Sura 2
Aheshimiwa Kabla ya Kuzaliwa
BAADA ya malaika Gabrieli kumwambia yule mwanamke kijana Mariamu kwamba atazaa mtoto mwanamume ambaye atakuwa mfalme wa milele, Mariamu auliza: “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?”
‘Roho takatifu itakuja juu yako,’ Gabrieli aeleza, “na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”
Ili kumsaidia Mariamu aamini ujumbe wake, Gabrieli aendelea: “Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”
Mariamu akubali neno la Gabrieli. Nalo jibu lake ni nini? ‘Tazama, mimi ni mjakazi wa Yehova!’ asema kwa kupaaza sauti. “Na iwe kwangu kama ulivyosema.”
Muda mfupi baada ya Gabrieli kuondoka, Mariamu ajitayarisha na kwenda kumtembelea Elisabeti, anayeishi pamoja na mume wake Zakaria katika nchi ya milima-milima ya Yudea. Kutoka nyumbani kwa Mariamu Nazareti, hiyo ni safari ndefu inayochukua labda siku tatu au nne.
Mariamu afikapo mwishowe nyumbani kwa Zakaria, aingia na kutoa salamu. Anapofanya hivyo, Elisabeti ajawa na roho takatifu, naye amwambia Mariamu hivi: ‘Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya salamu yako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu.’
Kusikia hivyo, Mariamu aitikia kwa shukrani za kutoka moyoni: ‘Moyo wangu wamwadhimisha Yehova, na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; kwa kuwa ametazama unyonge wa mjakazi wake, kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa; kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu.’ Hata hivyo, ijapokuwa upendeleo ambao ameonyeshwa, Mariamu aelekeza heshima yote kwa Mungu. “Jina lake ni takatifu,” yeye asema, “na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha.”
Mariamu aendelea kumsifu Mungu kwa wimbo wa kiunabii ulio na pumzi ya Mungu, akitangaza hivi: “Amefanya nguvu kwa mkono wake; amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; ili kukumbuka rehema zake; kama alivyowaambia baba zetu, Abrahamu na uzao wake hata milele.”
Mariamu akaa pamoja na Elisabeti kwa miezi mitatu hivi, na bila shaka yeye awa msaada mkubwa wakati wa hayo majuma ya mwisho ya mimba ya Elisabeti. Ni jambo jema kweli kweli kwamba hao wanawake wawili waaminifu, wote wawili wakiwa wanachukua mimba ya mtoto kwa msaada wa Mungu, wanaweza kuwa pamoja katika wakati huo wenye baraka wa maisha zao!
Je! wewe umeona heshima ambayo Yesu alipewa hata kabla ya kuzaliwa? Elisabeti alimwita “Bwana wangu,” na mtoto wake asiyezaliwa bado aliruka kwa shangwe Mariamu alipotokea kwanza. Kwa upande mwingine, baadaye wengine walimtendea bila heshima Mariamu na mtoto wake ambaye hajazaliwa bado, kama vile tutakavyoona. Luka 1:26-56.
▪ Gabrieli amwambia Mariamu nini ili kumsaidia aelewe jinsi angekuwa na mimba?
▪ Yesu aliheshimiwaje kabla ya kuzaliwa?
▪ Mariamu asema nini katika wimbo wa kiunabii katika kumsifu Mungu?
▪ Mariamu akaa pamoja na Elisabeti kwa muda gani, na kwa nini inafaa kwamba Mariamu akae pamoja na Elisabeti katika kipindi cha wakati huo?