Sura 37
Yesu Aondolea Mbali Huzuni ya Mjane
MUDA mfupi baada ya kumponya mtumishi wa ofisa wa jeshi, Yesu aondoka kwenda Naini, mji ulio kilometa 32 kusini-magharibi mwa Kapernaumu. Wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wanaambatana naye. Wakaribia mpakani mwa Naini inapoelekea jioni. Huko wakutana na mwandamano wa mazishi. Mwili wa kijina mmoja umebebwa kutoka katika mji ukazikwe.
Hali ya mama ni yenye huzuni hasa, kwa kuwa yeye ni mjane na huyo ni mwana wake wa pekee. Mumeye alipokufa, alipata faraja kwa sababu yeye alikuwa na mwana. Matumaini yake, tamaa, na fahari yalitiwa katika wakati ujao wa mwanaye. Lakini sasa hakuna mtu wa kumpa faraja. Huzuni yake ni kubwa sana wakati watu wa mjini wanapoambatana naye kwenda mahali pa mazishi.
Yesu anapomwona mwanamke huyo, moyo wake unaguswa kwa sababu ya huzuni yake kuu. Basi kwa huruma, lakini kwa uthabiti unaotoa tumaini, amwambia mwanamke yule: “Usilie.” Namna yake na tendo lake vyavuta fikira za umati. Basi anapokaribia na kuligusa jeneza ambalo limebeba maiti, wale wanaolibeba wanasimama. Ni lazima wote wawe wanataka kujua ni jambo gani atafanya.
Ni kweli kwamba wanaoambatana na Yesu wamemwona akiponya magonjwa ya watu wengi kwa mwujiza. Lakini labda hawajamwona akimfufua yeyote kutoka kwa wafu. Je! aweza kufanya jambo hilo? Akisema na mwili, Yesu aamuru: “Kijana, nakuambia, Inuka!” Yule mwanamume aketi! Aanza kunena, naye Yesu ampa mamaye.
Watu wanapoona ya kwamba kweli kijana yu hai, waanza kusema: “Nabii mkuu ametokea kwetu.” Wengine wasema: “Mungu amewaangalia watu wake.” Upesi habari zinazohusu tendo hili la kushangaza zaenea kotekote katika Yudea na nchi yote inayozunguka.
Yohana Mbatizaji angali gerezani, naye ataka kujifunza zaidi juu ya kazi ambazo Yesu anaweza kufanya. Wanafunzi wa Yohana wamwambia juu ya miujiza hiyo. Itikio lake ni nini? Luka 7:11-18.
▪ Kunatukia nini Yesu anapokuwa akikaribia Naini?
▪ Yesu aathiriwaje na kile anachoona, naye afanya nini?
▪ Watu wanaitikiaje mwujiza wa Yesu?