Jina la Mungu—Maana Yalo na Linavyotamkwa
MMOJA wa Waandikaji wa Biblia aliuliza hivi: “Ni nani aliyekamata upepo kwa makonzi yake? Ni nani aliyefunga maji ndani ya nguo yake? Ni nani aliyefanya imara ncha zote za nchi? Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe, kama wajua?” (Mithali 30:4) Sisi tunaweza kujuaje jina la Mungu ni jina gani? Hilo ni ulizo la maana. Uumbaji ni ushuhuda wenye nguvu wa kwamba bila shaka kuna Mungu, lakini hautuambii jina lake. (Warumi 1:20) Kwa kweli, hatungeweza kamwe kulijua jina la Mungu isipokuwa Muumba mwenyewe angetuambia. Naye amefanya hivyo katika Kitabu chake mwenyewe, Biblia Takatifu.
Pindi moja yenye maana sana, Mungu alitamka jina lake mwenyewe, akarudia kulisema na Musa akiwa anasikia. Musa aliandika masimulizi ya tukio hilo ambayo yametunzwa katika Biblia mpaka wakati wetu. (Kutoka 34:5) Mungu hata aliandika jina lake kwa “kidole” chake mwenyewe. Alipokwisha kumpa Musa zile tunazoita leo Amri Kumi, kwa muujiza Mungu aliziandika. Habari inasema: “Na wakati [Mungu] alipomaliza kuzungumza na Musa katika mulima Sinai, akamupa mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe zilizoandikwa kwa kidole cha Mungu.” (Kutoka 31:18, ZSB) Katika hizo Amri Kumi za awali jina la Mungu laonekana mara nane. (Kutoka 20:1-17) Hivyo Mungu mwenyewe amefunulia wanadamu jina lake, akifanya hivyo kwa mdomo na kwa maandishi. Hivyo, hilo ni jina gani?
Katika lugha ya Kiebrania jina hilo linaandikwa יהוה. Herufi nne hizo, zinazoitwa Tetragramatoni, zinasomeka katika Kiebrania kutoka kulia kwenda kushoto nazo zinaweza kuwakilishwa katika lugha nyingi za siku hizi kuwa YHWH au JHVH. Jina la Mungu lenye kuwakilishwa na herufi bubu hizo nne, laonekana karibu mara 7,000 katika “Agano la Kale,” au Maandiko ya Kiebrania ya awali.
Jina hilo ni namna ya kitenzi cha Kiebrania ha·wahʹ (הוה), maana yake “kuwa,” na kwa hakika jina hilo linamaanisha “Yeye Anafanya Iwe.”a Hivyo, jina la Mungu linamtambulisha kuwa Yeye ambaye hatua kwa hatua anatimiza ahadi zake na pasipo kushindwa anatimiza makusudi yake. Ni Mungu wa kweli tu ndiye angeweza kuwa mwenye jina hilo lenye kujaa maana.
Je! wazikumbuka njia tofauti-tofauti ambazo jina la Mungu lilionekana katika Zaburi 83:18 (ukurasa wa 5)? Mbili kati ya tafsiri hizo zilitumia mitajo ya cheo tu (BWANA,” “Mwenyezi-Mungu”) kuwa badala ya jina la Mungu. Lakini katika mbili za hizo, Yahweh na Yehova, unaweza kuona zile herufi nne za jina la Mungu. Ingawa hivyo, matamshi ni tofauti. Kwa nini?
Jina la Mungu Linatamkwaje?
Ukweli ni kwamba, hakuna mtu ajuaye kwa uhakika jinsi jina la Mungu lilivyotamkwa hapo awali. Kwa nini? Lugha ya kwanza kutumiwa katika kuandika Biblia ilikuwa Kiebrania, na lugha ya Kiebrania ilipokuwa ikiandikwa, waandikaji waliandika herufi bubu (konsonanti) tu—si irabu. Kwa sababu hiyo, waandikaji walioongozwa kwa roho ya Mungu walipoandika jina la Mungu, bila shaka walifanya ivyo hivyo wakaandika herufi bubu tu.
Ijapokuwa Kiebrania cha kale kilikuwa lugha iliyokuwa ikisemwa kila siku, halikuwa tatizo. Matamshi ya Jina hilo yalijulikana na Waisraeli na walipoliona katika maandishi walitia irabu (a, e, i, o, u) bila kufikiri (kama vile, kwa msomaji wa Kiswahili, herufi hizi za mkato “jng” zinavyowakilisha “jengo”).
Kuna mambo mawili yaliyotukia yakabadili hali hiyo. Kwanza, kulitokea wazo la kishirikina miongoni mwa Wayahudi la kwamba lilikuwa kosa kulitamka kwa sauti kuu jina la Mungu; basi walipolifikia katika kusoma kwao Biblia walitaja neno la Kiebrania ’Adho·naiʹ (“Bwana Mwenye Enzi Kuu”). Isitoshe, wakati uliposonga, lugha yenyewe ya kale ya Kiebrania ikaacha kusemwa katika maongezi ya kila siku, hivyo ndivyo hatimaye matamshi ya Kiebrania ya awali ya jina la Mungu yalivyosahauliwa.
Ili kuhakikisha kwamba matamshi ya lugha yote ya Kiebrania hayakupotea, wasomi wa Kiyahudi wa nusu ya pili ya miaka ya kwanza 1,000 W.K. walibuni mfumo wa nukta za kuwakilisha irabu zilizokosekana, wakaziweka hizo kwenye herufi bubu katika Biblia ya Kiebrania. Hivyo, irabu na herufi bubu zikaandikwa, na matamshi yakatunzwa kama yalivyokuwa wakati ule.
Jina la Mungu lilipofikiwa, badala ya kuweka alama za irabu zinazofaa juu yalo, mara nyingi waliweka alama nyingine za irabu ili kumkumbusha msomaji kwamba amepaswa aseme ’Adho·naiʹ. Hilo likatokeza endelezo la Iehoua, na, mwishowe, Yehova yakawa ndiyo matamshi yenye kukubaliwa ya jina la Mungu katika Kiswahili. Matamshi hayo yanatunza sehemu za muhimu za jina la Mungu kutoka Kiebrania cha awali.
Ni Matamshi Gani Ambayo Wewe Utatumia?
Ingawa hivyo, matamshi kama vile Yahweh, yalitoka wapi? Hizo ni namna ambazo wasomi wa siku hizi wamependekeza zitumiwe, wakijaribu kujua matamshi ya awali ya jina la Mungu. Baadhi yao, ingawa si wote, wanadhani kwamba labda Waisraeli waliokuwako kabla ya wakati wa Yesu walitamka jina la Mungu kuwa Yahweh. Lakini hakuna awezaye kuwa na hakika. Labda walilitamka hivyo, labda hawakutamka hivyo.
Ingawa hivyo, wengi wanapendelea kutamka Yehova. Kwa nini? Kwa sababu watu wengi wamezoea kutamka hivyo kuliko kutamka Yahweh. Lakini, haingekuwa afadhali kutumia namna ya jina hilo ambayo inaelekea kuwa karibu zaidi na matamshi yale ya awali? Sivyo kabisa, kwa maana siyo desturi ya kutamka majina ya Biblia.
Kwa kutumia mfano wenye kutokeza zaidi, fikiria jina la Yesu. Je! wewe unajua jinsi jamaa na rafiki za Yesu walivyomtaja katika mazungumzo ya kila siku alipokuwa akikua katika Nazareti? Ukweli ni kwamba, hakuna binadamu ajuaye hakika, ijapo labda alitajwa kama Yeshua (au labda Yehoshua). Kwa hakika hakutajwa kamwe kuwa Yesu.
Ingawa hivyo, masimulizi ya maisha yake yalipoandikwa katika lugha ya Kigiriki, waandikaji walioongozwa na Mungu hawakujaribu kutunza matamshi hayo ya awali ya Kiebrania. Bali, walitafsiri jina hilo katika Kigiriki hivi, I·e·sousʹ. Leo jina hilo linatafsiriwa kwa njia tofauti kulingana na lugha ya msomaji wa Biblia. Wasomaji wa Biblia Wakikuyu, Wataita na Wamaasai wanakuta Jesu. Wakamba wanaliendeleza hivi Yesũ (likitamkwa Yeso). Na Wasomali wanaliendeleza hivi Ciise (likitamkwa Iiseh).
Je! ni lazima tuache kulitumia jina la Yesu kwa sababu wengi wetu, au hata sote, hatujui hasa jinsi lilivyokuwa likitamkwa pale awali? Kufikia sasa, hakuna mtafsiri ambaye amependekeza tufanye hivyo. Tunapenda kutumia jina hilo, kwa maana linatambulisha aliye Mwana mpendwa wa Mungu, Yesu Kristo, aliyetoa damu ya uhai wake kwa ajili yetu. Je! ingekuwa ni kumheshimu Yesu kuacha kutumia jina lake mahali pote ambapo linatajwa katika Biblia na kutumia mtajo tu wa cheo kama “Mwalimu,” au “Mpatanishi”? Sivyo kabisa! Tunapotumia jina la Yesu kwa jinsi watu wengi wanavyolitamka katika lugha yetu, tunaweza kuwa na uhusiano naye.
Ingeweza kusemwa namna iyo hiyo juu ya majina yote tunayosoma katika Biblia. Tunayatamka katika lugha yetu wenyewe na hatujaribu kufuata mfano wa jinsi yalivyokuwa yakitamkwa hapo awali. Hivyo tunasema “Yeremia,” wala si Yir·meyaʹhu. Hali kadhalika tunasema Isaya, ijapokuwa katika siku zake inaelekea nabii huyo alijulikana kuwa Yesha‛-yaʹhu. Hata wasomi wanaojua jinsi majina hayo yalivyokuwa yakitamkwa hapo awali, wanayatamka kwa mtindo wa kisasa, wala si kwa mtindo wa kikale, wanaposema juu yao.
Ni hali moja na jina Yehova. Hata ijapo huenda namna ya kisasa ya kutamka Yehova isiwe sawasawa na lilivyokuwa likitamkwa hapo awali, kutolitamka hivyo hakuondoi umaana wa jina hilo. Kunamtambulisha Muumba, Mungu aliye hai, Aliye Juu Zaidi Sana ambaye Yesu aliambia hivi: “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe.”—Mathayo 6:9.
“Haliwezi Kuondolewa Libadilishwe na Jingine”
Ijapokuwa watafsiri wengi wanapendelea Yahweh, Biblia ya New World Translation na pia tafsiri nyingine kadha zinaendelea kutumia Jehovah kwa sababu watu wamezoea kutamka hivyo kwa karne nyingi. Zaidi ya hayo, namna hiyo ya kutamka, sawa na matamshi mengine, inatunza zile herufi nne za Tetragramatoni, yaani, YHWH au JHVH.b
Wakati wa mapema, Gustav Friedrich Oehler, profesa Mjeremani aliamua kama hivyo kwa sababu iyo hiyo. Alizungumza matamshi mbalimbali kisha akakata shauri hivi: “Kuanzia hapa na kuendelea mimi ninalitumia neno Yehova, kwa sababu, ni wazi kwamba jina hili limezoeleka likawa asili yetu katika maneno tunayoyatumia kwa ukawaida, na haliwezi kuondolewa libadilishwe na jingine.”—Theologie des Alten Testaments (Theolojia ya Agano la Kale), chapa ya pili, kilichochapishwa mwaka wa 1882, ukurasa wa 143.
Hali kadhalika, katika kitabu chake Grammaire de l’hébreu biblique (Sarufi za Kiebrania cha Biblia), chapa ya mwaka wa 1923, katika maelezo ya chini yaliyo katika ukurasa wa 49, Paul Joüon, msomi wa Kijesuiti anaeleza hivi: “Badala ya neno Yahweh (la kudhania tu), katika tafsiri zetu sisi tumetumia neno Jéhovah . . . ambalo ndiyo namna ya kawaida inayotumiwa kuandikwa katika Kifaransa.” Katika lugha nyingine nyingi watafsiri wa Biblia wanatumia namna hiyo, kama inavyoonyeshwa katika kisanduku kilicho katika ukurasa wa 8.
Basi, je! ni kosa kutumia Yahweh? Si kosa. Ni kwa vile tu inaelekea kwamba msomaji ataelewa upesi zaidi namna ya Yehova kwa sababu ‘imezoeleka ikawa asili’ katika lugha nyingi. Jambo la maana kwetu ni kutumia jina hilo na kulitangaza kwa wengine. “Mshukuruni Jehova, linganani jina lakwe, tangazani habari za vitendo vyakwe katika hizo kabila za watu, semani ya kwamba jina lakwe limetukuka sana.”—Isaya 12:4, The Old Testament in Swahili (Mombasa), chapa ya mwaka wa 1949.
Na tuone jinsi watumishi wa Mungu wametenda katika karne nyingi kupatana na amri hiyo.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Appendix 1A katika New World Translation of the Holy Scriptures, chapa ya 1984.
b Ona Appendix 1A katika New World Translation of the Holy Scriptures, chapa ya 1984.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Wasomi wengi wana mawazo tofauti-tofauti juu ya jinsi jina YHWH lilivyokuwa likitamkwa hapo awali.
Katika kitabu The Mysterious Name of Y.H.W.H., Dakt. M. Reisel alisema katika ukurasa wa 74 kwamba, “ni lazima iwe kwamba kutiwa kwa irabu katika Tetragramatoni kulikuwa YeHūàH au YaHūàH.”
Kasisi D. D. Williams wa Cambridge alishikilia wazo la kwamba “ushahidi unaonyesha, au unakaribia kuthibitisha, kwamba Jãhwéh hayakuwa ndiyo matamshi ya kweli ya Tetragramatoni . . . Labda Jina lenyewe lilikuwa JÃHÔH.”—Zeitschrift für die alttestamentliche Wissenschaft (Jarida la Maarifa ya Agano la Kale), 1936, Buku la 54, ukurasa wa 269.
Katika maelezo ya maneno ya kitabu cha Kifaransa Revised Segond Version, ukurasa wa 9, maelezo haya yametolewa: “Matamshi haya Yahvé yanayotumiwa katika tafsiri fulani za karibuni yanategemea mashahidi wachache wa kale, lakini hawana uthibitisho. Mtu akifikiria majina ya kibinafsi yanayotia ndani jina la Mungu, kama vile jina la Kiebrania la nabii Eliya (Eliyahou) huenda matamshi yakawa pia Yaho au Yahou.”
Katika mwaka wa 1749 Teller, msomi Mjeremani wa Biblia, alieleza hivi juu ya matamshi fulani tofauti-tofauti ya jina la Mungu ambayo alikuwa amesoma: “Diodoro kutoka Sisili, Makrobio, Klemensi Aleksandrino, Mtakatifu Jerome na Origenesi waliandika Jao; Wasamaria, Epifanio, Theodoreto waliandika Jahe, au Jave; Ludwig Kapelo anasoma Javoh; Drusio, Jahve; Hottinger, Jehva; Marsero, Jehovah; Kastelio, Jovah; na le Clerc, Jawoh, au Javoh.”
Hivyo ni wazi kwamba haijulikani tena jinsi jina la Mungu lilivyokuwa likitamkwa hapo awali. Wala hilo si jambo la maana sana. Kama lingekuwa jambo la maana, Mungu angalihakikisha kwamba matamshi yalitunzwa ili tuyatumie. Jambo la maana ni kutumia jina la Mungu kulingana na matamshi ambayo yamekuwa ya kawaida katika lugha yetu wenyewe.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Namna jina la Mungu linavyotamkwa katika lugha mbalimbali, kuonyesha jinsi namna ya kutamka Yehova imekubaliwa na mataifa yote
Bari - Yekowa
Chichewa - Yehova
Ciwemba - Yehoba
Kifaransa - Jéhovah
Kifiji - Jiova
Kiholanzi - Jehovah
Kiingereza - Jehovah
Kiitalia - Geova
Kijapani - Ehoba
Kijeremani - Jehova
Kikalenjin - Jehovah
Kikamba - Yeova
Kikuyu - Jehova
Kilingala - Jéhovah
Kiluo - Jehova
Kimambwe - Yeova
Kimaori - Ihowa
Kimaragoli - Yahova
Kimaasai - Jehova
Kimeru - Jehova
Kinyakyusa - Jihoba
Kinyamwanga - Yeova
Kinyarwanda - Yehova
Kinyore - Yehowah
Kipsigis - Jehoba
Kipolandi - Jehowa
Kireno - Jeová
Kispania - Jehová
Kisotho - Jehova
Kisukuma - Yehova
Kiswahili - Yehova
Kiswedi - Jehova
Kitonga - Jihova
Kixhosa - uYehova
Kiyoruba - Jehofah
Kizande - Yekova
Kizulu - uJehova
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
“Yehova” limejulikana kote kote kuwa ndilo jina la Mungu hata katika maneno yasiyo ya Kibiblia.
Franz Schubert alitunga muziki kwa ajili ya shairi lenye kichwa “Uweza Yote,” lililoandikwa na Johann Ladislav Pyrker, na humo jina hili Yehova linaonekana mara mbili. Pia limetumiwa mwishoni mwa tamasha ya mwisho ya mchezo wa kuigiza wenye muziki wa Verdi uitwao “Nabucco.”
Tena, mtungo wa sauti za waimbaji wa Arthur Honegger, mtungaji Mfaransa, unaoitwa “Mfalme Daudi,” unalipa jina Yehova umaarufu sana, naye Victor Hugo, mwandikaji Mfaransa mwenye sifa sana, alilitumia katika baadhi ya vitabu vyake zaidi ya 30. Yeye pamoja na Lamartine waliandika mashairi yenye vichwa “Yehova.”
Katika kitabu kinachoitwa Deutsche Taler (Sarafu ya Kijeremani), kilichochapishwa mwaka wa 1967 na Federal Bank ya Ujeremani, mna picha ya ile ambayo ni mojapo sarafu za zamani sana yenye jina “Yehova,” sarafu ya mwaka wa 1634 kutoka Jimbo la Mtawala mdogo wa Silesia. Kwa habari ya picha iliyo upande mwingine wa sarafu hiyo, inasema: “Chini ya jina YEHOVA lenye kung’aa, ngao yenye kuvikwa taji pamoja na nembo ya taifa ya Silesia inainuka katikati ya mawingu.”
Katika nyumba ya makumbusho katika Rudolstadt, Ujeremani, unaweza kuliona jina YEHOVA kwa herufi kubwa juu ya kola ya deraya ambayo wakati mmoja ilivaliwa na Gustavus wa Pili Adolph, mfalme wa Swedeni wa karne ya 17.
Ndivyo, kwa karne nyingi namna hii Yehova imekubaliwa na mataifa yote kuwa njia ya kutamka jina la Mungu, na watu wanaosikia hivyo mara hiyo wanatambua anayesemwa. Kama alivyosema Profesa Oehler, “Jina hili limezoeleka likawa asili yetu katika maneno tunayoyatumia kwa ukawaida, na haliwezi kuondolewa libadilishwe na jingine.”—Theologie des Alten Testaments (Theolojia ya Agano la Kale).
[Picha katika ukurasa wa 6]
Maelezo ya malaika mwenye jina la Mungu, juu ya kaburi la Papa Clement wa 13 katika Basilika ya Mt. Petro, katika Vatikani
[Picha katika ukurasa wa 7]
Sarafu nyingi zilifanywa zikiwa na jina la Mungu. Sarafu hii, ya tarehe ya mwaka wa 1661, ilitoka Nuremberg, Ujeremani. Maandishi ya Kilatini yanasema: “Chini ya uvuli wa mabawa yako”
[Picha katika ukurasa wa 9]
Nyakati za zamani, jina la Mungu likiwa kwa namna ya Tetragramatoni (herufi nne za Kiebrania) lilifanywa kuwa sehemu ya kupambia majengo mengi ya kidini
Basilika ya Katoliki ya Fourvière, katika Lyons, Ufaransa
Kathedro ya Bourges, katika Ufaransa
Kanisa katika La Celle Dunoise, Ufaransa
Kanisa katika Digne, Ufaransa kusini
Kanisa katika Sao Paulo, Brazili
Kathedro ya Strasbourg, Ufaransa
Kathedro ya Mtakatifu Marko, katika Venice, Italia
[Picha katika ukurasa wa 10]
Jina la Yehova linavyoonekana katika makao ya watawa katika Bordesholm, Ujeremani;
juu ya sarafu ya Kijeremani yenye tarehe ya mwaka wa 1635;
juu ya mlango wa kanisa katika Fehmarn, Ujeremani;
na juu ya jiwe la kaburi la mwaka wa 1845 katika Harmannschlag, Austria ya Chini