Sura 32
Ni Jambo Gani Lililo Halali Siku ya Sabato?
NI KATIKA siku nyingine ya Sabato Yesu anapotembelea sinagogi karibu na Bahari ya Galilaya. Yupo mwanamume mmoja mwenye mkono wa kuume uliopooza. Waandishi na Mafarisayo wanatazama kwa ukaribu waone kama Yesu atamponya. Mwishowe wanauliza: “Ni halali kuponya watu siku ya sabato?”
Viongozi wa kidini Wayahudi wanaamini kwamba kuponya ni halali siku ya Sabato ikiwa tu uhai umo hatarini. Kwa kielelezo, wao wanafundisha kwamba si halali kuunganisha mfupa uliovunjika au kufunga mahali palipoteguka katika siku ya Sabato. Kwa hiyo waandishi na Mafarisayo wanamwuliza Yesu maswali kwa jitihada ya kupata jambo la kumshtaki.
Lakini Yesu ajua mawazo yao. Wakati ule ule, yeye atambua kwamba wao wamechagua kufuata maoni ya kupita kiasi, yasiyo ya kimaandiko juu ya mambo ambayo yangevunja takwa la siku ya Sabato linalokataza kazi. Hivyo Yesu anaandaa mambo ili kuwa na mkabiliano wa kutazamisha kwa kumwambia mwanamume yule mwenye mkono uliopooza: “Ondoka, simama katikati.”
Sasa, akiwageukia waandishi na Mafarisayo, Yesu anasema: “Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa?” Kwa kuwa kondoo anafananisha akiba ya pesa, wao hawangemwacha shimoni mpaka kesho yake, labda awe mgonjwa na kuwaletea hasara. Zaidi ya hilo, Maandiko yanasema: “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake.”
Akitoa ulinganisho, Yesu anaendelea kusema, “Je! mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato.” Viongozi wa kidini wanashindwa kukanusha hoja hiyo ya akili, kusababu kwa huruma, nao wanabaki kimya.
Kwa kukasirishwa, na kuhuzunishwa na upumbavu wao wa moyo mgumu, Yesu anatazama huku na huku. Halafu amwambia mwanamume yule: “Nyosha mkono wako.” Naye aunyosha na mkono unaponywa.
Badala ya kufurahi kwamba mkono wa mwanamume huyo umerudishiwa afya, Mafarisayo wanaenda nje na mara hiyo wanatunga hila pamoja na wafuasi wa chama cha Herode ili kumwua Yesu. Chama hicho cha kisiasa kwa wazi ni kutia ndani washiriki wa kidini walio Masadukayo. Kwa kawaida, chama hicho cha kisiasa kinapingana na Mafarisayo waziwazi, lakini wameungana kwa uthabiti katika kumpinga Yesu. Mathayo 12:9-14; Marko 3:1-6; Luka 6:6-11; Mithali 12:10; Kutoka 20:8-10.
▪ Ni hali gani iliyoko inayotokeza mkabiliano wa kutazamisha kati ya Yesu na viongozi wa kidini Wayahudi?
▪ Wayahudi hawa wanaamini nini juu ya kuponya siku ya Sabato?
▪ Yesu atumia kielezi gani kukanusha maoni yao yenye makosa?