“Tokeni Kwake, Enyi Watu Wangu”
“Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake wala msipokee mapigo yake.”—Ufu. 18:4.
1. Mwito wa kutoka katika Babeli Mkuu ulitolewa lini, na ni kwa sababu gani jambo hilo lilifaa wakati huo?
“TOKENI kwake, enyi watu wangu.” Mwito huo umekuwa ukitangazwa tangu mwaka wa 1919, mwaka ambao katika huo mataifa yaliyokuwa yakipigana katika vita ya ulimwengu ya 1914-1918 yalipotia sahihi kwenye mapatano ya amani. Matengenezo ya dini za ulimwengu yalikuwa yameunga mkono vita hiyo ya ulimwengu. Namna gani juu ya wale ambao Mungu wa Biblia anawaita “watu wangu”? Wakristo hawa wenye amani walikuwa wametiwa chini ya utumwa, hata wakatiwa kifungoni, katika Babeli Mkuu na wapenzi wake wa kisiasa waliokuwa wakipigana katika Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.
2. Ni mwito gani kama huo uliokuwa umetolewa mapema kupitia kwa Yeremia?
2 Mwito wa ‘kutoka kwake’ ulikuwa umeandikwa katika Ufunuo 18:4. Kulikuwako mwito kama uo huo uliokuwa umeandikwa mapema katika Yeremia 51:45: “Enyi watu wangu; tokeni katikati yake, mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya [Yehova].”
3, 4. (b) Kulingana na Yeremia 50:8-10, ’wangeokolewa’ kutoka wapi? (b) Kufikia wakati wa kutimizwa kwa unabii huo wa baadaye, je! Babeli ilikuwa na uhusiano kama ule iliyokuwa nao pamoja na Yehova katika siku za Nebukadreza? Kwa sababu gani?
3 ‘Wajiokoe’ kutoka wapi? Yeremia 50:8-10 hujibu waziwazi hivi: “Kimbieni kutoka kati ya Babeli, mkatoke katika nchi ya Wakaldayo, mkawe kama mabeberu mbele ya makundi. Kwa maana juu ya Babeli nitaamsha na kuleta kusanyiko la mataifa makubwa, toka nchi ya kaskazini; nao watajipanga juu yake; kutoka huko atatwaliwa. . . . Nao Ukaldayo utakuwa mateka; wote wautekao watashiba, asema [Yehova].”
4 Wakati wa kutimizwa kwa maneno hayo ya kiunabii, Mfalme Nebukadreza wa Babeli angekuwa amekufa. Mmoja wa warithi wake wa kifalme, yaani, Belshaza, mwana wa Nabonida, ndiye angekuwa akitawala katika Milki ya Babeli, katika mwaka 539 K.W.K. Kwa hiyo kufikia wakati huo, kilichofananishwa kiunabii na Babeli tangu mwanzo wa utawala wa Nebukadreza katika mwaka 625 K.W.K. kilikuwa kimebadilika. Yehova alikuwa amemwita Nebukadreza “mtumishi wangu.” (Yer. 27:6) Vilevile wakati wa kuhamishwa kwa Myahudi nabii Danieli katika Babeli, Yehova alishughulika na Mfalme Nebukadreza kuhusiana na ndoto mbili za kiunabii zenye maana. (Dan., sura 2 na 4) Hata kufikia mwaka 592 K.W.K., matendo hodari ya Mfalme Nebukadreza yalitabiriwa katika unabii. (Eze. 29:17-20) Kwa hiyo, angaa wakati wa miaka hiyo Milki ya Babeli chini ya Nebukadreza ilitumiwa kama chombo cha Yehova katika kulipa kisasi juu ya ufalme wa Yuda usiokuwa mshikamanifu pamoja na mataifa jirani. Kazi ya Nebukadreza kulingana na mapenzi ya Yehova ilifananisha kazi ya Yesu Kristo katika huu “wakati wa mwisho,” tulipo sasa.
5. Kulingana na Isaya 44:28 mpaka 45:7, kufikia wakati wa kuanguka kwa Babeli, kazi ya Yesu Kristo ilifananishwa na kazi ya nani, nayo maelezo ya Danieli kuhusu mwandiko wa mkono uliokuwa juu ya ukuta yalipatanaje na vile Isaya alivyokuwa ametabiri?
5 Kulingana na Isaya 44:28 mpaka 45:7, wakati kuanguka kwa Babeli kulipokuwa kukikaribia, kazi iliyofananisha ile ambayo Yesu Kristo aliyetukuzwa angefanya katika “wakati wa mwisho” ilichukuliwa na Koreshi Mkuu, mtawala wa Milki ya mwungano ya Wamedi na Waajemi. Usiku ule ule Babeli ulipoanguka katika mwaka 539 K.W.K., nabii Danieli alifasiri mwandiko wa mkono uliokuwa ukutani aliokuwa ameuona Mfalme Belshaza: “PERESI [hesabu ya umoja ya neno la tatu la mwandiko wa mkono wa maneno yenye fumbo], ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.” Danieli aliyejionea kwa macho yake mwenyewe anaendelea na masimulizi yake hivi: “Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo akauawa. Na Dario, Mmedi, [akiwa mshiriki wa Koreshi] akaupokea ufalme.”—Dan. 5:28-31; 9:1, 2.
6. (a) Kilichofananishwa na Babeli katika siku za Belshaza kimeonyeshwa katika kitabu kipi cha Biblia, nacho ni kitu gani leo? (b) Ni nani aliyeuanzisha Babeli huo wa mfano, nao huo unatia ndani dini gani?
6 Kilichofananishwa na Babeli katika siku zake za mwisho ikiwa bibi mkubwa wa ulimwengu kinaonyeshwa katika kitabu cha Ufunuo kama vile kilivyoandikwa na mtume Yohana aliyeongozwa na Mungu kama mwaka wa 96 W.K. hivi, wakati ambapo masalio ya Babeli yalipokuwa yangali yakisimama. Kutokana na yale ambayo mtume Yohana aliandika katika Ufunuo 16:12 mpaka 19:3, inaonekana wazi kwamba Babeli ya siku za Belshaza iliyokuwa imehukumiwa maangamizi ilifananisha milki ya ulimwengu ya dini ya uongo iliyopo mpaka sasa. Milki hiyo, ambayo sasa yatia ndani dini zote za ulimwengu uliohukumiwa maangamizi, ilianzishwa na “mwindaji mwenye nguvu katika kupingana na Yehova.” Alikuwa Nimrodi, kitukuu wa Nuhu, naye aliuanzisha mji wa Babeli katika Mto Frati. (Ufu. 16:12; Mwa. 10:8-10, NW) Milki ambayo sasa inaitwa Babeli Mkuu inatia ndani dini zote ‘zinazompinga Yehova’ nayo sasa iko katika “wakati wa mwisho” wake.—Dan. 12:4.
7. (a) ‘Waokokaji’ hao walitoka wakati gani katika Babeli ya kale? (b) Waokokaji wanatoka katika Babeli Mkuu wakati gani, na kwa sababu gani wakati huo?
7 Watu wa Yehova wanaitwa ‘watoke’ kwenye hiyo milki ya kidini, na wafanye hivyo pasipo kuchelewa. Milki hiyo ndiyo iliyofananishwa na Babeli ambayo Yeremia alisema juu yake katika sura ya 50 na 51. Kwa habari ya Milki ya Kibabeli ya kale, Wayahudi waliokuwa uhamishoni pamoja na wenzao hawangeweza ‘kutoka kwake’ mpaka baada ya kuangushwa na Wamedi na Waajemi katika mwaka 539 K.W.K. (Isa. 14:12-17) Walakini, namna gani juu ya karne hii ya 20? Namna gani juu ya wale ambao Yehova awaita “watu wangu”? Hawa wanaamriwa ‘watoke’ katika Babeli Mkuu wa kisasa kabla hajaharibiwa katika “dhiki kubwa” inayokuja aliyoitabiri Yesu Kristo. (Mt. 24:21, 22; Ufu. 1:1; 7:14, 15) Sababu ya jambo hilo ni kwamba waokokaji hao wanahitaji kuepuka kupatwa na mapigo na uharibifu wa Babeli Mkuu, milki ya ulimwengu ya dini ya uongo ambayo ingali inasimama.—Ufu. 18:4.
8. Kutoka kwake kwa wale wanaoitwa watoke kwa Babeli Mkuu tangu mwaka 1919 kunaonyesha nini, naye ni nani aliyetumiwa kuhusiana na jambo hilo?
8 Hakutakuwako kutoka katika Babeli Mkuu baada ya wapenzi wake wa zamani wa kisiasa kumgeukia na kumwangamiza kabisa asiwepo kamwe. (Ufu. 17:15-18) Watu wa Yehova walio wakf wametoka kwake tangu mwaka 1919 W.K. uliofuata baada ya vita. Hilo laonyesha kwamba kwa maana fulani Babeli Mkuu ameanguka. Jinsi gani hivyo? Katika njia ya mfano. Katika mwaka 1919 uwezo wake wenye kutumikisha watu wa Yehova uliondolewa. Tangu wakati huo hawajapata tena kurudi katika utumwa wa kidini wa Babeli Mkuu, kama walivyokuwa wakati wa vita ya ulimwengu ya 1914-1918. Wa kupewa sifa kwa ajili ya kukombolewa kwao ni Yule aliyemwongoza Yeremia atabiri jambo hilo kuwa sehemu ya kusudi Lake. Yeye ni Yehova. Kusudi atimize hilo alimtumia Koreshi Mkuu wake, Bwana Yesu Kristo aliyetukuzwa. Koreshi huyu aliyefananishwa alianza kutawala katika ufalme wake wa kimbinguni katika mwaka 1914, baada ya kumalizika zile “nyakati saba” kama vile zilivyotabiriwa katika ndoto ya Nebukadreza. (Dan. 4:1-37) Tangu mwaka 1919 Koreshi Mkuu anayetawala amewakomboa kutoka katika Babeli Mkuu mamilioni ya watu wanaotafuta uhuru wa kidini. Wakiendelea kuwa waaminifu kwa ufalme wake, wataendelea kulindwa naye. Wala viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wala wakuu wa dini zisizo za Kikristo hawawatawali.
KURUDI KWENYE MJI MKUU ULIO JUU YA MLIMA KWATABIRIWA
9, 10. Je! kukombolewa kwa mabaki kutoka katika Babeli Mkuu kulikuwa jambo lililotokea pasipo kukusudiwa, nalo andiko la Yeremia 50:4, 5, 28 huonyesha kusudi lake lilikuwa kusudi gani?
9 Sasa baada ya kupita miaka 60 mtu ye yote asidhani kwamba kukombolewa kwa kikundi kidogo cha kidini kinachodharauliwa cha mabaki ya watu wa Yehova lilikuwa jambo lisilokusudiwa. Lilitukia ili kutimiza unabii wake mwenyewe wa Biblia. Katika unabii wake uliotolewa kupitia kwa Yeremia katika mwaka 614 K.W.K. ili kutabiri juu ya kuanguka kwa Babeli katika mwaka 539 K.W.K., twasoma hivi:
10 “Katika siku hizo, na wakati huo, asema [Yehova], wana wa Israeli watakuja, wao na wana wa Yuda pamoja; wataendelea njiani mwao wakilia, nao watamtafuta [Yehova], Mungu wao. Watauliza [njia ya] Sayuni [ulipokuwa mji mkuu juu ya mlima], na nyuso zao zitaelekea huko, wakisema, Njoni ninyi, mjiunge na [Yehova], kwa agano la milele ambalo halitasahauliwa. [Kwa kusudi gani? Kuna] sauti yao wakimbiao na kuokoka, kutoka katika nchi ya Babeli, ili kutangaza Sayuni kisasi cha [Yehova], Mungu wetu, kisasi cha hekalu lake.”—Yer. 50:4, 5, 28.
11. Je! unabii wa Yeremia unahusu Chama cha Kiyahudi cha Sayuni, nayo mambo ya hakika ya leo yanaonyesha nini kuhusu jambo hilo?
11 Hii haihusu kile Chama cha Sayuni kilichoanzishwa na Theodor Herzl Myahudi wa Austria katika mwaka 1897. Yerusalemu unaokaliwa na Wayahudi sasa waliupata kwa kutumia nguvu za silaha za vita katika ile Vita ya Siku Sita ya mwaka 1967, nao mlima wa hekalu unakaliwa na msikiti wa Waislamu uitwao “Kuba la Mwamba” ambao hauvuti fikira kwenye jina la Yehova. Mabaki wameurudia “Sayuni” upi katika amani tangu 1919?
12, Mabaki wamerudi kwa amani kwenye Sayuni upi tangu mwaka 1919?
12 Ni ule Mlima Sayuni ambao mtume Mkristo Yohana aliona katika njozi miaka 26 baada ya kuharibiwa kabisa kwa Yerusalemu wa Kiyahudi na majeshi ya Kirumi katika mwaka 70 W.K. Juu ya hilo, aliandika hivi: “Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao. . . . Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao; na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi [cha Mungu], na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne elfu, walionunuliwa katika nchi. . . . Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.”—Ufu. 14:1-4.
13. (a) Mistari michache baadaye, mtume Yohana anaripoti nini kuhusiana na Babeli Mkuu? (b) Yeye alipata kushtuka sana kwa sababu gani katika mwaka 1919?
13 Jambo lenye kupendeza ni kwamba, mistari michache tu baada ya kutupatia maelezo hayo, mtume Yohana anaandika hivi: “Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.” (Ufu. 14:8) Ujapofanya uasherati wa kidini pamoja na wanasiasa wa mataifa yote, Babeli Mkuu ulianguka katika njia yenye kushtua sana katika mwaka 1919, kwa habari ya kuwa tena na mamlaka na uvutano. Ulishtuka sana wakati Koreshi Mkuu, Mwana-Kondoo Yesu Kristo, alipowakomboa mabaki ya Waisraeli wa kiroho na kuwaweka waanze kufanya kazi ya kujenga upya kiroho.
14. (a) Je! mabaki waliokombolewa walitenda kulingana na usemi “dini ndiyo kasumba ya watu” au kile Ushirika wa Mataifa ulichodaiwa kuwa? (b) Walijielekeza kwenye mji mkuu upi uliokuwa juu ya mlima?
14 Watu wenye kutaka mapinduzi ambao kufikia mwaka 1919 walikuwa wamepata mamlaka ya kisiasa katika Europa (Ulaya) ya mashariki walitenda kulingana na usemi wao “Dini ndiyo kasumba ya watu.” Walakini yao si ndiyo iliyokuwa njia ya kuendewa na mabaki ya Waisraeli wa kiroho wa Yehova ambao sasa walikuwa wamekombolewa kutoka Babeli Mkuu wa kidini. Vilevile, Ushirika wa Mataifa ulikuwa umekusudiwa ufikiriwe na kukubaliwa katika Baraza ya Amani ya mwaka 1919, nacho Chama cha Mwungano cha Makanisa ya Kristo katika Amerika kiliukubali na kuuita “wonyesho wa kisiasa wa ufalme wa Mungu duniani.” Je! mabaki ya watu wa Yehova waliiona hiyo kuwa ndiyo njia yao? Hapana! Wakati walipofanya kusanyiko lao la watu wote huko Cedar Point, Ohio, U.S.A., Septemba 1-8, 1919, waliuonyesha waziwazi kuwa ufalme wa Mungu wa uongo wakatangaza waziwazi kwamba ungeshindwa. Walikataa cho chote kilichofanywa na wanadamu kuwa badala ya ufalme wa Mungu, wakajielekeza kwenye Mlima Sayuni wa kimbinguni, kwa kuwa huko walimwona kwa njia ya imani Mwana-Kondoo wa Mungu, Yesu Kristo, akiwa amesimama akiwa Mfalme anayetawala.—Ufu. 14:1-3; Ebr. 12:22.
15. Kwa sababu gani mabaki waliutafuta Sayuni wa kiroho wakilia, nao walijifunza Biblia upya wakiwa na maoni gani?
15 Kwa hiyo wakiwa na machozi ya ‘kilio’ chao cha furaha, mabaki waliokombolewa waligeuka wakamwacha Babeli Mkuu na kutafuta Mlima Sayuni wa kiroho, mahali ambapo Mfalme wao wa kimbinguni alikuwa amekuwa amesimama akitawala tangu zimalizike Nyakati za Mataifa katika mwaka 1914. Kupatana na kusudi lao la kitheokrasi, walijifunza Biblia upya, wakiwa na maoni mapya, kwa kuwa sasa waliweza kuona utimizo wa unabii wa Biblia wenye kuongezeka uliohusu ufalme wa Mungu kupitia kwa Kristo.
16. Kisasi walichokitangaza mabaki chawezaje kuwa kisasi “cha hekalu lake,” nazo ni ‘kazi gani za haki’ ambazo wangeweza kuzitangaza katika njia ya kutazamia?
16 Pasipo woga mabaki waliorudishwa walianza kutangaza “kisasi cha [Yehova], Mungu wetu, kisasi cha hekalu lake.” (Yer. 50:28) Wao wenyewe walikuwa sehemu ya hekalu la kiroho lake, hekalu la mfano ambalo washiriki wake ni Yesu Kristo aliye Jiwe Kuu la Pembeni pamoja na wale 144,000 washiriki wa jamii ya hekalu wakiwa chini yake. (1 Kor. 3:16, 17; Efe. 2:19-22) Katika wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza hao mabaki ya washiriki wa jamii ya hekalu walitendwa vibaya sana, nalo jaribio hilo baya sana la kuwaangamiza lilimpa Yehova sababu halali ya kuonyesha katika wakati wake kisasi chake juu ya Babeli Mkuu pamoja na wapenzi wake. Ndipo atakapotimiza kabisa unabii mrefu wa Yeremia. Wakiwa na imani yenye nguvu kwamba sehemu nyinginezo za unabii wa Yeremia zitatimizwa pasipo shaka lo lote, kwamba ni kama kwamba zimekwisha kutimizwa, mabaki waliorudishwa wanayachukua maneno ya Yeremia 51:10 na kusema hivi: “[Yehova] ameitokeza haki yetu; njoni, tutangaze katika Sayuni habari za kazi ya [Yehova], Mungu wetu.”
17. Yehova ameweka tayari chombo chake mwenyewe cha wakati unaofaa kwa ajili ya kazi gani ya kulipa kisasi?
17 Akiwa Mlipa Kisasi, Yehova ana chombo chake mwenyewe cha kutumia mkononi mwake naye atangaza kusudi lake la kuitumia katika maneno haya ya Yeremia 51:24: “Nami nitamlipa Babeli na wote wakaao ndani ya Ukaldayo, mabaya yao yote, waliyoyatenda katika Sayuni mbele ya macho yenu, asema [Yehova].”
18. Kwa sababu ya mashutumu yote ambayo yameletwa juu ya jina la Mungu, mabaki wangeweza kuonyesha tamaa inayofaa kuhusu jeuri na umwagaji wa damu wa Babeli Mkuu kulingana na maoni ya nani?
18 Ebu na tukumbuke mashutumu yote ambayo taratibu ya dini ya ulimwengu ya Kibabeli imeliletea jina la Mungu mmoja wa kweli aliye hai, sana sana kwa kuwatesa watu wake walio wakf wanaoheshimu na kulichukua jina lake. Ndipo tuwezapo kuthamini sana sababu kwa nini kwa haki kusudi la Yehova mwenyewe ni kufutilia mbali kabisa chombo hicho cha kidunia ambacho sana sana ndicho kimetumiwa na adui mkubwa Wake, Shetani Ibilisi. Kwa hiyo wale waliopo duniani wanaowakilisha Sayuni wa kimbinguni wanachukua tu maoni ya Yehova mwenyewe kuhusu jambo hilo na kukubaliana na kusudi lake lililotangazwa wanaposema hivi: “Udhalimu niliotendwa mimi, na uliotendwa mwili wangu, umpate Babeli; ndivyo atakavyosema yeye [akaaye] Sayuni; na Yerusalemu atasema, Damu yangu na iwe juu ya wakaao katika Ukaldayo.”—Yer. 51:35.
19. Ukatili katika maombi hayo kama vile unavyoweza kupingwa na ye yote unalinganaje na yale anayosema Yehova, akijisemea mwenyewe katika Yeremia 51:36, 37?
19 Mpingaji ye yote anayeyaona maombi hayo ya Sayuni na Yerusalemu kuwa ya ukatili na asidhani kwamba Yehova Mungu angekuwa mdhalimu kwa kuyajibu maombi hayo na kumchukulia hatua Babeli Mkuu wa leo. Yeye hasahau uhakika wa kihistoria wa kwamba Babeli Mkuu ametumia jeuri juu ya waabudu wa Yehova, hata akamwaga damu yao isiyo na hatia. Acha ajisemee mwenyewe katika maneno haya ya Yeremia 51:36, 37: “Basi, [Yehova] asema hivi, Tazama, nitakutetea, nami nitatwaa kisasi kwa ajili yako; nami nitaikausha bahari [ya biashara] yake, nitafanya chemchemi yake kuwa pakavu. Na Babeli utakuwa magofu.”
20. Hali ya mambo katika mahali ulipokuwa Babeli wa kale inashuhudia nini kuhusiana na matendo ya Yehova?
20 Unabii kama huo, kama vile ulivyotolewa katika mwaka 614 K.W.K., au miaka 75 kabla ya kutekwa kwa Babeli, ulionekana katika wakati huo kuwa usiowezekana kutimizwa. Katika mwaka 614 K.W.K. Babeli ilikuwa ikiinuka kufikia kilele chake cha juu sana katika mamlaka na utukufu. Walakini leo, mahali Babeli wa kale uliposimama kwa kiburi kwenye Mto Frati panashuhudia uhakika wa kwamba Yehova hakukosea katika unabii wake. Kuna mawe machache tu yanayosalia mahali hapo kati ya mawe ya kwanza ya Babeli. Uhakikisho wa Yehova kwa watu wake waliotendwa vibaya ulithibitika kuwa wa kweli. Yeye ‘aliwatetea’ katika mahakma ya ulimwengu wote; alitwaa kisasi kwa ajili yao. Kwa haki alihakikisha kwamba haki ya hukumu ilifanywa.
21, 22. Kulingana na Zaburi 137:8, 9, Koreshi Mkuu atakuwa na furaha gani?
21 Katika wakati ujao ulio karibu utumishi halali wa Koreshi aliyefananishwa, Yesu Kristo aliyetukuzwa, utakuwa wa furaha ahakikishapo kwamba haki ya hukumu imefanywa na Babeli Mkuu wa leo ametoa hesabu yake. Waabudu wa Yehova walioteseka mikononi mwake wanachukua maoni ya kimungu ya haki ya hukumu na kwa hivyo wanaweza kuungana na mtunga zaburi katika kusema hivi:
22 “Ee binti Babeli, uliye karibu na kuangamia, heri atakayekupatiliza, ulivyotupatiliza sisi. Heri yeye atakayewakamata wadogo wako, na kuwaseta wao juu ya mwamba.”—Zab. 137:8, 9.
23. Je! vyombo vya kidunia vitatumiwa kumwangamiza Babeli Mkuu, na hata hivyo ni nani atakayechukua daraka la kuangamizwa huko?
23 Katika wakati wake vyombo vya kibinadamu vya kidunia vitaruhusiwa vimwangamize Babeli Mkuu. (Ufu. 17:15-18) Walakini Yesu Kristo atakuwa na furaha ya kuchukua daraka la kufutiliwa mbali kwa hiyo milki ya ulimwengu ya dini ya uongo. Unabii wa Biblia unampa yeye sifa akiwa Koreshi Mkuu Zaidi kwa kuangushwa anakostahili Babeli Mkuu. Yeye, alipokuwa duniani kama mwanadamu, na vilevile wafuasi wake wametaabika katika mikono ya Babeli Mkuu yenye jeuri.—Ufu. 18:24.
24. (a) Babeli Mkuu amejionyeshaje kuwa mwenye kiburi kuhusiana na utawala? (b) Yeye ni “binti” ya nani, nayo ni mambo gani yenye msiba yatakayompata karibuni sana, na kwa namna gani?
24 Babeli Mkuu amekuwa mwenye kiburi sana. (Yer. 50:31, 32) Sasa anayemwona kuwa mpinzani wake si ule Yerusalemu au Sayuni wa kidunia unaposimama msikiti wa Kiislamu unaoitwa “Kuba la Mwamba,” bali ni Mlima Sayuni wa kimbinguni, kwa kuwa huko ndiko Koreshi Mkuu Zaidi anakotawala kama Mfalme. Ili auonyeshe upinzani huo, yeye anasema hivi: “Nimeketi malkia.” (Ufu. 18:7) Ikiwa yeye ataitwa “binti” kama vile ulivyoitwa Babeli wa kale, yeye kwa kweli ni binti wa Shetani Ibilisi. (Yohana 8:44; Yer. 50:42; 51:33) Imetabiriwa kwamba huyu kahaba wa kidini atapatwa na mambo mawili kwa haraka sana: “Kufiwa na watoto, na ujane.” (Isa. 47:9; Ufu. 18:7, 8; Yer. 50:9) Ama washiriki wa tengenezo lake la kidini watauawa katika ile “dhiki kubwa” inayokuja ama watakuwa wafu kwake kwa kumkataa, wakikiri kuwa wao si wanadini hata kidogo. Hilo litamfanya aomboleze weee!
25. Ikiwa ye yote wetu hataki kuhesabiwa kati ya hao “watoto” wa Kibabeli ambao watasetwa “juu ya mwamba,” lazima tufanyeje bila kukawia?
25 Je! ye yote wetu anataka kuhesabiwa kati ya “watoto” wa Babeli Mkuu wakati wa Mungu uliowekwa ufikapo wa kuwaseta “juu ya mwamba”? Ikiwa sisi hatutaki kuhesabiwa hivyo, sana sana ikiwa sisi tunadai kuwa kati ya wale ambao Mungu anaita “watu wangu,” vipi basi? Hakuna jambo jingine isipokuwa kuutumia kwa faida wakati unaobaki na kutii amri yenye rehema ya Mungu kupitia kwa Neno lake: “Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.”—Ufu. 18:4 Yer. 50:8.