Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • si kur. 175-181
  • Kitabu Cha Biblia Namba 40—Mathayo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kitabu Cha Biblia Namba 40—Mathayo
  • “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • YALIYOMO KATIKA MATHAYO
  • KWA NINI NI CHENYE MAFAA
  • Mathayo Atangaza: ‘Masihi Amekuja!’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1982
  • Kitabu Cha Biblia 42—Luka
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Kitabu Cha Biblia 41—Marko
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Kitabu Cha Biblia Namba 43—Yohana
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
Pata Habari Zaidi
“Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
si kur. 175-181

Kitabu Cha Biblia Namba 40—Mathayo

Mwandikaji: Mathayo

Mahali Kilipoandikiwa: Palestina

Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 41 W.K.

Wakati Uliohusishwa: 2 K.W.K.–33 W.K.

1. (a) Yehova ameweka tumaini gani mbele ya ainabinadamu tangu Edeni na kuendelea? (b) Tumaini katika Mesiya lilikujaje kuthibitishwa imara miongoni mwa Wayahudi?

TANGU wakati wa uasi katika Edeni, Yehova ameweka mbele ya ainabinadamu ahadi yenye kufariji kwamba atatoa ukombozi kwa ajili ya wapenda uadilifu wote kupitia Mbegu ya “mwanamke” wake. Yeye alikusudia kutokeza Mbegu hii, au Mesiya, kutoka kwa taifa la Israeli. Kwa kadiri karne zilivyopita, yeye alisababisha unabii tele uandikwe kupitia waandikaji Waebrania waliopuliziwa na Mungu, wakionyesha kwamba Mbegu huyo angekuwa Mtawala katika Ufalme wa Mungu na kwamba angetenda kwa ajili ya utakaso wa jina la Yehova, akiliondolea milele suto ambalo limerundikwa juu yalo. Mambo mengi yalitolewa kupitia manabii hao kuhusu huyu ambaye angekuwa mteteaji Yehova na ambaye angeleta ukombozi kutoka kwa hofu, uonezi, dhambi, na kifo. Maandiko ya Kiebrania yalipokamilishwa, tumaini katika Mesiya lilithibitishwa imara miongoni mwa Wayahudi.

2. Wakati wa kutokea kwa Mesiya, hali zilikuwaje zenye kufaa kwa kuenezwa kwa habari njema?

2 Wakati uo huo tamasha ya ulimwengu ilikuwa ikibadilika. Mungu alikuwa ameendesha mataifa katika matayarisho ya kutokea kwa Mesiya, na hali zilikuwa zafaa kuenezwa kwa habari za tukio hilo kwa mapana na marefu. Mamlaka ya tano ya ulimwengu, Ugiriki, ilikuwa imetoa lugha ya jumla, kipitio cha ulimwengu wote cha mawasiliano miongoni mwa mataifa. Rumi, mamlaka ya sita ya ulimwengu, ilikuwa imekamatanisha mataifa iliyotawala kuwa mamlaka moja ya ulimwengu na ilikuwa imetoa barabara za kufanya sehemu zote za milki zifikilike. Wayahudi wengi walikuwa wametawanywa kote kote katika milki hiyo, hivi kwamba wengine walikuwa wamejifunza juu ya taraja la Wayahudi la kuja kwa Mesiya. Na sasa, miaka zaidi ya 4,000 baada ya ile ahadi ya Edeni, Mesiya alikuwa ametokea! Yule Mbegu aliyengojewa muda mrefu alikuwa amekuja! Matukio yaliyo ya maana zaidi kufikia hapo katika historia ya ainabinadamu yalifunguka wakati Mesiya alipotimiza kwa uaminifu hapa duniani mapenzi ya Baba yake.

3. (a) Yehova alifanya mpango gani wa kuandika mambo yote ya maisha ya Yesu? (b) Kuna utofauti gani kwa kila Gospeli, na kwa nini zote nne zahitajika?

3 Kwa mara nyingine tena ulikuwa wakati wa maandiko yaliyopuliziwa na Mungu kufanyizwa ili kuandika matukio hayo yenye maana kubwa. Roho ya Yehova ilipulizia wanaume waaminifu wanne waandike masimulizi yasiyotegemeana, hivyo kutoa ushahidi wenye mijumlisho minne kwamba Yesu alikuwa Mesiya, Mbegu aliyeahidiwa na Mfalme, na kutoa habari za kirefu za uhai wake, huduma yake, kifo chake, na ufufuo wake. Masimulizi hayo yaitwa Gospeli (Injili), neno “gospeli” likimaanisha “habari njema.” Ingawa hayo manne yalingana na mara nyingi yazungumza visa vile vile, hayanakiliani tu. Gospeli tatu za kwanza mara nyingi huitwa sainoptiki, kumaanisha “maoni ya kufanana,” kwa kuwa yafuata njia ile moja katika kusimulia maisha ya Yesu duniani. Lakini kila mmoja wa waandikaji hao wanne—Mathayo, Marko, Luka, na Yohana—aeleza hadithi yake mwenyewe juu ya Kristo. Kila mmoja ana habari kuu na lengo lake kamili, aonyesha utu wake mwenyewe, na afikiria wasomaji wake hasa. Kadiri tunavyozidi kutafuta maandishi yao, ndivyo tunavyozidi kuthamini hali tofauti za kila mmoja na kwamba vitabu hivi vinne vya Biblia vilivyopuliziwa na Mungu vyafanyiza masimulizi yasiyotegemeana, yenye kukamilishana, na yenye kupatana ya maisha ya Yesu Kristo.

4. Ni nini kinachojulikana juu ya mwandikaji wa Gospeli ya kwanza?

4 Wa kwanza kuandika habari njema juu ya Kristo alikuwa ni Mathayo. Jina lake yawezekana ni namna ya kifupi ya “Mattithiah” ya Kiebrania, kumaanisha “Zawadi ya Yehova.” Yeye alikuwa mmoja wa mitume 12 waliochaguliwa na Yesu. Wakati Bwana-Mkubwa aliposafiri kote kote katika bara la Palestina akihubiri na kufundisha juu ya Ufalme wa Mungu, Mathayo alikuwa na uhusiano wa karibu, wa kindani pamoja naye. Mbele ya kuwa mwanafunzi wa Yesu, Mathayo alikuwa mtoza ushuru (kodi), kazi ambayo Wayahudi waliichukia kabisa, kwa kuwa iliwakumbusha daima kwamba hawakuwa huru bali walikuwa chini ya utawala wa milki ya Rumi. Kwa jina jingine Mathayo alijulikana kuwa Lawi naye alikuwa mwana wa Alfayo. Kwa utayari aliitikia mwaliko wa Yesu wa kumfuata.—Mt. 9:9; Mk. 2:14; Luka 5:27-32.

5. Mathayo ashuhudiwaje kuwa mwandikaji wa Gospeli ya kwanza?

5 Ingawa Gospeli inayohesabiwa kuwa ya Mathayo haimtaji yeye kwa jina kuwa mwandikaji, ushuhuda tele wa wanahistoria wa mapema wa kanisa wamshuhudia kuwa ndiye. Labda hakuna kitabu chochote cha kale ambacho mwandikaji wacho ashuhudiwa kwa uwazi zaidi na kauli moja kuliko kitabu cha Mathayo. Tangu kule nyuma kwa Papias wa Hierapolis (mapema karne ya pili W.K.) na kuendelea, tuna mstari wa mashahidi wa uhakika wa kwamba Mathayo aliandika Gospeli hii na kwamba ni sehemu asilia ya Neno la Mungu. Cyclopedia ya McClintock na Strong yaeleza hivi: “Vifungu kutoka Mathayo vyanukuliwa na Justin Martyr, na mwandikaji wa barua kwa Diogneto (ona katika Justin Martyr cha Otto, buku 2), na Hegesippus, Irenæus, Tatian, Athenagoras, Theofilo, Clement, Tertullian, na Origen. Si kutokana tu na habari, bali namna ya manukuu, kutokana na utulivu wa kuvutia kama wa mtaalamu aliyetulia, kutokana na kutokuwapo kwa vidokezo vyovyote vya shaka, kwamba twaona kuwa kuna uthibitisho kwamba kitabu hiki tulicho nacho hakikufanyiwa badiliko lolote la ghafula.”a Uhakika wa kwamba Mathayo alikuwa mtume na, kwa hiyo, alikuwa na roho ya Mungu ikimkalia wahakikisha kwamba yale aliyoandika yangekuwa kumbukumbu ya uaminifu.

6, 7. (a) Gospeli ya kwanza ya Mathayo iliandikwa lini na katika lugha gani? (b) Ni nini kinachoonyesha iliandikwa hasa kwa ajili ya Wayahudi? (c) Ni mara ngapi New World Translation ina jina Yehova katika Gospeli hii, na kwa nini?

6 Mathayo aliandika simulizi lake katika Palestina. Mwaka kamili haujulikani, lakini maandikisho kwenye mwisho wa hati fulani (zote za baada ya karne ya 10 W.K.) yasema kwamba ilikuwa ni 41 W.K. Kuna uthibitisho wa kuonyesha kwamba hapo awali Mathayo aliandika Gospeli yake katika Kiebrania kilichopendwa na wengi cha wakati huo na baadaye akaitafsiri katika Kigiriki. Katika kitabu chake De viris inlustribus (Kuhusu Wanaume Mashuhuri), sura ya 3, Jerome asema: “Mathayo, ambaye pia ni Levi, na ambaye kutoka mtoza ushuru alikuja kuwa mtume, kwanza kabisa alitunga Gospeli ya Kristo katika Yudea katika lugha na herufi za Kiebrania kwa ajili ya mafaa ya wale wa tohara waliokuwa wameamini.”b Jerome aongezea kwamba maandishi ya Kiebrania ya Gospeli hii yalihifadhiwa katika siku yake (karne za nne na tano W.K.) katika maktaba ambayo Pamfilo alikuwa amekusanya katika Kaisaria.

7 Mapema katika karne ya tatu, Origen, katika kuzungumza zile Gospeli, anukuliwa na Eusebio kuwa akisema kwamba ya “kwanza iliandikwa . . . kulingana na Mathayo, . . . aliyeitangaza kwa ajili ya wale ambao kutoka kwa dini ya Kiyahudi walikuja kuamini, ikatungwa kama ilivyokuwa katika lugha ya Kiebrania.”c Kwamba iliandikwa hasa kwa kufikiria Wayahudi yaonyeshwa na nasaba yayo, inayoonyesha ukoo wa kisheria wa Yesu kuanzia Abrahamu, na kwa marejezo yayo mengi kwa Maandiko ya Kiebrania, kuonyesha kwamba yalielekezea kuja kwa Mesiya. Ni jambo la akili kuamini kwamba Mathayo alitumia jina la kimungu Yehova katika namna ya Tetragrammatoni aliponukuu kutoka sehemu za Maandiko ya Kiebrania yaliyokuwa na jina hilo. Ndiyo sababu kitabu cha Mathayo katika New World Translation kina jina Yehova mara 18, kama tafsiri ya Kiebrania ya Mathayo iliyotokezwa awali na F. Delitzsch katika karne ya 19. Mathayo angalikuwa na mtazamo ule ule wa Yesu kuelekea jina la kimungu naye hangezuiwa na ushirikina uliokuwapo wa Kiyahudi juu ya kutotumia jina hilo.—Mt. 6:9; Yn. 17:6, 26.

8. Uhakika wa kwamba Mathayo alikuwa amekuwa mtoza ushuru waonyeshwaje katika yaliyomo katika Gospeli yake?

8 Kwa kuwa Mathayo hapo mbele alikuwa mtoza ushuru, ilikuwa ni asili kwamba angetaja kikamili pesa, tarakimu (hesabu), na thamani. (Mt. 17:27; 26:15; 27:3) Yeye alithamini sana rehema ya Mungu katika kumruhusu yeye, mtoza ushuru aliyedharauliwa, kuwa mhudumu wa habari njema na mshiriki wa karibu wa Yesu. Kwa hiyo, twaona Mathayo peke yake kati ya waandikaji wa Gospeli ndiye anayetupa usisitizo wa Yesu kurudilia kwamba rehema yatakwa kuongezea dhabihu. (9:9-13; 12:7; 18:21-35) Mathayo alitiwa moyo sana na fadhili zisizostahiliwa za Yehova na kwa kufaa aandika baadhi ya maneno yenye kufariji sana aliyosema Yesu: “Njoni kwangu, nyinyi nyote mnaomenyeka na kulemewa na mizigo, nami nitawaburudisha nyinyi. Bebeni nira yangu na kujifunza kwangu, kwa maana mimi ni mwenye tabia pole na hali kujishusha katika moyo, na nyinyi mtapata burudisho la nafsi zenu. Kwa maana nira yangu ni ya fadhili na mzigo wangu ni mwepesi.” (11:28-30, NW) Jinsi maneno hayo ya upole yalivyokuwa yenye kuburudisha kwa huyo aliyekuwa mtoza ushuru hapo kwanza, ambaye, bila shaka, wananchi wenzake walimtukana tu!

9. Ni nini habari kuu na mtindo wa utoaji-habari wa Mathayo?

9 Mathayo hasa alikazia kwamba habari kuu ya fundisho la Yesu ilikuwa ni “ufalme wa mbinguni.” (4:17) Kwake, Yesu alikuwa ndiye Mfalme-Mhubiri. Yeye alitumia usemi “ufalme” mara nyingi sana (zaidi ya mara 50) hivi kwamba Gospeli yake yaweza kuitwa Gospeli ya Ufalme. Mathayo alihangaikia zaidi utoaji wenye kueleweka wa hotuba na mahubiri ya peupe ya Yesu kuliko mfuatilio wa karibu wa kronolojia (tarehe za matukio). Kukazia kwa Mathayo habari kuu ya Ufalme kulimwongoza aache mpangilio wa kikronolojia katika sura 18 za kwanza. Hata hivyo, sura 10 za mwisho (19 mpaka 28) kwa ujumla hufuatia utaratibu wa kikronolojia na pia kuendelea kukazia Ufalme.

10. Ni kadiri gani ya yaliyomo inayopatikana katika Mathayo pekee, na Gospeli hiyo yahusisha kipindi gani?

10 Asilimia 42 ya simulizi la Gospeli ya Mathayo haipatikani katika yoyote ya zile Gospeli tatu nyingine.d Hiyo ni kutia na angalau mifano, au vielezi kumi: Magugu katika shamba (13:24-30), hazina iliyofichwa (13:44), lulu ya thamani kubwa (13:45, 46), juya (wavu) (13:47-50), yule mtumwa asiye na rehema (18:23-35), wafanya kazi na dinari (20:1-16), baba na watoto wawili (21:28-32), ndoa ya mwana wa mfalme (22:1-14), wale wanawali kumi (25:1-13), na talanta (25:14-30). Kwa ujumla, kitabu hiki chatoa simulizi lacho tangu kuzaliwa kwa Yesu, 2 K.W.K., mpaka kukutana kwake na wanafunzi wake kabla tu ya kupaa kwake, 33 W.K.

YALIYOMO KATIKA MATHAYO

11. (a) Kwa kueleweka Gospeli hiyo yaanzaje, na ni matukio gani ya mapema yanayosimuliwa? (b) Ni nini baadhi ya utimizo mbalimbali wa kiunabii ambao Mathayo aelekezea uangalifu wetu?

11 Kutanguliza Yesu na habari za “ufalme wa mbinguni” (1:1–4:25). Kwa kueleweka, Mathayo aanza na nasaba ya Yesu, akitoa uthibitisho wa haki ya kisheria ya Yesu ya kuwa mrithi wa Abrahamu na Daudi. Kwa hiyo, uangalifu wa msomaji Myahudi wavutwa. Kisha twasoma simulizi la kuchukuliwa kimwujiza kwa mimba ya Yesu, kuzaliwa kwake katika Bethlehemu, ziara ya wanajimu, kasirani ya Herode yenye kusababisha machinjo ya wavulana wote katika Bethlehemu chini ya miaka miwili, kutoroka kwa Yusufu na Mariamu katika Misri na yule mtoto mchanga, na kurejea kwao hatimaye ili wakae katika Nazareti. Mathayo ni mwangalifu kuvuta fikira kwenye utimizo mbalimbali wa unabii ili kuthibitisha Yesu kuwa Mesiya aliyetabiriwa.—Mt. 1:23—Isa. 7:14; Mt. 2:1-6—Mik. 5:2; Mt. 2:13-18—Hos. 11:1 na Yer. 31:15; Mt. 2:23—Isa. 11:1, kielezi-chini.

12. Ni nini kinachotukia kwenye ubatizo wa Yesu na mara tu baada ya hapo?

12 Simulizi la Mathayo sasa laruka kwenda mbele karibu miaka 30. Yohana Mbatizaji anahubiri katika nyika (jangwa) ya Yudea: “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” (Mt. 3:2) Yeye anabatiza Wayahudi wenye kutubu katika mto Yordani na kuonya Mafarisayo na Masadukayo juu ya ghadhabu itakayokuja. Yesu aja kutoka Galilaya naye abatizwa. Bila kukawia roho ya Mungu yamshukia, na sauti kutoka mbinguni yasema: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” (3:17) Kisha Yesu aongozwa mpaka nyikani, ambako, baada ya kufunga siku 40, ashawishwa na Shetani Ibilisi. Safari tatu ampinga Shetani kwa manukuu ya Neno la Mungu, mwishowe akisema: “Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana [Yehova, NW] Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.”—4:10.

13. Ni kampeni gani yenye kusisimua inayoanza sasa katika Galilaya?

13 “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Maneno hayo yenye kusisimua sana yatangazwa sasa katika Galilaya na Yesu aliyepakwa mafuta. Aita wavuvi wanne wa samaki waache nyavu zao wamfuate na kuwa “wavuvi wa watu,” naye asafiri pamoja nao “katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.”—4:17, 19, 23.

14. Katika Mahubiri ya Mlimani yake, Yesu anena juu ya furaha zipi, naye asema nini juu ya uadilifu?

14 Mahubiri ya Mlimani (5:1–7:29). Umati unapoanza kumfuata, Yesu aenda juu mlimani, aketi chini, na kuanza kufundisha wanafunzi wake. Afungua hotuba yake yenye kusisimua kwa ‘furaha’ (NW) tisa: Wenye furaha ni wale wanaotambua uhitaji wao wa kiroho, wale wanaomboleza, wapole, wale wanaoona njaa na kiu ya uadilifu, wenye rehema, wenye kutakata katika moyo, wenye amani, wale wanaoteswa kwa ajili ya uadilifu, na wale wanaosutwa na kunenewa uwongo. “Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.” Yeye awaita wanafunzi wake “chumvi ya dunia” na “nuru ya ulimwengu” na kueleza uadilifu, ulio tofauti sana na kawaida ya waandishi na Mafarisayo, unaotakwa ili kuingia Ufalme wa mbinguni. ‘Basi ninyi mwe wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.’—5:12-14, 48.

15. Yesu asema nini juu ya sala na juu ya Ufalme?

15 Yesu aonya kuhusu zawadi na sala za kinafiki. Afundisha wanafunzi wake wasali kwa ajili ya utakaso wa jina la Baba, kwa ajili ya Ufalme Wake uje, na kwa ajili ya riziki yao ya kila siku. Katika mahubiri yote Yesu atanguliza Ufalme. Yeye ashauri wale wanaomfuata wasiwe na wasiwasi au kufanya kazi kwa ajili tu ya utajiri wa kimwili, kwa maana Baba ajua mahitaji yao halisi. “Basi, endeleeni,” asema, “kuutafuta kwanza ufalme na uadilifu wake, na mambo yote hayo mengine yataongezwa kwa nyinyi.”—6:33, NW.

16. (a) Ni nini shauri la Yesu juu ya mahusiano pamoja na wengine, naye asema nini juu ya wale wanaotii mapenzi ya Mungu na wale wasioyatii? (b) Mahubiri yake yana tokeo gani?

16 Bwana-Mkubwa ashauri juu ya mahusiano pamoja na wengine, akisema: “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo.” Wale wachache wanaopata barabara inayoenda kwenye uhai watakuwa wale wanaofanya mapenzi ya Baba yake. Wafanya kazi wanaovunja sheria watajulikana kwa matunda yao nao watakataliwa. Yesu afananisha yule anayetii semi zake na “mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.” Hotuba hii ina matokeo gani juu ya umati unaosikiliza? ‘Washangaa mno kwa mafundisho yake,’ kwa maana afundisha “kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.”—7:12, 24-29.

17. Yesu aonyeshaje mamlaka yake akiwa Mesiya, na ni hangaiko gani la upendo analoonyesha?

17 Kuhubiri Ufalme kwapanuliwa (8:1–11:30). Yesu afanya miujiza mingi—akiponya wakoma, waliopooza, na waliopagawa na roho waovu. Hata adhihirisha mamlaka juu ya upepo na mawimbi kwa kutuliza tufani, naye ainua msichana fulani kutoka kwa wafu. Jinsi Yesu anavyohurumia umati aonapo jinsi walivyokonda na kutawanywa-tawanywa, “kama kondoo wasio na mchungaji”! Ni kama anavyowaambia wanafunzi wake, “mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”—9:36-38.

18. (a) Yesu awapa mitume wake maagizo na onyo gani? (b) Kwa nini ni ole kwa “kizazi hiki”?

18 Yesu achagua na kuwapa utume mitume 12. Awapa maagizo yaliyo wazi juu ya jinsi ya kufanya kazi yao na kukazia fundisho kuu la kufundisha kwao: “Katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.” Yeye awapa onyo la upole lenye hekima na la upendo: “Mmepata bure, toeni bure.” “Iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.” Watachukiwa na kunyanyaswa, hata na watu wa ukoo wa karibu, lakini Yesu awakumbusha: “Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.” (10:7, 8, 16, 39) Wafunga safari, wakafundishe na kuhubiri katika majiji waliyogawiwa! Yesu atambulisha Yohana Mbatizaji kuwa mjumbe aliyetumwa mbele yake, “Eliya” aliyeahidiwa, lakini “kizazi hiki” hakikubali wala Yohana wala yeye, Mwana wa Adamu. (11:14, 16) Kwa hiyo ole kwa kizazi hiki na miji ambayo haikutubu kwa kuona kazi zake zenye nguvu! Lakini wale wanaokuwa wanafunzi wake watapata burudiko kwa ajili ya nafsi zao.

19. Mafarisayo wanapotilia shaka mwenendo wake siku ya Sabato, Yesu awashutumuje?

19 Mafarisayo wakanushwa na kushutumiwa (12:1-50). Mafarisayo wajaribu kumtafutia Yesu kosa juu ya suala la Sabato, lakini yeye akanusha mashtaka yao na kuanza kulaani vikali unafiki wao. Yeye awaambia hivi: “Wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake.” (12:34) Hakuna ishara itakayotolewa isipokuwa ile ya Yona nabii: Mwana wa Adamu atakuwa ndani ya ardhi siku tatu usiku na mchana.

20. (a) Ni kwa nini Yesu anena katika vielezi? (b) Ni vielezi gani vya Ufalme anavyotoa sasa?

20 Vielezi saba vya Ufalme (13:1-58). Ni kwa nini Yesu anena kwa vielezi? Aeleza hivi wanafunzi wake: “Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.” Yeye ajulisha rasmi wanafunzi wake kuwa wenye furaha kwa sababu waona na kusikia. Jinsi anavyowatolea maagizo yenye kuburudisha sasa! Baada ya kueleza kielezi cha mpandaji, Yesu atoa vielezi vya magugu katika shamba, punje ya haradali, chachu, hazina iliyofichwa, lulu ya thamani kubwa, na juya—vyote hivyo vikionyesha jambo fulani kuhusiana na “ufalme wa mbinguni.” Hata hivyo, watu wakwazika kwa ajili yake, na Yesu awaambia hivi: “Nabii hakosi kupata heshima isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe.”—13:11, 57.

21. (a) Ni miujiza gani anayofanya Yesu, nayo yamtambulisha kuwa nini? (b) Ni njozi gani inayotolewa kuhusu kuja kwa Mwana wa Adamu katika Ufalme wake?

21 Huduma na miujiza zaidi ya “Kristo” (14:1–17:27). Yesu asikitishwa sana na ripoti ya kukatwa kichwa kwa Yohana Mbatizaji kwa amri ya ukatili mkubwa ya Herode Antipa. Kimwujiza alisha umati wa 5,000 na zaidi; atembea juu ya bahari; apinga uchambuzi zaidi kutoka kwa Mafarisayo, ambao, yeye asema, ‘wavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo’; aponya waliopagawa na roho waovu, “viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi”; na kwa mara nyingine alisha zaidi ya 4,000 kwa boflo (mikate) saba na samaki wachache wadogo. (15:3, 30) Kwa kujibu swali la Yesu, Petro amtambulisha, akisema: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu ampongeza Petro na kujulisha rasmi hivi: “Juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa [kundi, NW] langu.” (16:16, 18) Sasa Yesu aanza kunena juu ya kifo chake kinachokaribia na juu ya ufufuo wake kwenye siku ya tatu. Lakini pia yeye aahidi kwamba baadhi ya wanafunzi wake “hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.” (16:28) Siku sita baadaye, Yesu aandamana na Petro, Yakobo, na Yohana juu ya mlima mrefu ili wamwone akigeuka sura katika utukufu. Katika njozi, waona Musa na Eliya wakizungumza naye, nao wasikia sauti fulani kutoka mbinguni ikisema: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.” Baada ya kushuka kutoka mlimani, Yesu awaambia kwamba “Eliya” aliyeahidiwa amekwisha kuja tayari, nao wafahamu kwamba yeye anena juu ya Yohana Mbatizaji.—17:5, 12.

22. Yesu ashauri nini juu ya msamaha?

22 Yesu ashauri wanafunzi wake (18:1-35). Akiwa Kapernaumu Yesu aongea na wanafunzi wake juu ya unyenyekevu, shangwe kubwa ya kumpata tena kondoo aliyepotea, na kutatua ugomvi kati ya ndugu. Petro auliza: ‘Nimsamehe ndugu yangu mara ngapi?’ naye Yesu ajibu: “Mimi nakuambia, si, Mpaka mara saba, bali, Mpaka mara sabini na saba.” Ili kuongeza mkazo kwenye hilo, Yesu atoa kielezi cha mtumwa ambaye bwana-mkubwa wake alimsamehe deni la dinari milioni 60. Mtumwa huyo baadaye alifanya mtumwa mwenzake afungwe gerezani kwa sababu ya deni la dinari 100 pekee, na kama tokeo, mtumwa huyo asiye na rehema alikabidhiwa vilevile kwa wanagereza.e Yesu ajulisha jambo hili: “Hali moja na hiyo Baba yangu wa kimbingu atashughulika nanyi pia ikiwa nyinyi hamsamehei kila mmoja ndugu yake kutoka mioyoni mwenu.”—18:21, 22, 35, NW.

23. Yesu aeleza nini juu ya talaka na kuhusu njia ya kwenda kwenye uhai?

23 Siku za umalizio za huduma ya Yesu (19:1–22:46). Mwendo wa matukio wawa wa haraka na wasiwasi waongezeka wakati waandishi na Mafarisayo wanapoghadhibishwa zaidi na huduma ya Yesu. Waja kumtega kuhusiana na jambo la talaka lakini washindwa; Yesu aonyesha kwamba msingi pekee wa Kimaandiko wa talaka ni uasherati. Mwanamume kijana tajiri amjia Yesu, akimwuliza njia ya kwenda kwenye uhai wa milele, lakini aenda zake amehuzunika wakati akutapo ni lazima auze vyote alivyo navyo na kuwa mfuasi wa Yesu. Baada ya kutoa kielezi cha wafanya kazi na dinari, kwa mara nyingine Yesu anena juu ya kifo na ufufuo wake, naye asema: “Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”—20:28.

24. Yesu anapoingia kwenye juma la mwisho la maisha yake ya kibinadamu, awa na mapambano gani na wapinzani wa kidini, naye ashughulikiaje maswali yao?

24 Sasa Yesu aingia kwenye juma la mwisho la uhai wake wa kibinadamu. Aingia Yerusalemu kwa shangwe ya ushindi akiwa ‘Mfalme, aliyempanda mwana-punda.’ (21:4, 5) Asafisha hekalu kwa kuondoa wabadilisha-pesa na wengine wenye kujipatia faida, nayo chuki ya maadui wake yaongezeka awaambiapo hivi: “Watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu na kuingia katika ufalme wa Mungu.” (21:31) Vielezi vyake vyenye kutaja mambo wazi vya shamba la mzabibu na karamu ya ndoa vyalenga shabaha. Kwa ustadi ajibu swali la ushuru la Mafarisayo kwa kuwaambia walipe “Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.” (22:21) Hali moja na hiyo ageuza swali lenye mtego la Masadukayo na kutetea tumaini la ufufuo. Kwa mara nyingine Mafarisayo wamjia kwa swali linalohusu Sheria, na Yesu awaambia kwamba amri kuu zaidi ni kumpenda Yehova kabisa, na ya pili ni mtu kupenda jirani yake kama ajipendavyo. Kisha Yesu awauliza, ‘Kristo aweje mwana wa Daudi na Bwana yake?’ Hakuna awezaye kujibu, na baada ya hapo hakuna anayethubutu kumwuliza.—22:45, 46.

25. Yesu ashutumuje vikali waandishi na Mafarisayo?

25 ‘Ole wenu, wanafiki’ (23:1–24:2). Akinena na umati kwenye hekalu, Yesu ashutumu vikali tena waandishi na Mafarisayo. Si kwamba tu wamejifanya wasistahili kuingia ndani ya Ufalme bali pia wazidisha ujanja wao wote ili wazuie wengine wasiingie. Kama vile makaburi yaliyopakwa chokaa, wao waonekana wazuri kwa nje-nje, lakini ndani wamejawa na ufisadi na kuoza. Yesu amalizia na hukumu hii juu ya Yerusalemu: “Nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa.” (23:38) Aondokapo hekaluni, Yesu atabiri uharibifu walo.

26. Ni ishara gani ya kiunabii anayotoa Yesu kuhusu kuwapo kwake katika utukufu wa kifalme?

26 Yesu atoa ‘ishara ya kuwapo kwake’ (24:3–25:46). Juu ya Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wamwuliza juu ya ‘ishara ya kuwapo kwake na umalizio wa mfumo wa mambo.’ Katika kujibu Yesu aelekeza mbele kwenye wakati wa vita, ‘taifa juu ya taifa na ufalme juu ya ufalme,’ upungufu wa chakula, matetemeko ya dunia, na kuongezeka kwa kuvunja sheria, duniani pote kuhubiriwa kwa “habari njema hizi za ufalme,” kuwekwa kwa “mtumwa mwaminifu mwenye busara,” na sehemu nyingine nyingi za ishara yenye kujumlisha mengi ambayo ingetia alama ‘kuwasili kwa Mwana wa mwanadamu katika utukufu wake ili aketi kwenye kiti cha enzi chake cha utukufu.’ (24:3, 7, 14, 45-47; 25:31, NW) Yesu amalizia unabii wake wa maana kwa vielezi vya wanawali kumi na talanta, ambavyo vyaahidi thawabu zenye shangwe kwa walio macho na walio waaminifu, na kielezi cha kondoo na mbuzi, kinachoonyesha watu wa mfano wa mbuzi wakienda “kwenye kukatiliwa mbali kwa milele, bali waadilifu kwenye uhai wa milele.”—25:46, NW.

27. Ni matukio gani yanayotia alama siku ya mwisho ya Yesu duniani?

27 Matukio ya siku ya mwisho ya Yesu (26:1–27:66). Baada ya kusherehekea Sikukuu-Kupitwa, Yesu aanzisha kitu kipya pamoja na mitume wake waaminifu, akiwaalika washiriki mkate usiotiwa chachu na divai kuwa vifananishi vya mwili wake na damu yake. Kisha waenda Gethsemane, ambako Yesu asali. Huko Yuda aja na umati wenye silaha na kumsaliti Yesu kwa kumbusu kinafiki. Yesu atwaliwa kwa kuhani wa juu, na makuhani wakuu na Sanhedrini nzima watafuta mashahidi bandia juu ya Yesu. Kwa kulingana na unabii wa Yesu, Petro amkana anapotiwa kwenye mtihani. Yuda, kwa kughairi, atupa pesa zake za usaliti kwenye hekalu na kwenda zake na kujinyonga. Asubuhi Yesu aongozwa mbele ya gavana Mrumi Pilato, ambaye amkabidhi akatundikwe kwa kubanwa na kundi lililochochewa na makuhani ambalo lapaaza sauti hivi: “Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.” Askari wa liwali wafanyia cheo chake mzaha wenye dharau na kisha wamwongoza kumpeleka Golgotha, ambako atundikwa juu ya mti katikati ya wanyang’anyi wawili, kukiwa na ishara juu ya kichwa chake inayosema, “HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI.” (27:25, 37) Baada ya saa nyingi za mateso, mwishowe Yesu afa karibu saa tisa alasiri na kisha alazwa ndani ya kaburi la ukumbusho jipya la Yusufu wa Arimathaya. Hiyo imekuwa ndiyo siku kubwa zaidi katika historia yote!

28. Mathayo afikisha simulizi lake kwenye upeo kwa habari zipi zilizo bora zaidi, naye amalizia kwa utume gani?

28 Ufufuo wa Yesu na maagizo ya mwisho (28:1-20). Sasa Mathayo afikisha kwenye upeo simulizi lake kwa habari njema zaidi ziwezekanazo kuwapo. Yesu aliye mfu amefufuliwa—aishi tena! Mapema katika siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena na “Mariamu yule wa pili” waja kwenye kaburi na kusikia tangazo la malaika la uhakika huo wenye shangwe. (28:1) Ili kuthibitisha hilo, Yesu mwenyewe awatokea. Maadui hata wajaribu kukomesha uhakika wa kufufuliwa kwake, wakihonga askari ambao walikuwa wakilinda kwenye kaburi waseme, “Wanafunzi wake walikuja usiku na kuiba yeye huku sisi tumelala.” Baadaye, katika Galilaya, Yesu afanya mkutano mwingine pamoja na wanafunzi wake. Agizo lake la kuwaaga ni lipi? Hili: “Nendeni . . . mkafanye wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote, kuwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la roho takatifu.” Je! watakuwa na uongozi katika kazi hii ya kuhubiri? Uneni wa Yesu wa mwisho anaoandika Mathayo watoa uhakikisho huo: “Tazama! Mimi nipo pamoja nanyi siku zote hadi umalizio wa mfumo wa mambo.”—28:13, 19, 20, NW.

KWA NINI NI CHENYE MAFAA

29. (a) Mathayo awekaje daraja kutoka kwenye Maandiko ya Kiebrania mpaka ya Kigiriki? (b) Ni pendeleo gani lililoonewa shangwe na Yesu ambalo lingali wazi kwa Wakristo leo?

29 Kitabu cha Mathayo, cha kwanza cha Gospeli zile nne, chatoa kweli kweli daraja bora kutoka kwa Maandiko ya Kiebrania kuingia kwenye Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Bila kukosea, chatambulisha Mesiya na Mfalme wa Ufalme ulioahidiwa wa Mungu, chajulisha matakwa ya kuwa wafuasi wake, na chaeleza wazi kazi iliyo mbele yao duniani. Kwanza Yohana Mbatizaji, kisha Yesu, na mwishowe wanafunzi wake walienda wakihubiri, “Ufalme wa mbinguni umekaribia.” Zaidi ya hayo, amri ya Yesu yahusu mpaka kwenye umalizio wa mfumo wa mambo: “Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.” Kweli kweli lilikuwa, na lingali pendeleo tukufu na bora sana kushiriki katika hii kazi ya Ufalme, kutia ‘kufanya wanafunzi [kutoka kwa watu wa, NW] mataifa yote,’ kwa kufanya kazi kufuatia kigezo cha Bwana-Mkubwa.—3:2; 4:17; 10:7; 24:14; 28:19.

30. Ni sehemu gani hasa ya Mathayo imetambulika kwa ajili ya thamani yayo yenye kutumika?

30 Hakika Gospeli ya Mathayo ni “habari njema.” Ujumbe wayo uliopuliziwa na Mungu ulikuwa ni “habari njema” kwa wale walioufuata katika karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida, na Yehova Mungu amehakikisha kwamba umehifadhiwa kuwa “habari njema” mpaka siku hii. Hata wasio Wakristo wamelazimika kukiri uwezo wa Gospeli hii, kama, kwa kielelezo, kiongozi Mhindu Mohandas (Mahatma) Gandhi alisema: “Kwa vyovyote zinywe sana chemchemi zinazotolewa kwako katika Mahubiri ya Mlimani . . . Kwa maana fundisho la Mahubiri hayo lilikusudiwa kwa ajili ya kila mmoja wetu.”f

31. Ni nani wameonyesha uthamini halisi kwa ajili ya shauri katika Mathayo, na kwa nini kuna faida kujifunza Gospeli hii tena na tena?

31 Hata hivyo, ulimwengu wote, kutia na sehemu ile inayodai kuwa ya Kikristo, waendelea kuwa na matatizo yao. Wamebaki Wakristo wachache sana wa kweli wanaoona kuwa hazina, kujifunza, na kutumia Mahubiri ya Mlimani na shauri lote jinginelo lililo timamu la habari njema kwa kulingana na Mathayo na hivyo kupata mafaa yasiyokadirika. Kuna faida kujifunza tena na tena maonyo mazuri ya Yesu juu ya kupata furaha ya kweli, na pia juu ya maadili na ndoa, uwezo wa upendo, sala inayokubalika, thamani za kiroho kinyume cha za kimwili, kutafuta Ufalme kwanza, kustahi mambo matakatifu, na kulinda na kuwa watiifu. Mathayo sura 10 hutoa maagizo ya utumishi ya Yesu kwa wale wanaohubiri habari njema za “ufalme wa mbinguni.” Mifano mingi ya Yesu ina masomo muhimu kwa ajili ya wote ‘wenye masikio ya kusikia.’ Zaidi ya hayo, unabii mbalimbali wa Yesu, kama kutabiri kwake kwa kirefu ‘ishara ya kuwapo kwake,’ (NW), wajenga tumaini lenye nguvu na uhakika katika wakati ujao.—5:1–7:29; 10:5-42; 13:1-58; 18:1–20:16; 21:28–22:40; 24:3–25:46.

32. (a) Toa kielezi jinsi unabii uliotimizwa watoa uthibitisho wa Umesiya wa Yesu. (b) Utimizo huo mbalimbali watupa uhakikisho gani wenye nguvu leo?

32 Gospeli ya Mathayo yajaa unabii mbalimbali uliotimizwa. Mengi ya manukuu yake kutoka Maandiko ya Kiebrania yaliyopuliziwa na Mungu yalikuwa ni kwa kusudi la kuonyesha utimizo huo. Yatoa uthibitisho usiopingwa kwamba Yesu ndiye Mesiya, kwa maana haingaliwezekana kabisa kutangulia kupanga mambo hayo yote. Linganisha, kwa kielelezo, Mathayo 13:14, 15 na Isaya 6:9, 10; Mathayo 21:42 na Zaburi 118:22, 23; na Mathayo 26:31, 56 na Zekaria 13:7. Utimizo huo mbalimbali watupa uhakikisho wenye nguvu, pia, kwamba matabiri yote ya kiunabii ya Yesu mwenyewe, yaliyoandikwa na Mathayo, kwa wakati wake yangekuwa kweli na makusudi matukufu ya Yehova kwa habari ya “ufalme wa mbinguni” yatimie.

33. Wapenda uadilifu sasa waweza kushangilia katika maarifa na tumaini gani?

33 Jinsi Mungu alivyotabiri kwa ukamili maisha ya Mfalme wa Ufalme, hata katika mambo madogo madogo! Jinsi Mathayo aliyepuliziwa na Mungu alivyoandika vilivyo utimizo wa unabii huo mbalimbali kwa uaminifu! Wanapofikiria utimizo na ahadi zote mbalimbali za kiunabii zilizoandikwa katika kitabu cha Mathayo, wapenda uadilifu waweza kushangilia katika maarifa na tumaini la “ufalme wa mbinguni” kuwa chombo cha Yehova cha kutakasia jina lake. Ufalme huo ukiwa mikononi mwa Yesu Kristo ndio utakaoleta baraka zisizoelezeka za maisha na furaha kwa wapole na wenye njaa ya kiroho “katika uumbaji mpya, wakati mwana wa mwanadamu atakapoketi juu ya kiti cha enzi chake kitukufu.” (Mt. 19:28, NW) Yote hayo yamo katika habari njema zenye kusisimua “kulingana na Mathayo.”

[Maelezo ya Chini]

a 1981 Chapa-murdio, Buku 5, ukurasa 895.

b Tafsiri kutoka kwa maandishi ya Kilatini yaliyohaririwa na E. C. Richardson na kuchapishwa katika mfululizo “Texte und Untersuchungen zur Geschichte der altchristlichen Literatur,” Leipzig, 1896, Buku 14, kurasa 8, 9.

c The Ecclesiastical History, VI, XXV, 3-6.

d Introduction to the Study of the Gospels, 1896, B. F. Westcott, ukurasa 201.

e Katika siku ya Yesu, dinari ililingana na mshahara wa siku moja; kwa hiyo dinari 100 zililingana na sehemu moja ya tatu hivi ya mshahara wa mwaka mmoja. Dinari milioni 60 zililingana na mshahara ambao ungetaka maelfu ya maisha ili kukusanya.—Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 614.

f Mahatma Gandhi’s Ideas, 1930, cha C. F. Andrews, ukurasa 96.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki