Kitabu Cha Biblia Namba 17—Esta
Mwandikaji: Mordekai
Mahali Kilipoandikiwa: Shushani, Elamu
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 475 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: 493–c. (karibu) 475 K.W.K.
1. Ni hadithi gani inayofunuliwa katika kitabu cha Esta?
IKIELEZWA kwa wepesi, hii ni hadithi ya Ahasuero, mfalme wa Uajemi, ambaye hudhaniwa na wengine kuwa Shasta 1, ambaye mahali pa mke wake Vashti asiye mtiifu pachukuliwa na Esta Myahudi wa kike, binamu ya Mordekai. Hamani Mwagagi atunga hila ya kuua Mordekai na Wayahudi wote, lakini atundikwa juu ya mti wake mwenyewe, huku Mordekai akipanda ngazi kuwa waziri mkuu na Wayahudi waokolewa.
2. (a) Ni kwa nini wengine wametilia shaka kupuliziwa na Mungu kwa kitabu cha Esta? (b) Jina la Mungu laonekana latumiwa kwa namna gani katika kitabu cha Esta?
2 Bila shaka, kuna wale watakao kusema kwamba kitabu cha Esta hakikupuliziwa na Mungu wala hakina mafaa bali ni hadithi tu ya kimapokezi yenye kupendeza. Msingi wa dai lao ni kukosekana kwa jina la Mungu. Ingawa ni kweli kwamba Mungu hatajwi moja kwa moja, katika maandishi ya Kiebrania kwaonekana visa vinne tofauti vya herufi za Tetragramatoni, zile herufi za kwanza za maneno manne mfululizo, yakiendeleza YHWH (Kiebrania, יהוה), au Yehova. Herufi hizo za kwanza zaonekana kwa umaarufu katika angalau hati tatu za Kiebrania za kale na pia zimeonyeshwa katika Masora kwa herufi nyekundu. Pia, kwenye Esta 7:5 yaelekea kuna herufi za tangazo la kimungu “mimi nitajithibitisha kuwa.”—Ona vielezi-chini (NW) juu ya Esta 1:20; 5:4, 13; 7:7, na pia 7:5.
3. Ni matukio gani yanayoonyesha imani katika Mungu na sala kwake, na ni matukio gani yanayodokeza uongozaji wa Mungu wa mambo?
3 Katika maandishi yote ni wazi sana kwamba Mordekai alikubali na kutii sheria ya Mungu. Alikataa kusujudia aheshimu binadamu ambaye yaelekea alikuwa Mwamaleki; Mungu alikuwa amewatia alama Waamaleki waangamizwe. (Esta 3:1, 5; Kum. 25:19; 1 Sam. 15:3) Usemi wa Mordekai kwenye Esta 4:14 waonyesha kwamba yeye alitazamia wokovu kutoka kwa Yehova na kwamba alikuwa na imani katika mwelekezo wa kimungu wa mwendo wote wa matukio. Kufunga kwa Esta, pamoja na kitendo kama hicho cha Wayahudi wale wengine, kwa siku tatu kabla hajaingia kwa mfalme chaonyesha kutegemea Mungu. (Esta 4:16) Pia, uelekezaji wa Mungu wa matukio wadokezwa na kupata kwa Esta kibali machoni pa Hegai, mtunzaji wanawake, na mfalme kukosa usingizi usiku ule alioitisha maandishi rasmi akakuta kumbe Mordekai hakuwa ameheshimiwa kwa ajili ya kitendo chake kizuri cha wakati uliopita. (Esta 2:8, 9; 6:1-3; linganisha Mithali 21:1.) Hakuna shaka kuna mrejezo wa sala katika maneno, “kwa habari ya kufunga na kilio.”—Esta 9:31.
