Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • gm sura 6 kur. 71-86
  • Ile Miujiza—Je! Kweli Ilitukia?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ile Miujiza—Je! Kweli Ilitukia?
  • Biblia—Neno la Mungu au la Binadamu?
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sababu Wengine Hawaamini
  • Ni kinyume cha Sheria za Asili?
  • Vipi Ile ya Bandia?
  • ‘Miujiza Haitukii Sasa’
  • Twaweza Kujuaje?
  • Mwujiza Wenye Kushuhudiwa Vizuri Zaidi
  • Kaburi Lililo Tupu
  • Mkataa Aliofikia Luka Yule Tabibu
  • Walimwona Yesu Aliyefufuliwa
  • Miujiza Hutukia Kikweli
  • Je, Kweli Miujiza Hutukia?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Kwa Nini Upendezwe na Miujiza?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Miujiza ya Yesu—Je, Kweli Ilitukia?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Miujiza ya Yesu Unaweza Kujifunza Nini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
Pata Habari Zaidi
Biblia—Neno la Mungu au la Binadamu?
gm sura 6 kur. 71-86

Sura 6

Ile Miujiza—Je! Kweli Ilitukia?

Siku moja katika 31 W.K., Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakisafiri kwenda Naini, jiji moja kaskazini mwa Palestina. Walipokaribia lango la jiji hilo, walikutana na andamano la maziko. Aliyekufa alikuwa mwanamume kijana. Mama yake alikuwa mjane, naye alikuwa amekuwa mwana wake wa pekee, kwa hiyo sasa alibaki peke yake tu. Kulingana na maandishi, Yesu “alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema.”—Luka 7:11-15.

1. (Tia ndani utangulizi.) (a) Ni mwujiza gani aliofanya Yesu karibu na jiji la Naini? (b) Miujiza ni ya maana kadiri gani katika Biblia, hata hivyo je! watu wote huamini kwamba ilitukia kweli kweli?

HIYO ni hadithi yenye kuchangamsha moyo, lakini je! ni ya kweli? Wengi huona vigumu kuamini kwamba mambo hayo yalitukia kikweli. Hata hivyo, miujiza ni sehemu iliyomo katika maandishi ya Biblia. Kuamini Biblia kwamaanisha kuamini kwamba miujiza hiyo ilitukia. Kwa kweli, kigezo chote cha ukweli wa Biblia chategemea mwujiza mmoja wa maana sana: ufufuo wa Yesu Kristo.

Sababu Wengine Hawaamini

2, 3. Ni njia gani moja ya kufikiri aliyotumia David Hume mwanafalsafa wa Scotland katika kujaribu kuthibitisha kwamba miujiza haitukii?

2 Je! unaamini miujiza? Au je wahisi katika muhula (wakati) huu wa kisayansi, haipatani na kufikiri kuzuri kuamini miujiza—yaani, matukio yasiyo ya kawaida yanayoonyesha uthibitisho wa kujiingiza kwa mtu mwenye nguvu zinazozidi za kibinadamu? Ikiwa huamini, wewe siye wa kwanza. Karne mbili zilizopita, mwanafalsafa wa Scotland David Hume alikuwa na tatizo lilo hilo. Yaweza kuwa sababu zako za kutoamini zafanana na zake.

3 Vipingamizi vya Hume vya wazo la miujiza vilitia ndani mambo matatu ya kutokeza.1 Kwanza, yeye aliandika hivi: “Mwujiza ni uvunjaji wa sheria za asili.” Binadamu ametegemea tangu zamani za kale sheria za asili. Yeye amejua kwamba kitu kitaanguka kikiangushwa, kwamba jua litachomoza kila asubuhi na kutua kila usiku, na kadhalika. Kisilika, yeye ajua kwamba sikuzote matukio yatafuata vigezo hivyo vya kawaida. Hakuna chochote kitakachotukia ambacho hakipatani na sheria za asili. ‘Uthibitisho’ huo, akahisi Hume, “ni kamili kama vile hoja yoyote iliyoonekana maishani” kupinga uwezekano wa miujiza.

4, 5. Ni sababu gani mbili zinazotokezwa na David Hume kukanusha uwezekano wa miujiza?

4 Hoja ya pili aliyotoa ilikuwa kwamba watu hupumbazwa kirahisi. Wengine hutaka kuamini maajabu na miujiza, hasa inapohusu dini, na mingi iitwayo miujiza imekuja kuonekana ni bandia. Hoja ya tatu ilikuwa kwamba kwa kawaida miujiza huripotiwa katika nyakati za kutojua. Kadiri watu wanavyokuwa wenye elimu zaidi, ndivyo miujiza michache zaidi inavyoripotiwa. Kama alivyosema Hume, “Matukio hayo ya kustaajabisha hayatukii kamwe katika siku zetu.” Hivyo, yeye alihisi hilo lilithibitisha kwamba haikutukia kamwe.

5 Mpaka leo hii, hoja zilizo nyingi za kupinga miujiza hufuata kanuni hizo za msingi, kwa hiyo acheni tuchunguze vipingamizi vya Hume, kimoja baada ya kingine.

Ni kinyume cha Sheria za Asili?

6. Kwa nini si jambo la kufikiri vizuri kupinga wazo la miujiza kwa msingi wa kwamba hiyo ni ‘kuvunja sheria za asili’?

6 Vipi juu ya kipingamizi kwamba miujiza ni ‘kuvunja sheria za asili’ na kwa hiyo haiwezi kuwa ya kweli? Kijuu-juu, huenda hilo likaonekana kuwa lenye kusadikisha; lakini changanua yanayosemwa hasa. Kwa kawaida, mwujiza waweza kufasiliwa kuwa kitu fulani kinachotukia nje ya sheria za asili za kawaida.a Ni tukio lisilotazamiwa hata kidogo hivi kwamba watazamaji wanasadikishwa wameshuhudia kujiingiza kwa mtu mwenye uwezo unaozidi ule wa kibinadamu. Hivyo, maana halisi ya kipingamizi hicho ni: ‘Miujiza haiwezekani kwa sababu ni ya kimwujiza!’ Mbona usichunguze uthibitisho kabla ya kurukia mkataa kama huo?

7, 8. (a) Kwa habari ya sheria za asili kama tuzijuavyo, ni katika njia zipi wanasayansi wamekuwa na akili pana katika rai yao juu ya yanayowezekana na yasiyowezekana? (b) Ikiwa twaamini Mungu, twapaswa pia kuamini nini kuhusu uwezo wake wa kufanya mambo yasiyo ya kawaida?

7 Ukweli ni kwamba, watu walioelimika leo hawako tayari kabisa kama David Hume kusisitiza kwamba sheria za asili zinazojulikana huwa kweli kila mahali na nyakati zote. Wanasayansi wako tayari kudhania-dhania juu ya kama, badala ya ile kawaida ya pande tatu za urefu wa kutambaa, upana, na urefu wa kwenda juu, kwaweza kuwa pande nyingine zaidi katika ulimwengu wote mzima.2 Wao hutoa nadharia juu ya kuwapo kwa mashimo meusi, nyota kubwa mno ambazo hujibomokea mpaka msongamano unakuwa kama kwamba una kipimo. Katika ujirani wazo muundo wa anga husemekana umepotoshwa sana hivi kwamba wakati husemekana umesimama tuli.3 Wanasayansi hata wamejadiliana juu ya kama, chini ya hali fulani, wakati ungeenda nyuma badala ya mbele!4

8 Stephen W. Hawking, Profesa wa Hisabati ya Lokasi katika Cambridge University, alipokuwa akizungumza jinsi ulimwengu wote mzima ulivyoanza, alisema: “Katika nadharia ya uhusianifu wa ujumla ya vitabu bora sana . . . mwanzo wa ulimwengu mzima wote lazima uwe msongamano usio kamili wenye umoja na mpindiko wa anga-wakati. Chini ya hali hizo, sheria zote zijulikanazo za fizikia zingevunjika.”5 Kwa hiyo, wanasayansi wa ki-siku-hizi hawakubali kwamba kwa sababu jambo fulani ni kinyume cha sheria za kawaida za asili hakiwezi kutukia kamwe. Katika hali zisizo za kawaida, vitu visivyo vya kawaida vyaweza kutukia. Kwa hakika, tukiamini Mungu mweza yote, twapaswa kukubali kwamba ana uwezo wa kusababisha matukio yasiyo ya kawaida—ya kimwujiza—yatukie inapolifaa kusudi lake.—Kutoka 15:6-10; Isaya 40:13, 15.

Vipi Ile ya Bandia?

9. Je! ni kweli kwamba baadhi ya miujiza ni udanganyifu? Fafanua jibu lako.

9 Hakuna mtu anayefikiri vizuri anayeweza kukana kwamba hakuna miujiza ya bandia. Kwa kielelezo, wengine hudai wana uwezo wa kuponya wagonjwa kupitia uponyaji wa kimwujiza wa imani. Daktari mmoja wa tiba, William A. Nolan, alifanya uwe mradi wake maalumu kuchunguza maponya hayo. Alifuatia maponya mengi yaliyodaiwa miongoni mwa waponyaji wa kievanjeli katika United States na waitwao wapasuaji-wawasiliani roho wa Asia. Tokeo lilikuwa nini? Alikuta wote ni vielelezo vya kukatisha tamaa na udanganyifu.6

10. Je! wahisi kwamba uhakika wa kwamba baadhi ya miujiza imeonyeshwa kuwa bandia wathibitisha kwamba miujiza yote ni udanganyifu?

10 Je! madanganyo hayo yamaanisha kwamba miujiza ya kweli haikupata kutukia kamwe? Kwa lazima sivyo. Nyakati nyingine twasikia juu ya noti za pesa za benki zilizoigizwa zikitawanywa, lakini hiyo haimaanishi pesa zote zimeigizwa (ni za bandia). Watu fulani wagonjwa huamini sana walaghai, madaktari wadanganyi, na kuwapa pesa nyingi. Lakini hiyo haimaanishi kwamba madaktari wote ni wadanganyi. Wasanii fulani wamekuwa na ustadi wa kuiga picha za kuchorwa za “kiolezo cha kale.” Lakini hilo halimaanishi kwamba picha zote za kuchorwa ni bandia. Wala uhakika wa kwamba mingine inayodaiwa kuwa miujiza kwa wazi ni vibandia haumaanishi kwamba miujiza ya kweli haiwezi kutukia kamwe.

‘Miujiza Haitukii Sasa’

11. Ni kipi kilichokuwa kipingamizi cha tatu cha David Hume kwa wazo la miujiza?

11 Kipingamizi cha tatu kilitolewa muhtasari katika usemi huu: “Matukio hayo ya kustaajabisha hayatukii kamwe katika siku zetu.” Hume alikuwa hajapata kuona mwujiza, kwa hiyo alikataa kuamini kwamba miujiza ingeweza kutukia. Hata hivyo, kutoa sababu kwa njia hiyo hakuna upatano. Mtu yeyote anayefikiri lazima akubali kwamba, kabla ya siku za mwanafalsafa huyo wa Scotland, ‘matukio ya kustaajabisha’ yalitukia ambayo hayakurudiwa wakati wa maisha yake. Matukio gani?

12. Ni matukio gani ya ajabu yaliyotukia wakati uliopita yasiyowezwa kufafanuliwa na sheria za asili zinazotenda leo?

12 Jambo moja ni kwamba, uhai ulianzia duniani. Kisha, namna fulani za uhai zikapewa ufahamu. Hatimaye, binadamu akatokea, aliyepewa hekima, uwezo wa kuwaza, uwezo wa kupenda, na uwezo wa dhamiri. Hakuna mwanasayansi yeyote anayeweza kufafanua kwa msingi wa sheria za asili zinazotenda leo ni jinsi gani mambo hayo yasiyo ya kawaida yalivyotukia. Hata hivyo tuna uthibitisho ulio hai kwamba yalitukia.

13, 14. Ni mambo gani yaliyo ya kawaida leo ambayo yangalionekana kuwa ya kimwujiza kwa David Hume?

13 Na vipi juu ya ‘matukio ya kustaajabisha’ ambayo yametukia tangu siku ya David Hume? Tuseme tungeweza kusafiri turudi kwenye wakati uliopita tumwambie juu ya ulimwengu wa leo. Wazia ukijaribu kumfafanulia kwamba mfanya biashara mmoja katika Nairobi aweza kusema na mtu aliyeko umbali wa maelfu ya kilometa katika London bila hata kuinua sauti yake; kwamba mechi ya kandanda katika Hispania yaweza kuonwa duniani pote wakati ule ule inapochezwa; kwamba vyombo vikubwa sana zaidi ya meli za baharini za siku ya Hume zaweza kuinuka kutoka ardhini na kubeba watu 500 kupitia hewani kwenda maelfu ya kilometa kwa saa chache. Waweza kuwazia itikio lake? ‘Haiwezekani! Matukio hayo ya kustaajabisha hayatukii kamwe katika siku zetu!’

14 Hata hivyo ‘ajabu’ hizo hutukia katika siku zetu. Kwa nini? Kwa sababu binadamu, akitumia kanuni za kisayansi ambazo Hume hakuziwazia, amejifunza kuunda simu, televisheni, na eropleni. Basi, je! ni vigumu mno kuamini kwamba pindi fulani wakati uliopita Mungu angeweza, katika njia tusizozielewa bado, kutimiza mambo ambayo kwetu ni ya kimwujiza?

Twaweza Kujuaje?

15, 16. Ikiwa miujiza ilitukia kikweli, ni njia gani pekee ambayo tungeweza kujua juu yayo?

15 Bila shaka, kusema kwamba yaweza kuwa miujiza ilitukia hakumaanishi kwamba ilitukia. Twaweza kujuaje, katika karne hii ya 20, kama kule nyuma katika nyakati za Biblia Mungu alifanya miujiza ya kweli kupitia watumishi wake duniani au la? Ni uthibitisho wa aina gani ambao wewe ungetazamia kwa mambo kama hayo? Wazia mkabila asiyestaarabika ambaye ametolewa kutoka makao yake ya porini akatembelee jiji kubwa. Arejeapo, aweza kuwasimuliaje watu wake maajabu ya ustaarabu? Hawezi kufafanua jinsi motokaa inavyofanya kazi au ni kwa nini muziki hutoka kwa redio inayochukulika. Hawezi kuunda kompyuta ili athibitishe kwamba kuna kitu kama hicho. Awezayo tu ni kusimulia aliyoona.

16 Tumo katika hali hiyo kama watu wa kabila la mtu huyo. Ikiwa Mungu amefanya miujiza, njia pekee tunayoweza kujifunza juu yayo ni kutokana na mashahidi waliojionea. Mashahidi hao waliojionea hawawezi kufafanua jinsi miujiza hiyo ilivyotukia, wala hawawezi kuifanya tena. Wanaweza tu kutuambia waliyoona. Bila shaka, mashahidi waliojionea waweza kudanganywa. Pia wanaweza kwa urahisi kutia chumvi na kutoa habari ya kupotosha. Basi, ikiwa tutauamini ushuhuda wao, twahitaji kujua kwamba mashahidi hao waliojionea ni wasema kweli, ni wa kiwango cha juu, na wamejithibitisha kuwa wana makusudi mazuri.

Mwujiza Wenye Kushuhudiwa Vizuri Zaidi

17. (a) Ni mwujiza gani unaoshuhudiwa vizuri zaidi katika Biblia? (b) Ni hali zipi zilizoongoza mpaka kwenye kifo cha Yesu?

17 Mwujiza unaoshuhudiwa vizuri zaidi katika Biblia ni ufufuo wa Yesu Kristo, kwa hiyo mbona usitumie huo kuwa jaribio. Kwanza, fikiria mambo ya hakika yanayoripotiwa: Yesu alikamatwa jioni ya Nisani 14—ambayo ilikuwa usiku wa Alhamisi katika njia yetu ya ki-siku-hizi ya kuhesabu juma.b Alitokea mbele ya viongozi wa Wayahudi waliomshtaki kukufuru na wakaamua alipaswa kufa. Viongozi wa Kiyahudi hao walimpeleka Yesu mbele ya Pontio Pilato liwali Mroma, aliyeshindwa na mkazo wao na kumkabidhi auawe. Labda baadaye Ijumaa asubuhi—bado ni Nisani 14 kwenye kalenda ya Kiyahudi—alipigiliwa misumari kwenye mti wa mateso na baada ya saa chache akawa amekufa.—Marko 14:43-65; 15:1-39.

18. Kulingana na Biblia, ripoti ya ufufuo wa Yesu ilianza kueneaje?

18 Baada ya askari Mroma kudunga ubavu wa Yesu kwa mkuki ili kuhakikisha alikuwa amekufa kweli kweli, mwili wa Yesu ulizikwa katika kaburi jipya. Kesho yake, Nisani 15 (Ijumaa/Jumamosi), ilikuwa sabato. Lakini asubuhi ya Nisani 16—Jumapili asubuhi—wanafunzi fulani walienda kwenye kaburi hilo wakalikuta liko tupu. Baada ya muda mfupi, hadithi zikaanza kuenea kwamba Yesu alikuwa ameonwa akiwa hai. Itikio la kwanza kwa hadithi hizo lilikuwa lile lile ambalo lingekuwako leo—kutokuamini. Hata mitume walikataa kuamini. Lakini wao wenyewe walipomwona Yesu aliye hai, hawakuwa na uchaguzi ila kukubali kwamba kweli kweli alikuwa amefufuliwa kutoka kwa wafu.—Yohana 19:31–20:29; Luka 24:11.

Kaburi Lililo Tupu

19-21. (a) Kulingana na Justin Martyr, Wayahudi walikabilianaje na kuhubiri kwa Wakristo juu ya ufufuo wa Yesu? (b) Twaweza kuwa na uhakika kaburi la Yesu lilikuwaje katika Nisani 16?

19 Je! Yesu alikuwa amefufuliwa, au je! yote hayo ni mambo ya kubuni tu? Jambo moja ambalo watu huko nyuma wangeelekea kusema ni: Je! mwili wa Yesu ungali katika kaburi lake? Wafuasi wa Yesu wangalikabili kizuizi kikubwa sana kama wapinzani wao wangeonyesha maiti yake yenyewe ikiwa ingali ndani ya kaburi layo kuwa uthibitisho wa kwamba hakuwa amefufuliwa. Hata hivyo, hakuna maandishi yoyote kwamba walifanya hivyo. Badala yake, kulingana na Biblia, waliwapa pesa askari waliopewa mgawo wa kulinda kaburi hilo na kuwaambia: “Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelela.” (Mathayo 28:11-13) Sisi pia tuna uthibitisho ulio nje ya Biblia kwamba viongozi hao wa Kiyahudi walitenda hivyo.

20 Karibu karne moja baada ya kifo cha Yesu, Justin Martyr aliandika kitabu kinachoitwa Dialogue With Trypho. Katika hicho, alisema: “Nyinyi [Wayahudi] mmetuma kotekote ulimwenguni wanaume waliochaguliwa na kutawazwa rasmi ili kutangaza kwamba uzushi wa kukana Mungu na wa kuhalifu sheria ulikuwa umetokana na Yesu fulani, mdanganyi Mgalilaya, ambaye tulimsulubisha, lakini wanafunzi wake wakamwiba kaburini usiku, ambamo alikuwa amewekwa.”7

21 Trypho alikuwa Myahudi, na Dialogue With Trypho kiliandikwa ili kutetea Ukristo dhidi ya Dini ya Kiyahudi. Hivyo, haielekei Justin Martyr angalisema aliyosema—kwamba Wayahudi walishtaki Wakristo kuwa waliiba mwili wa Yesu kaburini—kama Wayahudi hawangekuwa wametoa shtaka hilo. Ama sivyo, kwa urahisi angalishtakiwa kusema uwongo. Justin Martyr angalisema hivyo ikiwa tu Wayahudi wangekuwa wamepeleka kikweli wajumbe kama hao. Nao wangalifanya hivyo ikiwa tu kaburi hilo lingekuwa tupu kikweli katika Nisani 16, 33 W.K. na ikiwa hawangeweza kuelekeza kwenye mwili wa Yesu katika kaburi kuwa uthibitisho kwamba hakuwa amefufuliwa. Kwa hiyo kwa kuwa kaburi hilo lilikuwa tupu, ni nini lililokuwa limetukia? Je! kweli wanafunzi hao waliiba mwili huo? Au je! uliondolewa kimwujiza kuwa uthibitisho kwamba Yesu alikuwa amefufuliwa kikweli?

Mkataa Aliofikia Luka Yule Tabibu

22, 23. Ni nani aliyekuwa mwanamume mmoja mwenye elimu wa karne ya kwanza aliyechunguza ufufuo wa Yesu, na ni vyanzo gani vya habari vilivyopatikana kwake?

22 Mwanamume mmoja mwenye elimu ya juu wa karne ya kwanza aliyefikiria kwa uangalifu uthibitisho huo alikuwa ni Luka, tabibu. (Wakolosai 4:14) Pia Luka aliandika vitabu viwili ambavyo sasa ni sehemu ya Biblia: kimoja kilikuwa ni Gospeli, au historia ya huduma ya Yesu, na kile kingine, kinachoitwa Matendo ya Mitume, kilikuwa historia ya mweneo wa Ukristo katika miaka iliyofuata kifo cha Yesu.

23 Katika utangulizi wa Gospeli yake, Luka arejezea uthibitisho mwingi uliopatikana kwake lakini ambao haupatikani tena kwetu. Yeye anena juu ya hati zilizoandikwa juu ya maisha ya Yesu alizochunguza. Pia yeye asema kwamba alinena na mashahidi waliojionea maisha, kifo, na ufufuo wa Yesu. Kisha, asema: “Nimejitafutia kwa usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo.” (Luka 1:1-3) Kwa wazi, utafiti wa Luka ulikuwa kamili. Je! alikuwa mwanahistoria mzuri?

24, 25. Wengi wana rai gani kuhusu sifa za Luka akiwa mwanahistoria?

24 Wengi wetu tumeshuhudia kwamba alikuwa hivyo. Nyuma katika 1913, Sir William Ramsay katika mhadhara mmoja alielekeza juu ya uhistoria wa vitabu vya Luka. Mkataa wake? “Luka ni mwanahistoria wa daraja la kwanza; taarifa zake si uhakika wa kutegemeka tu; yeye ajua maana halisi ya kihistoria.”8 Watafiti wa karibuni zaidi wamefikia mkataa uo huo. The Living Word Commentary, kilipokuwa kikitoa utangulizi wa mabuku yacho juu ya Luka, chasema: “Luka alikuwa mwanahistoria (na aliye sahihi) na pia mwanatheolojia.”

25 Dakt. David Gooding, aliyekuwa zamani profesa wa Kigiriki cha Agano la Kale katika Ireland Kaskazini, ajulisha rasmi kwamba Luka alikuwa “mwanahistoria wa kale kufuatia desturi ya wanahistoria wa Agano la Kale na kufuatia desturi ya Thucydides [mojawapo wanahistoria wenye kusifiwa sana wa ulimwengu wa kale]. Kama wao atakuwa amejitahidi sana kuchunguza vyanzo vyake, katika kuteua habari yake, na katika kuipanga habari hiyo. . . . Thucydides aliunganisha njia hiyo akiwa na tamaa kubwa ya usahihi wa kihistoria: hakuna sababu ya kufikiri kwamba Luka alifanya punde kuliko hivyo.”9

26. (a) Mkataa wa Luka kuhusu ufufuo wa Yesu ulikuwa nini? (b) Yaweza kuwa ni nini kilichomtia nguvu katika mkataa huo?

26 Mkataa wa mwanamume huyu mwenye kustahili sana ulikuwa nini juu ya sababu gani kaburi la Yesu lilikuwa tupu katika Nisani 16? Katika Gospeli yake na katika kitabu cha Matendo, Luka aripoti kuwa uhakika kwamba Yesu alifufuliwa kutoka wafu. (Luka 24:1-52; Matendo 1:3) Hakuwa na shaka juu ya yote hayo. Labda imani yake katika mwujiza wa ufufuo ilitiwa nguvu na mambo aliyojionea mwenyewe. Ingawa ni wazi hakuwa shahidi aliyejionea ufufuo huo, yeye aripoti alikuwa shahidi wa miujiza iliyofanywa na mtume Paulo.—Matendo 14:8-10; 20:7-12; 28:8, 9.

Walimwona Yesu Aliyefufuliwa

27. Ni nani baadhi ya waliodai kuwa walimwona Yesu?

27 Kimapokeo mbili za zile Gospeli huhesabiwa kuwa ziliandikwa na wanaume waliomjua Yesu, wakamwona akifa, na waliodai walimwona kihalisi baada ya ufufuo wake. Wao ni mtume Mathayo, aliyekuwa hapo zamani mtoza kodi, na Yohana, mtume mpendwa wa Yesu. Mwandikaji mwingine wa Biblia, mtume Paulo, alidai pia aliona Kristo aliyefufuliwa. Kuongezea hayo, Paulo aorodhesha kwa majina wengine walioona Yesu akiwa hai baada ya kifo chake, na asema kwamba pindi moja Yesu aliwatokea “ndugu zaidi ya mia tano pamoja.”—1 Wakorintho 15:3-8.

28. Ufufuo wa Yesu ulikuwa na tokeo gani juu ya Petro?

28 Mmoja ambaye Paulo hutaja kuwa shahidi aliyejionea kwa macho ni Yakobo, ndugu-nusu wa kimwili wa Yesu, ambaye lazima awe alikuwa amemjua Yesu tangu utoto. Mwingine ni mtume Petro; mwanahistoria Luka aripoti kwamba alitoa ushahidi usio na hofu juu ya ufufuo wa Yesu majuma machache tu baada ya kifo cha Yesu. (Matendo 2:23, 24) Barua mbili katika Biblia huhesabiwa kimapokeo kuwa za Petro, na katika ya kwanza ya hizo Petro aonyesha kwamba imani yake katika ufufuo wa Yesu ingali ilikuwa kichocheo chenye nguvu hata miaka mingi baada ya tukio hilo. Yeye aliandika hivi: “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu.”—1 Petro 1:3.

29. Ijapokuwa hatuwezi kunena na mashahidi waliojionea ufufuo huo, ni uthibitisho gani wenye kutokeza unaopatikana kwetu?

29 Hivyo, kama ambavyo Luka angeweza kunena na watu waliodai waliona na kunena na Yesu baada ya kifo chake, ndivyo tuwezavyo kusoma maneno ambayo baadhi yao waliandika. Nasi twaweza kujiamulia kama watu hao walidanganywa, kama walikuwa wakijaribu kutudanganya, au kama walimwona kikweli Kristo aliyefufuliwa. Kusema kweli, haiwezekani kuwa walidanganywa. Baadhi yao walikuwa marafiki wa karibu wa Yesu mpaka kifo chake. Baadhi yao walikuwa mashahidi wa maumivu yake makali juu ya mti wa mateso. Waliona damu na maji yakimiminika kutoka lile jeraha la mkuki lililotiwa na askari. Askari huyo alijua, na wao walijua, kwamba bila shaka Yesu alikuwa amekufa. Baadaye, wao wasema, walimwona Yesu akiwa hai wakanena naye kikweli. La, haingeweza kuwa walidanganywa. Basi, je! walikuwa wakijaribu kutudanganya katika kusema kwamba Yesu alikuwa amefufuliwa?—Yohana 19:32-35; 21:4, 15-24.

30. Kwa nini haiwezekani kwamba wale mashahidi wa mapema waliojionea ufufuo wa Yesu walikuwa wakisema uwongo?

30 Ili kujibu hilo, jambo la kujiuliza ni hili: Je! wao wenyewe waliamini waliyokuwa wakisema? Ndiyo, bila shaka. Kwa Wakristo, kutia ndani wale waliodai kuwa mashahidi waliojionea, ufufuo wa Yesu ulikuwa msingi kamili wa imani yao. Mtume Paulo alisema: “Kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure . . . Kama Kristo hakufufuka, imani yetu ni bure.” (1 Wakorintho 15:14, 17) Je! hayo yasikika kama maneno ya mwanaume aliyekuwa akisema uwongo anaposema aliona Kristo aliyefufuliwa?

31, 32. Ni dhabihu zipi zilizofanywa na Wakristo wa mapema, na ni kwa nini huo ni uthibitisho wenye nguvu kwamba Wakristo hao walikuwa wakisema kweli waliposema kwamba Yesu alikuwa amefufuliwa?

31 Fikiria lililomaanishwa na kuwa Mkristo katika siku hizo. Hakukuwako kufaidika na umashuhuri, mamlaka, au utajiri. Ni kinyume kabisa. Wengi wa Wakristo wa mapema ‘kwa furaha walinyang’anywa mali zao’ kwa ajili ya imani yao. (Waebrania 10:34) Ukristo ulihusisha maisha ya kujidhabihu na mnyanyaso ambayo katika visa vingi yaliishia katika kifo cha aibu, chenye maumivu cha kufia imani kama shahidi.

32 Baadhi ya Wakristo walitoka katika familia zenye fanaka, kama vile mtume Yohana ambaye bila shaka baba yake alikuwa na biashara yenye kufanikiwa ya samaki katika Galilaya. Wengi walikuwa na mataraja mazuri, kama vile Paulo ambaye, alipoukubali Ukristo, alikuwa amekuwa mwanafunzi wa Gamalieli, rabi mwenye kujulikana sana na alikuwa ameanza kujiletea sifa machoni pa watawala Wayahudi. (Matendo 9:1, 2; 22:3; Wagalatia 1:14) Hata hivyo, wote waliyapa kisogo mambo ambayo ulimwengu huu ulitoa kusudi waeneze ujumbe wenye kutegemea uhakika wa kwamba Yesu alikuwa amefufuliwa kwa wafu. (Wakolosai 1:23, 28) Kwa nini wafanye dhabihu hizo kwa ajili ya jambo ambalo walijua lilitegemea uwongo? Jibu ni, hawangefanya hivyo. Walikuwa na nia ya kuteseka na kufa kwa ajili ya jambo ambalo walijua lilitegemea kweli.

Miujiza Hutukia Kikweli

33, 34. Kwa kuwa ufufuo ulitukia kikweli, twaweza kusema nini juu ya ile miujiza mingine ya Biblia?

33 Hakika, uthibitisho wa hati wasadikisha kabisa. Kwa kweli Yesu alifufuliwa kwa wafu katika Nisani 16, 33 W.K. Na kwa kuwa ufufuo huo ulitukia, ile miujiza mingine yote ya Biblia yawezekana—miujiza ambayo pia tuna ushuhuda thabiti wa mashahidi waliojionea. Uyo huyo mwenye Uwezo aliyemfufua Yesu kwa wafu alimwezesha Yesu pia kufufua mwana wa yule mjane wa Naini. Yeye pia alimtia nguvu Yesu afanye ile miujiza midogo zaidi—lakini bado ya ajabu—ya kuponya. Yeye ndiye aliyewezesha kulishwa kimwujiza kwa umati, na Yeye pia aliwezesha Yesu kutembea juu ya maji.—Luka 7:11-15; Mathayo 11:4-6; 14:14-21, 23-31.

34 Hivyo, uhakika wa kwamba Biblia hueleza juu ya miujiza si sababu ya kutilia shaka ukweli wayo. Badala yake, uhakika wa kwamba miujiza hiyo ilitukia katika nyakati za Biblia ni uthibitisho wenye nguvu kwamba kwa kweli Biblia ni Neno la Mungu. Lakini kuna shtaka jingine linalofanywa dhidi ya Biblia. Wengi husema kwamba hiyo hujipinga yenyewe na kwa hiyo haiwezi kuwa ni Neno la Mungu. Je! hilo ni kweli?

[Maelezo ya Chini]

a Twasema “kwa kawaida,” kwa sababu miujiza fulani katika Biblia yaweza kuwa ilihusisha matukio ya asili, kama vile matetemeko ya ardhi au maporomoko ya ardhi. Hata hivyo, yangali huonwa kuwa miujiza kwa sababu mambo hayo yalitukia wakati ule ule yalipohitajiwa na kwa hiyo bila shaka kwa mwelekezo wa Mungu.—Yoshua 3:15, 16; 6:20.

b Siku ya Kiyahudi ilianza karibu saa kumi na mbili jioni na kuendelea mpaka saa kumi na mbili jioni iliyofuata.

[Blabu katika ukurasa wa 81]

Maadui wa Ukristo walisema kwamba wanafunzi waliiba mwili wa Yesu. Ikiwa ndivyo ilivyokuwa, ni kwa nini Wakristo wangekuwa na nia ya kufa kwa ajili ya imani iliyotegemea ufufuo wake?

[Sanduku katika ukurasa wa 85]

Kwa Nini Hakuna Miujiza Leo?

Nyakati nyingine swali hili hutokezwa: ‘Kwa nini hakuna miujiza leo?’ Jibu ni kwamba miujiza ilitimiza kusudi layo huko nyuma, lakini leo Mungu hututazamia tuishi kwa imani.—Habakuki 2:2-4; Waebrania 10:37-39.

Katika siku za Musa, miujiza ilitukia ili kuthibitisha sifa za kumstahilisha Musa. Ilionyesha kwamba Yehova alikuwa akimtumia na pia kwamba kwa kweli agano la Sheria lilikuwa lenye chanzo cha kimungu na kwamba tangu wakati huo Waisraeli walikuwa watu wachaguliwa wa Mungu.—Kutoka 4:1-9, 30, 31; Kumbukumbu la Torati 4:33, 34.

Katika karne ya kwanza, miujiza ilisaidia kuthibitisha sifa za kustahili kwa Yesu na, baada yake, za kundi changa la Kikristo. Ilisaidia kuonyesha kwamba Yesu alikuwa yule Mesiya aliyeahidiwa, kwamba baada ya kifo chake mahali pa Israeli la kimwili palichukuliwa na kundi la Kikristo, na hivyo kwamba Sheria ya Musa haikuwa ikiongoza tena.—Matendo 19:11-20; Waebrania 2:3, 4.

Baada ya siku za mitume, wakati wa miujiza ulikuwa umepita. Mtume Paulo alifafanua hivi: “Ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.”—1 Wakorintho 13:8-10.

Leo, tuna Biblia kamili, ambayo hutia ndani mafunuo na shauri lote la Mungu. Tuna utimizo wa unabii, na tunaelewa kwa kiwango kikubwa makusudi ya Mungu. Hivyo, hakuna uhitaji tena wa miujiza. Hata hivyo, roho ile ile ya Mungu iliyowezesha miujiza hiyo ingalipo na hutokeza matokeo yanayotokeza uthibitisho wenye nguvu kadiri ileile wa uwezo wa kimungu. Tutaona zaidi juu ya hilo katika sura ya baadaye.

[Picha katika ukurasa wa 75]

Wengi wana rai ya kwamba kutegemeka kwa sheria za asili, kama vile uhakika wa kwamba jua huchomoza kila asubuhi ni uthibitisho wa kwamba miujiza haiwezi kutukia

[Picha katika ukurasa wa 77]

Kuumbwa kwa dunia kuwa makao ya vitu vilivyo hai kulikuwa ni ‘tukio la kustaajabisha’ ambalo halikurudiwa

[Picha katika ukurasa wa 78]

Ungeweza kuelezaje maajabu ya sayansi ya ki-siku-hizi kwa mtu aliyeishi miaka 200 iliyopita?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki