Ungamo
Maana: Kutangaza au kukiri, hadharani au faraghani, (1) jambo ambalo mtu anaamini au (2) dhambi zake.
Je, ibada ya kitubio, pamoja na kule kuungama sikioni mwa padre, kama inavyofundishwa na Kanisa Katoliki ni ya Kimaandiko?
Jinsi padre anavyotajwa
Njia ya kimapokeo inayotumiwa, ambayo bado inatumiwa mara nyingi, ni: “Padre unibariki kwa kuwa nimetenda dhambi. . . . Sijaungama tangu . . . ”—Chuo Kidogo cha Sala, uku. 37.
Mt. 23:1, 9, UV: “Kisha Yesu akawaambia . . . Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni.”
Dhambi zinazoweza kusamehewa
“Sikuzote Kanisa limefundisha kwamba kila dhambi, hata iwe nzito kadiri gani, inaweza kusamehewa.”—The Catholic Encyclopedia (yenye nihil obstat na imprimatur), R. C. Broderick (Nashville, Tenn.; 1976), uku. 554.
Ebr. 10:26, UV: “Kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi.”
Marko 3:29, UV: “Mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele.”
Jinsi malipizi yanavyopasa kuonyeshwa
Mara nyingi padre ambaye husikiliza maungamo humwagiza mtu anayetubu akariri mara kadhaa sala ya “Baba Yetu” na “Salamu Maria.”
Mt. 6:7, UV: “Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke [yaani, kutamka kwa kurudia-rudia kusiko na maana], kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.”
Mt. 6:9-12, UV: “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, . . . Utusamehe deni zetu.” (Hakuna mahali katika Biblia tunapoamriwa kusali kwa Maria au kupitia yeye. Ona Wafilipi 4:6, pia ukurasa wa 185, 186, chini ya kichwa “Maria.”)
Rom. 12:9, UV : “Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.”
Je, Yesu hakuwapa mitume wake mamlaka ya kusamehe dhambi?
Yoh. 20:21-23, UV: “Kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.”
Mitume waliyaelewaje maneno hayo nao waliyatumiaje? Biblia haitaji kisa chochote ambapo mmoja wa mitume alisikiliza ungamo la mtu kisha akampa msamaha. Hata hivyo, matakwa ya kusamehewa na Mungu yameandikwa katika Biblia. Mitume, wakiongozwa na roho takatifu, wangeweza kufahamu ikiwa mtu alikuwa akitimiza matakwa hayo na kwa hiyo wangeweza kutangaza kwamba Mungu alikuwa amemsamehe au hakuwa amemsamehe. Ona mfano katika Matendo 5:1-11, pia 1 Wakorintho 5:1-5 na 2 Wakorintho 2:6-8.
Ona pia kichwa “Urithi wa Upapa.”
Wasomi wana maoni tofauti kuhusu chanzo cha desturi ya kuungama masikioni mwa padre
The Catholic Encyclopedia, ya R. C. Broderick, yaeleza hivi: “Kuungama masikioni mwa mapadre kumekubaliwa tangu karne ya nne.”—Uku. 58.
New Catholic Encyclopedia inasema hivi: “Wanahistoria wengi wa Kikatoliki na wa Kiprotestanti, huona chanzo cha malipizi ya faraghani kuwa nidhamu ya kawaida kwa makanisa ya Ireland, Wales, na Uingereza, ambako Sakramenti, pamoja na Malipizi, zilitolewa kwa ukawaida na padre mkuu wa nyumba ya watawa, pamoja na mapadre wake watawa. Inaonekana kwamba maungamo ya kurudiwa-rudiwa na maungamo ya ujitoaji yalianzishwa kwa ajili ya watu wa kawaida, kufuatia desturi ya watawa ya kuungama na mwelekezo wa kiroho wa hadharani na faraghani. . . . Hata hivyo, katika karne ya 11 ndipo dhambi za siri zilianza kusamehewa wakati wa ungamo na kabla ya kutimizwa kwa malipizi.”—(1967), Buku la 11, uku. 75.
Mwanahistoria A. H. Sayce anaripoti hivi: “Maandishi ya desturi za kidini yaonyesha kwamba katika Babilonia pia, kulikuwa na desturi ya kuungama hadharani na faraghani. Kwa kweli, yaonekana kwamba ungamo la faraghani limekuwa ndiyo njia ya kale zaidi na ya kawaida zaidi.”—The Religions of Ancient Egypt and Babylonia (Edinburgh, 1902), uku. 497.
Mashahidi wa Yehova huamini nini kuhusiana na ungamo?
Kuungama imani kwa kutangaza hadharani
Rom. 10:9, 10: “Ukitangaza waziwazi lile ‘neno lililo katika kinywa chako mwenyewe,’ kwamba Yesu ni Bwana, na kuonyesha imani moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokolewa. Kwa maana kwa moyo mtu huonyesha imani kwa ajili ya uadilifu, lakini kwa kinywa mtu hufanya tangazo la hadharani kwa ajili ya wokovu.”
Mt. 10:32, 33: “Basi, kila mtu anayekiri mbele ya wanadamu kwamba yuko katika umoja pamoja nami [Yesu Kristo], mimi pia nitakiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni kwamba niko katika umoja pamoja naye; lakini yeyote yule anayenikana mimi mbele ya watu, mimi pia nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”
Mtu anapofanya dhambi dhidi ya Mungu
Mt. 6:6-12: “Lakini wewe unaposali, ingia ndani ya chumba chako cha faragha na, baada ya kufunga mlango wako, sali kwa Baba yako aliye mahali pa siri . . . ‘Baba yetu uliye mbinguni, jina lako na litakaswe . . . na utusamehe madeni yetu, kama vile ambavyo sisi pia tumewasamehe wadeni wetu.’”
Zab. 32:5: “Mwishowe niliungama dhambi yangu kwako [Mungu], wala sikufunika kosa langu. Nilisema: ‘Nitaungama makosa yangu kwa Yehova.’ Nawe mwenyewe ukanisamehe kosa la dhambi zangu.”
1 Yoh. 2:1: “Yeyote akitenda dhambi, tuna msaidizi kwa Baba, Yesu Kristo, mtu mwadilifu.”
Mtu anapomkosea mwenzake au anapokosewa
Mt. 5:23, 24: “Basi, ikiwa unaleta zawadi yako kwenye madhabahu na hapo ukumbuke kwamba ndugu yako ana jambo fulani juu yako, acha zawadi yako hapo mbele ya madhabahu, na uende zako; kwanza fanya amani yako pamoja na ndugu yako, na ndipo, ukiisha kurudi, itoe zawadi yako.”
Mt. 18:15: “Ndugu yako akitenda dhambi, nenda ufunue kosa lake kati yako na yeye peke yake.”
Luka 17:3: “Ndugu yako akitenda dhambi mkemee, na akitubu msamehe.”
Efe. 4:32: “Iweni wenye fadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma nyororo, mkisameheana kwa hiari kama vile Mungu pia kupitia Kristo alivyowasamehe ninyi kwa hiari.”
Mtu anapofanya kosa zito na anataka kusaidiwa kiroho
Yak. 5:14-16: “Je, kuna yeyote mgonjwa [kiroho] kati yenu? Na awaite kwake wanaume wazee wa kutaniko, nao wasali juu yake, wakimpaka mafuta katika jina la Yehova. Na sala ya imani itamponya huyo asiyejisikia vizuri, na Yehova atamwinua. Pia, ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa [na Mungu]. Kwa hiyo ungameni waziwazi dhambi zenu kwa mtu na mwenzake na kusali kwa ajili ya mtu na mwenzake, ili mponywe.”
Met. 28:13: “Anayefunika makosa yake hatafanikiwa, lakini yeye anayeyaungama na kuyaacha ataonyeshwa rehema.”
Namna gani ikiwa watu wanaofanya dhambi hawatafuti msaada?
Gal. 6:1: “Akina ndugu, hata mtu akijikwaa katika kosa fulani kabla ya yeye kulijua, ninyi mlio na sifa za kustahili kiroho jaribuni kumrekebisha upya mtu huyo katika roho ya upole, huku kila mmoja wenu akiendelea kujiangalia, ili wewe pia usije ukajaribiwa.”
1 Tim. 5:20: “Watu walio na mazoea ya kutenda dhambi uwakaripie mbele ya watazamaji [yaani, mbele ya wale ambao wao binafsi wanalijua jambo hilo], ili wengine pia waogope.”
1 Kor. 5:11-13: “Lakini sasa ninawaandikia ninyi mwache kuchangamana katika ushirika pamoja na mtu yeyote anayeitwa ndugu ambaye ni mwasherati au mtu mwenye pupa au mwabudu-sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi, hata msile chakula pamoja na mtu wa namna hiyo. . . . ‘Ondoeni yule mtu mwovu kati yenu.’”