4. Kitabu cha Esta chathibitishwaje kuwa asilia na cha kweli?
4 Mambo mengi ya hakika huthibitisha maandishi hayo kuwa asilia na ya kikweli. Kilikubaliwa na watu wa Kiyahudi, ambao kwa wepesi waliita kitabu hicho Meghil·lahʹ, maana yake “kunjo; hati-kunjo.” Chaonekana kilitiwa na Ezra ndani ya vitabu vya Kiebrania vilivyokubaliwa, ambaye bila shaka angekikataa kuwa hekaya. Mpaka leo, Wayahudi huadhimisha sikukuu ya Purimu, au Kura, katika kusherehekea ukombozi mkubwa huo katika wakati wa Esta. Kitabu hicho chaeleza adabu na desturi za Kiajemi kwa njia ya kimaisha na kwa kupatana na kweli zijulikanazo za historia na vitu vilivyovumbuliwa vya kiakiolojia (kwa kuchimbuliwa). Kwa kielelezo, kitabu cha Esta chaeleza kwa usahihi jinsi Waajemi walivyoheshimu mtu. (6:8) Machimbuzi ya kiakiolojia yamefunua kwamba maelezo ya jumba la mfalme kama yanavyotolewa katika kitabu cha Esta yanapatana hata katika jambo lililo dogo zaidi.—5:1, 2.a
5. Ni ukamili gani unaolipa simulizi la Esta uhalisi, na lugha yapatana na kipindi gani?
5 Usawasawa huo waonekana pia katika simulizi lenyewe, katika kutaja kwa uangalifu maofisa wa baraza na watumishi, hata kutaja majina ya wana kumi wa Hamani. Ukoo wa Mordekai na Esta wafuatishwa kurudi nyuma hadi kwa Kishi wa kabila la Benyamini. (2:5-7) Marejezo yamefanywa kwa maandishi rasmi ya serikali ya Kiajemi. (2:23; 6:1; 10:2) Lugha ya kitabu hicho ni Kiebrania cha baadaye, pamoja na kuongezwa kwa maneno na semi nyingi za Kiajemi na Kiaramu, mitindo ambayo yafanana na ile ya Mambo ya Nyakati, Ezra, na Nehemia, hivyo kupatana kabisa na kipindi ambacho kiliandikwa.
6. (a) Ni kipindi gani cha wakati kinachoonyeshwa kwa kitabu cha Esta? (b) Ushuhuda wadokeza nini juu ya mwandikaji, na pia mahali na wakati wa kuandika?
6 Hudhaniwa kwamba matukio ya Esta ni ya siku zile ambazo milki hodari ya Kiajemi ilikuwa imefikia kilele chake na yanahusisha karibu miaka 18 ya utawala wa Ahasuero (Shasta 1). Kipindi hicho cha wakati, kinachofikia karibu 475 K.W.K., chaonyeshwa na ushuhuda kutoka vyanzo vya Kigiriki, Kiajemi, na Kibabuloni.b Mordekai, shahidi aliyejionea na mhusika mkuu katika simulizi hilo, yaelekea sana alikuwa ndiye mwandikaji wa kitabu hicho; simulizi hilo la kindani na lenye kutia mengi laonyesha kwamba mwandikaji lazima awe aliishi katikati ya matukio hayo katika Shushani jumba la mfalme.c Ingawa hatajwi katika kitabu chochote cha Biblia, hakuna shaka kwamba Mordekai alikuwa mtu halisi wa historia. La kupendeza ni kwamba maandishi-kabari yasiyoonyeshwa tarehe yamepatikana ambayo yaelezwa na A. Ungnad wa Ujerumani kuwa yakirejezea Mardukâ (Mordekai?) kuwa ofisa mkuu kwenye baraza la Susa (Shushani) wakati wa utawala wa Shasta 1.d Ni huko Shushani ambako Mordekai bila shaka alikamilisha maandishi ya matukio ya Esta bila kukawia baada ya kutukia kwayo, yaani, karibu 475 K.W.K.
YALIYOMO KATIKA ESTA
7. Ni hali gani ya hatari inayotokea kwenye karamu ya Ahasuero, na ni hatua gani anayochukua mfalme kwa sababu hiyo?
7 Malkia Vashti aondolewa (1:1-22). Ni mwaka wa tatu wa utawala wa Ahasuero. Afanya karamu kubwa kwa ajili ya maofisa wa milki yake, akiwaonyesha utajiri na utukufu wa ufalme wake kwa siku 180. Kisha, kuna sikukuu tukufu ya siku saba kwa watu wote katika Shushani. Wakati uo huo, Vashti malkia afanya karamu kwa ajili ya wanawake. Mfalme ajivunia utajiri na utukufu wake na, akichangamshwa na divai, aita Vashti aje aonyeshe uzuri wake kwa watu na wakuu. Malkia Vashti azidi kukataa. Kwa kushauriwa na maofisa wa baraza, wanaotaja kwamba kielelezo hicho kibaya huenda kikasababisha mfalme apoteze heshima yake katika milki yote, Ahasuero amwondoa Vashti asiwe malkia na achapisha hati zenye kutoa wito kwa wake wote ‘wawaheshimu waume zao’ na kila mume ‘atawale nyumbani mwake.’—1:20, 22.
8. (a) Ni matukio gani yanayoongoza kwenye Esta kuwa malkia? (b) Ni hila gani anayofunua Mordekai, na ni maandishi gani yanayofanywa kuhusu hilo?
8 Esta awa malkia (2:1-23). Baadaye, mfalme aweka makamishna watafute mabikira warembo zaidi katika mikoa yote 127 ya milki yake na kuwaleta Shushani, ambako watatayarishwa kwa kurembwa ili waletwe kwa mfalme. Kati ya wanawake vijana wanaochaguliwa ni Esta. Esta ni yatima wa Kiyahudi, “wa umbo mzuri na uso mwema,” ambaye amelelewa na binamu yake Mordekai, ofisa mmoja katika Shushani. (2:7) Jina la Kiyahudi la Esta, Hadasa, lamaanisha “Mhadasa” (aina fulani ya mti). Hegai, mtunzaji wa wanawake, apendezwa na Esta na amtendea kipekee. Hakuna anayejua yeye ni Myahudi wa kike, kwa maana Mordekai amemwagiza atunze hilo kuwa siri. Wanawake hao wachanga waletwa kwa mfalme kwa zamu. Achagua Esta kuwa malkia wake mpya, na karamu yafanywa ya kusherehekea kutawazwa kwake. Muda mfupi baadaye, Mordekai asikia juu ya njama ya kumwua mfalme, na amwambia Esta amjulishe “kwa jina la Mordekai.” (2:22) Hila hiyo yafichuliwa, wala-njama hao wanyongwa, na maandishi yawekwa katika vitabu vya kifalme.
9. Mordekai amkasirishaje Hamani, na ni amri gani ya kifalme anayopata Hamani juu ya Wayahudi?
9 Njama ya Hamani (3:1–5:14). Karibu miaka minne yapita. Hamani, yaelekea mzao wa mfalme Agagi Mwamaleki ambaye Samweli aliua, awa waziri mkuu. (1 Sam. 15:33) Mfalme amtukuza na kuagiza watumishi wake wote katika lango la mfalme wainame mbele ya Hamani. Hiyo ni kutia na Mordekai. Hata hivyo, Mordekai akataa kufanya hivyo, akijulisha watumishi wa mfalme kuwa yeye ni Myahudi. (Linganisha Kutoka 17:14, 16.) Hamani afoka kwa hasira na, agunduapo kwamba Mordekai ni Myahudi, aona katika hilo nafasi kubwa ya kuwakomesha kabisa Mordekai na Wayahudi wote. Kura (puri) yapigwa ili kuamua siku njema ya kuangamiza Wayahudi. Akitumia kibali chake kwa mfalme, Hamani ashtaki Wayahudi juu ya kukosa kutii sheria na kuuliza kwamba kuharibiwa kwao kuagizwe kwa maandishi. Hamani atoa mchango wa talanta za fedha 10,000 (zalingana na karibu dola 66,060,000) za kugharimia machinjo hayo. Mfalme akubali, na maagizo yaliyoandikwa, yenye muhuri wa pete wa mfalme, yapelekwa katika milki yote, Adari 13 ikiwekwa kuwa siku ya machinjo ya Wayahudi.
10. Mordekai na Esta wachukua hatua gani ya imani katika nguvu za Yehova?
10 Wasikiapo sheria hiyo, Mordekai na Wayahudi wote waingilia kuomboleza katika magunia na majivu. Kuna “kufunga, na kulia, na kuomboleza.” (Esta 4:3) Ajulishwapo na Mordekai juu ya tatizo la Wayahudi, hapo kwanza Esta asita kuwatetea. Kifo ndicho adhabu ya kutokea mbele ya mfalme bila kualikwa. Lakini, Mordekai aonyesha imani yake katika nguvu za Yehova kwa kujulisha rasmi kwamba kama Esta atakosa kuwatetea, bado atakufa na wokovu ‘utawatokea Wayahudi kwa njia nyingine.’ Zaidi ya hayo, je! haiwezekani kwamba Esta amekuwa malkia “kwa ajili ya wakati kama huo”? (4:14) Aonapo suala hilo, Esta akubali kuhatarisha uhai wake, na Wayahudi wote katika Shushani wafunga pamoja naye kwa siku tatu.
11. Esta atumiaje kibali chake kwa mfalme, lakini Hamani amfanyia Mordekai hila gani?
11 Kisha, akiwa amevaa mavazi bora kabisa ya kifalme, Esta ajitokeza mbele ya mfalme. Apata kibali machoni pa mfalme, na anyoosha kumwelekea Esta fimbo yake ya dhahabu, akiponyoa maisha yake. Sasa amwalika mfalme na Hamani kwenye karamu. Wakati wa sherehe hiyo, mfalme amsihi atoe ombi lake, akimhakikishia atapewa, “hata nusu ya ufalme,” ndipo Esta anapowaalika hao wawili kwenye karamu nyingine kesho yake. (5:6) Hamani aenda zake mwenye shangwe. Lakini pale kwenye lango la mfalme yuko Mordekai! Kwa mara nyingine akataa kuheshimu Hamani au kutetemeka mbele yake. Shangwe ya Hamani yageuka kuwa kasirani. Mke wake na marafiki wadokeza atengeneze mti wa kimo cha mikono 50 (meta 22.3) na kupata agizo kutoka kwa mfalme aning’inize Mordekai juu yao. Bila kukawia Hamani aamuru mti huo utengenezwe.
12. Ni badiliko gani la matukio linalosababisha Ahasuero amheshimu Mordekai, hivyo kumdunisha Hamani?
12 Mambo yageuka (6:1–7:10). Usiku huo mfalme hawezi kulala. Aagiza kitabu cha maandishi kiletwe asomewe, naye agundua kwamba hajathawabisha Mordekai kwa ajili ya kuokoa uhai wake. Baadaye, mfalme auliza ni nani aliye uani. Ni Hamani, ambaye amekuja kuuliza kibali cha mfalme kwa ajili ya kifo cha Mordekai. Mfalme auliza Hamani ni jinsi gani mtu aliyempendeza mfalme apasa kuheshimiwa. Akidhania mfalme amfikiria yeye, Hamani aeleza juu ya programu ya heshima yenye mapambo mengi. Lakini mfalme amwamuru hivi: “Ukamfanyizie vivyo hivyo Mordekai, Myahudi”! (6:10) Hamani hana jingine la kufanya ila kumvisha Mordekai fahari ya kifalme, kumketisha kwenye farasi wa mfalme, na kumwongoza kuzunguka njia kuu ya mjini, akipaaza sauti mbele yake. Akiwa amedunishwa, Hamani afanya hima kurudi nyumbani akiomboleza. Mke wake na marafiki hawana kitulizo. Hamani amekusudiwa kuangamia!
13. Esta afunua nini kwenye karamu hiyo, ikiongoza kwenye afa gani kwa Hamani?
13 Sasa ni wakati wa Hamani kuhudhuria karamu pamoja na mfalme na Esta. Malkia ajulisha rasmi kwamba yeye na watu wake wameuzwa, waangamizwe. Ni nani aliyethubutu kutokeza uovu huo? Esta asema: “Ni mtesi, tena ni adui, ndiye huyu Hamani, mtu mbaya kabisa.” (7:6) Mfalme ainuka kwa hamaki na kutembea nje kwenye bustani. Akiwa peke yake na malkia, Hamani amsihi kwa ajili ya uhai wake, na mfalme, arejeapo, aghadhibika zaidi aonapo Hamani juu ya kitanda cha malkia. Mara moja aagiza kwamba Hamani atundikwe juu ya mti ule ule ambao Hamani alikuwa ametayarisha kwa ajili ya Mordekai!—Zab. 7:16.
14. Mfalme athawabishaje Esta na Mordekai, na apendelea Wayahudi kwa amri gani iliyoandikwa?
14 Mordekai apandishwa cheo, Wayahudi waokolewa (8:1–10:3). Mfalme ampa Esta mali zote za Hamani. Esta ajulisha Ahasuero uhusiano wake na Mordekai, ambaye mfalme apandisha kwenye cheo cha awali cha Hamani, akimpa pete yake ya kifalme yenye muhuri. Kwa mara nyingine, Esta ahatarisha uhai wake kwa kwenda mbele ya mfalme akaombe amri iliyoandikwa ya kuangamiza Wayahudi wote itanguliwe (iondolewe). Hata hivyo, “sheria za Waajemi na Wamedi” haziwezi kutanguliwa! (1:19) Kwa hiyo mfalme apatia Esta na Mordekai mamlaka ya kuandika sheria mpya na kuitia muhuri kwa pete ya mfalme. Agizo hilo lililoandikwa, lapelekwa katika milki yote kwa njia ile ile kama lile la awali, lakabidhi Wayahudi haki ya ‘kujikusanya na kusimamia maisha zao, kuangamiza na kuua na kulifisha jeshi lote la watu na la jimbo watakaowaondokea, wao na wadogo wao na wanawake; na kuyachukua mali yao kuwa nyara,’ siku ile ile ambayo sheria ya Hamani yaanza kufanya kazi.—8:11.
15. (a) Ni nini tokeo la pigano hilo, na ni karamu gani anayoanzisha Mordekai? (b) Mordekai apandishwa kwenye cheo gani, naye atumia mamlaka yake kwa kusudi gani?
15 Siku iliyowekwa, Adari tarehe 13, iwadiapo, hakuna binadamu awezaye kusimama mbele ya Wayahudi. Esta aombapo mfalme, pigano laendelea kwenye siku ya 14 katika Shushani. Kwa ujumla, 75,000 ya maadui wa Wayahudi wauawa katika milki yote. Wengine 810 wauawa katika buruji la Shushani. Kati yao ni wana kumi wa Hamani, wanaouawa siku ya kwanza na kuning’inizwa kwenye miti siku ya pili. Hakuna nyara zinazotwaliwa. Mnamo tarehe 15 ya Adari, kuna pumziko, na Wayahudi wala karamu na kushangilia. Sasa Mordekai atoa maagizo yaliyoandikwa kwa Wayahudi waadhimishe sikukuu hii ya “Puri, yaani kura,” kila mwaka mnamo tarehe 14 na 15 za Adari, na hilo wafanya hadi wa leo. (9:24) Mordekai aadhimishwa katika ufalme na kutumia cheo chake akiwa wa pili kwa Mfalme Ahasuero ‘akiwatafutia watu wake wema, na kuiangalia hali njema ya wazao wao wote.’—10:3.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
16. Wakristo wanapata katika kitabu cha Esta kanuni gani za kimungu na kigezo gani kinachostahili?
16 Ingawa hakuna mwandikaji mwingine yeyote anayenukuu lolote kutoka Esta kwa njia ya moja kwa moja, kitabu hicho chapatana kabisa na Maandiko yale mengine yaliyopuliziwa na Mungu. Kwa kweli, chatoa mifano fulani mizuri ya kanuni za Biblia zinazotajwa baadaye katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo na zinazotumika kwa waabudu wa Yehova katika vizazi vyote. Uchunguzi wa vifungu vifuatavyo utaonyesha hilo kuwa hivyo na pia utajenga imani ya Kikristo: Esta 4:5—Wafilipi 2:4; Esta 9:22—Wagalatia 2:10. Shtaka lililofanyiwa Wayahudi, kwamba hawakutii sheria za mfalme, lafanana na shtaka lililotokezwa kuwahusu Wakristo wa kwanza. (Esta 3:8, 9; Mdo. 16:21; 25:7) Watumishi wa kweli wa Yehova hukabiliana na mashtaka hayo bila hofu na kwa kutegemea kwa sala nguvu za kimungu za kuokoa, kufuatia kigezo kizuri cha Mordekai, Esta, na Wayahudi wenzao.—Esta 4:16; 5:1, 2; 7:3-6; 8:3-6; 9:1, 2.
17. Mordekai na Esta walielelezaje mwendo unaofaa katika kujitiisha wenyewe kwa Mungu na kwa “mamlaka iliyo kuu”?
17 Tukiwa Wakristo, hatupaswi kufikiri kwamba hali yetu ni tofauti na ile ya Mordekai na Esta. Sisi pia twaishi chini ya “mamlaka iliyo kuu” katika ulimwengu mgeni. Ni tamaa yetu kuwa raia wenye kutii sheria katika nchi yoyote tunayokaa, lakini wakati uo huo, twataka kutofautisha kwa usahihi kati ya ‘kulipa Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu.’ (Rum. 13:1; Luka 20:25) Waziri Mkuu Mordekai na Malkia Esta waliweka vielelezo vizuri vya ujitoaji na utii katika wajibu wao kwa nchi. (Esta 2:21-23; 6:2, 3, 10; 8:1, 2; 10:2) Hata hivyo, bila hofu Mordekai alitofautisha kati ya kutii amri ya kifalme ya kusujudu mbele ya Hamani, Mwagagi mwenye kuchukiza. Zaidi ya hayo, alihakikisha kwamba rufani ya kutafuta rekebisho la kisheria ilikatwa wakati Hamani alipofanya njama ya kuangamiza Wayahudi.—3:1-4; 5:9; 4:6-8.
18. (a) Ni nini kinachothibitisha kitabu cha Esta kuwa ‘kilichopuliziwa na Mungu na chenye mafaa’? (b) Kinatiaje moyo uteteaji wa faida za Ufalme wa Mungu?
18 Ushuhuda wote waonyesha kitabu cha Esta kuwa sehemu ya Biblia Takatifu, ‘yenye pumzi ya Mungu na yenye mafaa.’ Hata bila ya kutaja Mungu au jina lake moja kwa moja, kinatoa vielelezo bora vya imani. Mordekai na Esta hawakubuniwa tu na msimuliaji hadithi fulani, bali wao walikuwa watumishi halisi wa Yehova Mungu, watu walioweka uhakika kamili katika nguvu za Yehova za kuokoa. Ingawa wao waliishi chini ya “mamlaka iliyo kuu” katika bara la kigeni, walitumia kila njia ya kisheria ili kutetea faida za watu wa Mungu na ibada yao. Sisi leo twaweza kufuata vielelezo vyao katika ‘kutetea na kuthibitisha kisheria habari njema’ za Ufalme wa Mungu wa wokovu.—Flp. 1:7, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Vo. 1, page 764; Vol. 2, pages 327-31.
b Insight on the Scriptures, Vol. 2. pages 613-16.
c Cyclopedia ya McClintock na Strong, chapa-mrudio 1981, Buku III, ukurasa 310.
d A. Ungnad, “Keilinschriftliche Beiträge zum Buch Esra und Ester,” Zeitschrift für die alttestamentliche Wissenschaft, LVIII (1940-41), kurasa 240-4.