Utiaji-damu Mishipani—Ni Salama Kadiri Gani?
Kabla ya kukubali njia yoyote ya kitiba iliyo hatari, mtu mwenye kufikiri atajifunza manufaa na hatari zinazoweza kutokea. Namna gani utiwaji-damu mishipani? Sasa ni chombo kikuu katika utibabu. Matabibu wengi ambao hupendezwa kihalisi na wagonjwa wao huenda wasisite hata kidogo juu ya kuwapa damu. Imeitwa zawadi ya uhai.
Mamilioni wamechanga damu au wakaipokea. Kanada ilikuwa na wachangaji 1.3 katika idadi ya watu milioni 25 kwa miaka ya 1986-87. “[Katika] mwaka wa karibuni zaidi ambao tarakimu zao zapatikana, yuniti za damu kati ya milioni 12 na milioni 14 zilitumiwa katika utiaji-damu mishipani katika United States pekee.”—The New York Times, Februari 18, 1990.
“Sikuzote damu imeonea shangwe ‘ubora wa kimwujiza,’” aandika Dakt. Louise J. Keating. “Kwa miaka yayo ya kwanza 46, akiba ya damu ilihisiwa na matabibu na umma pia kuwa ilikuwa salama kuliko ilivyokuwa hasa.” (Cleveland Clinic Journal of Medicine, Mei 1989) Hali ilikuwaje wakati huo, na ikoje sasa?
Hata miaka 30 iliyopita, wataalamu wa magonjwa na wafanya kazi wa benki za damu walishauriwa hivi: “Damu ni baruti! Inaweza kufanya mema mengi au madhara makubwa. Vifo kutokana na utiwaji-damu mishipani hulingana na vya dawa ya nusukaputi au upasuaji wa kuondoa kidoletumbo. Inasemekana kuna karibu kifo kimoja katika utiwaji-damu mishipani 1,000 hadi 3,000 au yawezekana 5,000. Katika eneo la London kumeripotiwa kifo kimoja kwa kila chupa 13,000 za utiwaji-damu mishipani.”—New York State Journal of Medicine, Januari 15, 1960.
Je! tangu hapo hatari zimeondolewa hivi kwamba sasa utiwaji-damu mishipani ni salama? Kusema wazi, kila mwaka mamia ya maelfu huwa na matokeo mabaya ya utiwaji-damu, na wengi hufa. Kwa sababu ya maelezo yaliyotangulia, jambo linaloweza kuja akilini mwako ni magonjwa yanayobebwa na damu. Kabla ya kuchunguza upande huu, fikiria baadhi ya hatari ambazo hazijulikani sana.
DAMU NA KINGA YAKO DHIDI YA MAAMBUKIZO
Mapema katika karne ya 20, wanasayansi waliongeza kina cha uelewevu wa utata mzuri ajabu wa damu. Walijifunza kwamba kuna namna mbalimbali za damu. Kulinganisha damu ya mchangaji na ya mgonjwa ni jambo la umaana wenye hatari katika utiaji-damu mishipani. Ikiwa mtu mwenye damu ya namna ya A anapokea damu ya namna ya B, anaweza kuwa na tokeo hatari la kuharibikiwa na chembe nyekundu. Hiyo yaweza kuharibu nyingi za chembe zake nyekundu na kumwua kwa haraka. Ingawa kuipa damu namna yayo na kuzilinganisha hufanywa sasa kwa ukawaida, makosa hutokea. Kila mwaka watu huuawa na matokeo ya kuharibikiwa na chembe nyekundu.
Mambo hakika huonyesha kwamba suala la kutopatana kwa damu huzidi zile namna chache kwa kulinganishwa ambazo hospitali hujaribu kulinganisha. Kwa nini? Basi, katika makala yake “Utiwaji-Damu Mishipani: Matumizi, Matumizi Mabaya, na Hatari,” Dakt. Douglas H. Posey, Jr., aandika: “Karibu miaka 30 iliyopita Sampson alisimulia habari za utiaji-damu mishipani kuwa njia hatari kwa kulinganishwa . . . [Tangu hapo] angalau vipinga chembe nyekudu 400 zaidi vimetambuliwa na kuainishwa. Hakuna shaka kwamba hesabu itazidi kuongezeka kwa sababu utando wa chembe nyekundu ni tata mno.”—Journal of the National Medical Association, Julai 1989.
Wanasayansi wanachunguza sasa matokeo ya utiaji-damu mishipani juu ya mfumo wa mwili wa kinga. Hiyo yaweza kumaanisha nini kwako wewe au mwanaukoo anayehitaji damu?
Madaktari wanapopandikiza moyo, ini, au kiungo kingine, huenda mfumo wa kinga wa mwenye kukipokea ukahisi tishu hiyo ngeni na kuikataa. Hata hivyo, utiaji-damu mishipani ni upandikizaji wa tishu. Hata damu ambayo imelinganishwa “ifaavyo” yaweza kukinza mfumo wa kinga. Kwenye kongamano moja la wataalamu wa magonjwa, ilionyeshwa kwamba mamia ya karatasi zenye habari za kitiba ‘zimefungamanisha utiaji-damu mishipani na maitikio ya kinga ya mwili.’—“Kesi Yaongezeka Dhidi ya Utiaji-Damu Mishipani,” Medical World News, Desemba 11, 1989.
Kazi kubwa ya mfumo wako wa kinga ni kutambua na kuharibu chembe hatari za kansa. Je! mfumo wa kinga uliokinzwa waweza kuongoza kwenye kansa na kifo? Angalia ripoti mbili.
Jarida Cancer (Februari 15, 1987) lilitoa matokeo ya uchunguzi uliofanywa Uholanzi: “Katika wagonjwa wenye kansa ya utumbompana, athari mbaya kubwa ilionekana kwa wenye kuishi muda mrefu. Katika kikundi hiki kulikuwako muda wa kuishi wenye kuongezeka miaka 5 kwa ujumla wa asilimia 48 kwa wagonjwa waliotiwa damu mishipani na asilimia 74 ya wasiotiwa damu mishipani.” Matabibu kwenye Chuo Kikuu cha Kalifornia Kusini walichunguza wagonjwa mia moja waliofanyiwa upasuaji wa kansa. “Kima cha kurudia-rudia kwa kansa zote za kikoromeo kilikuwa asilimia 14 kwa wale wasiopokea damu na asilimia 65 kwa wale waliopokea. Kwa kansa ya uvungu wa kinywa, kishimo kilicho nyuma ya pua, na koo au tundu la pua, kima cha kurudia-rudia kilikuwa asilimia 31 bila kutiwa damu mishipani na asilimia 71 pamoja na kutiwa damu mishipani.”—Annals of Otology, Rhinology & Laryngology, Machi 1989.
Michunguzo hiyo hudokeza nini kwa habari ya utiaji-damu mishipani? Katika makala yake “Utiaji-Damu Mishipani na Upasuaji wa Kansa,” Dakt. John S. Spratt alifikia mkataa huu: “Huenda daktari mpasuaji wa kansa akaja kuwa daktari mpasuaji asiyetumia damu.”—The American Journal of Surgery, Septemba 1986.
Kazi nyingine kubwa ya mfumo wa kinga ni kukukinga na maambukizo. Hivyo inaeleweka kwamba michunguzo fulani ilionyesha kwamba wagonjwa waliopokea damu wanaelekea zaidi kupatwa na maambukizo. Dakt. P. I. Tartter alifanya uchunguzi juu ya upasuaji wa utumbompana na puru. Kati ya wagonjwa waliopewa damu, asilimia 25 walisitawisha maambukizo, wakilinganishwa na asilimia 4 ya wale ambao hawakupokea damu. Aripoti hivi: “[Visa vya] utiwaji-damu mishipani vilishirikishwa na matatanisho ya maambukizo ilipotiwa kabla, wakati wa, au baada ya upasuaji . . . Hatari ya maambukizo ya baada ya upasuaji iliendelea kuongezeka kwa hesabu ya yuniti za damu zilizopewa.” (The British Journal of Surgery, Agosti 1988) Wale waliohudhuria mkutano mmoja wa 1989 wa Shirika la Amerika la Benki za Damu walijifunza hili: Ingawa asilimia 23 ya wale waliopokea damu iliyochangwa wakati wa upasuaji wa kubadilisha nyonga walisitawisha maambukizo, wale ambao hawakupewa damu hawakuwa na maambukizo hata kidogo.
Dakt. John A. Collins aliandika kuhusu athari hii ya utiaji-damu mishipani: “Ingekuwa ukweli ulio kinyume kabisa ikiwa ‘utibabu’ ulio na uthibitisho mdogo sana wa kutimiza lolote lenye kustahiki ungeonekana baadaye kuzidisha mojapo matatizo makubwa wanayokabili wagonjwa.”—World Journal of Surgery, Februari 1987.
BILA MAGONJWA AU INAJAWA NA HATARI?
Ugonjwa wenye kubebwa na damu huwasumbua-sumbua matabibu wengi wenye kudhamiria na pia wagonjwa wengi. Ugonjwa gani? Kusema wazi, huwezi kuweka mpaka kwa ugonjwa mmoja tu; kwa kweli ni mengi.
Baada ya kuzungumzia yale magonjwa yanayojulikana vizuri zaidi, jarida Techniques of Blood Transfusion (1982) huelekeza kwenye “magonjwa mengine ya kuambukiza yanayohusiana na utiaji-damu mishipani,” kama vile kaswende, ambukizo la saitomegalovairasi, na maleria. Kisha lasema: “Magonjwa mengine kadhaa yameripotiwa pia kuwa yapitishwa na utiaji-damu mishipani, kutia na maambukizo ya vairasi ya malengelenge, mononukleosisi yenye kuambukiza (vairasi Epstein-Barr), toksoplasmosisi, traipanosomiasisi [Malale ya Kiafrika na ugonjwa wa Chagas], lishmaniasisi, bruselosisi [homa ya viwimbiwimbi], homa ya chawa, filariasisi, surua, salmonelosisi, na homa ya kupe wa Kolorado.”
Kwa kweli, orodha ya magonjwa kama hayo inakua. Huenda ukawa ulisoma kichwa kikuu cha habari kama vile “Ugonjwa Lyme Kutokana na Utiawaji-Damu Mishipani? Haielekei, Lakini Wastadi Wana Hadhari.” Je! damu kutoka kwa mtu fulani aliyechunguzwa na kuonekana kuwa ana ugonjwa wa Lyme ni salama kadiri gani? Kikoa cha maofisa wa afya kiliulizwa kama wangekubali damu kama hiyo. “Wote walijibu la, ingawa hakuna aliyependekeza kukataa damu kutoka kwa wachangaji kama hao.” Umma wapaswa kuhisije juu ya damu iliyowekwa katika benki ambayo wastadi wenyewe hawangeikubali?—The New York Times, Julai 18, 1989.
Sababu ya pili ya kuhangaikia ni kwamba damu iliyokusanywa katika bara moja ambamo ugonjwa fulani ni mwingi sana huenda ikatumiwa mbali sana, ambako wala umma wala matabibu hawako chonjo kwa hatari hiyo. Kukiwa na ongezeko la usafiri leo, kutia na wakimbizi na wahamiaji, hatari inakua hivi kwamba huenda magonjwa mapya yakawa katika vitu vilivyofanyizwa kwa damu.
Zaidi ya hilo, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza alionya hivi: “Huenda ikawa lazima kuchunguza akiba ya damu ili kuzuia ambukizo la magonjwa kadhaa ambayo hapo kwanza hayakufikiriwa kuwa yenye kuambukiza, kutia ndani lukemia, limfoma, na kichaa [au ugonjwa wa Alzheimer].”—Transfusion Medicine Reviews, Januari 1989.
Ingawa hatari hizo zinaogopesha, nyingine zimetokeza hofu yenye kuenea zaidi.
ULE MWENEO POTE WA UKIMWI
“UKIMWI umebadili milele njia ambayo madaktari na wagonjwa hufikiri juu ya damu. Na hilo si wazo baya, wakasema madaktari waliokusanyika kwenye Taasisi za Afya ya Taifa kwa ajili ya kongamano juu ya utiaji-damu mishipani.”—Washington Post, Julai 5, 1988.
Ule mweneo pote wa UKIMWI (Ukosefu wa Kinga Mwilini), kwa kulipa kisasi, umeamsha watu waone hatari ya kupatwa na magonjwa yenye kuambukiza kutokana na damu. Mamilioni wameambukizwa sasa. Unaenea bila kudhibitiwa. Na kima cha vifo vyao ni karibu sana asilia 100.
UKIMWI unasababishwa na vairasi (kiini cha ugonjwa) inayotokeza upungufu wa kinga ya kibinadamu mwilini (HIV), inayoweza kuenezwa na damu. Lile pigo la ki-siku-hizi la UKIMWI lilifunuka katika 1981. Mwaka wenyewe uliofuata, wastadi wa afya walijifunza kwamba vairasi hiyo ingeweza kupitishwa katika vitu vilivyofanyizwa kwa damu. Sasa inakubaliwa kwamba kiwanda cha damu kiliitikia polepole, hata baada ya michunguzo kupatikana ya kutambua damu yenye vizuia-bakteria vya HIV. Hatimaye kuchunguza damu iliyochangwa kukaanza katika 1985,a lakini hata wakati huo vitu vilivyofanyizwa kwa damu ambavyo tayari vilikuwa akibani havikuchunguzwa.
Baada ya hapo umma ulihakikishiwa, ‘Sasa akiba ya damu ni salama.’ Hata hivyo, baadaye ilifunuliwa kwamba UKIMWI una “muda wa kusitawi” ulio hatari. Baada ya mtu kuambukizwa, huenda miezi ikapita kabla hajatokeza vizuia-bakteria vinavyoweza kugundulika. Bila kujua kwamba anahifadhi vairasi, huenda akachanga damu ambayo ikichunguzwa matokeo yangekuwa hasi. Hili limetukia. Watu wamesitawisha UKIMWI baada ya kutiwa mishipani damu kama hiyo!
Hali ikawa yenye kutia hofu hata zaidi. Jarida The New England Journal of Medicine (Juni 1, 1989) liliripoti juu ya “Maambukizo ya kimya ya HIV.” Ilithibitishwa kwamba watu wanaweza kubeba vairasi ya UKIMWI kwa miaka mingi bila ya hiyo kuweza kuchunguzika kwa michunguzo ya kisasa isiyo ya moja kwa moja. Wengine wangependa kupunguza uzito wa visa hivyo kuwa ni vya mara chache tu, lakini vinathibitisha “kwamba hatari ya kuambukizwa UKIMWI kupitia damu na sehemu zayo haiwezi kuondolewa kabisa.” (Patient Care, Novemba 30, 1989) Mkataa wenye kufadhaisha: Mchunguzo hasi (usioonyesha ugonjwa) usichukuliwe kuwa uhakikisho kwamba hakuna ugonjwa. Ni wangapi ambao bado watapata UKIMWI kutokana na damu?
KIATU KIFUATACHO? AU VIATU VIFUATAVYO?
Watu wengi wanaokaa katika vyumba vya ghorofa wamesikia kiatu kimoja kikigonga sakafu juu yao; ndipo huenda wakawa na wasiwasi wakingojea mgongo wa pili. Katika tatizo la damu, hakuna yeyote ajuaye ni migongo mingapi hatari ambayo bado itagonga.
Vairasi ya UKIMWI iliitwa HIV, lakini wastadi fulani sasa wanaiita HIV-1. Kwa nini? Kwa sababu walipata vairasi nyingine ya namna ya UKIMWI (HIV-2). Inaweza kusababisha dalili za UKIMWI nayo imeenea sana katika maeneo fulani. Zaidi ya hilo, “haigunduliwi kwa upatani na michunguzo ya UKIMWI inayotumiwa sasa hapa,” laripoti The New York Times. (Juni 27, 1989) “Mavumbuzi mapya . . . hufanya iwe vigumu zaidi kwa benki za damu kuwa na hakika mchango ni salama.”
Au namna gani vairasi zenye uhusiano wa mbali na vairasi ya UKIMWI? Tume ya rais (U.S.A.) ilisema kwamba vairasi moja kama hiyo “inaaminiwa kuwa kisababishi cha lukemia/limfoma ya chembe-T ya watu wazima na ugonjwa mkali wa neva.” Vairasi hii tayari imo ndani ya idadi ya watu wanaochanga damu na inaweza kuenezwa kwa damu. Watu wana haki ya kutaka kujua, ‘Uchunguzi wa benki ya damu kwa ajili ya vairasi hizo nyingine una mafanikio kadiri gani?’
Kwa kweli, ni kupita tu kwa wakati kutakakoonyesha ni vairasi ngapi zenye kubebwa na damu zinazootea katika akiba ya damu. “Yasiyojulikana huenda yakawa sababu zaidi ya hangaiko kuliko yanayojulikana,” aandika Dakt. Harold T. Meryman. “Vairasi zenye kupitishika ambazo nyakati za tangu kuambukia hadi kutambulika zapimwa kwa miaka mingi zitakuwa vigumu kushirikishwa na utiaji-damu mishipani na hata vigumu zaidi kugunduliwa. Kile kikundi cha HTLV hakika ndicho cha kwanza tu kutokea cha hizo.” (Transfusion Medicine Reviews, Julai 1989) “Kana kwamba ugonjwa wa UKIMWI wenye kuenea pote si balaa la kutosha, . . . hatari kadhaa za utiaji-damu mishipani zilizodokezwa au kuaridhiwa karibuni zimevuta uangalifu wakati wa miaka ya 1980. Haihitaji kuwaza sana kubashiri kwamba kuna magonjwa mengine hatari yenye vairasi nayo yapitishwa na utiwaji-damu mishipani wa asili ile ile moja.”—Limiting Homologous Exposure: Alternative Strategies, 1989.
“Viatu” vingi sana vimegonga tayari hivi kwamba Vitovu vya Udhibiti wa Magonjwa hupendekeza kuwe na “hadhari ya kotekote.” Yaani, ‘wafanya kazi wa afya wapaswa kudhania kwamba wagonjwa wote wanaambukiza HIV na vileta magonjwa vingine vinavyobebwa na damu.’ Kukiwa na sababu nzuri, wafanya kazi wa afya na washiriki wa umma wanakadiria upya maoni yao juu ya damu.
[Maelezo ya Chini]
a Hatuwezi kudhania kwamba damu yote inachunguzwa bado. Kama kielelezo, inaripotiwa kwamba kufikia mwanzo wa 1989, asilimia yapata 80 ya benki za damu za Brazili hazikuwa chini ya udhibiti wa serikali, wala hazikuwa zikichunguza damu kwa ajili ya UKIMWI.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
‘‘Karibu 1 katika [visa] 100 vya utiaji-damu mishipani huambatana na homa yenye joto, homa zenye baridi, au ugonjwa wa ngozi wenye vipele na mwasho. . . . Karibu 1 katika visa 6,000 vya kutiwa chembe nyekundu mishipani hutokeza uharibifu wa chembe nyekundu. Hilo ni tokeo hatari kwenye kinga dhidi ya maambukizo ambalo huenda likatukia mara hiyo au kwa mtindo wa kukawizwa siku kadhaa baada ya kutiwa chembe mishipani; huenda likatokeza mara hiyo kushindwa kwa [figo] kufanya kazi, mshtuko, kuganda kwa damu ndani ya mishipa, na hata kifo.”—Kongamano la Taasisi za Afya ya Taifa (NIH), 1988.
[Sanduku katika ukurasa wa 9]
Niels Jerne mwanasayansi Mdenmarki alishiriki Zawadi ya Nobeli ya Utibabu ya 1984. Alipoulizwa kwa nini alikataa kutiwa damu mishipani, yeye alisema: “Damu ya mtu ni kama alama za vidole vyake—hakuna namna mbili za damu zinazofanana kabisa.”
[Sanduku katika ukurasa wa 10]
DAMU, MAINI YALIYOHARIBIWA, NA . . .
“Ukweli ulio kinyume ni kwamba, UKIMWI wenye kubebwa na damu . . . haujapata kamwe kuwa tisho kubwa kama magonjwa mengine—kwa kielelezo, mchochota wa ini,” likaeleza Washington Post.
Ndiyo, idadi kubwa sana wamekuwa wagonjwa sana na wakafa kutokana na huo mchochota wa ini, ambao hauna utibabu hususa. Kulingana na U.S.News & World Report (Mei 1, 1989), karibu asilimia 5 ya wale wanaopewa damu katika United States hupata mchochota wa ini—watu 175,000 kila mwaka. Karibu nusu wanakuwa wabebaji wenye kusedeka, na angalau 1 kati ya 5 husitawisha cirrhosis au kansa ya ini. Inakadiriwa kwamba 4,000 hufa. Ebu wazia juu ya vichwa vikuu vya habari ambavyo ungesoma ikiwa ndege jumbo-jeti ingeanguka, ikiua wote waliomo. Lakini vifo 4,000 hujumlika kuwa jumbo-jeti moja iliyojaa watu ikianguka kila mwezi!
Kwa muda mrefu matabibu walijua kwamba mchochota wa ini usio mkali (aina ya A) ulienezwa kupitia chakula kisicho safi au maji yasiyo safi. Kisha wakaona kwamba namna nyingine hatari zaidi ilikuwa inaenezwa kupitia damu, hawakuwa na njia ya kuchunguza damu ili kuipata. Hatimaye Wanasayansi wenye akili sana walijifunza jinsi ya kutambua alama za vairasi hii (aina ya B). Kufikia miaka ya mapema ya 1970, damu ilikuwa ikichunguzwa katika mabara fulani. Akiba ya damu ilionekana kuwa salama nao wakati ujao wa damu ulionekana kuwa mwangavu! Au je! ulikuwa hivyo?
Kabla ya muda mrefu kupita ilikuwa wazi kwamba maelfu waliopewa damu iliyochunguzwa bado walisitawisha mchochota wa ini. Wengi, baada ya ugonjwa wenye kudhoofisha walipata habari kwamba maini yao yameharibiwa. Lakini ikiwa damu ilikuwa imechunguzwa, kwa nini jambo hilo lilikuwa likitukia? Damu ile ilikuwa na namna nyingine, iitwayo mchochota wa ini Non-A, Non-B (NANB). Kwa mwongo mmoja, ilisumbua utiaji-damu mishipani—asilimia kati ya 8 na 17 ya wale waliotiwa damu mishipani katika Israeli, Italia, Japani, Hispania, Swedeni na United States waliambukizwa ugonjwa huo.
Ndipo kukaja vichwa vikuu vya habari kama vile “Vairasi Yenye Fumbo ya Mchochota wa Ini Usio wa A, Usio wa B Imetambuliwa Hatimaye”; “Kuvunja Homa Katika Damu.” Tena, ujumbe ukawa, ‘Kile kisababishi chenye kuepa chapatikana!’ Katika Aprili 1989, umma uliambiwa kwamba uchunguzi unapatika kwa ajili ya NANB, unaoitwa sasa mchochota wa ini C.
Huenda ukataka kujua kama kitulizo hicho kilitolewa mapema mno. Kwa kweli, watafiti Waitalia wameripoti vairasi nyingine ya mchochota wa ini, yenye kigeugeu, ambayo huenda ikawa ndiyo inayosababisha theluthi ya visa hivyo. “Baadhi ya wenye mamlaka,” likaonelea jarida Harvard Medical School Health Letter (Novemba 1989) “wana wasiwasi kwamba A, B, C, na D si ndizo alfabeti zote za vairasi ya mchochota wa ini; nyingine bado huenda zikaibuka.” The New York Times (Februari 13, 1990) lilitaarifu hivi: “Wataalamu wanashuku sana kwamba vairasi nyinginezo zaweza kusababisha mchochota wa ini; zikigunduliwa, zitaitwa mchochota wa ini E na kadhalika.”
Je! benki za damu zinakabiliwa na mitafuto-tafuto mirefu zaidi kwa ajili ya michunguzo ili kufanya damu iwe salama? Akitaja tatizo la gharama, mwelekezi wa Msalaba Mwekundu wa America alitoa elezo hili lenye kufadhaisha: “Sisi hatuwezi kuendelea tu kuongeza uchunguzi baada ya uchunguzi kwa kila kisababishi chenye kuambukiza kinachoweza kuenezwa.”—Medical World News, Mei 8, 1989.
Hata uchunguzi wa mchochota wa ini B ni wenye kosa; bado wengi huupata kutokana na damu. Zaidi ya hilo, je! watu watatosheka kwa uchunguzi uliotangazwa wa mchochota wa ini C? Jarida The Journal of the American Medical Association (Januari 5, 1990) lilionyesha kwamba mwaka waweza kupita kabla vizuia-bakteria vya ugonjwa huo havijagunduliwa na uchunguzi. Kwa wakati uliopo, watu waliotiwa damu mishipani huenda wakakabili maini yaliyoharibiwa—na kifo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]
Ugonjwa wa Chagas hutoa kielezi cha jinsi damu inavyopeleka ugonjwa kwa watu walio sehemu za mbali. Jarida “The Medical Post” (Januari 16, 1990) laripoti kwamba ‘watu milioni 10-12 katika Latini Amerika wana maambukizo yenye kusedeka.’ Imepata kuitwa “mojapo hatari za maana sana za utiaji-damu mishipani katika Amerika Kusini.” “Kunguni mwenye kuua” huuma usoni jeruhi anayelala, hunyonya damu, na kunya juu ya kidonda hicho. Huenda jeruhi huyo akabeba ugonjwa wa Chagas kwa miaka kadhaa (huku yawezekana akichanga damu) kabla ya kusitawisha matatizo ya moyo yenye kuua.
Kwa nini hilo lihangaishe watu walio katika kontinenti za mbali? Katika “The New York Times” (Mei 23, 1989), Dakt. L. K. Altman aliripoti juu ya wagonjwa waliokuwa na ugonjwa wa Chagas baada ya kutiwa damu mishipani, ambao mmoja wao alikufa. Altman aliandika: “Huenda visa zaidi vikawa vilipita bila kugunduliwa kwa sababu [madaktari hapa] hawaujui sana ugonjwa wa Chagas, wala hawang’amui kwamba unaweza kuenezwa kwa utiaji-damu mishipani.” Ndiyo, damu inaweza kuwa kichukuzi ambacho kwacho magonjwa husafiria kwa mapana.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Dakt. Knud Lund-Olesen aliandika: “Kwa kuwa . . . watu fulani walio katika vikundi hatari sana hujitolea kuwa wachanganji-damu kwa sababu wakati huo wanachunguzwa kidesturi kwa ajili ya UKIMWI, mimi nahisi kwamba kuna sababu ya kutokuwa na nia ya kuruhusu kutiwa damu mishipani. Mashahidi wa Yehova wamekataa hilo kwa miaka mingi. Je! walitazama ndani ya wakati ujao?”—“Ugeskrift for Læger” (Doctors’ Weekly), Septemba 26, 1988.
[Picha katika ukurasa wa 9]
Papa alipigwa risasi akanusurika. Baada ya kuondoka hospitalini, alirudishwa kwa muda wa miezi miwili, “akiwa anataabika sana.” Kwa nini? Kwa sababu ya ambukizo linaloweza kuleta kifo la saitomegalovairasi kutoka damu aliyopokea
[Hisani]
UPI/Bettmann Newsphotos
Vairasi ya UKIMWI
[Hisani]
CDC, Atlanta, Ga.