Sura ya 36
Jiji Kubwa Lateketezwa
Njozi ya 12—Ufunuo 18:1–19:10
Habari: Anguko na uharibifu wa Babuloni Mkubwa; ndoa ya Mwana-Kondoo yatangazwa
Wakati wa utimizo: Kutoka 1919 mpaka baada ya ile dhiki kubwa
1. Ni nini kitakachotia alama mwanzo wa dhiki kubwa?
CHA GHAFULA, chenye kugutusha, chenye kuteketeza—ndivyo kitakuwa kifo cha Babuloni Mkubwa! Kitakuwa mojapo matukio yenye msiba mkuu zaidi sana katika historia yote, kikifanyiza mwanzo wa “dhiki kubwa kama ambayo haijapata kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka sasa, la, wala haitatukia tena.”—Mathayo 24:21, NW.
2. Ingawa milki za kisiasa zimeinuka na zikaanguka, ni milki ya aina gani ambayo imedumu?
2 Dini bandia imekuwapo kwa muda mrefu. Imekuwapo bila kikomo tangu siku za Nimrodi mwenye kiu cha damu ambaye alipinga Yehova na akaanzisha watu kujenga Mnara wa Babeli. Yehova alipovuruga ndimi za waasi hao na kuwatawanya juu ya dunia, dini bandia ya Babuloni ilienda pamoja nao. (Mwanzo 10:8-10; 11:4-9) Tangu hapo, milki za kisiasa zimeinuka na zikaanguka, lakini dini ya Kibabuloni imedumu. Imechukua sura na maumbo mengi, ikiwa milki ya ulimwengu ya dini bandia, Babuloni Mkubwa aliyetolewa unabii. Sehemu yake yenye kutokeza zaidi sana ni Jumuiya ya Wakristo, ambayo ilikua kutokana na mchanganyo wa mafundisho ya Kibabuloni ya mapema zaidi na mafundisho ya “Ukristo” ulioasi imani. Kwa sababu ya historia ndefu, ndefu mno ya Babuloni Mkubwa, watu wengi wanaliona kuwa jambo gumu kuitikadi kwamba itaangamizwa wakati wowote.
3. Ufunuo unathibitishaje hukumu ya maangamizi ya dini bandia?
3 Kwa hiyo inafaa kwamba yaupasa Ufunuo uthibitishe hukumu ya uangamivu wa dini bandia kwa kutupatia maelezo mawili yenye mambo mengi ya kuanguka kwake na matukio yanayofuata yakiongoza kwenye kufanywa ukiwa wake mkubwa. Sisi tumekwisha kumwona yeye akiwa ndiye “kahaba mkubwa” ambaye mwishowe anateketezwa na wale ambao hapo zamani walikuwa wapenzi wake wa milki ya kisiasa. (Ufunuo 17:1, 15, 16, NW) Sasa, katika njozi nyingine bado, sisi tutamwona akiwa jiji, kifananisho cha kidini cha Babuloni wa kale.
Babuloni Mkubwa Aanguka
4. (a) Yohana anafuata kuona njozi gani? (b) Sisi tunaweza kumtambuaje malaika, na ni kwa nini inamfaa yeye atangaze anguko la Babuloni Mkubwa?
4 Yohana aendelea na simulizi, akituambia: “Baada ya vitu hivi mimi nikaona malaika mwingine akishuka kutoka katika mbingu, akiwa na mamlaka kubwa; na dunia ilinururishwa kutokana na utukufu wake. Na yeye akalia kwa sauti imara, kusema: ‘Yeye ameanguka! Babuloni Mkubwa ameanguka.’” (Ufunuo 18:1, 2a, NW) Hii ni mara ya pili kwa Yohana kusikia tangazo hilo la kimalaika. (Ona Ufunuo 14:8.) Hata hivyo, wakati huu umaana walo umekaziwa na utukufu wa huyo malaika wa kimbingu, kwa kuwa utukufu wake unanururisha dunia kwa ujumla! Yeye anaweza kuwa nani? Karne nyingi mapema nabii Ezekieli, akiripoti juu ya njozi ya kimbingu, alitaarifu kwamba “dunia yenyewe iling’aa kwa sababu ya utukufu [wa Yehova].” (Ezekieli 43:2, NW) Malaika pekee wa kung’aa kwa utukufu unaolinganika na wa Yehova angekuwa Bwana Yesu, ambaye ni “ule mrudisho wa utukufu [wa Mungu] na uwakilisho barabara wa kuwako kwake kwenyewe.” (Waebrania 1:3, NW) Katika 1914, Yesu alipata kuwa Mfalme mbinguni, na tangu wakati huo amekuwa akitumia mamlaka juu ya dunia akiwa Mfalme na Hakimu mshirika wa Yehova. Inafaa, basi, kwamba imempasa yeye atangaze kuanguka kwa Babuloni Mkubwa.
5. (a) Malaika huyo anatumia nani kutoa habari ya anguko la Babuloni Mkubwa? (b) Hukumu ilipoanza juu ya wale wenye kudai kuwa “nyumba ya Mungu,” Jumuiya ya Wakristo ilikuwa hali gani?
