Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 9/15 kur. 14-19
  • Yehova Hawaachi Watu Wake

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Yehova Hawaachi Watu Wake
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • KUTENDA KWA KUMTUMAINI YEHOVA
  • MKONO WA YEHOVA WAONEKANA
  • KUTAMBULISHWA KWA UHODARI NA KUFUNULIWA KWA UJASIRI
  • BADILILO KUTOKA KWENYE DHIKI KUINGIA WENYE FURAHA
  • YEHOVA AWATEGEMEZA WATU WAKE
  • YEHOVA AWAKOMBOA WENYE HAKI
  • Kitabu Cha Biblia Namba 17—Esta
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Alitenda kwa Hekima, Ujasiri, na Bila Ubinafsi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Taifa Laokolewa na Mungu Lisiangamizwe
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Esta
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2006
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 9/15 kur. 14-19

Yehova Hawaachi Watu Wake

“[Yehova] hatawatupa watu wake, wala hatauacha urithi wake.”​​—⁠Zab. 94:14.

1, 2. Nabii Samweli pamoja na mtunga zaburi walisemaje juu ya uhusiano wa Yehova na watu wake?

“(YEHOVA) hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu.” Ndivyo alivyokuwa amesema nabii Samweli. Vivyo hivyo, mtunga zaburi alitangaza kwamba: “Yehova hatawatupa watu wake, wala hatauacha urithi wake.”​​—⁠1 Sam. 12:22; Zab. 94:14.

2 Je! wewe mwenyewe unayatumaini maneno hayo? Je! Esta, Mordekai pamoja na Wayahudi wa siku zao wangeweza kuwa na hakika kwamba Yehova hatawaacha watu wake? Tutaona.

KUTENDA KWA KUMTUMAINI YEHOVA

3. (a) Kulitukiaje Esta alipokwenda mbele ya Mfalme Ahasuero bila kualikwa? (b) Ni nini ombi la Esta?

3 Sasa ni siku ya tatu tangu Wayahudi wenye dhiki walioko katika Milki ya Uajemi walipoanza kufunga na kumwomba Yehova. Kwa uhodari, Malkia Esta asiye mchoyo amejivika vazi la kifalme na, bila kualikwa, asimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme. Akiwa katika kiti chake cha enzi, Mfalme Ahasuero amwona malkia wake. Je! anahukumiwa kuangamizwa? Hapana. Amnyoshea fimbo yake ya dhahabu naye anakaribia, na kugusa ncha ya fimbo. Esta amepata kibali ya mfalme na kumsikia akiuliza: “Malkia Esta, wataka nini? nayo ni haja gani uliyo nayo? utapewa hata nusu ya ufalme.” Kwa kuitikia, yeye amwalika Mfalme Ahasuero pamoja na Waziri mkuu Hamani kwa karamu, nao mwaliko wake wa ukarimu unakubaliwa.​​—⁠Esta 5:1-5.

4. Baada ya karamu ya Esta, ni jambo gani ambalo limeharibu furaha ya Hamani?

4 Baadaye siku iyo hiyo, mfalme Mwajemi pamoja na Hamani Mwagagi wahudhuria karamu ya divai ya Esta. Baada ya muda, mfalme amwuliza Esta: “Dua yako ni nini?” Katika kujibu, yeye amwalika Ahasuero na Hamani kwa karamu siku ifuatayo. Wakati wa kuondoka, Hamani ni mwenye furaha. Walakini wakati Myahudi Mordekai mwenye kushika ukamilifu anapokataa kutetema kwa sababu yake, Mwagagi huyo ajawa na hasira, ijapokuwa anajizuia. Baada ya kuingia nyumbani kwake mwenyewe, Hamani amwita mkewe pamoja na rafiki zake. Hawezi kujizuia bali ajisifu na kuwaambia namna ambavyo Ahasuero amemtukuza juu zaidi ya wakuu wengine wote pamoja na watumishi wa mfalme.​​—⁠Esta 5:6-11.

5. Mkewe Hamani pamoja na rafiki zake wapendekeza kwamba Hamani afanye nini juu ya Mordekai?

5 “Zaidi ya hayo,” aendelea Hamani, “naye malkia Esta hakumkaribisha mtu ye yote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme.” Hata hivyo, jambo moja lamsumbua sana Mwagagi mwenye kujisifu, kwa kuwa anaongeza hivi: “Bali haya yote yanifaa nini, pindi nimwonapo yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme?” Zareshi mke wa Hamani pamoja na rafiki zake wana hakika kwamba wana jawabu. “Na ufanyizwe mti wa mikono hamsini urefu wake,” wakasema. “Na kesho useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa kicheko pamoja na mfalme karamuni.” Ebu wazia! maiti ya Mordekai ikining’inia juu ya mti wenye urefu wa mikono 50 (futi 73 au metres 22)! ‘Vema!’ afikiri Hamani mwenye kiburi, naye aufanyiza mti huo.​​—⁠Esta 5:12-14.

6. Kama vile Mordekai na Esta, Wakristo watiwa mafuta leo waonyesha nia gani?

6 Tungojeapo matukio ya siku ya pili, tunakuwa na wakati wa kutafakari juu ya mwendo wa Mordekai na Esta. Wote wawili walimtumaini Yehova na kutafuta uongozi wake. Kwa sababu ya kuwapenda watu wa Yehova, Esta hata alihatirisha maisha yake, akienda kwa uhodari mbele ya mfalme bila kualikwa. Vivyo hivyo, Wakristo watiwa mafuta wa leo wanaonyesha upendo kwa watu wote wa Mungu, kama Mordekai na Esta. Na wajapoteswa na wapinzani wa kidini, watumishi wa kisasa wa Mungu wanatenda kwa kumtumaini kabisa.

MKONO WA YEHOVA WAONEKANA

7. Yehova anaweza kufaaya nini na wenye mamlaka ya kiserikali ili atimize kusudi lake?.

7 Yehova anapochagua kufanya hivyo, yeye aweza kuwaongoza wenye mamlaka katika serikali ili atimize kusudi lake. Kwa kufaa basi, mithali yenye kuongozwa na roho yasema hivi: “Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa [Yehova]; kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo.” (Mit. 21:1; Dan. 2:21) Ebu angalia sasa namna mkono wa Aliye Juu Zaidi ulivyoonekana wazi zaidi katika siku za Mordekai na Esta.

8. Ni jambo gani latukia pindi moja wakati Ahasuero anakosa usingizi?

8 Ahasuero ameshindwa kupata usingizi usiku uliotangulia karamu yake ya pili, inaelekea sababu ni kwamba mkono wa Yehova unafanya kazi. Labda akifikiri kwamba amekosa katika njia fulani, mfalme aagiza asomewe kitabu cha maandishi ya kifalme. Mwishowe, asikia ripoti juu ya ushikamanifu wa Mordekai alipoufunua uhaini wa kumwua mfalme wa watumishi wawili waliomhudumia mfalme, Bigthani na Tereshi. Walakini mfalme ajifunza kwamba tendo hili halikuthawabishwa. Kwa hiyo mfalme huyo Mwajemi aazimia kwamba lazima Mordekai aonyeshwe heshima.​​—⁠Esta 6:1-3.

9. Akifikiri kwamba yeye mwenyewe ndiye ataheshimiwa, ni sherehe gani yenye mapambo mengi ambayo Hamani amependekeza?

9 Mapema asubuhi inayofuata, Hamani mwenye hila apewa ruhusa ya kuingia mbele ya Mfalme Ahasuero. Lakini kabla Mwagagi huyu hajatimiza hila yake yenye kuua juu ya Mordekai, mfalme auliza hivi: “Afanyiwe nini yule ambaye mfalme apenda kumheshimu?” Hamani asema moyoni mwake: “Ni nani ambaye mfalme aweza kumheshimu kuliko mimi?” Ndipo anasema hivi: ‘Aletwe farasi wa mfalme ambaye ametiwa taji ya kifalme. (Farasi wa kawaida tu hamtoshi Hamani mwenye kiburi!) Mtu yule na avikwe vazi la kifalme ambalo mfalme mwenyewe amezoea kulivaa. Kisha, mtu yule ampande yule farasi kuipitia njia kuu ya mjini, na kupiga mbiu mbele yake, na kusema: “Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu.” Esta 6:4-9.

10. (a) Ni pigo gani lenye kuvunja moyo linalompata Hamani? (b) Baada ya sherehe ya kumheshimu Mordekai, je! Hamani anapata faraja yo yote kutoka kwa mkewe na rafiki zake?

10 “Haraka,” asema Ahasuero, “twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, na fanyia hivi Modekayi Muyuda anayeketi langoni mwa mufalme; lisipunguzwe neno moja la yote uliyoyasema.” Lo! pigo lenye kuangamiza namna gani kwa Hamani mwenye kiburi! Lakini afanyeje? Kukataa kutii kungemaanisha kifo hakika. Hivyo muda mrefu haukupita kabla Mordekai kumpanda farasi wa mfalme kuipitia njia kuu ya mjini akiwa amevikwa vazi la kifalme huku Hamani aliyeshushwa akisema mbele yake: “Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mutu mufalme anayependezwa kumuheshimu.” Baadaye, Mordekai arudi langoni pa mfalme naye Hamani afanya haraka kwenda nyumbani kwake, akiomboleza na kufunika kichwa chake kwa aibu. Mkewe na rafiki zake hawamfariji, bali wasema: “Kama Mordekai uliyeanza kupunguka mbele yake ni wa uzao wa Wayuda, hutamshinda, lakini hakika utaanguka mbele yake.” Ndiyo, kwa mke wa Mwagagi huyo pamoja na rafiki zake, uhakika wa kwamba alazamika kufanya sherehe ya kumheshimu Mordekai hadharani inaonwa kuwa ishara ya mabaya kwamba Hamani ataanguka mbele ya Myahudi huyu. Hata kabla ya Hamani kumaliza kusikia maneno haya yenye kuogopesha watumishi wanaomhudumia mfalme wafika na kumchukua kwenda katika karamu ya pili ya Esta.​​—⁠Esta 6:10-14, ZSB.

KUTAMBULISHWA KWA UHODARI NA KUFUNULIWA KWA UJASIRI

11, 12. (a) Esta asema nini juu yake na watu wake wakati wa karamu yake ya pili ambayo Ahasuero na Hamani wamehudhuria? (b) Hamani anatendaje anapoonyeshwa kuwa msingiziaji na mhaini, walakini ni kwa sababu gani Esta hamhurumii?

11 Wakati wa karamu, Ahasuero auliza: “Malkia Esta, dua yako ni nini?” Uhodari wahitajiwa ili kujibu, walakini malkia asema: “Mfalme, ikiwa nimepata kibali machoni pako, na mfalme akiona vema, nipewe maisha yangu kuwa dua yangu, na watu wangu kuwa haja yangu. Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; ila hata hivyo msiba wetu haulinganishwi na hasara ya mfalme.”​​—⁠Esta 7:1-4.

12 Ni nini hii? Basi, Malkia Esta ni Myahudi, nao watu wake wameamriwa waangamizwe! Ahasuero ataka kujua ni nani mwenye kufanya hivyo. Kwa uhodari, Esta asema: “Ni mtesi, tena ni adui, ndiye huyu Hamani, mtu mbaya kabisa.” Malkia amefanya ifaavyo kwa kumfunua huyu Mwamaleki ambaye sasa anaogopa sana akiwapo. Kwa uhodari, Esta amemshtaki Hamani kuwa mwenye hatia ya kusingizia vibaya sana naye amemtambulisha kuwa mwenye kufanya hila juu ya faida za mfalme Mwajemi mwenyewe. Kwa kuona hasira sana, mfalme atoka na kuingia katika bustani ya nyumba ya kifalme. Hamani mwenye kuogopa sana, kwa kujua kwamba hawezi kutarajia rehema yo yote kutoka kwa Ahasuero, aanguka juu ya kitanda alichokuwa akikalia Esta. Amsihi sana kwa ajili ya maisha yake. Walakini Esta hamhurumii, kwa kuwa hilo halingempendeza Yehova, ambaye ameamuru kwamba Waamaleki waangamizwe kabisa.​​—⁠Esta 7:5-8.

13. Ni jambo gani linalompata Hamani kwa amri ya Mfalme Ahasuero?

13 Arudipo kutoka bustanini, Ahasuero amwona Hamani mwenye kukata tamaa akiwa penye kitanda alipokuwapo Esta, apaza sauti hivi: “Je! atamfanyia malkia jeuri hata machoni pangu nyumbani mwangu?” Na mara hiyo, mfalme amhukumia huyo Mwagagi mwovu kuuawa. Upesi maiti ya Hamani ikawa ikining’inia juu ya mti ule ule alioufanyiza kwa ajili ya Mordekai Myahudi. Ndipo tu hasira ya mfalme yatulia.​​—⁠Esta 7:8-10.

14. Ni ulinganifu gani wa kisasa unaoweza kufanywa kuhusiana na kujitambulisha kwa Esta kuwa Myahudi na kumfunua Hamani kwa uhodari kuwa adui ya watu wa Mungu?

14 Tuangaliapo nyuma, twaona kwamba, Esta mwenye uhodari hakufunua tu kwamba yeye ni Myahudi, bali pia alimfunua Hamani kuwa adui ya watu wa Mungu. Kwa kulinganisha leo, wale ambao wamekuwa wafuasi watiwa mafuta wa Yesu Kristo tangu Vita ya Pili ya Ulimwengu wamekuwa wakijitambulisha kwa uhodari kuwa Wayahudi wa kiroho pamoja na wale wa zamani, na kwa hiyo, kama mashahidi wa Yehova. (Isa. 43:10-12) Nao bila shaka wana maadui wengi. Kwa mfano, kama vile Hamani, viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wametafuta kuwaangamiza watu wa Yehova. Lakini kwa uhodari Wakristo wa kweli wamewafunua adui hawa wenye chuki ambao hila zao hazitawafikisha po pote kama vile zile za Mwamaleki mbaya Hamani hazikumfikisha po pote. Ndivyo ilivyo kwa sababu watu wa Yehova ambao hunena neno la Mungu kwa uhodari, wana tegemezo la kimungu katika kukabiliana na hila na mateso.​​—⁠Isa. 54:17; Matendo 4:29-31.

BADILILO KUTOKA KWENYE DHIKI KUINGIA WENYE FURAHA

15. Nyumba ya Hamani inafanyiwa nini, naye Mordekai awekwa kwenye cheo gani?

15 Ahasuero ampa Esta nyumba ya Hamani aliyeuawa, kwa kuwa amemjulisha uhusiano wake na Mordekai. Vilevile, mfalme atoa pete yake ambayo ameiondoa kwa Hamani, na kumpa Myahudi huyu mshikamanifu, na kufanya Mordekai waziri mkuu mahali pa Mwagagi huyo. Akitenda kulingana na mamlaka ya amri ambayo amepewa na mfalme, Esta amweka Mordekai juu ya nyumba ya Hamani.​​—⁠Esta 8:1, 2.

16. Akiitikia kusihi kwa Esta, Ahasuero anatoa ruhusa gani kuhusiana na Wayahudi?

16 Akihatirisha maisha yake kwa mara nyingine tena kwa ajili ya watu wake, Esta aenda mbele ya mfalme bila kualikwa na kuanguka miguuni pake huku akilia. Ahasuero amnyoshea fimbo yake ya dhahabu naye Esta ainuka, na kusema: ‘Mfalme akiona vema na ikiwa mimi nimepata kibali machoni pake, acha barua iandikwe ya kuondoa hila ya Hamani. Kwa maana nawezaje kuona mabaya ya watu wangu na kuangamizwa kwa jamaa zangu?’ Kwa kuwa sheria za Wamedi na Waajemi haziwezi kutanguliwa, Ahasuero awapa Esta na Mordekai mamlaka ya kuandika kwa jina lake barua ya kiserikali kwa ajili ya Wayahudi wajipiganie.​​—⁠Esta 1:19; 8:3-8.

17, 18. (a) Mordekai anafanya jambo gani mahali pote katika Milki ya Uajemi kwa ajili ya Wayahudi, nao wapewa haki gani kuhusiana na Adari 13? (b) Wayahudi wanatendaje kwa sababu ya amri ya kujipigania?

17 Kwa hiyo, waziri mkuu aliyewekwa karibuni achukua hatua. Tarehe 23 ya mwezi wa Siwani (Mei-Juni), waandishi wa mfalme waitwa naye Mordekai awaamuru waandike amri Wayahudi wajipiganie. Upesi itawafikia Wayahudi, wale watu wengine pamoja na maafisa wa serikali​—⁠maakida, maliwali wadogo na wakuu​—⁠katika majimbo yote 127 ya utawala wa Uajemi. Mordekai ahalalisha barua hizo kwa kuziweka muhuri kwa pete ya mfalme. Nayo hiyo sheria mpya yasemaje? Mfalme Ahasuero amewapa Wayahudi haki ya kukusanyika na kupigania maisha zao, na kuangamiza wale wanaoonyesha uadui. Ndiyo, wataweza kujipigania tarehe 13 ya mwezi wa Adari (Februari-Machi), siku ambayo hapo kwanza ilikuwa imewekwa kuwa siku ya kuangamizwa kwao! Bila kukawia na wakipanda farasi wepesi wa kupeleka barua, matarishi wawahimiza farasi wao, wakipeleka amri ya Wayahudi wajipiganie katika kila sehemu ya milki hiyo iliyotapakaa.​​—⁠Esta 8:9-14.

18 Waziri mkuu Mordekai atoka mbele ya mfalme huku akivalia vazi la kifalme la rangi ya samawi na nyeupe. Avalia na joho ya kitani safi na rangi ya zambarau pamoja na taji kubwa ya dhahabu kichwani pake. Bila shaka, ana sababu nzuri ya kufurahi kwa sababu ya amri hiyo ya Wayahudi wajipiganie. Kwa kweli, furaha yaenea pote Shushani, na mwishowe Wayahudi washangilia na kufanya karamu na kuwa na siku nzuri mahali pote katika milki hiyo. Zaidi ya hayo, kuwaogopa Wayahudi kumewaangukia watu wote, na wengi wao wanageuka na kufuata Wayahudi.​​—⁠Esta 8:15-17.

19. Kwa kufikiria hila ya Hamani, amri ya kujipigania pamoja na matukio yanayohusiana nayo, je! wewe waona kitia-moyo cho chote kwa Wakristo wa leo?

19 Kufikiria yale ambayo yametendeka kunawatia moyo Wakristo wa siku ya leo. Kama vile Hamani alivyofanya hila kuwaangamiza Wayahudi wa asili, vivyo hivyo viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wametafuta kuwaangamiza Wayahudi wa kiroho, ndugu za kiroho za Kristo. Yesu, akitumia mamlaka ya kifalme juu ya dunia kama alivyofanya Ahasuero juu ya Milki ya Uajemi, ameruhusu majaribio kama hayo, walakini vilevile, amewawezesha wafuasi wake watiwa mafuta kupigania maisha zao wakiwa mashahidi Wakristo wa Yehova. Zaidi ya hayo, maelfu ya watu wenye mioyo minyofu, kama vile walivyofanya wale waliogeuka na kufuata Wayahudi katika siku za Esta, wamechukua msimamo wao pamoja na hawa Wayahudi wa kiroho kwa kuikubali ibada ya kweli.​​—⁠Zek. 8:23; Gal. 6:16.

YEHOVA AWATEGEMEZA WATU WAKE

20. Kunatukia nini kati ya Wayahudi na adui zao katika Adari 13 na 14?

20 Sasa miezi imepita na siku ya 13 ya Adari imefika. Wakiwa wamejikusanya katika miji yao, Wayahudi wawatia mikononi wale wanaotafuta kuwaumiza. Hakuna hata mtu mmoja ambaye ameweza kusimama mbele ya watu wa Mungu. Kwa hakika, hata wanasaidiwa na maafisa wa serikali kwa sababu watu hao wanamwogopa sana Mordekai. Walakini sana sana Wayahudi wanawaua wale wawachukiao kwa sababu Yehova anawategemeza. Katika Shushani ngomeni peke yake wanaume 500, na wana 10 wa Hamani wameuawa. Katika milki yote, adui 75,000 wameangamizwa, walakini Wayahudi hawateki nyara mahali po pote. Kupatana na ombi ambalo Esta amefanya, Mfalme Ahasuero amewapa Wayahudi walioko katika mji mkuu Shushani siku ya ziada ya kupigana, ambayo katika hiyo waua wanaume zaidi 300 walakini hawateki nyara zo zote. Vilevile maiti za wale wana 10 wa Hamani zinatundikwa juu ya mti. Adui zao wakiwa wameangamizwa, Wayahudi wenye kushinda waifanya siku ya 14 ya Adari katika majimbo yote na siku ya 15 katika Shushani kuwa wakati wa karamu na kushangilia.​​—⁠Esta 9:1-19.

21. Mordekai anawawekea Wayahudi wajibu wa kuadhimisha sikukuu gani kila mwaka, nalo kusudi lake ni nini?

21 Yehova amewakomboa watu wake nao wanapaswa kukumbuka jambo hilo. Kupatana na hilo, Mordekai awapelekea Wayahudi mahali pote katika milki hiyo barua zilizoandikwa. Sababu gani? Kuwawekea wajibu wa kuadhimisha kila mwaka siku ya 14 na ya 15 ya Adari kuwa siku za karamu, kupelekeana zawadi na kufurahi. Baadaye, barua nyingine kuhusu jambo hilo yapelekewa Wayahudi ikionyesha kwamba Malkia Esta anakubaliana na jambo hilo. Karamu hii ya kukombolewa yaitwa Purimu, jina linalotokana na tendo la Hamani la kutumia Puri, au kura, kuamua ni siku gani ingefaa kutimiza hila yake ya kuwaangamiza Wayahudi ambayo mwishowe ilimgeuka.​​—⁠Esta 9:20-32.

YEHOVA AWAKOMBOA WENYE HAKI

22. Mordekai akiwa na cheo cha juu sana katika serikali aendelea kuwafanyiaje watu wa Mungu?

22 Kwa habari ya Esta, Mordekai na Wayahudi wengine hatari imepita. Yehova hakuwaacha watu wake. Wakati uendeleapo, Mfalme Ahasuero atoza kodi katika nchi zote na visiwa vya bahari. (Kwa mfano, wakati fulani katika wakati wa utawala wake alimaliza nyingi ya kazi ya ujenzi iliyoanzishwa na babaye Dario wa Kwanza katika Persepoli.) Katika cheo cha juu sana cha serikali​—⁠kwa hakika, wa pili kwa mfalme peke yake​—⁠yuko Mordekai. Myahudi huyu mwaminifu, mwenye kibali na anayeheshimiwa na watu wa Mungu walio wakf, aendelea kutenda kwa faida yao na kuwatakia amani wazao wao wote.​​—⁠Esta 10:1-3.

23. Mordekai na Esta walionyesha sifa gani njema?

23 Kweli kweli, Mordekai alikuwa mwanamume mwenye imani, uhodari, uthabiti, ukamilifu na ushikamanifu kwa Yehova na kwa watu wa Mungu. Esta alikuwa mwanamke mwenye akili, aliyekaa kimya ilipokuwa lazima, walakini aliyesema kwa uhodari katika wakati ufaao. Yeye alikubali mashauri kutoka kwa Mordekai, hata wakati kuyafuata kulipohatirisha maisha yake. Kwa hakika, mwanamke huyu mwenye sura nzuri na mtiifu, alionyesha upendo, kutokuwa mchoyo pamoja na ushimamanifu kwa watu wake. Wote wawili yeye na Mordekai walimtumaini Yehova kabisa na kutafuta uongozi wake wa kimungu kupitia kwa sala.

24. Kwa sababu ya yale yaliyotukia Mungu alipokuwa akishughulika na Mordekai, Esta na Wayahudi wengine, leo watu wa Yehova wanaweza kuwa na uhakika gani?

24 Lo! mifano bora namna gani kwa watu wa Mungu leo! Wanatumikia bega kwa bega na kukabiliana na upinzani pamoja na mateso na kuwa washikamanifu kwa Yehova na kwa mmoja na mwenzake. Ndiyo, wao wana hakika kwamba Yehova Mungu atawategemeza na kuwakomboa, sawasawa na alivyowategemeza na kuwakomboa Esta na Mordekai, na watu wao. (Flp. 1:27-30) Ni kweli, “mateso ya mwenye haki ni mengi, lakini [Yehova] humponya nayo yote.” (Zab. 34:19) Kwa hiyo, sifa za Mungu wetu na zitangazwe nasi tumtumaini sikuzote, kwa kuwa Yehova hawaachi watu wake. ​—⁠Kutoka The Watchtower Mar. 15, 1979.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Esta hamhurumii naye Hamani mwovu ahukumiwa kufa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki