Kitabu cha Biblia Namba 66—Ufunuo
Mwandikaji: Mtume Yohana
Mahali Kilipoandikiwa: Patmo
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 96 W.K.
1. (a) Kuhusu vifananisho vya Ufunuo, watumishi wa Mungu watakubaliana na nini? (b) Kwa nini Ufunuo kimewekwa kwa usahihi kuwa cha mwisho katika Biblia?
JE! VIFANANISHO vya Ufunuo vimekusudiwa kuogofya? Sivyo hata kidogo! Huenda utimizo wa ule unabii ukawaogofya waovu, lakini watumishi waaminifu wa Mungu watakubaliana na utangulizi uliopuliziwa na Mungu na maelezo ya malaika mwishoni: “Mwenye furaha ni yeye ambaye husoma kwa sauti kubwa na wale ambao husikia maneno ya unabii huu.” “Mwenye furaha ni yeyote anayeshika maneno ya unabii wa hati-kunjo hii.” (Ufu. 1:3; 22:7, NW) Ingawa kiliandikwa kabla ya vitabu vile vingine vinne vyenye pumzi ya Mungu vilivyoandikwa na Yohana, kwa usahihi Ufunuo kimepangwa mwisho katika mkusanyo wa vitabu 66 vyenye pumzi ya Mungu vinavyojumlika kuwa Biblia yetu, kwa maana Ufunuo ndicho kipelekacho wasomaji wacho mbali katika wakati ujao, kwa kutoa njozi yenye kuhusisha pande zote juu ya mambo ambayo Mungu akusudia kwa ainabinadamu, na hiyo yaleta kile kichwa kikuu cha Biblia, utakaso wa jina la Yehova na kuondolewa malawama kwa enzi kuu yake kwa njia ya Ufalme chini ya Kristo, yule Mbegu Aliyeahidiwa, kwenye upeo mtukufu.
2. Ufunuo ulimjia Yohana kwa njia gani, na kwa nini kichwa cha kitabu hiki chafaa sana?
2 Kulingana na ule mstari wa kichwa, huu ni “ufunuo kwa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa . . . Na yeye alituma malaika wake na kuutoa kwa njia ya ishara kupitia yeye kwa mtumwa wake Yohana.” Hivyo basi Yohana alikuwa mwandikaji tu, si mwanzishi, wa habari hizi. Kwa hiyo Yohana siye mfunuzi, wala kitabu hiki si ufunuo wa Yohana. (1:1) Huku kuondolelewa utaji kwa mtumwa wa Mungu juu ya makusudi Yake mazuri ajabu kwa wakati ujao kwafanya kichwa cha kitabu hiki kifae sana, kwa maana jina lacho la Kigiriki A·po·kaʹly·psis (Apokalipsi) lamaanisha “Kuondoa Kifuniko” au “Kuondoa Utaji.”
3. Ufunuo chamwonyesha kuwa nani yule mwandikaji Yohana, na kwa nini kichwa cha kitabu hiki chafaa sana?
3 Alikuwa nani Yohana huyu arejezewaye kuwa mwandikaji wa Ufunuo katika sura yacho ya kwanza? Twaambiwa kwamba yeye alikuwa mtumwa wa Yesu Kristo, na pia ndugu na mshiriki katika dhiki, na kwamba alipelekwa uhamishoni katika kisiwa cha Patmo. Kwa wazi alijulikana sana na wasomaji wake wa kwanza, ambao haikuhitajiwa kabisa ajitambulishe zaidi kwao. Ni lazima iwe ni mtume Yohana. Kukata shauri hivi kwaungwa mkono na walio wengi wa wanahistoria wa kale. Papias, aliyeandika katika sehemu ya kwanza ya karne ya pili W.K., asemwa kuwa alikiona kitabu hiki kuwa chenye asili ya kimitume. Justin Martyr, wa karne ya pili, asema hivi katika “Maongezi [yake] Pamoja na Trifo, Myahudi” (LXXXI): “Kulikuwako mwanamume fulani pamoja nasi, ambaye jina lake lilikuwa Yohana, mmoja wa mitume wa Kristo, aliyetoa unabii, kwa ufunuo mmoja aliofanyiwa.”a Irenaeus amtaja wazi kabisa mtume Yohana kuwa ndiye mwandikaji, hali moja na Clement wa Aleksandria na Tertullian, ambao ni wa mwisho wa karne ya pili na mapema katika karne ya tatu. Origen, msomi maarufu wa Kibiblia wa karne ya tatu, alisema hivi: “Mimi nasema juu ya yule aliyeegemea nyuma kwenye kifua cha Yesu, Yohana ambaye ameacha nyuma Gospeli moja, . . . na aliandika pia Apokalipsi.”b
4. (a) Ni nini chaonyesha badiliko la mtindo katika Ufunuo kwa kulinganishwa na miandiko mingine ya Yohana? (b) Ni nini chathibitisha Ufunuo kuwa sehemu asilia ya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu?
4 Uhakika wa kwamba miandiko mingine ya Yohana ilitia mkazo sana juu ya upendo haumaanishi kwamba hangeweza kuwa aliandika Ufunuo ulio na nguvu na msukumo mwingi sana. Yeye na Yakobo ndugu yake ndio waliojawa sana na ghadhabu kuelekea Wasamaria wa jiji fulani hivi kwamba wakataka kuita moto ushuke kutoka mbinguni. Ndiyo sababu walipewa jina zaidi la “Boanerge,” au ‘Wana wa Ngurumo.’ (Mk. 3:17; Luka 9:54) Badiliko hili la mtindo halipasi kusababisha ugumu wowote tukumbukapo kwamba katika Ufunuo habari yenye kuhusika ni tofauti. Aliyoona Yohana katika njozi hizi hayakufanana na chochote alichokuwa ameona kabla ya hapo. Upatano wa kutokeza wa kitabu hiki pamoja na sehemu nyingine yote ya unabii wa Maandiko wathibitisha bila shaka kwamba hicho ni sehemu asilia ya Neno la Mungu lenye pumzi Yake.
5. Ni lini Yohana alipoandika Ufunuo, na chini ya hali zipi?
5 Kulingana na ushuhuda wa mapema kabisa, Yohana aliandika Ufunuo karibu 96 W.K., yapata miaka 26 baada ya uharibifu wa Yerusalemu. Hiyo ingekuwa kuelekea mwisho wa utawala wa Maliki Domitian. Kwa kuhakikisha hilo, Irenaeus katika kitabu chake “Dhidi ya Mazushi” (V, xxx) asema hivi juu ya Apokalipsi: “Kwa maana hilo halikuonwa muda mrefu sana tangu wakati huo, bali karibu na siku yetu, kuelekea mwisho wa utawala wa Domitian.”c Eusebio na Jerome wote wawili wakubliana na ushuhuda huu. Domitian alikuwa ndugu ya Tito, aliyeongoza majeshi ya Kirumi kuharibu Yerusalemu. Yeye akawa maliki kwenye kifo cha Tito, miaka 15 kabla ya kitabu cha Ufunuo kuandikwa. Alidai kwamba aabudiwe kuwa mungu na akajitwalia kichwa Dominus et Deus noster (kumaanisha “Bwana na Mungu wetu”).d Ibada ya maliki haikusumbua wale walioabudu miungu bandia, lakini haingeweza kuingiliwa na Wakristo wa mapema, waliokataa kuacha imani yao iridhiane na jambo hili. Hivyo, kuelekea mwisho wa utawala wa Domitian (81-96 W.K.), mnyanyaso mkali ulikuja juu ya Wakristo. Yafikiriwa kwamba Domitian ndiye aliyempeleka Yohana uhamishoni Patmo. Domitian alipouawa katika 96 W.K., mwandamizi wake alikuwa Nerva maliki mwenye kuvumilia zaidi maoni ya watu, ambaye kwa wazi alimfungua Yohana. Ni wakati wa kifungo hiki cha gerezani katika Patmo kwamba Yohana alipokea njozi alizoandika.
6. Twapaswa kukiona kitabu cha Ufunuo kuwa nini, nacho chaweza kugawanywaje?
6 Ni lazima tuthamini kwamba mambo ambayo Yohana aliona na kuambiwa ayaandikie makundi hayakuwa mfululizo tu wa njozi zisizohusiana, zilizoandikwa vivi hivi tu. Sivyo, kitabu kizima cha Ufunuo, kutoka mwanzo mpaka mwisho, hutupa picha (wazo) yenye ushikamano mzuri juu ya mambo yajayo, kikitoka kwenye njozi moja mpaka nyingine mpaka ufunuzi kamili wa makusudi ya Ufalme wa Mungu ufikiwe mwishoni mwa njozi hizo. Kwa hiyo twapaswa kukiona kitabu cha Ufunuo kuwa ujumla na kuwa chenye kujumlishwa na sehemu zinazohusiana, zenye upatano, kikitupeleka mbali ndani ya wakati ujao kuanzia wakati wa Yohana. Baada ya utangulizi wacho (Ufu. 1:1-9), kitabu hicho chaweza kuonwa kuwa kimegawanywa katika njozi 16: (1) 1:10–3:22; (2) 4:1–5:14; (3) 6:1-17; (4) 7:1-17; (5) 8:1–9:21; (6) 10:1–11:19; (7) 12:1-17; (8) 13:1-18; (9) 14:1-20; (10) 15:1–16:21; (11) 17:1-18; (12) 18:1–19:10; (13) 19:11-21; (14) 20:1-10; (15) 20:11–21:8; (16) 21:9–22:5. Njozi hizi zafuatwa na umalizio wenye kuchochea, ambamo Yehova, Yesu, malaika, na Yohana wote wasema, wakifanya mchango wa mwisho wakiwa ndio wakuu katika kipitio cha uwasiliano.—22:6-21.
YALIYOMO KATIKA UFUNUO
7. Yohana asema nini juu ya chanzo cha Ufunuo, naye asema ashirikiana mambo gani kwa ujumla pamoja na wale walio katika yale makundi saba?
7 Utangulizi (1:1-9). Yohana aeleza Chanzo cha kimungu na sehemu ya kimalaika ya kipitio ambacho kupitia hicho ufunuo watolewa, naye aendelea kuelekeza maneno yake kwa wale walio katika makundi saba katika wilaya ya Asia. Yesu Kristo amewafanya “kuwa ufalme, makuhani kwa Mungu na Baba yake,” Yehova Mungu, Mweza Yote. Yohana awakumbusha kwamba yeye ni mshiriki pamoja nao “katika dhiki na ufalme na uvumilivu katika uandamani pamoja na Yesu,” wakiwa uhamishoni katika Patmo.—1:6, 9, NW.
8. (a) Yohana aagizwa kufanya nini? (b) Yeye aona nani katikati ya vinara vya taa, na Mmoja huyu aeleza nini?
8 Jumbe kwa yale makundi saba (1:10–3:22). Njozi ya kwanza ianzapo, kwa pumzi ya Mungu Yohana ajikuta katika siku ya Bwana. Sauti yenye nguvu kama ya tarumbeta yamwambia aandike katika hati-kunjo ayaonayo na kuyapeleka kwa yale makundi saba, katika Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia, na Laodikia. Akiigeukia sauti hiyo, Yohana aona “mtu fulani kama mwana wa binadamu” katikati ya vinara saba vya taa, akiwa na nyota saba katika mkono wake wa kulia. Huyu ajitambulisha kuwa “wa Kwanza na wa Mwisho,” Yule aliyepata kuwa mfu lakini sasa anaishi milele na milele na aliye na funguo za kifo na za Hadesi. Kwa hiyo yeye ndiye Yesu Kristo aliyefufuliwa. Aeleza hivi: “Zile nyota saba humaanisha malaika wa makundi saba, na vile vinara vya taa saba humaanisha makundi saba.”—1:13, 17, 20, NW.
9. Ni pongezi na shauri gani ambalo lapewa kwa makundi katika Efeso, Smirna, Pergamo, na Thiatira?
9 Yohana aambiwa amwandikie malaika wa kundi la Efeso, ambalo, lijapofanya kazi kwa jasho, kuvumilia, na kukataa kuchukuliana na watu wabaya, limeacha upendo walo wa kwanza na lapaswa kutubu na kufanya matendo ya hapo kwanza. Kundi katika Smirna laambiwa kwamba lijapokuwa na dhiki na umaskini, kwa uhakika lina utajiri na halipaswi kuogopa: “Jithibitishe mwenyewe kuwa mwaminifu mpaka kifo, na mimi nitakupa wewe taji la uhai.” Kundi katika Pergamo, linalokaa “palipo na kiti cha ufalme cha Shetani,” laendelea kushika sana jina la Kristo lakini lina waasi-imani katikati yalo, na ni lazima hawa watubu au sivyo Kristo atafanya vita nao kwa upanga mrefu wa kinywa chake. Katika Thiatira kundi lina ‘upendo na imani na huduma na uvumilivu,’ hata hivyo lamvumilia “huyo mwanamke Yezebeli.” Hata hivyo, waaminifu washikao sana msimamo wao watapokea “mamlaka juu ya mataifa.”—2:10, 13, 19, 20, 26, NW.
10. Ni jumbe gani zipelekwazo kwa makundi katika Sardi, Filadelfia, na Laodikia?
10 Kundi katika Sardi lina sifa ya kuwa hai, lakini limekufa kwa sababu matendo yalo hayafanywi kikamili mbele za Mungu. Hata hivyo, wale washindao hawatafutwa majina yao katika kitabu cha uhai. Kundi katika Filadelfia limeshika neno la Kristo, hivyo basi yeye aahidi kuliweka kundi kutoka “ile saa ya mtihani, inayopasa kuja juu ya dunia yote kwa ujumla inayokaliwa.” Kristo atamfanya ashindaye awe nguzo katika hekalu la Mungu Wake. Kristo asema: “Nitaandika juu yake yeye jina la Mungu wangu na jina la jiji la Mungu wangu, Yerusalemu jipya . . . na hilo jina jipya langu.” Akijirejezea kuwa “mwanzo wa uumbaji wa Mungu,” Kristo aliambia kundi la Laodikia kwamba halina moto wala si baridi na litatapikwa kutoka kinywa chake. Ingawa wajisifia mali, wale walio katika kundi hilo kwa kweli ni maskini, vipofu, na uchi. Wao wahitaji mavazi ya nje, na kuhitaji dawa ya macho ili waone. Kristo atakuja ndani ale pamoja na mtu yeyote amfunguliaye mlango. Kwa yule ashindaye, Kristo atampa kuketi pamoja naye juu ya kiti chake cha ufalme, kama vile ameketi pamoja na Baba yake juu ya kiti Chake cha ufalme.—3:10, 12, 14, NW.
11. Ni njozi gani tukufu yafuata kuja kwenye uangalifu wa Yohana?
11 Njozi ya utakatifu na utukufu wa Yehova (4:1–5:14). Njozi ya pili yatupeleka mbele za kiti cha ufalme cha Yehova cha kimbingu kilicho cha fahari. Tamasha ile ina mng’ao mwingi sana katika uzuri wayo, kama vito vya thamani kwa uangavu. Kuzunguka hicho kiti cha ufalme wameketi wazee 24 waliovaa mataji. Viumbe hai wanne wamhesabia Yehova utakatifu, naye aabudiwa kuwa mwenye kustahili “kupokea utukufu na heshima na nguvu” kwa sababu ya kuwa ndiye Muumba wa vitu vyote.—4:11, NW.
12. Ni nani peke yake astahiliye kuifungua hati-kunjo yenye vifungo saba?
12 “Mmoja aketiye juu ya kiti cha ufalme” ashika hati-kunjo yenye vifungo saba. Lakini ni nani astahiliye kuifungua hati-kunjo? Astahiliye tu ni yule “Simba ambaye ni wa kabila la Yuda, mzizi wa Daudi”! Mmoja huyu, ambaye pia ndiye “Mwana-Kondoo ambaye alichinjwa,” aichukua hati-kunjo kutoka kwa Yehova.—5:1, 5, 12, NW.
13. Ni njozi gani yenye mambo mengi yaandamana na kufunguliwa kwa vile vifungo sita vya kwanza?
13 Mwana-Kondoo afungua vifungo sita vya hati-kunjo (6:1–7:17). Sasa njozi ya tatu yaanza. Mwana-Kondoo aendelea na kufungua vile vifungo. Kwanza, mpanda farasi aliye juu ya farasi mweupe aenda “akishinda na kukamilisha ushindi wake.” Halafu mpandaji wa farasi rangi-moto aondoa amani duniani na mwingine aliye juu ya farasi mweusi atoa nafaka kwa vipimo. Farasi mweupe-mweupe apandwa na Kifo, na Hadesi afuata kwa ukaribu. Kifungo cha tano chafunguliwa, na “wale waliochinjwa kwa sababu ya neno la Mungu” waonwa wakiomba kulipizwa kisasi kwa damu yao. (6:2, 9, NW) Kwenye kufunguliwa kwa kifungo cha sita, kuna tetemeko kubwa la dunia, jua na mwezi vyatiwa giza, na wenye uweza wa dunia waomba milima iwaangukie na kuwaficha kutoka kwa Yehova na hasira ya Mwana-Kondoo.
14. Ni nini chafuata kuonwa kwa habari ya watumwa wa Mungu na umati mkubwa usiohesabika?
14 Baada ya hilo, njozi ya nne yaanza. Malaika wanne waonwa wakizuia zile pepo nne za dunia mpaka watumwa wa Mungu watiwe muhuri katika vichwa vyao. Hesabu yao ni 144,000. Baadaye Yohana aona umati mkubwa usiohesabika kutoka mataifa yote, wamesimama mbele za Mungu na Mwana-Kondoo, nao wawasifu kwa wokovu, wakitoa utumishi mchana na usiku katika hekalu la Mungu. Mwana-Kondoo mwenyewe ‘atawachunga na kuwaelekeza kwenye chemchemi za maji ya uhai.’—7:17, NW.
15. Ni nini chafuata kufunguliwa kwa kifungo cha saba?
15 Kifungo cha saba chafunguliwa (8:1–12:17). Kuna kimya mbinguni. Halafu tarumbeta saba zapewa kwa wale malaika saba. Mipulizo ya tarumbeta sita za kwanza ndiyo ijumlikayo kuwa njozi ya tano.
16. (a) Ni nini chafuata mpulizo wa tarumbeta tano za kwanza, na ni nini ulio wa kwanza wa zile ole tatu? (b) Tarumbeta ya sita yapeleka habari gani?
16 Tarumbeta tatu za kwanza zipulizwapo kwa kufuatana, maafa yanyesha juu ya dunia, bahari, na mito na pia vibubujiko vya maji. Kwenye tarumbeta ya nne, theluthi ya jua, mwezi, na nyota yatiwa giza. Kwenye mvumo wa tano, nyota moja kutoka mbinguni yaachilia tauni ya nzige ambao wawashambulia wale ambao “hawana muhuri wa Mungu juu ya vipaji vya nyuso zao.” Huu ni “ole mmoja,” na mbili zaidi zinakuja. Tarumbeta ya sita yapeleka habari juu ya kufunguliwa kwa malaika wanne ambao watokea ili kuua. “Mamiriadi mawili ya mamiriadi” ya wapanda farasi yaleta maafa na machinjo zaidi, lakini bado watu hawatubu maovu yao.—9:4, 12, 16, NW.
17. Ni matukio gani yafikiayo upeo katika tangazo la kwamba ole wa pili umepita?
17 Njozi ya sita ianzapo, malaika mwingine imara ashuka kutoka mbinguni na kujulisha kwamba “katika siku za kuvumisha kwa malaika wa saba . . . siri takatifu ya Mungu kulingana na habari njema” yapasa kumalizwa. Yohana apewa hati-kunjo ndogo aile. Ni “tamu kama asali” katika kinywa chake, lakini yafanya tumbo lake liwe chungu. (10:7, 9, NW) Mashahidi wawili watoa unabii kwa siku 1,260 wakiwa katika nguo za magunia; halafu wauawa na “hayawani-mwitu ambaye apanda kutoka katika abiso,” na mizoga yao yaachwa siku tatu na nusu “katika njia pana ya jiji kubwa.” Wale wanaokaa duniani washangilia juu yao, lakini hilo lageuka kuwa ogopesho kubwa wakati Mungu awainuapo kwenye uhai. Katika saa hiyo, kuna tetemeko kubwa la dunia. “Ole wa pili umepita.”—11:7, 8, 14, NW.
18. Ni tangazo gani la maana latukia kwenye mvumo wa tarumbeta ya saba, na sasa ni wakati uliowekwa kwa ajili ya jambo gani?
18 Sasa malaika wa saba apuliza tarumbeta yake. Sauti za kimbingu zatangaza hivi: “Ufalme wa ulimwengu ulipata kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake.” Wale “wazee ishirini na wanne” wamwabudu Mungu na kutoa shukrani, lakini mataifa yawa na hasira. Ni wakati wa Mungu uliowekwa kuhukumu wafu na kuthawabisha watakatifu wake na “kuangamiza wale wanaoangamiza dunia.” Patakatifu pake pa hekalu pafunguliwa, na ndani humo mwaonekana lile sanduku la agano lake.—11:15, 16, 18, NW.
19. Ni ishara na vita gani ionekanayo mbinguni, tokeo ni nini, na hilo lahusishaje ole wa tatu?
19 Kufuata tangazo hili la kusimamishwa kwa Ufalme, njozi ya saba yaonyesha mara hiyo “ishara kubwa” mbinguni. Ni mwanamke azaaye “mwana, wa kiume, ambaye apaswa kuchunga mataifa yote kwa ufito wa chuma.” “Drakoni mkubwa wa rangi-moto” asimama tayari kummeza mtoto, lakini mtoto huyo anaswa kwenda kwenye kiti cha ufalme cha Mungu. Mikaeli afanya vita na drakoni huyo, naye amvurumisha chini duniani huyu “nyoka wa awali kabisa, mmoja ambaye huitwa Ibilisi na Shetani.” Ni “ole kwa ajili ya dunia”! Drakoni amnyanyasa mwanamke na kwenda zake kufanya vita na wanaobaki wa mbegu yake.—12:1, 3, 5, 9, 12; 8:13, NW.
20. Ni hayawani-mwitu gani wawili ambao wafuata kuonekana katika njozi, nao wana uvutano gani juu ya wanadamu duniani?
20 Hayawani-mwitu kutoka baharini (13:1-18). Sasa njozi ya nane yaonyesha hayawani-mwitu mwenye vichwa saba na pembe kumi, akipanda kutoka baharini. Apata nguvu zake kutoka kwa yule drakoni. Kimoja cha vichwa vyake kilikuwa kana kwamba kimechinjwa mpaka kifo, lakini kiliponywa, na dunia yote ikamsifu hayawani. Atamka makufuru juu ya Mungu na kufanya vita pamoja na watakatifu. Lakini, tazama! Yohana aona hayawani-mwitu mwingine, huyu akipanda kutoka duniani. Ana pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini aanza kusema kama drakoni. Awaongoza vibaya wakaaji wa dunia na kuwaambia wafanye mfano kwa ajili ya hayawani-mwitu wa kwanza. Wote washurutishwa waabudu mfano huo au sivyo wauawe. Bila alama au hesabu ya huyo hayawani-mwitu, hakuna awezaye kununua wala kuuza. Hesabu yake ni 666.
21. Yohana aona nini juu ya Mlima Sayuni, malaika washuhudia na kutangaza juu ya nini, na mzabibu wa dunia waondolewaje mbali?
21 “Habari njema za milele” na jumbe ambazo zahusiana nazo (14:1-20). Kwa utofautiano wenye kufurahisha, katika njozi ya tisa, Yohana amwona Mwana-Kondoo juu ya Mlima Sayuni, na pamoja naye kuna 144,000 walio na majina ya Mwana-Kondoo na ya Baba juu ya vipaji vya nyuso zao. “Wanaimba kana kwamba ni wimbo mpya mbele ya kiti cha ufalme,” wakiisha ‘kununuliwa kutoka miongoni mwa ainabinadamu wakiwa matunda ya kwanza kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.’ Malaika mwingine atokea katikati ya mbingu, akiwa na “habari njema za milele kujulisha wazi” kwa kila taifa na ajulisha wazi hivi: “Hofuni Mungu na kumpa yeye utukufu.” Na bado malaika mwingine atangaza hivi: “Babuloni Mkubwa ameanguka!” Mwingine, wa tatu, atangaza kwamba wale waabuduo hayawani-mwitu na mfano wake watakunywa hasira ya Mungu. Mmoja aliye “kama mwana wa binadamu” atupa mundu wake, na malaika mwingine pia atupa mundu wake na kukusanya mzabibu wa dunia, akiutupa ndani ya “shinikizo la divai kubwa la kasirani ya Mungu.” Kama vile shinikizo la divai likanyagwavyo nje ya jiji, damu yaja juu kufikia hatamu za wale farasi, “kwa kitalifa cha farlong’i elfu moja mia sita” (karibu kilometa 296).—14:3, 4, 6-8, 14, 19, 20, NW.
22. (a) Nani wafuata kuonwa wakitukuza Yehova, na kwa nini? (b) Mabakuli saba ya kasirani ya Mungu yamiminwa wapi, na ni matukio gani yenye kutikisa ulimwengu yafuata?
22 Malaika wenye zile tauni saba za mwisho (15:1–16:21). Njozi ya kumi yaanza kwa muono mwingine mfupi wa ua wa kimbingu. Wale ambao wamepata ushindi juu ya hayawani-mwitu wamtukuza Yehova, yule “Mfalme wa umilele,” kwa maana kazi zake ni kubwa na za ajabu. Malaika saba watoka katika patakatifu mbinguni na kupewa mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa kasirani ya Mungu. Ya kwanza sita yamiminwa katika dunia, bahari, na mito na vibubujiko vya maji, na pia juu ya jua, kiti cha ufalme cha hayawani-mwitu, na ule mto Frati, yakikausha maji yao kuwaachia njia “wafalme kutoka zukio la jua.” Semi za roho waovu zakusanya ‘wafalme wa dunia nzima yote inayokaliwa kuwakusanya pamoja kwenye vita ya ile siku kubwa ya Mungu Mweza Yote’ kwenye Har–Magedoni. Bakuli la saba lamiminwa juu ya hewa, na katikati ya ajabu za kiasili zenye kuogofya, lile jiji kubwa lagawanyika sehemu tatu, majiji ya mataifa yaanguka, na Babuloni apokea ‘kikombe cha divai ya kasirani ya hasira yake.’—15:3; 16:12, 14, 19, NW.
23. (a) Hukumu ya Mungu yafikilizwaje juu ya Babuloni Mkubwa? (b) Ni matangazo na maombolezo gani ambayo yaandamana na anguko lake, na ni sifa gani yenye shangwe yavuma kotekote mbinguni?
23 Hukumu ya Mungu juu ya Babuloni; ndoa ya Mwana-Kondoo (17:1–19:10). Njozi ya 11 yaanza. Tazama! Ni hukumu ya Mungu juu ya “Babuloni Mkubwa, mama ya makahaba,” ‘ambaye wafalme wa dunia walifanya uasherati na yeye.’ Akiwa amelewa damu ya watakatifu, yeye apanda hayawani-mwitu wa rangi nyekundu-nyangavu mwenye vichwa saba na pembe kumi. Hayawani huyu “alikuwako, lakini hayuko, na bado yu karibu kupanda atoke ndani ya abiso.” Pembe zake kumi zapigana na Mwana-Kondoo, lakini kwa sababu yeye ni “Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme,” yeye awashinda. Pembe kumi zamgeukia kahaba na kumnyafua, na njozi ya 12 ianzapo, malaika mwingine, ambaye utukufu wake wanurisha dunia, ajulisha hivi: “Yeye ameanguka! Babuloni Mkubwa ameanguka!” Watu wa Mungu waamriwa watoke ndani yake, wasije wakashiriki katika tauni zake. Wafalme na watu hodari wengine wa dunia wamlilia, wakisema: “Ni vibaya mno, ni vibaya mno, wewe jiji kubwa, Babuloni wewe jiji imara, kwa sababu katika saa moja hukumu yako imewasili!” Mali zake nyingi zimemalizwa fyu. Kama vile jiwe kubwa la kusagia huvurumishwa ndani ya bahari, hivyo kwa mrusho wa kasi Babuloni amevurumishwa chini, asionekane tena kamwe. Mwishowe damu ya watakatifu wa Mungu imelipiwa kisasi! Mbinguni kwavuma mara nne kwa wito huu: “Sifuni Yah, enyi watu!” Sifuni Yah kwa sababu amefikiliza hukumu juu ya yule kahaba mkubwa! Sifuni Yah kwa sababu Yehova ameanza kutawala akiwa mfalme! Shangilieni na kuwa na shangwe nyingi mno kwa sababu “ndoa ya Mwana-Kondoo imewasili na mke wake amejitayarisha mwenyewe”!—17:2, 5, 8, 14; 18:2, 10; 19:1, 3, 4, 6, 7, NW.
24. (a) Ni ya kukata maneno kadiri gani vita ifanywayo na Mwana-Kondoo? (b) Ni nini litukialo wakati wa ile miaka elfu, na ni nini kifuatacho kwenye mwisho wayo?
24 Mwana-Kondoo afanya vita kwa uadilifu (19:11–20:10). Katika njozi ya 13, “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana” aongoza majeshi ya kimbingu katika vita ya uadilifu. Wafalme na wanaume imara wawa mizoga kwa ndege wa mbinguni, na yule hayawani-mwitu na yule nabii bandia wavurumishwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kiberiti. (19:16, NW) Njozi ya 14 ianzapo, malaika aonekana “akija chini kutoka katika mbingu mwenye ufunguo wa abiso na mnyororo mkubwa katika mkono wake.” “Drakoni, nyoka wa awali kabisa, ambaye ndiye Ibilisi na Shetani,” akamatwa na kufungwa kwa miaka elfu. Wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza wawa ‘makuhani wa Mungu na wa Kristo na kutawala wakiwa wafalme pamoja na yeye kwa miaka elfu.’ Baada ya hapo, Shetani atafunguliwa aende nje kupotosha mataifa ya dunia, lakini atavurumishwa, pamoja na wale wamfuatao, ndani ya ziwa la moto.—20:1, 2, 6, NW.
25. Ni njozi gani ya kusisimua ifuatayo, na ni nani atarithi mambo yaonwayo?
25 Siku ya Hukumu na utukufu wa Yerusalemu Jipya (20:11–22:5). Ile njozi ya 15 yenye kusisimua yafuata. Wafu, wakubwa na wadogo, wahukumiwa mbele za kiti cheupe kikubwa cha Mungu. Kifo na Hadesi vyavurumishwa ndani ya ziwa la moto, ambalo “humaanisha kifo cha pili,” na pamoja nao avurumishwa mtu yeyote asiyepatikana ameandikwa katika kitabu cha uhai. Yerusalemu Jipya lashuka kutoka mbinguni, na Mungu afanya hema pamoja na ainabinadamu, akifuta kila chozi kutoka kwenye macho yao. Hakuna kifo, maombolezo, kilio, wala maumivu tena! Ndiyo, Mungu ‘anafanya vitu vyote kuwa vipya,’ naye ahakikisha ahadi yake, akisema: “Andika, kwa sababu maneno haya ni ya uaminifu na ya kweli.” Wale wanaoshinda watarithi vitu hivyo, lakini waoga, wale wasio na imani, na wale wasio na maadili au wazoeao uwasiliani-roho au ibada ya sanamu hawatarithi.—20:14; 21:1, 5, NW.
26. (a) Ni usimulizi gani watolewa juu ya Yerusalemu Jipya? (b) Ni mambo gani yenye kuendeleza uhai yaonwa katika jiji hilo, na nuru yalo yatoka wapi?
26 Yohana sasa aonyeshwa, katika njozi ya 16 na njozi ya mwisho, “mke wa Mwana-Kondoo,” Yerusalemu Jipya, malango yalo 12 na mawe ya msingi 12 yakiwa na majina ya wale mitume 12. Ni la miraba minne, na fahari ya utukufu walo yawakilishwa na yaspa, dhahabu, na lulu ndani yalo. Yehova na Mwana-Kondoo ndio hekalu la jiji, nao ni nuru yalo pia. Ni wale tu walioandikwa katika hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo wawezao kuingia humo. (21:9, NW) Mto safi wa maji ya uhai watoka kwenye kiti cha ufalme kuteremkia ile njia pana ya jiji, na kila upande kuna miti ya uhai, ambayo yazaa mazao mapya ya matunda kila mwezi nayo ina majani ya kuponyea. Kiti cha ufalme cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwa katika jiji, na watumwa wa Mungu wataona uso Wake. “Yehova Mungu atatoa nuru juu yao, na wao watatawala wakiwa wafalme milele na milele.”—22:5, NW.
27. (a) Yohana apewa uhakikishio gani kuhusu unabii huo? (b) Ufunuo chamalizika kwa mwaliko gani wenye mkazo na kwa onyo gani?
27 Umalizio (22:6-21). Uhakikishio watolewa: “Maneno haya ni ya uaminifu na ya kweli.” Wenye furaha, kweli kweli, ni wale wote washikao maneno ya unabii! Akiisha kusikia na kuona mambo haya, Yohana aanguka kumwabudu malaika, ambaye amkumbusha kumwabudu Mungu pekee. Maneno ya unabii hayapasi kutiwa muhuri, “wakati uliowekwa u karibu.” Wenye furaha ni wale wanaopata mwingio ndani ya lile jiji, kwa maana nje kuna wachafu na “kila mmoja ambaye anapenda na kuendeleza uongo.” Yesu aeleza kwamba yeye mwenyewe alipeleka ushahidi huu kwa makundi kupitia malaika wake, na kwamba yeye ni “mzizi na mzao wa Daudi, na nyota nyangavu ya asubuhi.” “Na roho na bibi-arusi huendelea kusema: ‘Njoo!’ Na acheni yeyote anayesikia aseme: ‘Njoo!’ Na acheni yeyote anayeona kiu aje; acheni yeyote ambaye anataka atwae maji ya uhai bure.” Na acheni yeyote asiongeze wala kuondoa katika maneno ya unabii huu, fungu lake lisije likaondolewa “kutoka miti ya uhai kutoka jiji takatifu.”—22:6, 10, 15-17, 19.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
28. Ni kwa vielelezo gani sisi twaweza kuthamini kwamba Ufunuo chafunga maandishi yaliyoanzwa katika sehemu ya kwanza ya Biblia?
28 Kitabu cha Ufunuo chatoa umalizio mtukufu kama nini kwa mkusanyo uliopuliziwa na Mungu wa Biblia wa vitabu 66! Hakuna chochote kimeachwa nje. Hakuna sehemu zilizoachwa bila kuelezwa. Sasa twaona wazi ule upeo mtukufu na pia mwanzo. Sehemu ya mwisho ya Biblia yamalizia maandishi yaliyoanza katika sehemu ya kwanza. Kama vile Mwanzo 1:1 kielezavyo uumbaji wa Mungu wa mbingu na dunia halisi, ndivyo Ufunuo 21:1-4 kielezavyo mbingu mpya na dunia mpya na baraka zisizoelezeka zitakazoletwa kwa ainabinadamu, kama ilivyoelezwa kwa unabii pia kwenye Isaya 65:17, 18; 66:22; na 2 Petro 3:13. Kama vile binadamu wa kwanza alivyoambiwa angekufa hakika akikosa kutii, ndivyo Mungu kwa uhakika athibitisha kwamba “kifo hakitakuwapo tena” kwa walio watiifu. (Mwa. 2:17; Ufu. 21:4, NW) Nyoka alipotokea kwanza akiwa mdanganyi wa ainabinadamu, Mungu alitabiri kuchubuliwa kwa kichwa chake, na Ufunuo chafunua jinsi ‘nyoka wa awali kabisa, aliye Ibilisi na Shetani,’ avurumishwa mwishowe ndani ya uharibifu. (Mwa. 3:1-5, 15; Ufu. 20:10, NW) Ijapokuwa mwanadamu asiye mtiifu aliondoshwa kwenye mti wa uhai wa Kiedeni, miti ya ufananisho yatokea “kwa ajili ya kuponeshwa kwa mataifa” ya ainabinadamu watiifu. (Mwa. 3:22-24; Ufu. 22:2, NW) Kama vile mto ulivyotoka Edeni kutia maji katika bustani, ndivyo mto wa ufananisho, wenye kupa uhai na kuendeleza uhai, wafananishwa kuwa ukitiririka kutoka kwenye kiti cha ufalme cha Mungu. Hiyo yaenda sambamba na njozi ya mapema kidogo ya Ezekieli, na pia yakumbusha maneno ya Yesu juu ya “chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.” (Mwa. 2:10; Ufu. 22:1, 2, NW; Eze. 47:1-12; Yn. 4:13, 14) Kwa utofautiano na kuondoshwa kwenye kuwapo kwa Mungu, kama walivyokuwa mwanamume na mwanamke wa kwanza, washindi waaminifu watauona uso wake. (Mwa. 3:24; Ufu. 22:4) Ni jambo lenye mafaa kweli kweli kufikiria njozi hizi zinazosisimua za Ufunuo!
29. (a) Ufunuo chaunganishaje pamoja unabii unaohusu Babuloni? (b) Ni ulinganishi gani uonwao kati ya njozi za Ufalme, na pia za wale hayawani, katika Danieli na katika Ufunuo?
29 Angalia, pia, jinsi Ufunuo kinavyounganisha pamoja unabii unaohusu Babuloni mwovu. Isaya alikuwa ametangulia kuona anguko la Babuloni halisi muda mrefu kabla halijatukia, naye alikuwa amejulisha wazi hivi: “Ameanguka! Babuloni ameanguka!” (Isa. 21:9) Yeremia alitoa unabii pia juu ya Babuloni. (Yer. 51:6-12) Lakini Ufunuo chasema kwa ufananisho wa “Babuloni Mkubwa, mama wa makahaba na wa vitu vya kunyarafisha vya dunia.” Ni lazima yeye pia apinduliwe, na Yohana aona hilo katika njozi, akijulisha hivi: “Yeye ameanguka! Babuloni Mkubwa ameanguka!” (Ufu. 17:5; 18:2) Je! wakumbuka njozi ya Danieli ya ufalme uliosimamishwa na Mungu ambao utapondaponda falme nyingine zote na kusimama “mpaka nyakati zisizo dhahiri”? Angalia jinsi hili laungana na tangazo la kimbingu katika Ufunuo: “Ufalme wa ulimwengu ulipata kuwa ufalme wa Bwana yetu na wa Kristo wake, na yeye atatawala akiwa mfalme milele na milele.” (Dan. 2:44; Ufu. 11:15, NW) Na kama vile njozi ya Danieli ilivyosimulia ‘mmoja aliye mfano wa mwanadamu akija pamoja na mawingu ya mbingu kupewa mamlaka, na utukufu, na ufalme,’ ndivyo Ufunuo kitambulishavyo Yesu Kristo kuwa “Mtawala wa wafalme wa dunia” na kuwa “anakuja pamoja na mawingu,” naye asema kwamba “kila jicho litamwona.” (Dan. 7:13, 14; Ufu. 1:5, 7, NW) Kuna ulinganishi fulani wa kuangaliwa, pia, kati ya hayawani wa njozi za Danieli na hayawani wa Ufunuo. (Dan. 7:1-8; Ufu. 13:1-3; 17:12) Ufunuo chatoa uwanja mpana kweli kweli wa funzo lenye kutia nguvu imani.
30. (a) Ni muono gani kamili ambao Ufunuo chatoa juu ya kutakaswa kwa jina la Yehova kupitia Ufalme? (b) Ni nini chakaziwa kuhusu utakatifu, na hilo lahusu nani?
30 Ufunuo chatoa njozi nzuri kama nini yenye sehemu nyingi kuhusu Ufalme wa Mungu! Kwa njia yenye uvutio chakaza fikira kwenye mambo ambayo manabii wa zamani na Yesu na wanafunzi wake walisema kuhusu Ufalme. Hapa tuna muono uliotimilika wa kutetewa kwa jina la Yehova kupitia Ufalme: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Yehova Mungu, Mweza Yote.” Yeye astahili “kupokea utukufu na heshima na nguvu.” Kwa kweli, yeye ndiye ‘ametwaa nguvu kuu zake na kuanza kutawala akiwa mfalme’ kupitia Kristo. Mwana huyu wa kifalme, “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana,” aonyeshwa kuwa mwenye bidii kama nini apigapo mataifa na kukanyaga “shinikizo la divai ya kasirani ya hasira ya Mungu Mweza Yote”! Kichwa kikuu cha Biblia juu ya kuondolewa malawama kwa Yehova kizidipo kusonga kwenye upeo wacho, yakaziwa kwamba kila mtu na kila kitu kinachoshiriki katika makusudi yake ya Ufalme ni lazima kiwe kitakatifu. Mwana-Kondoo, Yesu Kristo, ambaye “ana ufunguo wa Daudi,” asemwa kuwa mtakatifu, na ndivyo malaika za mbinguni. Wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza wasemwa kuwa ‘wenye furaha na watakatifu,’ na yakaziwa kwamba “kitu chochote kisicho kitakatifu na yeyote ambaye huendeleza kitu cha kunyarafisha” kwa vyovyote ‘hakitaliingia jiji takatifu Yerusalemu.’ Hivyo wale ambao wamenunuliwa kwa damu ya Mwana-Kondoo ‘wawe ufalme na makuhani kwa Mungu wetu’ wana kitia-moyo chenye nguvu cha kudumisha utakatifu mbele za Yehova. “Umati mkubwa” pia ni lazima ‘wafue majoho yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo’ ili watoe utumishi mtakatifu.—Ufu. 4:8, 11; 11:17; 19:15, 16; 3:7; 14:10; 20:6; 21:2, 10, 27; 22:19; 5:9, 10; 7:9, 14, 15, NW.
31. Ni sehemu gani za Ufalme zavutwa kwenye uangalifu wetu katika kitabu cha Ufunuo pekee?
31 Njozi ya huu Ufalme wenye adhama na mtukufu wa Mungu mtukufu yang’aa wazi katika akili zetu tuonapo sehemu fulani ambazo zavutwa kwenye uangalifu wetu katika kitabu cha Ufunuo tu. Humu ndimo tuna njozi kamili ya warithi wa Ufalme wakiwa juu ya Mlima Sayuni pamoja na Mwana-Kondoo, wakiimba wimbo mpya ambao ni wao tu wawezao kuujua. Ndio Ufunuo wa pekee utuambiao hesabu ya wale walionunuliwa kutoka duniani wauingie Ufalme—144,000—na kwamba hesabu hii imetiwa muhuri kutoka yale makabila 12 ya ufananisho ya Israeli wa kiroho. Ufunuo peke yacho ndicho kionyeshacho kwamba hawa ‘makuhani na wafalme,’ washirikio pamoja na Kristo katika ufufuo wa kwanza, watatawala pamoja naye pia “kwa miaka elfu.” Ni Ufunuo pekee kitoacho muono kamili wa “jiji takatifu, Yerusalemu jipya,” kikionyesha utukufu walo mwangavu, Yehova na Mwana-Kondoo na hekalu lalo, malango yalo 12 na mawe ya msingi, na wafalme watawalao ndani yalo milele kwa nuru ya milele ambayo Yehova huangaza juu yao.—14:1, 3; 7:4-8; 20:6; 21:2, 10-14, 22; 22:5, NW.
32. (a) Njozi ya “mbingu mpya” na “jiji takatifu, Yerusalemu Jipya,” yajumlishaje yote yaliyokuwa yametabiriwa kuhusu Mbegu ya Ufalme? (b) Ni baraka gani ambazo Ufalme wahakikishia ainabinadamu duniani?
32 Yaweza kusemwa kikweli kwamba njozi hii ya “mbingu mpya” na “jiji takatifu, Yerusalemu Jipya,” yajumlisha pamoja yote ambayo Maandiko yametabiri kutoka nyakati za kale kuhusu ile Mbegu ya Ufalme. Abrahamu alitazamia mbegu ambayo kwayo ‘familia zote za dunia kwa uhakika zingejibariki’ na “jiji lenye misingi halisi, ambalo mjenzi na mfanyi wa jiji hilo ni Mungu.” Sasa, katika njozi ya Ufunuo, jiji hili la baraka latambulishwa wazi kwa ajili yetu kuwa “mbingu mpya”—serikali mpya, Ufalme wa Mungu, wenye kufanyizwa na Yerusalemu Jipya (bibi-arusi wa Kristo) na Bwana-arusi wake. Wakiwa pamoja watafikiliza serikali ya uadilifu juu ya dunia yote. Yehova aahidi ainabinadamu yenye uaminifu kwamba wao waweza kuwa “vikundi vyake vya watu” katika hali yenye furaha, isiyo na dhambi wala kifo kama ile iliyoonewa shangwe kabla ya uasi katika Edeni. Na kwa kutia mkazo, Ufunuo chatuambia mara mbili kwamba Mungu ‘atapangusa kabisa machozi kutoka macho yao.’—Mwa. 12:3; 22:15-18; Ebr. 11:10; Ufu. 7:17; 21:1-4, NW.
33. (a) Ni njozi gani nzuri sana ambayo Ufunuo chatoa juu ya makusudi ya kimungu yaliyotimizwa? (b) “Kila andiko” limethibitikaje kuwa ‘lenye pumzi ya Mungu, lenye kufaa,’ na kwa nini sasa ndio wakati wa kujifunza na kutii Neno la Mungu?
33 Ndiyo, ni umalizio mtukufu kama nini kwa Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu! Ni vizuri kama nini hivi “vitu ambavyo lazima vitukie karibuni”! (Ufu. 1:1, NW) Jina la Yehova, “Mungu wa semi zilizopuliziwa na Mungu za manabii,” limetakaswa. (22:6, NW) Miandiko ya kiunabii ya karne 16 yaonyeshwa kwa utimizo, na matendo ya imani za maelfu ya miaka yathawabishwa! “Nyoka wa awali kabisa” amekufa, vikosi vyake vimeharibiwa, na uovu haupo tena. (12:9) Ufalme wa Mungu watawala ukiwa “mbingu mpya” kwa sifa yake. Mibaraka ya dunia iliyorudishwa, iliyojazwa na kutiishwa kulingana na kusudi la Yehova lililoelezwa katika sura ya kwanza ya Biblia, yaendelea kwa umilele mtukufu mbele ya ainabinadamu. (Mwa. 1:28) Kwa kweli kila andiko limethibitika kuwa “lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.” Yehova amelitumia kikamili kuongoza wanadamu wenye kuweza mambo, wenye vifaa kamili mpaka siku hii iliyo nzuri sana. Kwa hiyo, sasa ndio wakati wa kujifunza Maandiko haya kuimarisha imani yako. Tii amri zayo ili upokee baraka ya Mungu. Zifuate katika kile kijia kinyoofu kiongozacho kwenye uhai wa milele. Kwa kufanya hivyo, wewe pia waweza kusema, kwa uhakika uliothibitishwa ambao kitabu cha mwisho cha Biblia chamalizika kwao: “Ameni! Njoo, Bwana Yesu.”—2 Tim. 3:16; Ufu. 22:20, NW.
34. Twawezaje sasa kuwa na shangwe isiyolinganika, na kwa nini?
34 Lo! twaweza kupata shangwe iliyoje isiyo na kifani kwa kushangilia “ufalme wa Bwana yetu na wa Kristo wake,” ile Mbegu, wakati uletapo utakaso wa milele kwa jina lisilo na kifani la “Yehova Mungu, Mweza Yote”!—Ufu. 11:15, 17, NW.
[Maelezo ya Chini]
a The Ante-Nicene Fathers, Buku 1, ukurasa 240.
b The Ecclesiastical History, Eusebio, VI, xxv, 9, 10.
c The Lives of the Caesars (Domitian, XIII, 2).
d The Ante-Nicene Fathers, Buku 1, kurasa 559-60.