5 Malaika huyu mwenye mamlaka kubwa anatumia nani katika kutoa habari kama hizo zenye kushangaza mbele ya aina ya binadamu? Kwani, ni wale watu wenyewe ambao wanaachiliwa likiwa tokeo la anguko hilo, wale wapakwa-mafuta wabakio duniani, jamii ya Yohana. Kutoka 1914 mpaka 1918, hao waliteseka sana mikononi mwa Babuloni Mkubwa, lakini katika 1918 Bwana Yehova na “mjumbe wa agano [la Kiabrahamu]” wake, Yesu Kristo, alianza hukumu pamoja na “nyumba ya Mungu,” wale wenye kudai kuwa Wakristo. Hivyo Jumuiya ya Wakristo iliyoasi imani ililetwa kwenye jaribio. (Malaki 3:1; 1 Petro 4:17, NW) Hatia ya damu yayo kubwa mno iliyopata wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, ushiriki wayo katika kunyanyasa mashahidi waaminifu wa Yehova, na itikadi zayo za Kibabuloni havikuisaidia katika wakati wa hukumu yayo; wala hapana sehemu nyingine yoyote ya Babuloni Mkubwa iliyostahili kibali cha Mungu.—Linga Isaya 13:1-9.
6. Inaweza kusemwaje kwamba Babuloni Mkubwa alikuwa ameanguka kufikia 1919?
6 Hivyo kufikia 1919 Babuloni Mkubwa alikuwa ameanguka, kufungulia njia watu wa Mungu waachiliwe na warudishwe, kana kwamba kwa siku moja, kwenye bara lao la ufanisi wa kiroho. (Isaya 66:8) Kufikia mwaka huo, Yehova Mungu na Yesu Kristo, Dario Mkubwa Zaidi na Sairasi Mkubwa Zaidi, walikuwa wameongoza mambo kwa werevu ili kwamba dini bandia isiweze tena kuwashikilia watu wa Yehova. Haingeweza tena kuwazuia wasimtumikie Yehova na kujulisha kwa wote ambao yamkini kusikia kwamba Babuloni Mkubwa aliye kama kahaba amehukumiwa uangamivu na kwamba kutetewa kwa enzi kuu ya Yehova kumekaribia karibu.—Isaya 45:1-4; Danieli 5:30, 31.
7. (a) Ingawa Babuloni Mkubwa hakuharibiwa katika 1919, Yehova alimwonaje? (b) Babuloni Mkubwa alipoanguka katika 1919, tokeo lilikuwa nini kwa watu wa Yehova?
7 Ni kweli, Babuloni Mkubwa hakuangamizwa katika 1919—kama vile jiji la Babuloni la kale halikuangamizwa katika 539 K.W.K. wakati lilipoanguka mikononi mwa majeshi ya Sairasi Mwajemi. Lakini kwa maoni ya Yehova, tengenezo hilo lilikuwa limeanguka. Yeye alikuwa amepata hukumu mbaya ya kimahakama, akingojea kufishwa; kwa hiyo dini bandia haingeweza kushikilia tena watu wa Yehova katika utekwa. (Linga Luka 9:59, 60.) Hao waliachiliwa wakatumikie wakiwa mtumwa mwaminifu na mwenye uangalifu wa Bwana-Mkubwa wakitoa chakula cha kiroho kwa wakati unaofaa. Wao walikuwa wamepokea hukumu ya ‘Mmefanya vema’ nao walipewa utume wajishughulishe tena na kazi ya Yehova.—Mathayo 24:45-47; 25:21, 23; Matendo 1:8, NW.
8. Ni tukio gani ambalo mlinzi wa Isaya 21:8, 9 hupigia mbiu, na ni nani leo anayetolewa kivuli na mlinzi huyo?
8 Mileani nyingi zilizopita Yehova alitumia manabii wengine watabiri tukio hili kubwa lenye kuanzisha muda maalumu. Isaya alisema juu ya mlinzi ambaye “aliendelea kuita kwa sauti kubwa kama simba: ‘Juu ya mnara wa lindo, O Yehova, mimi ninasimama daima mchana, na kwenye kilindio changu mimi nimewekwa mausiku yote.’” Na ni tukio gani analotambua mlinzi huyo na kupiga mbiu kwa ujasiri kama wa simba? Hili: “Yeye ameanguka! Babuloni ameanguka, na mifano yote ya kuchongwa ya miungu yake [Yehova] amevunja hadi kwenye dunia!” (Isaya 21:8, 9, NW) Mlinzi huyu anatolea kivuli vizuri jamii ya Yohana leo ambayo ni yenye kuamka kabisa, inapotumia gazeti Mnara wa Mlinzi na vichapo vingine vya kitheokrasi kuvumisha kotekote habari za kwamba Babuloni ameanguka.
Mshuko wa Babuloni Mkubwa
9, 10. (a) Uvutano wa dini ya Kibabuloni umepatwa na mpunguo gani tangu Vita ya Ulimwengu 1? (b) Malaika mwenye nguvu anaelezaje hali ya kuanguka ya Babuloni Mkubwa?
9 Anguko la Babuloni wa kale katika 539 K.W.K. lilikuwa mwanzo wa mshuko mrefu ambao ulimalizikia katika ukiwa wake. Hali kadhalika, tangu vita ya kwanza ya ulimwengu, uvutano wa dini ya Kibabuloni umeshuka sana kwa kadiri ya tufe lote. Kufuata vita ya ulimwengu ya pili, ibada ya Shinto ya maliki ilikatazwa katika Japani. Katika China, serikali ya Kikomunisti hudhibiti uwekwaji rasmi na utendaji wote wa kidini. Katika Ulaya kaskazini ya Kiprotestanti, watu walio wengi wamekuwa wasiopendezwa na dini. Na hivi majuzi Kanisa Katoliki la Roma limedhoofishwa na mifarakano na kutopatana kwa ndani katika milki yalo ya tufe lote.—Linga Marko 3:24-26.
10 Pasipo shaka miendo hii yote ni sehemu ya ‘kukauka kwa mto Eufrati’ katika kutayarishia shambulio linalokuja la kivita juu ya Babuloni Mkubwa. ‘Kukauka’ huku kunaonyeshwa, vilevile, katika tangazo la papa la Oktoba 1986 kwamba lazima kanisa ‘liwe mwomba-ombaji tena’—kwa sababu ya upungufu mkubwa mno. (Ufunuo 16:12) Hususa tangu 1919 Babuloni Mkubwa amekuwa akifichuliwa atazamwe na wote kuwa yeye ni bara-tupu la kiroho, kama malaika mwenye nguvu anavyotangaza hapa: “Na yeye amekuwa mahali pa kukaa roho waovu na mahali pa kujibanza kila pumzi isiyo safi na mahali pa kujibanza kila ndege asiye safi na mwenye kuchukiwa!” (Ufunuo 18:2b, NW) Karibuni atakuwa bara-tupu kama hilo kihalisi, akiwa ukiwa kama magofu ya Babuloni katika Iraki ya leo.—Ona pia Yeremia 50:25-28.
11. Ni katika maana gani Babuloni Mkubwa amekuwa “mahali pa kukaa roho waovu” na ‘mahali pa kujibanza pumzi zisizo safi na pa ndege wasio safi’?
11 Neno “roho waovu” hapa inaelekea ni mrudisho wa neno “roho waovu wenye umbo-mbuzi” (se‘i·rimʹ) linalopatikana katika elezo la Isaya kuhusu Babuloni aliyeanguka: “Na huko mizuka ya mikoa isiyo na maji kwa hakika italala chini, na nyumba zayo lazima zijawe na tai-bundi. Na huko mbuni lazima wakae, na roho waovu wenye umbo-mbuzi wenyewe wataenda wakirukaruka huko.” (Isaya 13:21, NW) Huenda isirejezee roho waovu halisi bali wanyama wakaa-jangwani wenye nywele za matimutimu ambao mwonekano wao ulifanya watazamaji wafikirie roho waovu. Katika magofu ya Babuloni Mkubwa, kuwako kitamathali kwa wanyama kama hao, pamoja na hewa tuli (“pumzi isiyo safi”) yenye sumu, na ndege wasio safi, huashiria hali yake ya kiroho iliyokufa. Yeye hatolei aina ya binadamu mataraja yoyote ya uhai.—Linga Waefeso 2:1, 2.
12. Hali ya Babuloni Mkubwa hulandaje unabii wa Yeremia katika sura ya 50?
12 Hali yake hulanda pia unabii wa Yeremia: “‘Kuna upanga dhidi ya Wakaldayo,’ ni tamko la Yehova, ‘na dhidi ya wakaaji wa Babuloni na dhidi ya wana-wafalme wake na dhidi ya wenye hekima wake. . . . Kuna mteketezo juu ya maji yake, na ni lazima yakaushwe kabisa. Kwa maana ni bara la mifano ya kuchongwa, na kwa sababu ya njozi zao zenye kujaa kikuli wao huendelea kutenda kikichaa. Kwa hiyo mizuka ya mikoa isiyo na maji itakaa pamoja na wanyama wenye kulia, na ndani yake yeye lazima mbuni wakae; naye hatakaliwa tena kamwe milele, wala yeye hatakaa kizazi baada ya kizazi.’” Ibada ya sanamu na kuimbwa kwa sala za kurudiwarudiwa hakuwezi kumwokoa Babuloni Mkubwa asipatwe na lipo linaloshabihi kuangushwa kwa Sodoma na Gomora na Mungu.—Yeremia 50:35-40, NW.
Divai Yenye Kuamsha Harara
13. (a) Malaika mwenye nguvu avutaje uangalifu kwenye mweneo mpana wa ukahaba wa Babuloni Mkubwa? (b) Ni utovu wa adili gani ulioenea sana katika Babuloni wa kale unaopatikana pia katika Babuloni Mkubwa?
13 Kisha malaika mwenye nguvu anaelekeza uangalifu kwenye mweneo mpana wa ukahaba wa Babuloni Mkubwa, akipiga mbiu hivi: “Kwa sababu ya divai yenye kuamsha harara ya uasheratia wake mataifa yote yameanguka yakiwa majeruhi, na wafalme wa dunia walifanya uasherati na yeye, na wauza-bidhaa wasafiri wa dunia wakawa na utajiri kwa sababu ya nguvu za anasa yake isiyo ya aibu.” (Ufunuo 18:3, NW) Yeye amefundisha mataifa yote ya aina ya binadamu katika njia zake zisizo safi za kidini. Katika Babuloni wa kale, kulingana na mwanahistoria Herodoto, kila mwanamwali alitakwa aufanyize uasherati ubikira wake katika ibada ya hekalu. Kufikia leo hii ufisadi wa kingono wenye kukirihisha unaonyeshwa kitaswira katika sanamu-choro zilizoharibiwa na vita kwenye Angkor Wat katika Kampuchea na katika mahekalu katika Khajuraho, India, ambazo huonyesha mungu wa Kihindu Vishnu akizungukwa na mandhari za kimahaba zenye kunyarafisha. Katika United States, mafumbuo ya utovu wa adili ambayo yalitetemesha ulimwengu wa waevanjeli wa TV katika 1987, na tena katika 1988, pamoja na ufunuo wa zoea lenye kuenea pote la ugoni-jinsia-moja wa wahudumu wa kidini, hutoa kielezi kwamba hata Jumuiya ya Wakristo huvumilia mazidio yenye kugutusha ya uasherati halisi. Hata hivyo, mataifa yote yamekuwa majeruhi ya aina ya uasherati mbaya hata zaidi.
14-16. (a) Ni uhusiano gani usio halali wa dini-siasa uliotukia katika Italia ya Ufashisti? (b) Wakati Italia ilipovamia Abisinia, ni taarifa gani walizotoa maaskofu wa Kanisa Katoliki la Roma?
14 Sisi tumekwisha pitia uhusiano haramu wa dini-siasa uliomweka Hitla katika mamlaka katika Ujeremani ya Nazi. Mataifa mengine pia yalitaabika kwa sababu ya dini kujidukiza katika mambo ya kiserikali. Mathalani, Katika Italia ya Ufashisti, katika Februari 11, 1929, Mwafaka wa Laterani ulitiwa sahihi na Mussolini na Kardinali Gasparri, ukifanya Jiji la Vatikani kuwa dola lenye enzi. Papa Pius 11 alidai kwamba yeye alikuwa ‘ameirudisha Italia kwa Mungu, na Mungu akamrudisha kwa Italia.’ Je! huo ulikuwa ni ukweli? Fikiria yaliyotokea miaka sita baadaye. Katika Oktoba 3, 1935, Italia ilivamia Abisinia, ikidai kwamba lilikuwa “bara la kishenzi ambalo lilikuwa lingali linazoea utumwa.” Ni nani, kwa kweli, aliyekuwa wa kishenzi? Je! Kanisa Katoliki lililaumu vikali ushenzi wa Mussolini? Ingawa papa alitoa taarifa zisizoeleweka, maaskofu wake walisema wazi kabisa katika kubariki majeshi yenye silaha ya Italia “bara-baba” lao. Katika kitabu The Vatican in the Age of the Dictators, Anthony Rhodes huripoti hivi:
15 “Katika Barua ya Uchungaji yake ya Oktoba 19 [1935], Askofu wa Udine [Italia] aliandika, ‘Si la wakati unaofaa wala lenye kufaa kwa sisi kutamka yanayofaa na yasiyofaa ya kisa hiki. Wajibu wetu tukiwa Waitalia, na hata hivyo zaidi tukiwa Wakristo ni kuchangia fanikio la silaha zetu.’ Askofu wa Padua aliandika katika Oktoba 21, ‘katika hizi saa ngumu ambazo sisi tunazipitia, sisi tunawaomba nyinyi mwe na imani katika watawala wetu na majeshi yenye silaha.’ Oktoba 24, Askofu wa Kremona aliweka wakfu bendera kadhaa za kijeshi na akasema: ‘Baraka ya Mungu na iwe juu ya askari-jeshi hawa ambao, juu ya udongo wa Kiafrika, watashinda mabara mapya na yenye rutuba kwa ajili ya ubunifu wa Italia, na hivyo kuwaletea utamaduni wa Kiroma na Kikristo. Italia na isimame kwa mara nyingine tena ikiwa mshauri wa ulimwengu kwa ujumla.’”
16 Abisinia ikatwaliwa kinguvu, kwa baraka ya makasisi wa Katoliki ya Roma. Je! yeyote wa hawa angeweza kudai, katika maana yoyote, kwamba wao walikuwa kama mtume Paulo katika kuwa ‘bila hatia ya damu ya watu wote’?
17. Hispania ilitesekaje kwa sababu ya viongozi wa kidini wayo kushindwa ‘kufua panga zao ziwe majembe ya plau’?
17 Ongezea Ujeremani, Italia, na Abisinia taifa jingine ambalo limekuwa jeruhi kwa uasherati wa Babuloni Mkubwa—Hispania. Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe ya 1936-39 katika bara hilo, kwa sehemu, ilianzishwa kwa sababu ya serikali ya kidemokrasi kuchukua hatua ya kupunguza nguvu kubwa mno za Kanisa Katoliki la Roma. Vita hiyo ilipoanza, Franko, kiongozi Mfashisti Mkatoliki wa majeshi ya Kimapinduzi, alijieleza mwenyewe kuwa “Jenerali Mkuu wa Kikristo wa Krusedi Takatifu,” jina la cheo ambalo baadaye aliacha. Mamia ya maelfu kadhaa ya Wahispania walikufa katika kupigana. Mbali na hilo, kulingana na kadirio dogo, Wateteaji wa Taifa wa Franko walikuwa wameua kimakusudi wanachama 40,000 wa Popular Front, hali hao wa pili nao walikuwa wameua kimakusudi makasisi—watawa wa kiume, mapadri, watawa wa kike, na makasisi wapya 8,000. Hilo ndilo ogofyo na msiba wa vita ya wenyewe kwa wenyewe, ikionyesha hekima ya kutii maneno haya ya Yesu: “Rudisha upanga wako mahali pao, kwa maana wale wote ambao huchukua upanga watapotelea mbali kwa upanga.” (Mathayo 26:52, NW) Ni jambo lenye kunyarafisha kama nini kwamba Jumuiya ya Wakristo hujiingiza katika umwagaji-damu mkubwa hivyo! Kweli kweli viongozi wayo wa kidini wameshindwa kabisa kabisa ‘kufua panga zao ziwe majembe ya plau’!—Isaya 2:4, NW.
Wauza-Bidhaa Wasafiri
18. Ni nani walio “wauza-bidhaa wasafiri wa dunia”?
18 Ni nani walio “wauza-bidhaa wasafiri wa dunia”? Pasipo shaka sisi tungewaita leo wachuuzi, wanabiashara wakubwa-wakubwa, walanguzi chapuchapu na biashara kubwa-kubwa. Hii si kusema kwamba ni kosa kufanya biashara halali. Biblia huandaa shauri la hekima kwa watu wa biashara, ikiwaonya dhidi ya utovu wa haki, pupa, na kadhalika. (Mithali 11:1; Zekaria 7:9, 10; Yakobo 5:1-5) Pato lililo kubwa zaidi ni “kujitoa kwa ajili ya Mungu pamoja na ujitoshelevu.” (1 Timotheo 6:6, 17-19, NW) Hata hivyo, ulimwengu wa Shetani haufuati kanuni za uadilifu. Ufisadi ni tele. Unapatikana katika dini, katika siasa—na katika biashara kubwa-kubwa. Wakati kwa wakati vyombo vya habari hufichua kashifa, kama vile maofisa wa serikali wa vyeo vya juu kutumia vibaya mali ya serikali na kuuza silaha kimagendo.
19. Ni mambo hakika gani ya uchumi wa ulimwengu husaidia kueleza sababu kwa nini wauza-bidhaa wasafiri wa dunia hupata mtajo usiopendeleka katika Ufunuo?
19 Uchuuzi wa kimataifa wa silaha unapanda juu sana kupita dola 1,000,000,000,000 kila mwaka, huku mamia ya mamilioni ya wanadamu wakinyimwa lazima za maisha. Hilo ni baya vya kutosha. Lakini silaha huonekana kuwa tegemezo la msingi la uchumi wa ulimwengu. Katika Aprili 11, 1987, makala moja katika Spectator ya London iliripoti hivi? “Kuhesabu viwanda vinavyohusiana moja kwa moja, kazi 400,000 zinahusika katika U.S. na 750,000 katika Ulaya. Lakini ajabu ni kwamba, kadiri daraka la kijamii na kiuchumi la kuunda silaha linavyoongezeka, lile swali hasa la kama waundaji wanakingwa vizuri limesahauliwa.” Faida kubwa mno zinapatikana kadiri mabomu na silaha nyinginezo zinachuuzwa kotekote duniani, hata na kwa wanaoweza kuwa maadui. Siku moja huenda mabomu hayo yakarudi katika mteketeo wa moto kuwaharibu wale wanaoyauza. Ni kinyume kama nini! Ongezea hilo ulanguzi unaohusika katika biashara hii ya silaha. Katika United States pekee, kulingana na Spectator, “kila mwaka kwa njia isiyoelezeka Pentagoni hupoteza silaha na vifaa vya thamani ya dola milioni 900.” Si ajabu kwamba wauza-bidhaa wa dunia wanatajwa isivyopendeleka katika Ufunuo!
20. Ni kielelezo gani kinachoonyesha kujihusisha kwa dini katika mazoea yenye ufisadi ya shughuli za biashara?
20 Kama ilivyotabiriwa na malaika mwenye utukufu, dini imehusika sana katika mazoea yenye ufisadi ya biashara. Mathalani, kuna kujihusisha kwa Vatikani katika anguko la Banco Ambrosiano katika 1982. Kesi hiyo imejikokota muda wote wa miaka ya 1980, lile swali ambalo halijajibiwa likiwa: Fedha zilienda wapi? Katika Februari 1987 mahakimu wa Milani walitoa waranti ili makasisi watatu wa Vatikani wakamatwe, kutia na askofu mkuu mmoja Mwamerika, kwa mashtaka ya kwamba wao walikuwa washiriki kwenye ufilisi wenye udanganyifu, lakini Vatikani ilitupilia mbali ombi la kuwakabidhi wakahukumiwe. Katika Julai 1987, katikati ya makelele ya kuteta, zile waranti zilibatilishwa na Mahakama ya Rufani ya juu zaidi sana kwa msingi wa mwafaka wa zamani kati ya Vatikani na serikali ya Italia.
21. Sisi twajuaje kwamba Yesu hakuwa na uhusiano na mazoea ya kibiashara yenye kutilika mashaka ya siku yake, lakini sisi tunaona nini leo katika dini ya Kibabuloni?
21 Je! Yesu alijihusisha katika mazoea ya kibiashara yenye kutilika mashaka ya siku yake? La. Yeye hata hakuwa mwenye mali yoyote, kwa maana yeye alikuwa “hana mahali pa kulaza chini kichwa chake.” Mtawala mmoja kijana tajiri alishauriwa na Yesu hivi: “Uza vitu vyote ulivyo navyo na kugawia maskini, na wewe utakuwa na hazina katika mbingu; na uje uwe mfuasi wangu.” Hilo lilikuwa shauri jema, kwa maana lingaliweza kumwondolea mbali wasiwasi wote juu ya mambo ya kibiashara. (Luka 9:58; 18:22, NW) Kwa kutofautisha, dini ya Kibabuloni mara nyingi ina mafungamano mabaya na biashara kubwa-kubwa. Mathalani, katika 1987 Albany Times Union liliripoti kwamba msimamizi wa mambo ya kifedha wa akidayosisi ya Miami, Florida, U.S.A., alikubali kwamba kanisa lina hisa katika makampuni ambayo hufanyiza silaha za nyukilia, sinema zisizofaa, na sigareti.
“Ondokeni Katika Yeye, Watu Wangu”
22. (a) Sauti kutoka katika mbingu inasema nini? (b) Ni nini kilichoongoza kwenye mshangilio wa watu wa Mungu katika 537 K.W.K., na katika 1919?
22 Maneno yanayofuata ya Yohana yanaelekeza kwenye utimizo zaidi wa kigezo cha kiunabii: “Na mimi nikasikia sauti nyingine kutoka katika mbingu ikisema: ‘Ondokeni katika yeye, watu wangu, ikiwa nyinyi hamtaki kushiriki pamoja na yeye katika madhambi yake, na ikiwa nyinyi hamtaki kupokea sehemu ya tauni zake.’” (Ufunuo 18:4, NW) Unabii wa anguko la Babuloni wa kale katika Maandiko ya Kiebrania unatia ndani pia amri ya Yehova kwa watu wake: “Kimbieni mtoke katikati ya Babuloni.” (Yeremia 50:8, 13, NW) Hali moja na hiyo, kwa sababu ya ukiwa unaokuja wa Babuloni Mkubwa, watu wa Mungu wanahimizwa sasa waponyoke. Katika 537 K.W.K. fursa ya kuponyoka kutoka Babuloni ilileta mshangilio mkubwa upande wa Waisraeli waaminifu. Katika njia iyo hiyo, kuachiliwa kwa watu wa Mungu kutoka utekwa wa Babuloni Mkubwa kuliongoza kwenye mshangilio upande wao. (Ufunuo 11:11, 12) Na tangu wakati huo mamilioni ya wengine yametii amri hiyo wakimbie.
23. Sauti kutoka katika mbingu inakaziaje umuhimu wa kukimbia kutoka katika Babuloni Mkubwa?
23 Je! ni jambo la muhimu kweli kweli kadiri hiyo kukimbia kutoka katika Babuloni Mkubwa, kujiondoa katika uanachama wa dini za ulimwengu na kujitenga kabisa? Ndivyo, kwa maana sisi tunahitaji kuchukua oni la Mungu juu ya dubwana hili la kale la kidini, Babuloni Mkubwa. Yeye hakuepa kumwita kahaba mkubwa. Kwa hiyo sasa sauti kutoka katika mbingu inamwarifu Yohana zaidi hivi kuhusu malaya huyu: “Kwa maana madhambi yake yametungamana pamoja moja kwa moja hadi kwenye mbingu, na Mungu amekumbuka matendo yake yasiyo ya haki. Rudisha kwa yeye hata kama vile yeye mwenyewe alirudisha, na fanya kwa yeye mara mbili ya vile yeye alifanya, ndiyo, mara mbili ya hesabu ya alivyofanya; katika kikombe ambacho ndani yacho yeye aliweka mchanganyiko wekea yeye mara mbili ya mchanganyiko huo. Kwa kadiri ambayo yeye alijitukuza mwenyewe na akaishi katika anasa ya kutoona aibu, kwa kadiri hiyo mpe yeye teso na ombolezo. Kwa maana katika moyo wake yeye hufuliza kusema, ‘Mimi naketi nikiwa malkia, na mimi si mjane, na mimi sitaona kamwe ombolezo.’ Hiyo ndiyo sababu katika siku moja tauni zake zitakuja, kifo na ombolezo na njaa kuu, na yeye atachomwa kabisa kwa moto, kwa sababu Yehova Mungu, ambaye alihukumu yeye, ni imara sana.”—Ufunuo 18:5-8, NW.
24. (a) Ni lazima watu wa Mungu wakimbie kutoka Babuloni Mkubwa ili waepuke nini? (b) Wale wanaoshindwa kukimbia kutoka katika Babuloni Mkubwa wanashiriki naye madhambi gani?
24 Ni maneno yenye nguvu, hayo! Kwa hiyo tendo linatakwa. Yeremia alihimiza watu katika siku yake watende, akisema: “Kimbieni kutoka katikati ya Babuloni, . . . kwa maana ni wakati wa kisasi ambacho ni cha Yehova. Kuna tendeo ambalo yeye analipa kurudisha kwa yeye. Ondokeni katikati yake, O watu wangu, na kila mmoja aandalilie nafsi yake mponyoko kutoka kasirani yenye kuwaka ya Yehova.” (Yeremia 51:6, 45, NW) Katika njia kama hiyo, sauti kutoka katika mbingu inaonya watu wa Mungu leo wakimbie kutoka Babuloni Mkubwa ili wasipokee sehemu ya tauni zake. Hukumu za Yehova zilizo kama tauni juu ya ulimwengu huu, kutia na Babuloni Mkubwa, zinapigiwa mbiu sasa. (Ufunuo 8:1–9:21; 16:1-21) Watu wa Mungu wanahitaji kujitenga wenyewe na dini bandia ikiwa wao wenyewe hawataki kupatwa na tauni hizi na mwishowe kabisa wafe naye. Waaidha, kubaki ndani ya tengenezo hilo kungewafanya washiriki katika madhambi yake. Wao wangekuwa na hatia kama yeye ya uzinzi wa kiroho na ya kumwaga damu “ya wale wote ambao wamechinjwa juu ya dunia.”—Ufunuo 18:24, NW; linga Waefeso 5:11; 1 Timotheo 5:22.
25. Ni katika njia zipi watu wa Mungu waliondoka katika Babuloni wa kale?
25 Ingawa hivyo, ni jinsi gani watu wa Mungu huondoka katika Babuloni Mkubwa? Katika kisa cha Babuloni wa kale, Wayahudi walikuwa sharti wafanye safari halisi kutoka katika jiji la Babuloni moja kwa moja hadi Bara la Ahadi. Lakini zaidi ya hilo lilihusika. Kiunabii Isaya aliambia Waisraeli hivi: “Geukeni mbali, geukeni mbali, ondokeni humo, msiguse kitu kisicho safi; ondokeni katikati yake, jitunzeni wenyewe safi, nyinyi ambao mnapeleka vyombo vya Yehova.” (Isaya 52:11, NW) Ndiyo, wao walipaswa waache mazoea yote yasiyo safi ya dini ya Kibabuloni ambayo yangeelekea kuitia kutu ibada yao kwa Yehova.
26. Wakristo Wakorintho walitiije maneno haya, ‘Ondokeni kutoka miongoni mwao na mwache kabisa kugusa kitu kisicho safi’?
26 Mtume Paulo alinukuu maneno ya Isaya katika barua yake kwa Wakorintho, akisema: “Msipate kuwa wenye kufungiwa nira isivyofaa pamoja na wasioitikadi. Kwa maana ni ushirika gani uadilifu unao pamoja na ukosefu wa kutii sheria? Au ni hisa gani nuru inayo pamoja na giza? . . . ‘Kwa hiyo ondokeni kutoka miongoni mwao, na kujitenga nyinyi wenyewe,’ asema Yehova, ‘Na acheni kabisa kugusa kitu kisicho safi.’” Haikuwa lazima Wakristo wa Korintho waache Korintho ili watii amri hiyo. Hata hivyo, wao walikuwa na lazima ya kuepuka kihalisi mahekalu yasiyo safi ya dini bandia, pamoja na kujitenga wenyewe kiroho na matendo yasiyo safi ya waabudu sanamu hao. Katika 1919 watu wa Mungu walianza kukimbia kutoka katika Babuloni Mkubwa kwa njia hiyo, wakijisafisha wenyewe mabaki yoyote ya mafundisho na mazoea yasiyo safi. Hivyo, waliweza kutumikia yeye wakiwa watu wake waliosafishwa.—2 Wakorintho 6:14-17, NW; 1 Yohana 3:3.
27. Ni milingano gani iliyopo kati ya hukumu juu ya Babuloni wa kale na juu ya Babuloni Mkubwa?
27 Anguko la Babuloni wa kale na ukiwa uliofuata lilikuwa adhabu kwa ajili ya madhambi yake. “Kwa maana moja kwa moja hukumu zake zimefika katika zile mbingu.” (Yeremia 51:9, NW) Hali moja na hiyo, madhambi ya Babuloni Mkubwa “yametungamana pamoja moja kwa moja hadi kwenye mbingu,” ili ziangaliwe na Yehova mwenyewe. Yeye ana hatia ya utovu wa haki, ibada ya sanamu, utovu wa adili, uonevu, unyakuzi, na uuaji kimakusudi. Anguko la Babuloni wa kale lilikuwa kwa sehemu, kisasi kwa yale ambayo lilikuwa limefanyia hekalu la Yehova na waabudu wa kweli wake. (Yeremia 50:8, 14; 51:11, 35, 36) Anguko la Babuloni Mkubwa na uharibifu wake utakaofuata hali moja na hiyo huonyesha kisasi kwa yale ambayo yeye amefanyia waabudu wa kweli katika muda wote wa karne zilizopita. Kweli kweli, uharibifu wake wa mwisho kabisa ni mwanzo wa “siku ya kisasi upande wa Mungu wetu.”—Isaya 34:8-10; 61:2, NW; Yeremia 50:28.
28. Ni kiwango gani cha haki anachotumia Yehova kwa Babuloni Mkubwa, na kwa sababu gani?
28 Chini ya Sheria ya Musa, ikiwa Mwisraeli aliiba kutoka wananchi wenzake, alikuwa sharti alipe ili kurudisha angalau maradufu katika kufidia. (Kutoka 22:1, 4, 7, 9) Katika uharibifu unaokuja wa Babuloni Mkubwa, Yehova atatumia kiwango kinacholinganika na hicho cha haki. Yeye atapokea maradufu ya yale aliyotoa. Hakutakuwa na rehema kwa sababu Babuloni Mkubwa hakuonyesha rehema yoyote kwa majeruhi wake. Yeye alijilisha kidusia juu ya watu wa dunia ili kujidumisha mwenyewe katika “anasa ya kutoona aibu.” Sasa yeye atateseka na kuomboleza. Babuloni wa kale alihisi alikuwa katika hali ya usalama kabisa, akijigamba: “Mimi sitaketi kama mjane, na mimi sitajua hasara ya watoto.” (Isaya 47:8, 9, 11, NW) Babuloni Mkubwa huhisi yu salama. Lakini uharibifu wake, ulioamriwa na Yehova ambaye “ni imara sana,” utatukia chakachaka, kana kwamba “katika siku moja”!
[Maelezo ya Chini]
a New World Translation Reference Bible, kielezi cha chini.
[Sanduku katika ukurasa wa 263]
“Wafalme . . . Walifanya Uasherati na Yeye”
Mapema katika miaka ya 1800 wauza-bidhaa wa Ulaya walikuwa wakiingiza kimagendo ndani ya China viasi vikubwa vya kasumba. Katika Machi 1839 maofisa Wachina walijaribu kukomesha uchuuzi huo usio halali kwa kukamata masanduku 20,000 ya dawa hiyo ya kulevya kutoka kwa wauza-bidhaa Waingereza. Hili liliongoza kwenye wasiwasi kati ya Uingereza na China. Mahusiano kati ya nchi hizo mbili yalipozorota, baadhi ya wamisionari Waprotestanti walihimiza Uingereza kwenda vitani, kwa taarifa kama hizi zifuatazo:
“Jinsi magumu haya yanavyoshangilisha moyo wangu kwa sababu mimi nafikiri huenda serikali ya Uingereza ikakasirishwa vikali, na Mungu, katika nguvu Zake huenda akavunjavunja migogoro inayozuia gospeli ya Kristo isiingie China.”—Henrietta Shuck, misionari wa Baptisti ya Kusini.
