Suluhisho Ni Nini?
“KUNA itikadi inayoongezeka kwamba hali-njema ya wanadamu, na labda hata kusalimika kwetu tukiwa spishi, kutategemea uwezo wetu wa kugundua maradhi yanayozuka. . . . Ni nini kingetupata leo ikiwa HIV ingekuwa kisababisha-maradhi chenye kuenezwa hewani? Na tuna uhakika gani kwamba ambukizo kama hilo haliwezi kufanya hivyo wakati ujao?” akasema D. A. Henderson—aliyetimiza fungu kubwa katika kumalizwa kwa ndui—kama ilivyoelezwa kikundi cha wanasayansi katika Geneva, Uswisi, katika 1993.
Magonjwa yazukayo yanaweza kugunduliwaje? Mfumo wa mapema wa kuonya mweneo wa maradhi ya kitropiki ni mfanyizo wa duniani pote wa maabara 35 ambayo huripoti kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Lakini, uchunguzi wa maabara haya ulionyesha kwamba ni maabara yasiyozidi nusu yaliyokuwa na vifaa vya kutosha kuweza kutambulisha encephalitis ya Kijapani, virusi-hanta, na homa ya Bonde la Ufa—yote yakiwa maradhi yenye kufisha. Ni asilimia 56 tu yaliyoweza kugundua homa-njano, kirusi kipitishwacho na mbu ambacho husababisha kutapika, kukosa kufanya kazi kwa ini, na kuvuja damu kwa ndani. Katika 1992 angalau watu 28 walikufa Kenya kwa sababu ya homa-njano kabla ya madaktari kugundua kisababishi. Kwa miezi sita walifikiri walikuwa wakipigana na malaria.
Udhaifu mwingine wa programu za uchunguzi ni kwamba haziwezi kutambua kuzuka kwa maradhi ya virusi yenye kutenda polepole. Kwa kielelezo, HIV, yaweza kujificha ndani ya mtu, kuenezwa kwa wengine, na kisha kujidhihirisha yenyewe kuwa UKIMWI hadi miaka kumi baadaye. Mweneo wa wakati huu wa UKIMWI ulizuka karibu kwa usawia katika mabara matatu na kushambulia haraka mataifa 20 tofauti. Kwa wazi, hakukuwa na onyo la mapema kwa jambo hilo!
Licha ya matatizo, wanasayansi wengi bado wanatazamia wakati ujao wakiwa na uhakika, wakiongea kwa kutarajia mazuri juu ya ugunduzi mkubwa na maendeleo makubwa ambayo yatakuja kwa hakika katika miaka inayokuja. Gazeti International Herald Tribune laripoti hivi: “Wanasayansi wengi wanasema kwamba tumaini zuri zaidi la maendeleo makubwa ya kweli, ni biotekinolojia, utumizi wa vitu vya kurithiwa katika chembe hai. Wanasayansi katika mashirika ya biotekinolojia wanatumaini kubuni chembe ambazo hutokeza vitu vyenye kuua vijidudu, yaani, aina mpya ya viuavijasumu vilivyochochewa kijeni.”
Hata hivyo, kuna sehemu zisizofaa kwa jambo hilo. Uchochezi wa kijeni umefanya iwezekane kutia jeni katika kirusi kisichodhuru ili kwamba hicho kirusi kipeleke jeni kwa watu. Tekinolojia hii yaweza kutumiwa kwa faida, labda ikifanya iwezekane hasa kutokezwa kwa hivyo viitwavyo eti viuavijasumu vilivyochochewa kijeni. Lakini tekinolojia hii yaweza pia kutumiwa kwa makusudi yenye kutokeza msiba.
Kwa kielelezo, jeni ziwezazo kutoka kwa Ebola zaweza kuingizwa kiaksidenti au kimakusudi katika kirusi, kama vile mafua makali au surua. Kisha kirusi hicho chenye kufisha chaweza kuenezwa kwa kukohoa au kupiga chafya. Dakt. Karl Johnson, ambaye ametumia muda wote wa maisha kuchunguza virusi kama vile Machupo na Ebola, alisema kwamba wakati utakuja karibuni ambapo “mtu yeyote mwenye mawazo ya kuumiza watu akiwa na vifaa vyenye kugharimu maelfu machache ya dola na akiwa na elimu ya biolojia ya chuoni angeweza kufanyiza viini vya kutokeza maradhi ambavyo Ebola ingeonekana kuwa isiyodhuru ikilinganishwa navyo.” Wanabiolojia wengine wana hangaiko lilo hilo.
Suluhisho
Kusuluhisha matatizo ya maradhi yenye kuambukiza si tu jambo la kutokeza dawa mpya. Huhusisha kusuluhisha matatizo yanayohusiana na maradhi kama vile umaskini, vita, wakimbizi, utumizi mbaya wa dawa za kulevya, kusongamana katika majiji, mitindo-maisha isiyo bora, uchafuzi, na kuhabiriwa kwa mazingira. Ebu sema kweli. Je, wafikiri binadamu yaelekea watasuluhisha matatizo haya yenye utata?
Neno la Mungu huonya hivi: “Msiwatumainie wakuu, wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake.” Basi, tumtumaini nani? Hilo andiko laendelea hivi: “Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, na tumaini lake ni kwa BWANA, Mungu wake, aliyezifanya mbingu na nchi.” Ni Yehova pekee, Muumba wa wanadamu, awezaye kusuluhisha mambo ambayo jamii ya binadamu inakabili bila kujua la kufanya.—Zaburi 146:3-6.
Neno la Yehova lililopuliziwa, Biblia, katika kurekodi unabii mkuu wa Yesu kuhusu “ishara ya . . . umalizio wa mfumo wa mambo,” lilitabiri taabu za kitiba zinazokipata kizazi chetu. Yesu alisema hivi: “Katika mahali pamoja baada ya pengine maradhi ya kuambukiza.”—Mathayo 24:3-8, New World Translation; Luka 21:10, 11, NW.
Hata hivyo, Biblia pia hutaja wakati ujao duniani chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu wakati ambapo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24; Mathayo 6:9, 10) Hivyo wale wanaomtumaini Yehova wana sababu imara ya kuamini kwamba wanadamu watiifu karibuni watapata kitulizo chenye kudumu si kutokana na maradhi yenye kufisha yanayokumba binadamu tu bali pia matatizo ambayo yanachangia maradhi. Wakristo wa kweli wanathamini jitihada za jamii ya kitiba katika pigano gumu dhidi ya vijiumbe-maradhi vyenye kufisha. Hata hivyo, wanajua kwamba ni Mungu tu aliye na suluhisho lenye kudumu kwa maradhi na kifo, yule ambaye ‘anaponya magonjwa yenu yote.’—Zaburi 103:1-3; Ufunuo 21:1-5; 22:1, 2.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Biblia iliahidi wakati ambapo hakuna atakayesema, “Mimi mgonjwa”