Je! Kifo Kinaweza Kushindwa?
JE! UMEPATA kufikiria uvutano ambao Yesu Kristo alileta katika historia ya kibinadamu? Kalenda ambayo watu wengi katika nchi za Uzunguni hutumia inategemea mwaka ambao inadhaniwa kwamba alizaliwa. Ni kama kitabu The World Book Encyclopedia kinavyosema: “Tarehe zinazotangulia mwaka huo zinapangwa kuwa ni K.K., au kabla ya Kristo. Tarehe zinazofuata mwaka huo zinatajwa kuwa ni A.D., au anno Domini (katika mwaka wa Bwana wetu).”
Kwa sababu gani Yesu anajulikana sana hivyo? Jambo moja ni kwa sababu ya miujiza ya ajabu aliyoifanya katika wilaya ya Galilaya. Eneo hilo lilikuwa katika upande wa kaskazini wa inayoitwa leo Jamhuri ya Israeli. Kuhusu wilaya hiyo mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza Flavio Yosefu aliandika hivi: “Kwa ujumla mchanga ni wenye rutuba na wenye kuzalisha; na umejaa mashamba ya miti ya namna zote . . . Zaidi ya hayo, miji mingi iko hapa.” Kwa kweli, yeye anadai, “kuna miji na vijiji mia mbili katika Galilaya.”a
Yesu Kristo alihubiri na kufanya miujiza ya kushangaza kati ya miji na vijiji hivyo vingi. Ingawa maandishi ya Biblia yanataja kwa jina miji michache kati ya hiyo, Yesu alifika kwenye miji mingi kati ya hiyo, kwa maana masimulizi yaliyoongozwa kwa roho yanasema hivi juu ya kuhubiri kwake katika eneo hilo: “Yesu alikuwa akizunguka katika miji na vijiji vyote, akifundisha katika masunagogi yao na kuhubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponyesha namna zote za magonjwa—Mt. 9:35, ZSB.
Wengi kati ya Wagalilaya ambao Yesu aliwahubiri walikuwa wanamjua, kwa maana yeye alikuwa amelelewa katikati yao kabisa—katika kijiji kile kidogo cha Nazareti, ambacho kilikuwa juu ya vilima vilivyokuwa umbali wa maili 18 (kilometre 28.8) upande wa kusini-magharibi wa Bahari ya Galilaya.
YESU AZURU NAINI
Ilikuwa katika mwaka 31 W.K., wakati wa mwaka wa pili wa huduma ya Yesu, kwamba mwana wa mjane huyo akafa katika mji wa Naini. Mji huo ulikuwa karibu tu maili tano au sita (kilometre 8 au 9.6) upande wa kusini-mashariki wa Nazareti, kijiji ambacho Yesu alikuwa amefanya makao. Wakati wa kufa kwa mwanamume huyo kijana, Yesu alikuwa akihubiri kuzunguka ufuo (kando) wa kaskazini wa Bahari ya Galilaya, ambapo alikuwa ametoka tu kutoa Mahubiri yake ya Mlimani yanayojulikana sana.
Biblia inasema kwamba, Yesu alipomaliza mahubiri hayo, “akaingia katika Kapernaumu.” Alipokuwa huko kwenye mji huo ulioko kando ya bahari, alimponya mtumwa wa afisa wa jeshi. “Upesi baada ya hayo [au, kama ambavyo hati nyingine za kale zinavyosema, “Katika siku iliyofuata”] alisafiri kwenda mji mmoja ulioitwa Naini, na wanafunzi wake na umati mkubwa walisafiri pamoja naye.”—Luka 7:1-11, New World Translation, chapa ya 971, maneno ya chini.
Safari hiyo ya kwenda upande wa kusini-magharibi kutoka Kapernaumu mpaka Naini ilikuwa ya maili 20 (kilometre 32) hivi, nayo ilikuwa safari ndefu kwa siku hata kwa watu waliokuwa wamezoea kusafiri kwa miguu. Yesu na kikundi chake walivuka bonde hilo na kukaribia lango la mji huo. Halafu, masimulizi yanatuambia hivi, “alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma.”—Luka 7:12, 13.
Kuhusu jambo hilo, Arthur P. Stanley, aliyetembelea sehemu hiyo wakati wa karne iliyopita, aliandika hivi katika kitabu chake Sinai na Palestina: “Katika mitelemko ya upande wa kaskazini... kuna kijiji kilicho magofu cha Naini. . . . Kilikuwa na lango moja tu, lile linalotokea upande wa kilima usio laini unaotelemka chini kwenye nchi iliyo tambarare. Kulingana na mila za [nchi za] Mashariki lazima iwe ni katika mtelemko huu mkubwa ambapo jeneza lilisimamishwa ‘karibu na lango’ la kijiji, walipokuwa ‘wanachukua nje maiti.’ . .. Sura ya nchi ya mahali hapo haitofautiani na mahali kwingine hata kwamba iwezekane kwa mtu kuikumbuka; walakini, kama ilivyo, na eneo dogo tunalopaswa kutafuta mahali ambapo kisa hicho chenye kugusa moyo kilipotokea, huenda pakawa ndipo pamojawapo penye kuvutia sana katika mandhari ya masimulizi ya Injili.”
Mtembezi mwingine wa karne ya 19 aliyetembelea mahali hapo, J. W. McGarvey, aliandika hivi katika kitabu chake Nchi za Biblia: “Naini iko juu ya mahali padogo panapochomoza, ikiwa na mtelemko mkubwa wa futi karibu 60 unaotelemka kwenye nchi tambarare iliyoko kaskazini ya hapo. Barabara inayotoka kaskazini inakuja mahali hapo kupitia bonde jembamba kwenye ncha yake ya upande wa magharibi, na kule mbali kutoka hapo kuna makaburi yaliyochongwa miambani . . . Yesu alipokuwa akikaribia lango la mji huo, akitoka upande wa Kapernaumu, ambapo alikuwa siku iliyotangulia, mwandamano wenye kumchukua mwana wa mjane ulikuwa ukienda mahali hapo pa kuzika watu, na hivyo wakakutana.”
MWUJIZA WENYE KUSHANGAZA
Alipokutana na umati huo wenye kuomboleza na mwanamke huyo mwenye majonzi mengi (huzuni), Yesu alimhurumia. Moyo wake uliguswa na huzuni yake nyingi. Kwa hiyo kwa upole, hata hivyo kwa uthabiti wenye kutoa uhakika, yeye alimwambia mwanamke huyo: “Usilie.” Kujiendesha na kutenda kwake kulivuta fikira za umati huo, hata kwamba ‘alipokaribia na kuligusa jeneza, wale waliokuwa wakilichukua walisimama.’ Lazima wote wawe walitaka kujua yale ambayo Yesu alikuwa anakaribia kufanya.
Ni kweli kwamba zaidi ya mwaka mmoja mapema, katika kijiji cha Kana, umbali wa maili fulani upande wa kaskazini, Yesu alikuwa amegeuza maji yakawa divai katika karamu ya arusi. Na ni kweli vilevile, kama ambavyo pengine waombolezaji wengine waliripoti, kwamba Yesu alikuwa ameponya watu maradhi kimwujiza katika miji na vijiji vingine vya karibu. Walakini kama inavyoonyeshwa na maandishi ya Biblia, Yesu hakuwa amepata kamwe kumfufua mtu ye yote kutoka kwa wafu. Je! angeweza kufanya jambo kama hilo?
Akielekeza maneno yake kwa maiti hiyo, Yesu aliamuru hivi: “Kijana, nakuambia, Inuka!” Nayo ajabu ya maajabu ikatokea! “Yule maiti akainuka, akaketi akaanza kusema. Akampa mama yake.”
Lilikuwa jambo lenye kutokeza kama nini! Ebu waza namna mwanamke huyo alivyojisikia. Wewe ungejionaje? Mtu akiwa katika hali kama hizo husema nini? Je! anasema ‘Asante kwa kumfufua mwana wangu’? Inaonekana maneno hayawezi kueleza kushukuru kwa ajili ya tendo kama hilo. Ulikuwa mwujiza kweli kweli!
“Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.” Bila shaka Yesu alikuwa nabii mkuu kutoka kwa Mungu.—Luka 7:13-17
JEI YEYE NDIYE MFANYA MIUJIZA ALIYEAHIDIWA?
Karne kumi na tano zilizokuwa zimetangulia, nabii Musa alikuwa amefanya miujiza ya ajabu kwa uwezo wa Mungu, hata akatenganisha Bahari Nyekundu (Shamu) ili taifa zima la Israeli lipite juu ya sakafu kavu. Walakini nabii mwenye kufanya miujiza mikubwa zaidi alikuwa ametabiriwa atakuja. Musa alisema hivi chini ya uongozi wa Mungu: “[Yehova], Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye.” (Kum. 18:15) Kwa hiyo, katika karne ya kwanza ulizo lilikuwa hili ‘Je! Yesu huyu wa Nazareti ndiye nabii wa Mungu ambaye alitabiriwa angekuja?’
Yohana Mbatizaji alikuwa ameamini kwamba Yesu alikuwa ndiye Yeye. Alikuwa ameona roho ya Mungu ikishuka juu ya Yesu baada ya kumbatiza katika Mto Yordani karibu miaka miwili iliyokuwa imetangulia. (Yohana 1:32-34) Sasa Yohana alikuwa kifungoni, akiwa amefungwa na Herode Antipa karibu mwaka mmoja uliokuwa umepita kwa ajili ya kusema wazi juu ya uhusiano wake wa uzinzi na mke wa nduguye.
Kwa hiyo ni huko kifungoni ambako ‘wanafunzi wa Yohana walimletea habari za hayo yote,’ sana-sana juu ya kufufuliwa kwa mwana wa yule mjane. Aliposikia ripoti hiyo, “ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu, akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”—Luka 7:18,19; Mt. 11:2, 3.
Hiyo si kusema Yohana alikuwa na shaka kwamba Yesu hakuwa ndiye yule nabii aliyeahidiwa. Walakini baada ya kusikia ripoti hiyo yenye kutokeza juu ya kurudishwa kwenye uzima kwa mwana wa yule mjane, yeye alitaka usemi wa kinywa wa moja kwa moja kutoka kwa Yesu wa kumtambulisha kuwa ndiye Masihi. Yohana alikuwa anataka kujua kama kulikuwako mwingine anayekuja, mrithi, ambaye angekamilisha utimizo wa mambo yote yaliyokuwa yametabiriwa kwamba yangefanywa na Masihi wa Mungu.
Kwa hiyo wanafunzi wa Yohana wale wawili walipomfikia Yesu na wakamjulisha ombi lake, masimulizi yanasema hivi: “Na saa ile ile [Yesu] aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu [wale wanafunzi wawili], akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiri habari njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.”—Luka 7:20-23.
Hakika ripoti hiyo ilimtia moyo Yohana. Ulikuwa uthibitisho wenye kuunga mkono kwamba kweli kweli Yesu alikuwa akifanya kazi zenye kutokeza ambazo zingemtofautisha nabii aliyetabiriwa na Musa. Hapakuwa pamepata kuwapo hapo mbeleni wonyesho wa nguvu za kimwujiza na mtu kama hizo! Kwa hiyo Yohana, ajapokuwa alikuwa ameachwa kifungoni, alikuwa na uhakika kwamba Yesu peke yake ndiye aliyekuwa nabii aliyetimiza yale ambayo Musa alikuwa ametabiri.
Hakuna shaka juu ya jambo hilo. Hata kifo kinaweza kushindwa kweli kweli, kama ilivyokuwa kwa habari ya yule mwana mfu wa mjane wa Naini!
[Maelezo ya Chini]
a Vita vya Wayahudi, Kitabu cha 3, sura ya 3, fungu la 2; Maisha ya Flavio Yosefu, fungu la 45.