Hatimaye, vita ikafyatuka—vita ambayo leo hujulikana kuwa Vita ya Kasumba. Kwa moyo wote wamisionari walichochea Uingereza kwa maelezo kama haya:
“Mimi nalazimika kutazama nyuma juu ya hali ya sasa ya mambo sana sana si kuwa ni shauri la kasumba au la Uingereza, kuwa ndilo kusudi kubwa la Mwelekezo wa Kimungu ili kufanya uovu wa mwanadamu utii makusudi Yake ya rehema kuelekea China katika kupenya ukuta wayo wa kujitenga.”—Peter Parker, misionari Mkongrigeshonali.
Misionari mwingine Mkongrigeshonali, Samuel W. Williams, aliongeza hivi: “Mkono wa Mungu ni wazi katika yale yote ambayo yamefanyika kwa jinsi ya kutokeza, na sisi hatutii shaka kwamba Yeye ambaye alisema alikuja kuleta upanga juu ya dunia amekuja hapa na kwamba ni kwa ajili ya uharibifu mwepesi wa maadui Wake na kusimamishwa kwa ufalme Wake. Yeye atapindua na kupindua mpaka Yeye awe amemthibitisha Mwana-Mfalme wa Amani.”
Kwa mintarafu ya chinjo lenye kuogofya la wanataifa Wachina, misionari J. Lewis Shuck aliandika: “Mimi huona mandhari kama hizo . . . kuwa ala za Bwana za moja kwa moja katika kuondolea mbali takataka ambayo inazuia usongaji mbele wa Ukweli wa Kimungu.”
Misionari Mkongrigeshonali Elijah C. Bridgman aliongeza: “Mara nyingi Mungu ametumia mkono imara wa mamlaka ya kiserikali ili kutayarisha njia kwa ajili ya ufalme Wake . . . Chombo katika nyakati hizi zenye maana ni cha kibinadamu; nguvu yenye kuelekeza ni ya kimungu. Gavana mkuu wa mataifa yote ametumia Uingereza kuadhibu na kunyenyekeza China.”—Manukuu yamechukuliwa kutoka “Ends and Means,” 1974, insha ya Stuart Creighton Miller iliyotangazwa katika The Missionary Enterprise in China and America (Durusi la Harvard lililohaririwa na John K. Fairbank).
[Picha katika ukurasa wa 264]
“Wauza-Bidhaa Wasafiri . . . Wakawa na Utajiri”
“Kati ya 1929 na mfyatuko wa Vita ya Ulimwengu 2, [Bernadino] Nogara [msimamizi wa mambo ya kifedha wa Vatikani] aligawia Vatikani jiji kuu na mawakili wa Vatikani kufanya kazi katika maeneo ya namna namna ya uchumi wa Italia—hasa katika nguvu za umeme, mawasiliano ya simu, karidhi na kazi za benki, njia za reli ndogondogo, na ufanyizaji wa zana za kilimo, saruji, na nyuzi za nguo za kubuniwa. Nyingi za shughuli hizi zilifanikiwa.
“Nogara alinyakua kampuni kadhaa kutia na La Società Italiana della Viscosa, La Supertessile, La Società Meridionale Industrie Tessili, na La Cisaraion. Akiunganisha hizi kuwa kampuni moja, ambayo aliita CISA-Viscosa na akaiweka chini ya usimamizi wa Baron Francesco Maria Oddasso, mmojapo makabwela wa Vatikani wenye kuitibariwa zaidi sana, kisha Nogara akaongoza mambo kwa werevu ili kampuni hiyo mpya itwaliwe na [kampuni] ya Italia iliyo kubwa zaidi sana ya kufanyiza nguo, SNIA-Viscosa. Hatimaye faida za Vatikani katika SNIA-Viscosa zikakua zikawa kubwa zaidi na zaidi, na baada ya wakati Vatikani ikachukua udhibiti—kama inavyoshuhudiwa na uhakika wa kwamba baadaye Baron Oddasso akawa makamu wa msimamizi.
“Ndivyo Nogara akapenya ndani ya kiwanda cha nguo. Yeye alipenya ndani ya viwanda vingine katika njia nyingine nyingine, kwa maana Nogara alikuwa mwenye vitimbi vingi. Mtu huyu asiye na ubinafsi . . . pengine alifanya mengi zaidi kutia uhai katika uchumi wa Italia kuliko mwanabiashara mwingine yeyote mmoja katika historia ya Italia . . . Benito Mussolini hakuweza kamwe kupata kabisa milki ambayo yeye aliotea ndoto, lakini yeye aliwezesha Vatikani na Bernadino Nogara kubuni utawala wa aina nyingine.”—The Vatican Empire, cha Nino Lo Bello, kurasa 71-3.
Hiki ni kielelezo kimoja tu cha ushirikiano wa karibu karibu kati ya wauza-bidhaa wa dunia na Babuloni Mkubwa. Si ajabu kwamba wauza-bidhaa hawa wataomboleza wakati mshirika wao wa kibiashara atakapokuwa hayupo tena!
[Picha katika ukurasa wa 259]
Wanadamu walipoenea katika dunia yote, walichukua dini ya Kibabuloni pamoja nao
[Picha katika ukurasa wa 261]
Jamii ya Yohana, kama mlinzi, hupiga mbiu kwamba Babuloni ameanguka
[Picha katika ukurasa wa 266]
Magofu ya Babuloni wa kale yanaonya kimbele juu ya angamio linalokuja la Babuloni Mkubwa