za kupitia kati ya wanadamu. Ndivyo na mabadiliko ya kijamii na ya kitabia yanayotia ndani kusafiri-safiri ugenini miongoni mwa matajiri na watu mashuhuri hadi zoea la kutumia sindano moja ya dawa za kulevya miongoni mwa wazoevu wa dawa za kulevya.”
“Historia ya hivi karibuni hutoa mifano ya wazi ya maambukizo madogo madogo ya kivairasi katika maeneo ya pekee ambayo huenda yakawa ishara ya maambukizo makubwa zaidi katika wakati ujao,” makala hiyo yaongeza. Mifano ni: vairasi iitwayo Marburg isiyojulikana mbeleni, vairasi hatari ya kitropiki iliyoambukiza wanasayansi wengi huko Ujerumani Magharibi katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1960; vairasi isababishayo homa ya Bonde la Ufa iliyoambukiza mamilioni na kuwaua maelfu huko Misri katika 1977; vairasi ya kitropiki iitwayo Ebola iliyoambukiza watu zaidi ya elfu moja huko Zaire na Sudan katika 1976 na kuua watu 500 hivi, wengi wao wakiwa madaktari na wauguzi waliokuwa wakiwatibu wenye kuambukizwa nayo.
Maambukizo ya kivairasi yenye kuleta maafa mengi hayatabiriwi kimbele mara nyingi. “Kwa mfano, katika 1918, aina tofauti ya vairasi yenye kudhuru vibaya sana itokanayo na mafua ya kibinadamu ilienea kuzunguka tufe lote, ikiua watu waliokadiriwa kuwa milioni 20,” lasema Science News. “Hivi karibuni zaidi, ulimwengu ulishtuliwa tena wakati wanadamu walipoanza kuambukizwa na vairasi ambayo labda wakati mmoja ilipatikana tu katika tumbili za Afrika. Vairasi ya UKIMWI imeambukiza sasa watu milioni 5 hadi milioni 10 katika nchi 149, kulingana na makadirio ya Shirika la Afya Ulimwenguni. Lakini kujapokuwa kushughulikiwa sana kwa tauni hii ya hivi karibuni sana, wenye kuchunguza vairasi wanahofu kwamba, mambo yenye kuhofisha zaidi yatungojea.”
Magonjwa ya kuambukiza yawe yenye kusononesha jinsi gani, hayo ni sehemu ya ishara yenye mambo mengi ya kuwapo kwa Yesu katika utukufu wa Ufalme, pamoja na mambo kama vita, njaa, na mitetemeko mikubwa ya nchi. (Marko 13:8; Luka 21:10, 11) Mambo hayo ni sababu ya kushangilia pia, kwani Luka aongeza maneno haya ya Yesu: “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.”—Luka 21:28.